MMEA WA KIJANI NA MKANGANYO WA KISIASA

Na, Antar Sangali,Bagamoyo

Tofauti na jirani zake (Kenya na Uganda), Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizopiga marufuku utafunaji ama uraji wa miraa (Gomba,mirungi au Ghati kama ijulikanavyo) hadharani. Utakuwa umefanya kosa sawa tu na aliyekutwa akitumia madawa mengine ya kulevya kama vile coccaine na heroine endapo kama utakaidi sheria iliyopo na kuamua kufanya hivyo.

Swali linabaki wazi: je, inawezekanaje nchi kama Tanzania yenye mtazamo tofauti kabisa na jirani zake wa Uganda na Kenya kuunda shirikisho na mataifa ya Afrika Mashariki wakati nchi hizo kama wadau halisi wa ushirikiano huo wananchi wake wanakula au kutafuna mirungi hadharani?.

Ni swali gumu linalohitaji majibu ya msingi. Na si majibu ya msingi tu, bali ufafanuzi yakinifu kuhusu kama Tanzania itaendelea na itikadi za kupinga utafunaji wa mmea huo wa kijani hadharani ama italegeza kamba na kuamua kuruhusu utafunaji wa mmea huo ya kijani hadharani.

Itakumbukwa kuwa, kwa miaka mingi kabla na mara tu baada ya uhuru, watu waliendelea kutafuna mirungi na hakukuwahi kuwa na kauli ya madaktari waliotaja kuwa kufanya hivyo kungeweza kusababisha madhara ya kiafya kama yale ya watumiaji wa Cocaine,heroine na mihadarati mingine mikali ikiwemo sigara ambayo hapa Tanzania tuna kiwanda kikubwa kiitwachoTCC.

Shirikisho la awali la Afrika mashariki lilikufa mwaka 1977 baada ya kuundwa kwake 1967 wakati ambao vita ya Israel na Palestina ilikuwa ikipamba moto Mashariki ya Kati na Waisrael kuchukua maeneo ya wapelestina baada ya kupambana na kuyateka maeneo hayo. Ni wazi mitazamo ya kisiasa kwa wakati ule baada ya Idd Amini kumpindua Dk Milton Obote, Mzee Jomo Kenyatta na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere waliingiwa na picha zilikuwa haziendi sanjari.

Lakini baada ya miaka mingi kupita, Yoweri Kaguta Mseveni, Daniel Arap Moi na Benjamin William Mkapa wakakaa na kutafakari, kupima na kuona kuwa upo umuhimu mkubwa wa nchi za Afrika Mshariki kuunganisha nguvu za kiuchumi, kiviwanda na kibiashara kwa minajili ya kuwa na hali ya uchumi ulio sawia wa watu wake na kwamba hiyo ni njia bora pengine mpya ya kuweza kuchupa katika mwendo unaofaa katika maisha ya watu dhidi ya umasikini wa nchi hizi na watu wake.

Haya ni mawozo swadakta na yanastahili sana kupewa mkono wa hogera baada ya kupita mchakato mkubwa wa uchambuzi na tathmini yakinifu hadi kufikia sura inayoleta bashara njema kwa mustakabali wa nchi hizi tatu na pengine ishaallah shirikisho linaweza likawavutia wanachama zaidi katika nchi za Afriaka Mashariki na Kati.

Lakini wakati wakubwa wetu wanapokuwa wakijadili mambo mengi ya kimsingi na pengine yenye manufaa makubwa kwa mataifa yetu, upande wa pili mababakabwela ambao starehe na nahau zao ni katika kula na kutafuna miraa wamekuwa wakishangaa kuwekwa kando kwa suala la miraa kuliwa hadhari nchini Uganda na Kenya wakati kwa upande wake-nchini Tanzania ni uvunjaji wa sheria na tena ni marufuku kabisa kulingana na sheria zilizopo.

Kwa maana nyingine ya wazi ni kwamba Mtanzania ukiwa Kenya au Uganda ni ruksa kula miraa lakini siyo Tanzania na si Mkenya wala Mganda mwenye haki kutafuna gomba akiwa Tanzania licha ya nchi zao kuruhusu starehe hiyo kisheria. Kwa upande wangu naona kuna mkanganyiko wa mambo na ni vema sasa Waziri mwenye dhamana Mh. Andrew Chenge katika shirikisho letu akalitazama kwa macho mawili suala hili na kulitolea ufafanuzi.

Nakereka mno na suala hili kutokana na kuijua nasaba iliyopelekea hadi miraa kujumuiishwa katika kundi la madawa ya kulevya. Kimsingi ni historia inayokwenda wakati Bw Augustine Mrema akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati mtoto mmoja wa kike ambaye ni binti wa DC wa zamani katika serikali ya TANU alipokorofishana na jamaa mmoja Mmeru raia wa Kenya mtaa wa Pemba na Lumumba jijini Dar es Salaam.

Binti huyo ambaye sasa ni mwanamama mtu mzima anayeishi mtaa wa Mafia alikimbia ofisini kwa  Bw Mrema akidai ameonewa na Mmeru huyo na hapo hapo fatiki kali ikazuka ya kuwakamata wauza miraa. Na ili kujipa uhalali wa kuwakomoa wala-mirungi ikajumuishwa katika orodha ya madawa ya kulevya. Bw Mrema siku zile alikuwa akiamua mpaka kesi za mke na mume ofisini kwake na kuonekana ni mtetezi wa akina mama, siri hii ilidhihirika mwaka 1995 baada ya Mrema kuona kuna kiwingu cha kumkinga asipate urais kupitia CCM akajitoa na kwenda NCCR-Mageuzi,ni wazi aliamua kwa jazba ya kisiasa.

Lakini kwanini pengine msomaji utajiuliza ni kwanini mpaka nimeaamua kuandika makala hii ni kutokana na kuona idadi kubwa ya viongozi serikalini,wafanyabiashara na askari hasa polisi wakiwa ni walaji wakubwa wa miraa huku wakiwakamata wanyonge na wachuuzi wa miraa .

Ndugu mwanchi, ukitaka kujua miraa inapendwa nenda katika taarab au densini na katika kumbi za madisco utashuhudia watu wanavyokula miraa huku wakitulia na sana sana wala ghati si wakorofi na watu wasiopenda bughudha walapo nahua zao wala miraa aghalab hawana karaha kama wanywa tembo.

Inanishangaza kuona kuna pombe mathalan komoni, pingu ,dengerua, uraka, mnazi na banana ambazo ni kali na zinadhuru sana watu afya zao lakini hazionekani ni haramu na kujumuishwa katika kundi la mihadarati lakini inaonekana miraa ndiyo kitu kisichofaa...!!

Kupitia makala hii na uwanja huu wa Bongo Mchicha ninamuuliza Waziri wa Afya Dk David Makyusa na Waziri wa Shirikisho la Afrika Mashariki Mh. Chenge waielezee hadhira kinagaubaga ni nini taabu na kadhia ya miraa kwa afya ikitofautishwa na pombe za kizembe ambazo zinaumiza afya za watu vijijini kuliko hata ulaji wa mirungi.

Sina ubishi iwapo zitatolewa sababu yakinifu za kitaalam juu ya athari za miraa, lakini pia nitashangaa kuona vibanda vya pombe almaarufu kama Grocery  na Pubs vinavyokithiri katika miji ya Tanzania na unywaji wake  visionekane ni kitu cha hatari kwa afya za watu na kuwakuta hata watoto chini ya umri wa miaka 18 wakichapa mtindi.

Lakini ikiwa hakuna hoja basi hata ile miti asilia iliyoota kule Soni, Mombo na Hedaryu ifyekwe kwakuwa wananchi wa maeneo hayo huwaambi kiti kwa kutafuna miraa itokanayo na miti iliyostawi tangu zama na zama. Tanzania marufuku miraa, Kenya wenzetu wanangiza pesa za kigeni kwa kuuza miraa na miraa inaliwa hadharani Holland na Uingereza-je,huko hakuna wataalam wajuao athari zake?

Wakubwa wekeni bayana kabla hatuja wataja kwa majina mmoja baada ya mwingine walao mirungi ilhali mkiwa serikalini na mkiwa na madaraka makubwa.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.