WATANZANIA HATUKO TAYARI KUYAISHI MACHUNGU YA MWAKA 1974/75

Na: Antar sangali, Bagamoyo [First posted on: 02/22/06]

Kama kuna jambo lililopita katika msafara mrefu wenye uthakili uliowahi kuwakumba watanganyika baada ya kupata uhuru na kujitawala basi ni kadhia ile ya hama hama ya Operesheni Vijiji vya Ujamaa iliyopita mwaka 1974/75.

Lilikuwa ni pigo kubwa takatifu lililowakumba watanganyika na kuwabebesha hasara isiyokadirika  hasa kwa wale wananchi wa Tanganyika waliokwishajistawisha kimaisha kwa kujiwekea kirasilimali vijijini mwao tayari katika kuyaendesha maisha yao.

Ukiitazama na kuichambua dhana yenye ya mpango mzima husika wa uanzishwaji wa Vijiji vya Ujamaa unaweza kuiona ilikuwa na dhamira njema kwasababu hata Uchina waliifuata sera hii na kupata mafanikio makubwa ya kimaendeleo na kuondokana na umasikini.

Tayari katika vijiji vingi vya kiasili wananchi walikuwa wamejijenga na kujiimarisha katika sekta za kilimo, ujenzi wa nyumba bora, ufugaji na mahusiano mema ya kijamii baina ya kabila moja na jingine, koo hii na koo nyingine na kuishi katika maisha ya ujamaa wa kale yaani ujima.

Wananachi hawa ambao walikuwa tayari wamejipanga katika mstari wa mbele kupambana na umasikini ghafla walipigwa kumbo zito ulipotimu mwaka 1974 kuelekea 1975 pale ilipotangazwa hama hama katika vijiji vya ujamaa huku serikali ya TANU ikiwa na maandalizi duni na mipango butu.


Mashamba ya watu, nyumba zao na mifugo ilisambaratishwa kwa dafaa moja kufumba na kufumbua na kauli ikawa kila mwananchi ahamie haraka katika kijiji cha ujamaa na lugha iliyotumika na wanasiasa ilikuwa ni kuhamia karibu na maeneo ya barabarani.

Wanasiasa katika chama cha TANU wakawahamasisha wananchi kituteni na kwamba watu wanatakiwa kuhamia huko kwasababu serikali imepania kuwapelekea kila kitu zikiwemo nyumba bora za kisasa, huduma za maji, umeme na matibabu (zote zitatolewa bure hivyo ni lazima kila mtu ahamie kijijini ima fa hima).

Ndani ya masaa 24 watu wakayakimbia makazi yao ya asili ,mashamba yao yaliyokuwa na mimea mingi ya kudumu mathalani katika Mikoa ya Ukanda wa Bahari, Lindi, Tanga Pwani, Morogoro na Mtwara mambo hayakuwa shwari na ikawa ni hamkani tupu huku miche iliyomea ya minazi, mikorosho, michungwa na matumnda mengine ikafa kwa kukosa matunzo kwa kukosa palizi za wakati.

Watu walihamishwa kama wamekubwa na vita na kahamishwa mithili ya wakimbizi katika nchi yao wenyewe na katika vijiji walikohamishiwa  hakukuwa na maandalizi yeyote ya watu lau kwa kupata lepe la usingizi wa siku moja na hawakujua ni wapi watapata chakula katika familia zao.

Nyumba zilivunjwa, mashamba yakakimbiwa na kuachiwa kuwa miliki ya nyani, nguruwe, tumbili na wanyama wengine waharibifu mwituni huku watu wakipigwa mzubao.

Katika maeneo waliohamishiwa baadhi ya wananchi kwa kukosa nyumba za kujihifadhi wengine wakaliwa na simba na kuyatupa maisha yao katika makazi mapya ya vijiji vya ujamaa kutokana na sera zimamoto za serikali ya TANU.

Wakati serikali ikiwahamishia watu hao katika vijiji vya ujamaa kwa mfumo wa zimamoto na kuyaacha mashamba yao katikati ya misitu minene ya mashamba, ghafla serikali ile ile na watu wale wale waliopitisha maazimio yale yale wakasema tena baada ya miaka 15 kupita--kwamba mwananchi asiyerudi katika shamba lake kijijini na kulipalilia litahesabiwa kuwa ni pori lisilo na mmiliki na litarudishwa katika mikono ya serikali na kugawiwa kwa wananchi wengine.

Tayari wananchi hawa waliohamishwa katika vijiji vyao vya asili na jadi walikuwa wamezingwa na hali ya umasikini na hawakuweza tena kurudi katika mashamba yao na kuyapalilia kama ambavyo walivyokuwa wakiishi kabla ya hamahama. Hiyo kama haitoshi wananchi hao walishindwa hata kuwasomesha watoto wao  katika shule zilizokuwa na elimu bora.

Hazikupita siku nyingi viongozi na masetla wale wale waliomo serikalini wakaanza kununua ardhi ile ile ya waliohamishwa ,mashamba yale yale mahali walikoondoshwa wananchi masikini dhofu wa hali katika miliki zao na kununuliwa na wao ambao tayari walikuwa wakipata mishahara minono na ambao walifanya israfu na ufisadi mkubwa wa ngawira za serikali na kuyafilisi mashirika yote ya umma.

Waliohamishwa mashambani walizidiwa kwa kila hali na wale walionunua mashamba hayo kwa elimu na kuwa wamiliki wa fedha, vyeo na wengi kati yao wakiwa wameshika hatamu za madaraka ya utawala serikalini.

Mashamba yote leo yamenunuliwa na mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi, wabunge na matajiri walioficha makucha yao katika zama zile za kujenga siasa ya ujamaa na kujitegemea nchini Tanganyika baada ya wazanzibari kusema vijiji vya ujamaa na ujamaa wenyewe utaishia katika kisiwa cha Chumbe kabla ya kuwasili katika visiwa vya Unguja na Pemba. Heri yake marehemu  Mzee Abeid Karume aliyeiona kwa mbali na kuipa mgongo sera hii ya hamahama ya vijiji vya ujamaa na siasa yake ya ujamaa mapema alfajiri kabla hakujacha.Ole wako Tanzania, maana vigogo walioko serikalini wanakuhujumu wakurudishe hukohuko (1974/75). Ni nani atakayekubali safari hii lakini?

Ninapoikumbuka ile kadhia ya hamahama na mashaka walioyapata watu katika kuhamishwa kibabe na leo makazi yao kumilikiwa na mabepari waliochuma wakati wengine wakijenga ujamaa na leo kugeuka na kuwa makupe na wanyonyaji wakubwa naota kama kuna mgogoro mkubwa wa ardhi unainyemelea Tanganyika katika Tanzania ya leo.

Kuna kundi la watanzaganyika wale waliohamishwa nyakati zile kizazi chao kinaanza kufumbua macho na kupata elimu, kumiliki fedha na kupata vyeo serikalini lakini wakitazama nyuma yao hawana miliki ya ardhi yao ya urithi na wanapopata wasia na hadithi simulizi wanaelezwa asili ya ardhi yao na kuporwa kwao kwa hila za kisiasa naliona kundi hilo iko siku litauliza na litakapokosa majawabu lolote laweza kuzuka.

Lakini kama pigo hili la vijiji vya ujamaa ni dogo kwa namna ya mbali, vita nyingine baridi ni ile ya Maafisa wa idara za Ardhi kuoingoza katika utapeli wa viwanja vya wananchi na kuwadhulumu baadhi ya watu masikini viwanja ,nyumba na mashamaba yao ya urithi.


Rais Jakaya Kiwete amekuja na kasi yenye matumaini na bashara njema kwa jamii na pale anapolizungumza kwa uwazi tatizo la ardhi nchini huwa anaigusa kwa namna kubwa jamii iliyoathiriwa na sera ya vijiji vya ujamaa na kupeperushwa katika masafa ya mbali kwa upepo wa matapeli waroho na madalali wa ardhi.


Kasi hii ya rais na mawaziri wake serikalini ifanyike kwa uwazi zaidi na ikibidi kila aliyedhulumiwa aidha kwa utajo wa sera na nguvu ya fedha iliyoharibu kupatikana kwa haki mahakamani huruma ipewe nafasi ili ubinadamu upate hadhi stahiki.

Hofu nilionayo ni kwa kiasi kikubwa operesheni ya hamahama ya vijiji vya ujamaa haikuikumba mikoa ya Bara na hivyo kufanya leo hii wananchi wengi wa Bara kuwa wamiliki na wanunuzi wakubwa wa ardhi na kuhamia Pwani kuliko ambavyo wale wa Pwani walivyohamia Bara na kumiliki ardhi na mashamba makubwa yenye hadhi ya kisetla na kimwinyi.

Iwepo mikakati ya makusudi katika kuhakikisha tishio la migogoro ya ardhi haipati nafasi kwa kuyashughulikia mapema masuala yote ambayo  kwa kiasi kikubwa yalijenga utata, yamejenga utata na yatajenga utata pengine utakaoibua tafrani na idhilali kwa jamii.

Watanzania ni wavumilivu, wastahamilivu na werevu wanaohitaji kuandaliwa kama ambavyo Mwalimu Julius Nyerere alivyowaandaa katika kudai uhuru, kuikubali siasa ya Ujamaa, kushiriki katika Azimio la Arusha, Iringa na Musoma na hatimaye  kukimbiza Mwenge wa uhuru kwa miaka yote 44 ya uhuru.Chondechonde viongozi wa serikali ya ari...,kasi..,na nguvu mpya, wakati wa kuwaandaa watanzania kuhusu masuala ya kumiliki ardhi ni sasa. Fanyani kila mwezalo kwaandaa sasa ili kuupoza mtafaruku wa ardhi unaoweza kuibuka katika siku za usoni.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.