Last updated: January 1, 2012 :

TANZANIA, NCHI YETU

 

 

WATOTO WA MAMA TUNAIANGAMIZA TANZANIA

Ni kweli kwamba serikali ina majukumu yake muhimu ya kuandaa sera nzuri zenye uwezo wa kuwaletea wananchi wengi maendeleo. Ni kweli pia kuwa ni jukumu la serikali kuweka msingi imara ambao utapelekea upatikanaji wa huduma muhimu za wananchi kama maji safi, nishati, huduma za elimu na afya, malazi, mawasiliano ya uhakika, uongozi bora, na utawala wa sheria. Ni ukweli usiopingika hata hivyo kuwa; ni jukumu la wananchi (binafsi au kwa ushirika) kutekeleza majukumu yao ya kuiletea Tanzania na hatimaye Afrika nzima maendeleo. Raisi wa zamani wa Marekani hayati John Kennedy aliwahi kusema maneno yaliyomfanya ahesabike miongoni mwa viongozi mashuhuri sana walioingoza Marekani. Katika hotuba yake ya kukabidhiwa uongozi, Kennedy alisema yafuatayo: Usijiulize ni nini unategemea kufanyiwa na serikali, jiulize ni nini utaifanyia serikali na nchi yako . Huu ndio ukweli ambao wamarekani wengi wamekuwa wanauishi kwa muda mrefu sasa. Ingawa serikali ya marekani inasifika duniani kwa juhudi zake za kumkomboa raia wake yeyote anayepatwa na matatizo makubwa ndani na nje ya nchi, wamarekani wengi sana wanahangaika kujua nini wafanye ili waisaidie nchi yao. Hali ndio hii hii hata kwa raia wa mataifa mengine tajiri duniani. Ingawa nimekuwa miongoni mwa watu wengi wanaopinga tabia ya kuiga tamaduni za kizungu au za kiarabu na kuzileta Tanzania, wakati huu ninaomba nipingane kidogo na marafiki zangu katika jambo hili. Utamaduni wa kuishi maisha ya kutoitegemea serikali kwa kila kitu una manufaa kuigwa. Ninashauri kuachana na maisha ya utoto-wa-mama. Watoto wa mama tunaliangamiza taifa letu la Tanzania....[Habari Kamili >>]

_______________________________________________

NISHATI YETU, MUSTAKABALI WETU

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa ikitegemea nishati ya umeme wa nguvu za maji ambapo Siali (Turbines), zinawekwa katika maeneo ya maporomoko ya maji na kisha kuzungushwa na maporomoko ya maji hayo--Matokeo yake: umeme huzalishwa. Lakini baada ya muda na mahitaji kuongezeka na kupelekea ugunduzi wa gesi ya Songosongo, Tanzania ilipata nishati ya nyongeza ya kuzalisha umeme kutokana na gesi hiyo ya asili. Hili ni jambo la kujivunia kwa sasa maana taifa letu limekuwa moja ya nchi waasisi wa matumizi ya umeme wa gesi katika bara zima la Africa. Hii ni kwamba, hadi sasa mradi wa gesi ya songosongo unazalisha asilimia 45 (nusu) ya umeme wote unaotumika nchini. Ingawa hili ni jambo zuri, lakini wataalamu wa Songosongo wanadhani kwamba wanaweza kuzalisha umeme zaidi ya hapo kama wakiruhusiwa kuboresha uzalishaji wao. Kwa hiyo jambo la kwanza tunalokuomba mheshimiwa Rais/waziri wa wizara husika ni kutoa vibali vyote vinavyohusika, si tu kuwezesha mradi wa songosongo kuzalisha umeme kadri ya uwezo wao, bali pia kuhimiza utafiti wa upatikanaji wa vyanzo vingine vya gesi nchini ili kwamba kama vyanzo vingine vya kutosha vikipatikana, nchi iweze si tu kujitosheleza ki-nishati, bali pia kuuza nje nishati ya ziada. Sambamba na hilo, wakati umefika sasa kwa serikali kufikiri na kubuni njia za kuelimisha watu wenye uwezo kuwekeza katika umeme unaotokana na miale ya jua (solar energy) pamoja na teknolojia mpya za kisasa kama vile uzalishaji wa umeme kwa njia ya upepo [wind power] wafanye hivyo...[Habari Kamili>>]

_______________________________________________

TUSIJIDANGANYE, HAKUNA FREE LUNCH DUNIANI

Mwanauchumi mashuhuri duniani, hayati Milton Friedman (1912-2006) aliwahi kusema kuwa hakuna kitu kama lanchi ya bure (there's no such thing as a free lunch). Ingawa hakuna uthibitisho kama Friedman ndio mtu wa kwanza duniani kutumia hiyo sentesi katika hotuba yake, watu wengi sana walimhusisha na huo usemi kwa muda mrefu wakati wa maisha yake. Milton mwenyewe aliwashangaza wasikilizaji wake wa taasisi ya CATO (CATO institute) nchini marekani (tarehe 6 May, 1993) aliposema kuwa vitu vizuri maishani vinapatikana bure (the best things in life are free). Hizi sentensi mbili zinapingana kwa kiasi fulani ingawa zinaelezea kitu kimoja. Si ajabu wanauchumi wengi duniani walipokea habari za kifo cha Friedman mwezi uliopita kwa masikitiko makubwa sana. Tafadhali marafiki zangu wa-jamaa (socialists) msianze kubeza uamuzi wa kutumia mifano ya Friedman katika makala hii. Nimeamua kutumia hotuba za Friedman ambaye wengi wenu mnamuita bepari (capitalist), kwa sababu kubwa mbili. Kwanza, matokeo ya mechi kati ya ubepari na ujamaa ni kwamba mabepari wameshinda 5-2. Pili, watanzania wengi sasa wameutambua uongo wenu wa-jamaa kwa sababu ya mali za nchi mnazojilimbikizia kila siku huku mkituambia watanzania wenzenu tufunge mikanda. Friedman alifafanua usemi wake kwa kusema kuwa; hakuna mtu anayetumia pesa za mwenzake kwa makini zaidi ya anavyotumia pesa zake mwenyewe (nobody spends somebody else's money as carefully as he spends his own)...[Habari Kamili >>]

Linux web hosting - Get rock solid web hosting at Webquarry!

www.bongotz.com ©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.