WAAFRIKA TUMESALITIWA AU TUMEKANWA

Na, Magabe Kibiti

Nimekuwa nasoma vitabu vya dini kwa muda mrefu sasa. Na kwa muda wote huu, nimekuwa nachukulia dini kama suala la kufikirika na linalohitaji imani kubwa sana kulielewa. Hata hivyo nakiri kuwa kwa muda wote huo nimekuwa napata changamoto kubwa kutoka kwa watu wa imani. Mafanikio waliyonayo wakristo, waislam, wahindu na wabudaha katika kueneza na kusimamia imani zao ni makubwa sana kuliko nilivyokadiria mwanzoni. Kwa kutambua hilo, na baada ya kuhangaika sana kutafuta suluhisho la matatizo lukuki ya Afrika kwa muda mrefu bila mafanikio ya maana, niliamua wiki hii kusoma vitabu vya dini kwa lengo moja tu, kutafuta sababu ya maana ya kuelezea chanzo cha matatizo ya Afrika.

Ilinichukua muda mfupi tu kabla sijasoma stori ambayo ilinishangaza. Ajabu ni kwamba, nimeisikia hiyo stori mara nyingi na sikuwahi kabisa kuihusisha na kitu chochote kinachoendelea duniani. Stori yenyewe iko kwenye kitabu kitakatifu cha wakristo (biblia). N istori  inayoeleza matukio yaliyotokea muda mfupi kabla ya kifo cha YESU (mwanzilishi wa dini ya kikristo). Stori inasema kuwa miongoni mwa watu waliopanga njama za kumuua YESU ni Yuda ambaye alikuwa rafiki na mwanafunzi wa YESU ! Stori pia inaeleza jinsi Petro ambaye pia alikuwa rafiki na mwanafunzi wa YESU alivyomkana hadharani kwamba hamjui kabisa ! Ona sasa, kama kawaida ya viumbe hai, utarukia kwenye hitimisho kuwa, Petro na Yuda ni watu waovu na hawakustahili kuzaliwa kabisa. Utashangaa kusikia kuwa hata leo hii, Afrika imejaa ma-Yuda na ma-Petro ambao ni waovu kuliko Yuda na Petro. Swali moja bado najiuliza; waafrika leo hii tumesalitiwa? Au tumekanwa?
Wakati mwingine nashawishika kulaumu historia ya Afrika ambayo pamoja na mambo mengine inaeleza jinsi ambavyo waafrika wamekuwa na ukarimu wa hali ya juu sana kwa watu wa mabara mengine. Nimeshangaa kusoma kuwa waafrika walikuwa na dini na imani zao kabla waarabu na wazungu hawajaleta uislam na ukristo Afrika. Nimeshangaa zaidi kusoma kwamba dini hizo mpya kwa waafrika ziliambatana pia na ukoloni,unyanyasaji, biashara haramu ya binadamu, na sasa vita na mauaji. Yaani kwamba, ukarimu wa waafrika wa miaka hiyo kwa wazungu na waarabu uliwaponza na bado unaendelea kuwaponza hadi leo. Hapa tena usiruke kwenye hitimisho kuwa wazungu na waarabu ni waovu sana. Leo hii katika Afrika kuna viongozi wa dini za ukristo na uislam ambao wanawashawishi wafuasi wao kufanya vita na mauaji dhidi ya waafrika ambao ni wafuasi wa dini zingine. Hapa ndio nachanganyikiwa, waafrika wenzetu hawa wanatusaliti? Au wanatukana?

Maprofesa wangu wa somo la maendeleo (Development studies) katika chuo kikuu cha Dar es salaam  walinifundisha mambo wanayodhani kuwa yamechangia  umasikini Afrika. Wanadai kuwa ukoloni, teknolojia duni, sera mbaya za benki ya dunia, vita, elimu duni n.k vimechangia sana katika matatizo lukuki ya bara hili. Usipokuwa makini, utarukia kuwalaumu wazungu ambao wamehusika kwa njia moja au nyingine katika yote yaliyotajwa hapo juu. Ukweli ambao hutausikia  ukisemwa ni huu; kila mwaka, waafrika wenye madaraka, wanaiba mabilioni ya pesa za serikali na kuziweka kwenye mabenki ya wazungu badala ya kuzitumia kununua teknolojia au kuinua elimu ya waafrika wenzao. Hushangai pia kusikia kuwa Tanzania kuna watu wanaiba mafuta ya transfoma za umeme na kwenda  kuyauza kwa shilingi mia tano huku wakisababisha transfoma hizo kuungua na kuleta hasara ya mabilioni ya shilingi kwa waafrika wenzao. Vipi kuhusu wahutu walioamua  kuanzisha mauaji dhidi ya watusi kwa sababu ambazo hata wazungu na waarabu hawajazielewa bado. Bado sijui niseme nini kuhusu waafrika hawa waovu, wanatusaliti? au wanatukana ?
Nilipokuja marekani miaka minne iliyopita, nilikutana na mmarekani mweusi mmoja aliyenistaajabisha sana. Kwanza alinishangaa sana kwamba nimefurahia kupata nafasi ya kuja
marekani. Hakutaka kusikia sababu yoyote ya mie kuwa na furaha na alinishauri kuwa nisifikirie kabisaaa kuishi hapa maisha yote. Alinambia kuwa amehangaika sana kutafuta sehemu Afrika ahamie kwa miaka mingi bila mafanikio. Huku akiniita ndugu (brother), aliendelea kudai kuwa yeye asili yake ni Afrika na ndiko anakostahili kuishi. Alinilaumu mimi  na wenzangu waliobaki Afrika kwa kunyea nyumba zetu na kukimbilia kwa majirani. Sijui kama lawama hizo nilizistahili au la, ila (nikikumbuka alichofanya IdiAmin), ninakubali kuwa alichosema ni ukweli kabisa kwamba waafrika leo hii tunaharibu (tunanyea) nchi zetu kwa sababu tu tunajua kuwa zikiharibika na kunuka, wale wenye uwezo tutakimbilia kwa wazungu na waarabu na kuacha wenzetu wakisota. Hivi huku ni kusalitiana ? Au ni kuwakana wenzetu !

Wafuasi wengi wa dini ya kikristo wamekuwa wakiwalaumu wayahudi kwa kifo cha YESU, wengi pia wamemlaumu Yuda na Petro kwa walichomfanyia rafiki yao. Kitu kimoja nimejifunza kutoka katika stori hii ya biblia ni kwamba; Afrika leo ina ma-Yuda na ma-Petro ambao ni hatari kwa wafrika wenzao. Ni sawa kuwalaumu wazungu na waarabu kwa ukoloni na yote waliyowafanyia waafrika. Lakini pia ni vizuri kujiuliza kama waafrika pia wamehusika kuwagandamiza waafrika wenzao.  Vipi walichofanya Mobutu na Abacha kwa waafrika wenzao, usaliti au? Hivi hao wanaouza madawa ya hospitali huku watu wakifa bila huduma ya afya ni wasaliti au wakanaji? Nifanye nini mie, ninaogopa siasa kuliko chochote kile hivi sasa, naumia  kusikia kuwa kuna watu leo hii Tanzania wanasema kuwa wakishindwa kwenye uchaguzi watachukua mapanga na kupigana. Hivi nani atafaidika na vita? Je baada ya vita tutaanza kuita waarabu na wazungu kwa ajili ya misaada? Afrika ni kwetu, tukiharibu sasa hatuna pa kwenda. Wazungu na waarabu hawajawahi kutu-penda. Sisi ambao hatuna nafasi kwenye siasa tunawaomba waliojaliwa kutuongoza wawe na imani. Kwa sababu bado hatujui kama watatusaliti zaidi au watatukana.

Mungu ibariki Afrika.

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

 

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.