TUMEANZA 2007 VIZURI...

Na,G

Kwa makadirio yote tunayoweza kusema, lazima tukubali kwamba mwaka 2007 umeanza vyema kwa watanzania na kwa Tanzania kwa ujumla. Mvua zimeanza kunyesha na kwa taarifa za hivi karibuni bwawa la mtera limefurika na kupita kina chake cha kawaida ambacho ni mita za ujazo milioni 37,000 sawa na kina cha mita 698.50 kutoka juu ya usawa wa bahari. Mabwawa mengine nayo yanajaa vyema kiasi kwamba mengine yanatoa umeme zaidi ya uwezo wake wa kawaida. Kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu watumiaji wa umeme Tanzania wameweza kupata umeme bila matatizo, bila mgawo.

Ingawa hilo ni jambo zuri la kufurahia, bado si suluhisho la kudumu, na hatutakiwi kufurahi kupita kiasi na kulegeza utafutaji wa suluhisho la kudumu la tatizo la nishati nchini.

Lakini kwa upande mwingine, kuondoka kwa tatizo la mgawo wa umeme ni habari njema kuwa tumeanza mwaka mpya vyema. Na pia ingawa bei ya umeme inapanda, lakini bado tunafurahia ukweli kwamba angalau upo kwa sasa.

Zaidi ya hilo Tanzania imepata uteuzi mkubwa sana kwa waziri wetu wa mambo ya nje, Dr. Asha-Rose Mtengeti Migiro kuteuliwa kuwa naibu katibu mkuu wa umoja wa Mataifa huko New York. Hili linatupatia imani kwamba ingawa ni mara ya kwanza kabisa kwa mwanamke tena kutoka nchi za dunia ya tatu kupata nafasi hiyo kubwa katika historia ya nchi yetu; kwa hili tunaweza kusema: huenda Mheshimiwa Rais Kikwete alifanya uteuzi mzuri kwa Dr. Migiro na sasa jumuiya ya kimataifa nayo imegundua kitu kizuri ambacho watanzania wamekuwa nacho kwa zaidi ya mwaka sasa.  

Dr. Migiro anaingia katika orodha ndefu ya watanzania ambao wamefanya vizuri kuliinua jina la Tanzania na watanzania katika duru za kimataifa. Tunakumbuka hivi karibuni Mama Mongela, balozi Nyaki, mheshimiwa Dr. Salim Ahmed Salim na wengine wengi. Kana kwamba hiyo haitoshi pia tumepata uteuzi mwingine wa mheshimiwa Amina salum Ali waziri wa nchi katika ofisi ya waziri kiongozi ambaye naye ameteuliwa kuwa mwakilishi wa jumuiya ya Afrika (African Union) kwenye umoja wa mataifa huko New York.

Basi tukiondoka kwenye habari ya watu maarufu wanaoipatia umaarufu nchi yetu, katika hatua mabayo inaweza kuungana na waziri wa michezo mheshimiwa Khatib, kwa kweli soka bado ndiyo mchezo maarufu kuliko yote duniani na katika upande huo pia tunafurahia kwamba timu yetu ya taifa imepiga hatua ndogo ya mAendeleo kwenye orodha ya timu za michezo duniani. Mwezi desemba mwaka jana tulikuwa nafasi ya 110 duniani na kwa mwezi januari mwaka 2007 tumepiga hatua moja mbele na sasa tuko nafasi ya 109. Heko Taifa Stars, ila tusiridhike na nafasi ya 109, jitahidini tutue Ghana 2008 na Afrika kusini 2010.  

Ingawa michezo mingine kama vile mpira wa kikapu, tennis, na soka kwa upande wa wanawake haijapewa kupaumbele kama ilivyo soka kwa upande wa wanaume; ni changamoto kubwa kwa waziri Khatib kuweka msisitizo pia katika nyanja zingine za michezo hususani kwa timu ya soka ya wananwake ili nayo ianze kufanya vyema katika duru za kimataifa.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

 

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.