NI WAKATI MUAFAKA SASA KWA “KINKED ECONOMIC SYSTEM” KUHALALISHWA TANZANIA

Na, Magabe Kibiti<First posted on: 2/12/06>

Fikara zangu zinapingana huku moyo wangu ukiwa mzito kuruhusu damu kuendelea kusambazwa mwilini kwa hali ya kawaida. Ni jambo ambalo nimelifanyia utafiti kwa miaka mingi sasa na imefikia wakati ambao sina cha kufanya zaidi ya kuanika hadharani matokeo ya utafiti wangu. Vidole vyangu vinakuwa vizito kuandika makala hii na nina hakika kuwa hata mhariri wa Bongotz atakuwa na kazi kubwa sana ya kuamua kama arushe makala hii hewani au la. Ukweli unabaki palepale kwamba, nipende nisipende lazima kuanzia sasa na kuendelea, niuishi ukweli wa mambo ambao ni mchungu sana kuliko mwarobaini. Ukweli wa mambo unanishawishi kuwa: sasa hivi ni wakati muafaka kwa Tanzania kuhalalisha mfumo wa kiuchumi ambao watalaamu wanauita kwa lugha ya kigeni: “kinked economic system.”

Jambo moja nakuombeni wasomaji wa makala hii pamoja na wale ambao mmesoma makala zangu zilizopita, ni kuwa na uchambuzi wa kina na utayari wa fikara “open mind” kabla ya kuamua kama mtakubaliana na mimi au la. Ninakubaliana pia na ukweli kuwa kwa sasa sina nafasi yoyote ya uongozi wa kisiasa au/na kiserikali kwenye serikali ya Kikwete, jambo ambalo linanikumbusha kuwa makala hii inaweza isipelekee mabadiliko yoyote katika sera za Mheshimiwa Kikwete. Hata hivyo nina msukumo kuwa huu ni mwanzo tu wa mjadala “debate” wenye nia ya kutafuta suluhisho la tatizo sugu la uchumi duni wa Tanzania. Tofauti na makala zilizopita, makala hii haitaongelea Afrika nzima inayotakiwa kuungana haraka sana iwezekanavyo; makala hii ni mahsusi kwa sasa kwa sehemu ndogo ya Afrika nilikozaliwa iitwayo Tanzania.

Mwanauchumi mmoja maarufu ametafsiri “kinked economic system” kama mfumo wa kiuchumi ambao unailazimisha jamii kuwaruhusu watu wachache sana katika jamii (mara nyingi chini ya asilimia 5 ya watu wote katika jamii hiyo ) kumiliki rasilimali na vyanzo vyote vya Kiuchumi kwa manufaa ya jamii. Mfumo huu unaitaka jamii kuruhusu watu wachache wenye uwezo--kumiliki viwanda, maliasili, mashamba, na biashara zote kwa mategemeo kuwa hatimaye watu hao watatoa ajira kwa wenzao, vyanzo vya pato, na malipo makubwa sana ya kodi kwa manufaa ya wenzao woooote waliosalia. Tofauti na ubepari ambao unampa kila mtu katika jamii nafasi sawa ya kuchakarika ili kufanikiwa katika jamii hiyo au ujamaa ambao umejaribu sana kuwawezesha watu wote katika jamii Kumiliki kwa pamoja kila kitu katika jamii hiyo bila mafanikio yoyote, “kinked economic system” inataka watu wachache tu wenye bahati kuwa mawakili wema wa mali zote katika jamii husika kwa manufaa ya pamoja ya wanajamii wote.

Msomaji wangu, kabla hujaanza kunihukumu kifungo cha maisha jehanam, nakukumbusha kuwa matokeo ya utafiti wangu yanashauri kuwa ni wakati muafaka sasa kwa Tanzania kuhalalisha huu mfumo usio sawa “kinked”. Nimetumia neno kuhalalisha kwa sababu ya ukweli usiopingika kuwa, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine Afrika imekuwa ikifuata mfumo huu kwa miaka mingi sasa kwa siri huku ikidhani au/na kushuhudia vinginevyo. Swali kwako msomaji, unafikiri ni watu wengi au wachache kiasi gani wanamiliki mabasi ya abiria Tanzania? Ni watu wangapi wanamiliki mahoteli na majumba makubwa Tanzania? Ni watu wangapi wanamiliki viwanda na maduka makubwa Tanzania? Au je, ni watu wengi au wachache kiasi gani unafikiri wanamiliki zaidi ya asilimia 90 ya uchumi wa Tanzania? Unataka kujua ? Jibu ni kwamba, ni kama asilimia mbili tu ya watanzania wote. Ndio, asilimia mbili tu ya watanzania ndio wanamiliki zaidi ya asilimia 90 ya utajiri wa Tanzania. Cha kushangaza ni kwamba, ukifanya utafiti unaweza hata kuwataja wote kwa majina.

Sina ugomvi wowote dhidi ya asilimia mbili ya watanzania wanaomiliki utajiri wetu na pia sio nia ya makala hii kuanzisha mgogoro wa kijamii kati ya wenye nacho na wasio nacho. Ninaandika makala hii kuuanika wazi ukweli wa mambo ambao watanzania wote tumekuwa tukiuishi kwa miaka yote ya uhuru wa nchi yetu. Ni ukweli ambao hatuna cha kufanya zaidi ya kuuishi kwasababu Asili imetupatia chaguo moja tu na sio zaidi. Ninakumbuka hotuba ya mwalimu Nyerere aliyoitoa mara tu baada ya viongozi wa serikali ya awamu ya pili kupitisha azimio la Zanzibar na kuua azimio la Arusha kwa siri …ni vyema kama watu hawa wangetuambia wazi kuwa azimio la Arusha limekufa……” Huu tu ndio ukweli pekee uliosalia, “kinked economic system” imekuwepo kwa siri vya kutosha na ni vyema sasa ikahalalishwa.

Swali la msingi kujiuliza ni moja: Je, “kinked economic system” ni nzuri kwa nchi yetu? Jibu la haraka ni NDIO. Mfumo huu ukihalalishwa ni mzuri sana na ukifuatwa vyema unaweza kubadilisha kabisa hali ya nchi yetu kiuchumi. Kama huamini hebu tafakari yafuatayo; Je, wajua kuwa zaidi ya asilimi 30 ya utajiri wote duniani inamilikiwa na watu watano tu? Ndio, watano tu! Je, wajua kuwa wamarekani watano wa familia moja ndio wanamiliki hisa nyingi za supa-maketi mashuhuri duniani la wal-Mart ! Je, wajua kuwa mwanzilishi na mmiliki wa kampuni kubwa la kutengeneza kompyuta duniani la Dell ni Michael Dell wa Marekani! Je, wajua kuwa miongoni mwa mabilionea duniani ni waanzilishi wawili wa kampuni la Microsoft ! Yap, huu ndio ukweli ambao wamarekani na nchi nyingi zilizoendelea duniani wamekuwa wakiuishi kwa muda mrefu sasa; kuwaruhusu watu wachache sana kumiliki sehemu kubwa sana ya utajiri wa jamii kihalali kwa manufaa ya wengine wote.

Kwa baadhi yenu wale mnaopenda waarabu kuliko wazungu bado ukweli wa mambo uko pale pale hata Uarabuni. Familia ya mfalme wa Saudi Arabia inamiliki zaidi ya asilimia 50 ya utajiri wote wa nchi hiyo! Hali ni hiyo hiyo kwa nchi nyingine zote za kiarabu kuanzia Iran mpaka Misri. Huu ni ukweli uliothibitishwa, hakuna jamii hata moja duniani iliyofanikiwa kuwawezesha wanajamii WOTE Kumiliki sawa utajiri wa hiyo jamii husika. Jamii zote kwa njia moja au nyingine zimekuwa zikiwaruhusu watu wachache kutajirika huku asilimia kubwa inayosalia kuishi maisha ya kawaida tu. Jamii ikikataa kuruhusu mfumo huu kwa hiari, wale wachache wanaojitajirisha kwa siri wataishi bila majukumu yoyote ya lazima ya kusaidia na kuwajali wasio nacho.Mfano mzuri ni baadhi ya matajiri wa kihindi Tanzania ambao huwanyanyasa waajiriwa wao kwa kutowalipa malipo halali, kuwapiga, na hata kuwafukuza kazi bila notisi kutokana na ukweli kuwa hakuna sheria zozote rasmi za kumbana mwajiri binafsi. Nchi zilizohalalisha “kinked economic system” zimeweka pia sheria kali za kuhakikisha kuwa, hao wachache wanalipa kodi inayotakiwa na kufuata sheria zote za kazi na za nchi.

Mfano mzuri ni Marekani, supa-maketi kubwa la Wal-Mart linaajiri zaidi ya watu milioni mbili kwa mwaka nchini humo pekee na linaagiza bidhaa za thamani ya dola billioni hamsini kwa mwaka kutoka China. Billionea Bill Gates ametenga zaidi dola billioni ishirini (pesa zake binafsi) kwa ajili ya kusaidia watu mbali mbali wenye shida duniani. Kuna mifano maelfu na maelfu ya mafanikio ya “kinked economic system” iliyohalalishwa na kufuatwa vyema. Kama nilivyoanza makala hii, Mie mwenyewe sijui kama mfumo huu utafanikiwa Tanzania. Inaniumiza moyo kukubaliana na ukweli kuwa huu ndio mfumo pekee uliothibithishwa na wasomi na wanauchumi wengi duniani. Kinachoumiza zaidi ni kujua kuwa tupende au tusipende, tuhalalishe au tuharimishe, ni watu wachache sana ndio wataendelea kumiliki sehemu kubwa sana ya utajiri wetu kwa miaka mingi sana ijayo.

Ninawaomba wasomaji wangu na wale wenye madaraka katika nchi kuupa mtazamo wa pekee mfumo huu. Kwa kuwa imethibitishwa kuwa Tanzania imekuwa ikifuata mfumo huu kwa siri bila kujua, kwa nini tusiukubali ukweli sasa na kupanga mipango na sheria madhubuti za namna ya kuufanya mfumo huu uwe kwa manufaa yetu wote. Ukweli ni kwamba tuna uwezo wa kutunga sheria za kuwabana waajiri binafsi wawajali wafanyakazi wao, tuna uwezo wa kuwasajili na kuwajua hao wamiliki wa mali zetu na kukusanya kodi nyingi za kutosha toka kwao ili kusaidia kujenga mashule, hosipitali, barabara na kuwalipa malipo mazuri wanajeshi, polisi, madakitari, walimu na wafanyakazi wote wa serikali. Tunaweza kabisa kuaandaa mazingira mazuri kwa wananchi wenzetu wenye uwezo kielimu na wenye vipaji kumiliki makampuni makubwa kama Tanesco na wakatupatia umeme wa uhakika kwa misingi ya kibiashara. Ukweli bado utabaki pale pale, tusipohalalisha Umiliki binafsi, tutahalalisha umiliki haramu uliowawezesha wakubwa serikalini na mashirika ya umma kujenga Mahekalu mbezi. NI WAKATI MUAFAKA SASA KUHALALISHA “KINKED ECONOMIC SYSTEM” kwa manufaa ya wanajamii wooooote.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.