DEMOKRASIA AFRIKA BADO "MDEBWEDO"

Na, Antar Sangali, Bagamoyo

Demokrasia barani Afrika bado inaonekana kubaki kuwa "demokrasia mdebwedo" kutokana na washiriki katika viwanja vya siasa kukosa uwezo wa kutambua kuwa wako madarakani kama watumishi wa umma na sio vinginevyo.

Naiita "Demokrasia Mdebwedo", kwasababu ni demokrasia isiyopewa nafasi katika kuamua na kuchagua kwa maslahi ya wengi. vita vimetapakaa, majanga, magonjwa na umasikini umekithiri lakini kila ajae madarakani hatimizi kiu ya wengi ilhali yeye amechaguliwa na umma wa watu wengi. Swali linalobaki wazi ni hili: kwanini?

Jacob Zuma (Jz) ameonekana kuwekewa vigingi na Rais Thabo Mbeki mapema mwezi huu kana kwamba Zuma ni gaidi katika nchi yake. Wakati Rais Mbeki anakataa katakata, Zuma ni kiongozi anayekubalika Afrika Kusini, ndani ya ANC wanachama wameamua kwa kauli moja iliyotaka Jz apete.

Zuma tayari amekuwa Rais wa ANC na kwa mujibu wa katiba ya ANC atakayeshika usukani wa chama hicho ndiye atakayewania uongozi wa wa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu ujao.

Wanasiasa kama akina Buthelez, Sixwalle, Mandelea na Winnie Mandela ambao wana nguvu za kisiasa katika Afrika Kusini wameonyesha kumuunga mkono Zuma katika mwelekeo mpya nchini humo. Mzee Mandela hajatamka hadharani anamtaka nani lakini kukaa kwake kimya kumetafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kama yuko nyumba ya kivuli cha Zuma.

Mwanasheria mkuu wa nchi hiyo naye wiki iliyopita ameibuka na kusema taratibu za mashitaka zimekamilika na Jz anaweza kushitakiwa mahakamani. Ni kauli iliyejenga suitafahamu kubwa duniani.

Somali na Sudan Kusini kuna vita, hali ya Ethiopia ni tata kila siku raia wa nchi hiyo wanakimbilia Kenya na wengine Tanzania. Rwanda na Burudi kumepungua mizozo ingawaje juhudi za ziada zinahitajika ikiwa ni pamoja Marais Piere Nkurunzinza na Poul Kagame kuwajenga wananchi wao katika dhana ya umoja wa kitaifa na kusahau yaliopita.

DRC na Uganda napo hususani kwenye maeneo ya misituni kuna piga nikupige na mauaji makubwa yanafanyika yakitesa na kuangamiza zaidi maisha ya wanawake na watoto wadogo. Marais Yoweri Museven na Joseph Kabila wanatakiwa kuweka mkazo zaidi ili kunusuru maisha ya watu hao huko mipakani na kuendeleza mazungumzo na waasi akina Joseph Konny na Jenerali Laurent Nkunda.

Lakini kubwa na la msingi ni viongozi katika kukataa kuwa vibaraka na watumishi wa wazungu katika mabara ya ulaya na Amerika. Viongozi mliopo katika Afrika ya leo hebu fuateni nyayo za akina Ahmed Sekeo Toure, Gamal Abdel Nasser, Kwame Nkuruma, Julius Nyerere,J omo Kenyatta, Patrice Lumumbana Mfalme Haile Sellasie.

Wakati mwingine waelezeni kinagaubaga na waulizeni wazungu nani analeta silaha za kivita Afrika zinazotengenezwa katika nchi zao huku zikipoteza maisha ya watu wasio na hatia kwa faida ya viwanda vyao na watu wao.

Wazee wetu niliowataja hapo juu walikuwa wakithubutu kusema wazi wazi kwamba hawataki hili hawataki lile kwa wakati muafaka bila ya kumuonea mtu aibu awe ametoka mashariki au magharibi.

Matokeo tayari yameoonyesha wakenya wanamtaka Odinga na tayari chama chake cha ODM kimezoa viti kibao vya ubunge na PANU ya Kibaki ikiwa na viti haba katika uchaguzi huo mkuu wa kihistoria nchini kenya lakini Kibaki anajidai ngunguri na hataki kabisa kusikia sauti za wakenya wengi walioelezea hoja zao kwenye saduku la kura.

Kitendo cha ODM kujipatia majimbo mengi ya uchaguzi ni kiashiria tosha kwamba Kibaki ameshindwa katika uchgauzi huo na hana hiari katika kumpisha Odinga Ikulu. Ni vigumu mtu akampigie mbunge wa ODM lakini kura akampe kiongozi wa KANU.

Hili halitakubalika katika maamuzi ya kumpata Rais halali wa Kenya ikiwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi hatakuwa makini. Nguvu ya Odinga sasa Imedhihirika katika nchi ya kenya ,kama kuna mtu aliyeipuuzia nguvu yake ni Mzee Daniel Arap Moi pale alipomtoa Odinga katika chama chake cha NP na kujiunga na KANU lakini alipoona kuna gozigozi akamwachia chama na kujiunga na NARC.

Katika pitapita zote za Odinga katika bahari za kisiasa hakuonekana kutetereka hadi alipoleta vuguvugu la kuanzishwa kwa ODM na kisha kujitoa na kuanzisha ODM yake na akamwachia Kalonzo Musyo ODM K.

Kibaki hakutanabahi na kujua nguvu ya Odinga akaanza kumuwekea vigingi hata pale Odinga alipotaka sharti la mabadiliko ya katiba lifanyike.

Wanasiasa hodari akiwemo Musalia Mudavadi waliona wazi kuwa Odinga ana mtaji mkubwa wa kuushawishi umma na alikubali kumuunga mkono na leo wakenya wameamua Raila Amolo Odinga awe Rais wao.

Hakuja haja kwa Kibaki kumuwekea ntimanyongo Odinga. Kibaki akubali maamuzi ya nguvu ya umma na sauti ya wengi. Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu akipingana nayo ataichafua Kenya na wakenya watakuwa wakimbizi katika dunia.

P.S. Viongozi wa Afrika nao wanapaswa kuvunja ukimya wao na kukemea hali ya kijeuri inayoonyeshwa na Kibaki. Mbeki, Kikwete, Mseveni, Kagame na Marais wengine, tungependa kujua mko upande gani?

Mungu ibariki Afrika.

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

 

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.