AWAMU YA TATU : MAPUNGUFU NA MAFANIKIO YAKE

Na, <Bongoz>

Awamu ya tatu ilikuwa awamu ya wastani kwa maana kwamba, siasa ya rais Mkapa haikuwa safi sana wala pia haikuwa chafu sana. Ingawa wengi wanaweza kupingana na hili, ila siasa ya mheshimiwa Mkapa kwa sehemu kubwa imekuwa nzuri lakini haikukosa dosari katika kila nyanja: kashfa nyingi za rushwa , mkikumbuka ya milioni 900, wizi wa fedha za EPA, ufisadi wa kiwira, mikataba mibovu ya madini, IPTL, Richmond, minofu ya samaki hadi kufikia swala zima la sukari lililopelekea mheshimiwa Idd Simba kuachia ngazi na haya yote yalidhaniwa kuwa na chanzo chake Ikulu. Si hilo tu, bali uchafu wa siasa ya awamu ya tatu ilivuka mipaka ya kiutendaji hadi kufikia kiwango cha kuwatunuku watu uwaziri eti kwasababu tu walikuwa na mahusiano ya karibu na Raisi (mama Mkapa anabeba lawama nyingi hapa).

Ingawa Rais Mkapa alionyesha upeo mkubwa wa uongozi bora, lakini uongozi wake kwa ujumla umeonyesha kutokuwa bora/makini sana (kama wengi tulivyotarajia). Yeye kama kiongozi amekuwa bora ila wanaomzunguka ukianzia na waziri mkuu ambaye amemtunza katika vipindi vyote viwili, wameonyesha utovu mkubwa wa maadili ya uongozi na hata uwezo wa kimsingi wa kufanya maamuzi kwa minaajili ya kuboresha maisha ya wananchi. Kwa lugha nyingine tangu askari wa miavuli mpaka mawaziri, wengi wao walikuwa wanatumika kwa manufaa yao binafsi badala ya manufaa ya taifa na wananchi kwa ujumla. Na hii ndiyo sababu Raisi Mkapa atahukumiwa na historia (ingawa wengi watapingana na hili) kama kiongozi mzuri maana pamoja na kuwa na viongozi wabaya kama Sumaye, aliweza kusukuma mipango mingi ya maendeleo inayoonekana dhahiri kadhalika kuboresha maisha ya wananchi.

Ukiangalia swala zima la historia ya siasa safi na uongozi bora katika Tanzania, kiufupi viongozi wetu wanaweza kugawanywa katika makundi yafuatayo.

Kundi la Warioba, hawa ni wale viongozi ambao kwa kiwango kikubwa kama siyo chote wameonyesha upeo mkubwa sana wa kuwa viongozi bora na wakati huo huo siasa yao imedhihirika kuwa safi katika kipindi chote ambacho walishikilia dhamana za uongozi walizopewa katika viwango tofauti. Viongozi wanaoanguka katika kundi hili wakiwemo watu kama akina Paul Sozigwa wameonyesha kufanya kazi kwa bidii sana na kupata mafanikio makubwa katika nyadhifa kubwa na ndogo walizopewa. Na walifanya kazi zao bila kutafuta umaarufu ikiwa na maana kwamba kama wanataka kufanya kitu hawasubiri waandishi wa habari wachukue picha kwanza ndiyo wafanye kitu. Wakati huo huo, hawa ni watu ambao katika muda wao wote wa utumishi, wamekuwa bila kashfa yoyote ile kisiasa inayowahusisha wao moja kwa moja. Kundi hili ni wale viongozi wachache ambao tumewahi kuwa nao. Wanasiasa safi na viongozi bora. Mifano imetolewa michache ila idadi yao ni kubwa zaidi kidogo ya waliotolewa mfano.

Kundi la Msuya linahusisha wale viongozi ambao ni viongozi bora kabisa ila wenye siasa chafu zaidi. Ni ukweli usiopingika kwamba katika miaka ya hivi karibuni hakuna kiongozi ambaye amekuwa na ujuzi na uzoefu mkubwa sana katika swala la uongozi na utawala kama Mheshimiwa Cleopa David Msuya. Lakini vile vile siasa ya huyu mheshimiwa imedhihirika kuwa chafu kupindukia kwa kiwango kikubwa na kwa bahati mbaya hatima hii imemfuata hata baada ya kustaafu maana hadi sasa bado ana kesi na taasisi na watu binafsi. Na kwa bahati mbaya katika kundi hili wanaangukia watu mabao ni vipenzi vya wengi kama Mheshimiwa sana Lowassa ambaye kuna dalili kubwa kwamba anaweza akakwaa nafasi ya ngazi ya juu katika serikali ya awamu ya nne. Orodha ya viongozi wa kundi hili nayo siyo chache.

Kundi ambalo linavutia zaidi ni kundi la muasisi wa chama ambalo napenda kuliita kundi la Kawawa, Waziri mkuu wa awali wa Tanganyika huru. Hili ni kundi la wale viongozi ambao walijaliwa siasa safi kabisa ila wakakosa kabisa uwezo wa uongozi. Viongozi hawa ni wale waliokwaa nyadhifa za uongozi kutokana na juhudi zao kubwa za kuhimiza sera za chama na kudumisha fikra za mwenyekiti. Ingawa tunaweza kujaribiwa kuamini kwamba hili lilitokea tu kwa awamu ya kwanza kwa sababu ya Mwalimu kuangalia zaidi utiifu wa watu wake zaidi ya sifa zao, lakini bahati mbaya tumekuwa na viongozi wa aina hii katika awamu zote mfano wa hivi karibuni ukiwa mheshimiwa Mudhihir Mohamed ambaye kimsingi hakuna swala hata moja kuhusiana na maendeleo ya nchi hii ambalo linahusishwa naye lakini bado alipata nafasi ya uongozi kwa sababu ya kusukuma mbele sera za chama.

Bahati mbaya sana mgawanyo wetu wa viongozi hauwezi kumalizika bila kugusia kundi la Sumaye ambalo kama wengi mlivyokwisha hisia, hili ni kundi la viongozi ambao siasa zao ni chafu kupindukia na utendaji wao wa uongozi ni mbaya mno. Lakini kwa namna fulani wameweza kufanya namna ya kupata madaraka wakati mwingine ya juu kabisa. Kwa sababu ya ubaya wa kundi hili hatutalizungumzia sana.

Kundi la mwisho ambalo baadhi ya viongozi wetu wanaangukia humo ni kundi la wale viongozi ambao wanaanza kazi ya uongozi wakiwa na mwelekeo fulani wa kisiasa na labda uwezo wa kiwango fulani cha uongozi. Lakini katika kipindi chao cha uongozi kadri wanavyoendelea na kazi zao za siku kwa siku katika nafasi yoyote ile waliyonayo, wanafanya tathmini ya usafi wa siasa yao na ubora wa uongozi wao. Labda kwa namna Fulani wanagundua kuwa wanapungukiwa kisiasa au ki-uongozi na wanaona iko haja ya kufanya marekebisho katika aidha siasa yao au katika mbinu zao za uongozi, na wanafanya hivyo. Katika mwenendo wao wa mabadiliko aidha ya kisiasa au ya ki-uongozi, baadhi yao wanafanikiwa kubadilika na kuwa wanasiasa safi na viongozi bora, na wengine wanaishia ku-Kolimbwa kabla hawajafikia lengo lao la kiwango cha usafi wa kisiasa na ubora wa uongozi ambao waliazimia kufikia.

Kama umefuatilia kwa karibu makala hii, utagundua kuwa misingi yetu miwili mbayo ndiyo hasa vigezo vya maendeleo yaani siasa safi na uongozi bora, inaangukia katika taasisi tofauti kiutendaji. Suala la siasa linaangukia katika chama tawala ambalo hadi sasa tumetawaliwa na chama kimoja tu cha Mapinduzi. Na suala la Uongozi bora linaanguka kwa serikali. Ili kufanya misingi hii ifanye kazi pamoja, waasisi wa taifa letu kwa CCM walionelea vyema kuleta swala la kofia mbili. Yaani kiongozi wa chama ndiye anakuwa mtawala wa serikali kama chama kikichaguliwa kuongoza serikali. Hii ikiwa na maana kwamba kunakuwa na kiongozi mmoja anayewajibika kuhakikisha kwamba siasa inakuwa safi katika chama na uongozi unakuwa bora kwa serikali. Inawezekana kama tukipata chama tofauti madarakani kikawa na sera tofauti na hizi za CCM, mambo yanaweza yakaeda vizuri. CCM yenyewe iliwahi kujaribu hili kwa miaka kadhaa lakini halikufanya kazi na kupelekea kurejeshwa kwa kofia mbili. Hivyo hadi sasa kofia mbili ndiyo sera ya Chama Cha Mapinduzi. Ingawa binafsi sijaelewa kwa nini kinaitwa chama cha Mapinduzi maana kwa miaka yote 41 sasa ya chama cha Mapinduzi hakujakuwa na Mapinduzi yoyote ambayo tumeyaona. Na ninaposema Mapinduzi simaanishi maendeleo kadhaa ambayo chama kimefanikiwa kuyasukuma katika miaka yote ya utawala wao. Kwa mapinduzi namaanisha mabadiliko mahsusi kiuchumi, kijamii, kisiasa na kimaendeleo ambayo yanaonyesha tofauti dhahiri ya jinsi mambo yalivyokuwa awali na jinsi yalivyo baada ya mapinduzi hayo.

Inawezekana kwamba labda mapinduzi haya yako njiani maana jina la chama linawakilisha malengo na makusudi mazima ya chama. Kwa hiyo kama bado hakujakuwa na Mapinduzi ina maana tuyategemee mapinduzi. Swali ni kwamba ni wakati gani bora zaidi wa kutegemea mapinduzi haya zaidi ya wakati wa kupata uongozi mpya madarakani?

Tukirudi nyuma kidogo kwa ile misingi yetu ya maendeleo, ambayo kama tulivyoona tayari tunao watu na tunayo ardhi, na serikali ya awamu ya tatu ya Rais Mkapa imetuonyesha kwamba kama siasa ikiwa safi kidogo na swala la uongozi likiwa bora kiasi, maendeleo makubwa yanaweza kufikiwa. Hii inatufanya tujiulize kwamba itakuwaje kama tukipata serikali yenye siasa safi kabisa na uongozi bora kabisa, ukweli ni kwamba tutafikia maendeleo makubwa sana na labda kukua kiuchumi kutoka uchumi wa dunia ya tatu.

Hivyo changamoto inabaki kwa Mheshimiwa rais Jakaya Mrisho Kikwete ambaye amemaliza kipindi chake cha kwanza na pengine atachaguliwa kuendelea na kipindi cha pili: je, ni kweli atakuwa na nguvu na uwezo na upeo wa kuleta haya Mapinduzi ambayo tumekuwa tukiahidiwa na Chama Cha Mapinduzi kwa zaidi ya miongo minne? Je, ataweza kuunda mfumo wa chama na serikali ambao utakuwa na viongozi wenye siasa safi kabisa na wenye sifa za uongozi bora ambao watawianisha misingi yetu yote minne ya maendeleo na kuleta maendeleo halisi ya Kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii katika taifa letu na kuboresha maisha ya wananchi wote ikiwa na maana ya wale wa mijini na wale wa vijijini, wale matajiri na maskini, wale waliosoma na wasiosoma. Tunachoweza kufanya sasa kama ambavyo tumefanya kwa vipindi vyote ni kusubiri na kuona kama Kikwete atakuwa ndiye yule kiongozi tuliyemtazamia kutuletea haya mapinduzi (Japo kipindi chake cha kwanza kinaashiria kuwa siye); na wakati huo huo kama atakuwa ndiye basi tumuombee dua kwamba ajaliwe hekima na maarifa, nguvu na afya njema kutekeleza yale yote yanayotakiwa kutekelezwa.

Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.