AFRIKA, NIPATIENI LUMUMBA NA SAMORA

Na: Antar Sangali, Bagamoyo <03/01/10 >

Damu ya Rais wa kwanza wa Msumbiji huru-hayati Samora Machel na Waziri Mkuu wa kwanza wa Kongo marehemu Patrice Lumumba bado inatiririka katika ardhi ya nchi zao kutokana na viongozi hao kujitoa mhanga katika kupigania maslahi na haki za wananchi huku wakiyaalaani hadharani mataifa makubwa ya kibeberu na yaliyotaka kuikandamiza Afrika.

Vifo vya viongozi hawa vilistusha na kurudisha nyuma maendeleo ya kiharakati kutokana na kuondokewa na viungo hivyo muhimu ambavyo katika kusukuma mbele maendeleo ya jamii na hasa katika mapambano ya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika na msimamo wa kujitegemea katika uhuru wa kweli, viongozi hao walihiyari hata kuyatoa maisha yao kwa kile walichokiamini.

Kufa kwa Lumumba na Samora lilikuwa pigo zito kwa maendelo ya nchi za kusini mwa Afrika, furaha na mafanikio makubwa kwa mabeberu waliokuwa wakizitazama rasilimali zilizoko Afrika kwa uchu na kujenga mbinu za kuwagawa waafrika katika makundi ya utengano na kubaguana kutokana na asili zao.

Mkutano wa kuigawa Afrika uliofanyika Berlin huko Ujarumani mwaka 1884/85 ulikuwa mkakati wa kuhalalisha fikra na matamanio ya waupe kuhusu jinsi watakavyozitumia rasilimali na nguvu kazi ya mweusi ili kujenga na kuziendeleza nchi zao na vizazi vyao kiviwanda, kiteknolojia, na kielimu.

Haikuwepo sababu ya msingi ya wazungu kuitisha mkutano wa kuigawa Afrika ilhali wao si waafrika au kutaka kuweka himaya na tawala zao na kuchota maliasili za Bara hili na kuibakisha Afrika na watu wake wakiwa na umasikini hohehahe.

Lumumba na Samora ni viongozi walionekana kuwa tishio na vikwazo katika kuyakataa matakwa ya sera na hila za wazungu waliokuwa wakitaka kuiburuza Afrika lakini pia viongozi hawa walitumiwa vema na wazungu (ingawa kwa hila mbaya) kuwafarakanisha waafrika--jambo ambalo hadi sasa wamefanikiwa na kuliacha bara hili katika tabu za magonjwa, njaa na vita visivyokwisha.

Lumumba na Samora waliamini katika mioyo yao kuwa Afrika ni ya waafrika wenyewe, Asia ni ya waasia ,ulaya ni ya wazungu, na marekani ni ya wamarekani. Misimamo hii thabiti ndiyo iliyokatisha mapema maisha ya viongozi hawa shupavu kutokana na kukataa kwao upumbavu wa kuwa watumwa wa fikra na kuukumbatia ukoloni mamboleo.

Mali asili na rasilimali za Kongo zilihitajiwa kwa udi na uvumba na mabeberu hao ili ziwanufaishe wao na nchi zao, lakini Lumumba yeye alisema tena kwa ujasiri, kwamba mali hizo ni za wakongo wenyewe na vizazi vyao. Masikini leo hii Kongo imeshamiri vita na kibaraka aliyemsaliti Lumumba Joseph Kasavubu akawa sehemu ya usaliti huo.

Matakwa ya wazungu yalikumbatiwa na Rais Mobutu Seseseko aliyekufa akiacha nchi yake katika janga kubwa la vita na wazungu wameigeuza ardhi ya nchi hiyo kuwa soko kuu la kuchota urithi wa nchi hiyo na kuuzia bidhaa zao za silaha huku wakiiba maliasili usiku na mchana.

Wazungu hawataki kuamini kuwa Afrika ni ya waafrika na wanataka kuingilia mambo ya ndani ya Afrika na kuwapangia waafrika hatma yao katika maendeleo, demokrasia na kurithisha kwa lazima itikadi na tamaduni zao ambazo mababu zetu wa kale waliziita ni tamaduni za kinyama.

Wazungu walianza zamani kuiba maliasili, vipaji vya ugunduzi katika zana za ufundi stadi, uchongaji, utiaji wa nakshi, madawa ya miti shamba na utabibu vikahamishiwa katika maabara zao na kisha wakajifanya wao wameendelea na kukiita kila kitu chetu ni cha kishenzi na waafrika tukakubali kuitii dhana hii ya kipumbavu na leo hii ikitutafuna sisi wenyewe.

Wazungu waliwaleta watu wao mapema huku wakiwapachika vyeo a kuwaita wagunduzi wa vitu vyetu ambavyo tayari vilikuwa vimegunduliwa na mababu zetu walioishi enzi hizo. Mfano, utasikia watu wakipiga kelele kuwa "John Speke ndiye aliyegundua ziwa Victoria." Kagundua wapi ziwa victoria wakati wasukuma na wajita walikwa wakivua sato na sangara kitika ziwa Victora kabla Speke hajafanikiwa kutia mguu katika fukwe za ziwa hilo? kina Carl Pettters, Stanley Burton, David Livingstone, Vasco Da Gama, na wengine wengi waliukuja kwa lengo moja na lengo moja pekee: kupeleleza jinsi ya kuiibia Afrika huku wakiandika mikataba ya hadaa.

Mabeberu hawakutaka kubaki kwao na kila siku macho yao yalikuwa Afrika huku wakiwaleta maafisa wao katika nchi za Afrika kabla na baada ya kujitawala ili kuandaa fitna na kupanga safu ya viongozi waliokubaliana nao na kuwaona ni vibaraka wao ikiwa ni pamoja na kuwapangia mauaji vingozi waliojitoa hadharani kupinga masharti yao ya kijinga.

Tazama mwaka 1957 hadi 1959 Frank Curlucci aliyekuwa Afisa maalum wa marekani anayeshughulikia siasa katika nchi ya Kongo akiweka mikakati na mbinu ya kuitazama nchi hiyo na kulijulisha Taifa lake katika kila hatua ya maendeleo ya Kongo na nani ni kikwazo asiyetii lile wanalolitaka wao. Afisa huyu Curlucci mwaka 1962 hadi 1964 alihamishiwa visiwani Zanzibar pia akifuatilia masuala ya siasa na kujua jinsi gani itikadi ya kikomonisti iliyokuwa ikifuatwa na mataifa ya kirusi, Cuba na China itakavyokwamishwa na isienee katika kisiw hicho, na Afrika Mashariki yote. Afisa huyu baada ya kufanya vizuri kazi yake mwaka 1957 alifanywa kuwa Naibu Mkurugenzi wa shirika la kijajsusi la Amerika (CIA) na baadaye akawa waziri wa ulinzi katika serikali ya Reonad Reagan.

Marekani katika kuweka kwake mkazo na kuitazama Afrika ilimtuma na kumpa kazi Afisa mwingine maalum aliyeitwa Jesse Mac Knight aliyekuwa akishughulikia siasa katika Bara la Afrika kana kwamba Afrika hii ni sehemu ya Marekani wakati mwafrika akikamatwa tu huko kwao akifanya utafiti wa hali ya kisiasa aliweza/anaweza kushitakiwa kwa kesi ya ujasusi au agaidi.

Pia kulikuwa na Afisa mwingine aliyeitwa Petterson aliyekuwa Naibu mwakilishi wa ubalozi wa marekani Zanzibar, Fredrick Picard mkuu wa shughuli za kibalozi mara baada ya Mapinduzi ya 1964, Duncun Sandys aliitwa Katibu wa Makoloni na William .C. Trimble Mkurugenzi aliyepewa jukumu na kazi ya kuitazama Afrika ya Magharibi.

Bila shaka mikakati na mbinu za aina kama hii ndizo zilizogharimu maisha ya akina Lumumba na Samora kutokana na kuwaambia wazungu kinywa wazi bakini kwenu na iacheni Afrika ijiamulie mambo yake na kujipangia maendelelo yake.

Mwanazuoni mmoja wa Kijamaika aliyewahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam marehemu Dk Walter Rodney aliwahi kuandika kitabu chake alichokiita How Europe Underdeveloped Afrika katika kuonyesha hisia zake na jinsi wazungu wanavyoinyonya, kuiburuza na kuikandamiza Afrika kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kijamii.

Leo mabeberu hao hao wameanzisha mahakama wanazoziita za kimataifa na kutoa hukumu kutokana na mashitaka wanayoyaona wao ni makosa lakini baadhi ya viongozi katika mataifa yanayojiita makubwa au wale wanaouza silaha zinazopiganisha watu katika Bara la Afrika hawafikishwi katika mahakama hizo na wala hawagushwi japo kwa tuhuma.

Kifo cha Lumumba hakijaelezwa bayana ni akina nani hasa walihusika na je watafikishwa lini mahakamani katika mauaji hayo ya kinyama na kuiachia Kongo kidonda kisichopona na machangu makubwa katika Afrika yetu.

Samora ndege yake ilidondoshwa katika mpaka wa nchi yake na Afrika Kusini lakini hadi leo hii hakuna juhudi wala mwelekeo wa kumpata na kumjua aliyehusika na ushetani huo uliopoteza maisha ya kiongozi huyo thabitI wa kiafrika na mtetezi wa maslahi ya Bara lake.

Juhudi za mabeberu ni kudhoofisha nguvu na mapinduzi ya kifikra yalioasisiwa na vuguvugu la PAFMECA, nchi tano zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi kusini mwa Afrika na vilevile wakiihofia AU, zamani ilifahamika kama OAU.

Afrika ni lazima isimame kidete ili kupinga na kukataa njama za kuliharibu bara hili kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi kwa saabu tu za kigezo cha kuendelea kwa nchi za wazungu, waarabu, waisrael na wamarekani ili hatimaye Afrika ijitegemee na kuamua mambo yake yenyewe. Afrika, nipatieni wapiganaji hodari na shupavu kama Lumumba na Samora.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.