CHANGAMOTO KWAKO RAIS KIKWETE: MAENDELEO HALISI NI HUDUMA BORA ZA KIJAMII

Na: Magabe Kibiti (Posted: 02/04/06)

Bado sina uhakika kama ni jukumu langu kumshauri mheshimiwa Rais Kikwete au la, sina uhakika pia kama ushauri wangu kama mwananchi wa kawaida unaweza Kupelekea mabadiliko yoyote ya sera za chama cha mapinduzi. Nina hakika katika jambo moja tu kwamba Mheshimiwa Kikwete amechaguliwa kuwa Rais wa Tanzania kwa zaidi ya asilimia 80 ya wapiga kura wa Tanzania. Hii ni kusema kwamba Mhe Rais Kikwete amepewa mtaji “CAPITAL” na watanzania wengi ili autumie kuwaletea maendeleo. Ni ukubwa wa mtaji huu aliopewa Rais ndio umenishawishi kuandika makala hii. Sio nia ya makala hii kuanzisha upinzani dhidi ya Mheshimiwa Rais na wala sio nia ya makala hii kuanzisha ushabiki wa kisiasa kwa kila anachofanya Rais Kikwete. Makala hii ni changamoto kwa Rais Kikwete kutumia vyema dhamana aliyopewa na watanzania.

Kwanza kabisa, Nawaomba wenzangu wanauchumi mniwie radhi kwa kusema hadharani kuwa ukweli wa mambo unaonyesha kuwa sera za uchumi za Tanzania zimeshindwa kuiletea Tanzania maendeleo yoyote ya kiuchumi. Zaidi ya asilimia 80 ya watanzania hawapati huduma muhimu za kijamii kama maji salama, nishati, mawasiliano, na ajira. Tusipokubaliana kuwa sera za sasa zimeshindwa na kutafuta suluhisho lingine la matatizo yetu kiuchumi tutakuwa tunajidanganya. Haijalishi kama takwimu zote zitaonyesha kuwa tunakusanya kodi zaidi sasa kuliko miaka kumi na tano iliyopita wakati mawasiliano ya barabara kati ya majiji makubwa mawili Tanzania ya Dar es salaam na Mwanza ni ya wasiwasi. Sera yoyote ya kiuchumi ambayo imeshindwa kutoa suluhisho la maana kwa hata mahitaji muhimu ya binadamu ni mbovu na inabidi kuachwa.

Inasikitisha sana kusikia kuwa zaidi ya watanzania milioni nne wana upungufu Mkubwa sana wa chakula (wanakabiliwa na njaa) hivi sasa. Mheshimiwa Kikwete, ni wakati muafaka sasa kuachana na sera za zima moto na kutafuta suluhisho la kudumu la matatizo yanayoikabili nchi yetu. Ninakuhakikishia kwamba ninaunga mkono kwa sasa mbiu yako ya kasi, ari na nguvu mpya. Mwanzo wako kiutendaji unatia moyo kwa sasa na ninakuhakikishia kuwa nitakuwa mvumilivu vya kutosha na kukupa muda wa kutosha kubadili mwelekeo wa mambo. Hata hivyo, nakukumbusha kwamba, Marais watatu waliokutangulia, waliwaomba wananchi kuwapa muda wa kutosha ili walete maendeleo na wakashindwa kutimiza ahadi zao. Sio nia ya makala hii kuwalaumu marais wastaafu kwa mapungufu yao wakati wa uongozi wao, makala hii inakukumbusha kuwa ahadi na maneno matamu pekee havitatutoa katika lindi la ufukara tunaloita maisha kwa sasa.

Historia ya dunia imerekodi baadhi ya marais waliofanikiwa kubadilisha kabisa mwelekeo wa nchi zao Kiuchumi na kuziletea maendeleo kwa kuendesha nchi hizo kama biashara au familia zao binafsi. Rais wa zamani wa Marekani Dwight Eisenhower (1953-61) aliamua kutumia nafasi yake ya Uraisi kulazimisha ujenzi wa mabarabara makubwa ili kuunganisha majimbo yote ya marekani (interstate highways). Watu wengi na idara nyingine za serikali zilipinga sana uamuzi wa kutumia sehemu kubwa sana ya bajeti kwenye barabara pekee bila mafanikio. Eisenhower hakutishika na aliendelea na mradi wa barabara na leo hii kila mtu anamshukuru kwa hilo. marais wengine maarufu wa marekani kama Lincoln, Roosevelt, Kenedy, Reagan na Clinton walitumia nafasi zao na juhudi zao binafsi bila kujali wapinzani wao ambao walikuwa wengi sana kuiletea marekani maendeleo makubwa sana. Mkumbuke waziri wa zamani wa Uingereza-Thatcher, au vipi kuhusu Kansela wa zamani wa Ujerumani Helmut Kohl (1982-98) aliyefanya kila awezalo kuunganisha Ujerumani mbili zilizotengana na kupelekea Muungano wa Ulaya yote.

Zaidi ya wote ni waziri mkuu wa zamani wa Malaysia ( nchi iliyokuwa masikini kama Tanzania ) Dr Mahathir Mohamed (1981-2003) ambaye alitumia pesa zake binafsi kujenga jiji la Kuala Lumpur na kulifanya liwe na hadhi ya Kimataifa kiasi cha kuwavutia wawekezaji wa nje kuwekeza zaidi ya dola bilioni hamsini katika nchi hiyo. Mfalme wa nchi ndogo ya kiarabu ya UAE alitumia pesa zake binafsi kujenga Dubai na kuwashawishi wanasiasa nchini humo kulifanya jiji la Dubai soko huria na leo hii kila mwafrika anataka kwenda Dubai kufanya shopping. Vipi kuhusu familia ya mfalme wa Saudi Arabia iliyotumia pesa zake binafsi kujenga miundo mbinu ya jiji la Riyadhi na kupelekea kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na mizunguko ya fedha kwa manufaa ya wengi. Madhumuni makubwa ya mifano hii ni kukupa changamoto mhe Rais kutumia kila ulichonacho kutuletea maendeleo watanzania. Ukweli ni kwamba maamuzi mengine yatakumbana na upinzani Mkubwa kutoka kwa wanasiasa na wanauchumi-vihiyo. Mhe Kikwete, kumbuka mtaji waliokupa watanzania ili uwaletee maendeleo.

Wiki mbili zilizopita niliandika makala ya kuitaka Tanzania ihalalishe mfumo wa kiuchumi usio sawa “kinked economic system” kwa ajili ya manufaa ya watanzania wote. Mhe Rais, tunajua sasa kuwa wamiliki wa uchumi wa nchi yetu ni pungufu ya asilimia mbili ya watanzania wote na baadhi yetu sasa tuko tayari kuuhalalisha mfumo huo kwa sababu ndio chaguo pekee tulilonalo. Mie binafsi nitakuunga mkono asimia mia moja kama ukiwataka hao matajiri wachache kuwekeza katika biashara, kilimo na viwanda bila kuwa na wasiwasi wa ujamaa na utaifishaji. Nitakuunga mkono kama ukiwaruhusu viongozi wa serikali kuanzisha miradi Tanzania badala ya kuficha pesa katika mabenki ya nje. Nitapiga vigelegele kama ukiiunganisha mikoa yote ya Tanzania kwa mawasiliano ya uhakika ya barabara.

Mheshimiwa Kikwete, kumbuka kuwa maendeleo ya kweli ya nchi sio wingi wa mashangingi wanayoendesha viongozi wa serikali na wanasiasa. Maendeleo ya kweli ya nchi sio wingi wa mawaziri na watendaji wa serikali. Maendeleo ya nchi sio takwimu zinazoonyesha maongezeko katika ukusanyaji wa kodi na ukuaji wa uchumi bila kujali idadi ya watu wanaonufaika katika ukuaji huo.Mheshima Rais Kikwete, maendeleo ya Kweli na mafanikio ya sera zako za uchumi yatapimwa na idadi ya watanzania watakaopata huduma muhimu za kijamii kama maji salama, afya, elimu, mawasiliano, miundo mbinu, ajira na chakula cha uhakika. Sitashauri hata siku moja kwamba ufanikishe watanzania wote kumiliki sawa rasilimali zote za uchumi na wala sitashauri kuwa na sera za kumtajirisha kila mtanzania kwa sababu ujamaa ni sera iliyoshindwa jaribu la nyakati (test of times). Itakuwa heri kwako kama ukifanikiwa kupunguza namba ya watanzania wanaoishi maisha duni kutoka zaidi ya asilimia 80 ya sasa hadi chini ya asilimia 20 kwa miaka kumi unayotegemea kuwa madarakani.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.