BALOZI KARUME SULUHISHO LA TATU ZANZIBAR

Na, Antar Sangali - Bagamoyo [Posted first on: 02/23/08]

Mwishoni mwa mwezi wa Januari mwaka 2008 Mtoto wa pili wa Rais wa Kwanza wa Visiwa vya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amaan Karume Balozi Ali Karume aliianika hadharani azma yake ya kuwania urais wa Zanzibar mwaka 2010.

MwanaCCM huyo ametamka kinagaubaga kwamba hafanyi kampeni hivi sasa bali anakusudia kuwania urasi mwaka 2010 kupitia chama chake na kwamba hana maskhara katika kukusudia kwake huko.

Balozi Karume mwanadiplomasia na mchumi aliyefuzu kitaaluma kutaja kwake nia ya kuutaka urais wa visiwa hivyo ndicho kiu kilichonishawishi niamue kuandika makala hii.

Lipo kundi la watu wenye mtazamo hasi wanaomuona na kumuhukumu bila ya hatia Balozi huyo katika mbio hizo za urais na kusema ni sawa nchi ya Zanzibar kuwa chini ya ufalme katika kubadilishana madaraka ya urais kwa kigezo cha ati kwanini “anatoka Amani na kuingia Ali”.

Kilichonisukuma kuandika makala hii ni mambo matatu,kwanza ni ukomavu wa Balozi Karume kidiplomasia na kisiasa, pili uthubutu wake katika kukabili uhalisi wa hali ya hewa ya kisiasa ya sasa visiwani humo na tatu uwezo binafsi alionao katika utambuzi wa turufu za siasa za Tanzania, Zanzibar, Afrika Mashariki, Afrika na Dunia kwa ujumla.

Tamko la Balozi Karume la kutaka kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ikiwa atashinda urais visiwani humo si kwamba linalenga kuzika hasama na utengano uliopo bali pia ni mpya na adimu sana katika vinywa vya wanasiasa wa Tanzania hususani toka kambi ya Chama Cha Mapinduzi.

Kauli hiyo ni “piku” katika jozi ya karata za siasa na kwamba si rahisi kutamkwa na kiongozi asiye na uthubutu,uwezo na upembuzi wa mambo lakini pia haitamkwi kiwepesiwepesi na mwanasiasa butu asiyetambua miiko na mizungu ya diplomasia au ishara za mabadiliko katika siasa.

Kauli ya Balozi Karume ni mithili ya jawabu katika matatizo ya kudumu ya Zanzibar bila ya kutazama anayetamka ni mtoto kutoka nyumba ya Abeid Karume, Thabit Kombo, Mtoro Rehan Kingo, Salmin Amor, Aboud Jumbe au Abdallah Kassim Hanga. Ni kauli iliyobeba ujumbe hai katika siasa za Zanzibar.

kimsingi visiwa hivyo vinahitaji kiongozi mwenye fikra mpya, mikakati endelevu na utashi wa wazi katika kufuta matabaka kwa lengo la kuleta umoja kamili na maelewano ya kudumu miongoni mwa wazanzibar.

Swali la kwanini Balozi Ali awe mgombea wa urais wa Zanzibar mwaka 2010 akitaka kuingia badala ya Kakaye jawabu lake ni fupi, si Ali kama Ali, bali uwezo wa Ali na utashi mpya anaoukusudia ndiyo kigezo na pengine ni mtaji au ni tiketi yake kabla ya mchakato mzima wa kumpata mgombea kuanza ndani ya CCM.

Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliposema kuwa Rais wa Nchi yetu hataangaliwa kwamba anatoka kabila gani au dini ipi,inathibitisha pia kwamba ni mtazamo dhaifu kuitazama nyumba anayotoka Rais anayehitajiwa ima iwe ni yenye mnasaba wa uongozi au nyumba ya mtu asiye na umaarufu.

Uwezo wa Mzee Abeid Karume kiuongozi haukufanana kamwe na Dk. Kwame Nkurumah wa Ghana, na uwezo wa Jomo Kenyata wa Kenya pengine ulipishana sana na ule aliokuwa nao Julius Nyerere wa Tanganyika. Hapa nazungumzia zaidi uwezo katika uongozi bila ya kutazama kabila, amilia au dini ya kiongozi tunayetaka atuongoze.

Itapendeza sana ikiwa watajitokeza wagombea wengine zaidi katika kuwania urais wa Zanzibar mwaka 2010 kupitia CCM lakini wenye uthubutu na utashi wa wazi kama wa Balozi Ali katika kuitazama nchi hiyo na mikakati mipya aliyonayo.

Tuliwahi kumsikia Dk Salmin Amour Juma mwaka 1995 akisisitiza na kukataa kata kata kuunda serikali ya pamoja kwa kile alichodai hawezi kuchaganya mchele na kokoto kati ya CCM na CUF licha ya ushindi mwembamba alioupata.

Mwaka 1957 na 1963 tuliona jinsi Abeid Karume alivyoomba kuunganisha viti kati ya ASP na ZPPP lakini kiongozi wa ZPPP Mohamed Shamte alivyompiga chenga ya mwili 1963 na kukubali kuungana na ZNP cha Ali Muhsin Al Barwan na hatimaye yakazuka Mapinduzi ya damu Januari 12.1964.

Rais Jakaya Kikwete ni Rais pekee wa mfano Barani Afrika katika kukubali kama kuna matatizo na mitafaruku katika nchi yake na hatimaye kutafuta njia za utatuzi huku viongozi wengi Afrika wakiabudu vita na miifarakano.

Kuchaguzliwa kwake kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika (AU) ni alama tosha ya kuanza kwake kuchukua uzoefu aliouanzisha Tanzania wa kuvikutanisha vyama vya CCM na CUF katika meza ya mazungumzo yanayoendelea.

Muafaka wa kwanza kati ya CCM na CUF ulisukumwa kwa juhudi za Jumuiya ya Madola chini ya Katibu Mkuu wake Chief Emeka Anyaok huku viongozi waliokuwepo katika madaraka wakikana kuwa hakukuwa "mgogoro wa kisiasa Zanziabar" baada ya uchaguzi wa 1995.

Rais Kikwete akiwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Tanzania aliweza kutofautiana kimawazo na Balozi Mohamed Ramiya aliyekuwa waziri katika serikali ya Dk Salmain katika mkutano ulioitwa wa kimataifa juu ya Demokrasia (International Conference on Democracy) ambao ulifanyika katika ukumbi wa Bwawani Zanzibar pale aliposimama na kutamka wazi wazi kuwa kuna mgogoro unaohitaji kupatiwa utatuzi na suluhu.

Dk. Salmin hakuota kuunda serikali ya pamoja, Rais Aman Karume ndiyo huyo anamaliza muda wake akiwa hana hata waziri toka chama chochote cha upinzani huko Zanzibar ilhali nchi hiyo ikiwa na joto kubwa lililotanda la upinzani.

Mitafaruku imetokea katika zama ya utawala wa Rais Dk Salmin na pia Karume akiwa madarakani na kupelekea kile kilichoitwa muafaka na leo yakiendelea mazungumzo yanayotafuta muafaka mwingine wa tatu wa visiwa hivyo.

Balozi Karume bila shaka ameanza kuona mbali kisiasa, kauli yake inajiwekea akiba pia katika siku za usoni hata kama atashindwa katika uchaguzi wa Urais, lakini Rais mstaarab toka chama kitakachoshinda ni wazi ataona soni na kuamua kumchagua Balozi Ali katika kuunda serikali ya pamoja huko Zanzibar.

Matokeo ya uchaguzi nchini Kenya na vurugu zinazoendelea huku watu wasio na hatia wakipoteza maisha ni fundisho katika nchi yetu na mustakabali mzima wa siasa katika kujenga umoja na dhima ya kuamsha maelewano ya kisiasa.

Nchini Ethiopia watu hubaguana kwa ukabila kati ya Amharic na Tigray, wasomali wanauana kwa thamani na utukufu wa koo zao, wakenya leo wanachomeana nyumba kwasababu zinazotajika licha ya wizi wa kura, lakini kujitokeza kwa Ukikuyu na Uluo na pia tumeona kadhia ya Utusi na Uhutu huko Rwanda na Burundi.

Kauli yenye nia ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa huko Zanzibar kwa mtazamo wangu mdogo naiona ni kama taa yenye mwanga katika kiza kinene cha taharuki na kutoaminiana miongoni mwa wazanzibar wenyewe.

Wajumbe wa halmashuri Kuu ya Taifa ya CCM, Kamati Kuu ya Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ndiyo wenye maamuzi kisiasa nani awe mgombea kutokana na kwasababu zile zile za mchakato wa kidemokrasia.

Mabadiliko si lazima yasubiri mgombea na mshindi toka nje ya CCM, ndani ya CCM anaweza kujitokeza kiongozi mwenye kupenda kufanya mabadiko na ikawa ni sehemu ya mabadiliko hayo na kisha historia ikajiandika.

Mzee Ali Hassan Mwinyi alipoingia madarakani 1985 alifanya mabadiliko ya sera za kuichumi ikiwa ni pamoja na kukubaliana na matakwa au masharti ya IMF,sera ya soko huria na maboresho katika sura ya Azimio la Arusha. Maduka ya Ushirika yakafa, RTC, NMC na ile adha na adhabu ya kujipanga kwenye misururu mirefu toka alfajiri ikaondoka na leo imebaki kuwa ni historia kana kwamba hilo jambo halikuwapo nchini.

Kimsingi mimi simtazami tu Balozi Ali katika asili ndani ya nyumba ya Mzee Karume, bali navutiwa na uwezo wake, taaswira aliyonayo katika uga wa siasa ikisukumwa na utashi wake katika kufikia mabadiliko ya kudumu na ya pamoja huko Zanzibar.

Kumnyima nafasi au kumbeza kwasababu ati ni mdogo wake Rais Aman na kupuuzia uwezo wake ni sawa na kumyima haki au kumtia msiba wa nakama kwa kuzaliwa katika familia ya Mzee Karume.

Akiwekewa "kauzibe" mwaka 2010 kwa sababu ati yeye ni mtoto wa Mzee Karume hata akitaka tena kuwania urais mwaka 2020 ataambiwa vile vile kuwa Kaka yake Amaan aliwahi kuwa Rais na hivyo hana nafasi.

Zanzibar na hasa CCM kwa upande huo inahitaji kumpata mgombea shupavu, mwenye mvuto, mbinu na uhodari katika kujenga hoja na kujibu kwa nguvu ya hoja kwenye viriri vya kisiasa na kwenye jukwaa la jumuiya kimataifa.

Mnaochambua na kukosoa masuala ya siasa hebu itazameni kweli katika kina cha tafakuri yakinifu katika kuficha batili isiyobebwa na uzito wenye mantiki kamili katika kuziba ufa kabla ya kujenga ukuta.

Mungu ibariki Afrika.

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

 

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.