BARUA YA WAZI KWA WAZIRI KHATIB: "UTAMADUNI WETU NDIO MUSTAKABALI WETU"

Na, G

Pongezi nyingi mheshimiwa waziri kwa uteuzi wako huo kuongoza wizara hiyo kwani ingawa takwimu zetu zinawezekana zisiwe sahihi, lakini kwa kadri tunavyokumbuka wewe unaweza kuwa waziri wa kwanza wa wizara inayohusu utamaduni na michezo ambaye uliwahi kufanya kazi katika sekta ya utamaduni.

Tukianza na idara ya habari, hii ni idara ambayo kimsingi inaitikia tu mwenendo wa matukio kadri yanavyotokea na kuwajulisha wananchi matukio hayo. Kitu kikubwa sana unachoweza kufanya katika hili, ni kuongeza uhuru wa vyombo vya habari, kwani kwa kiwango kikubwa hatuna mamlaka na hatutawali utokeaji wa matukio unaosababisha habari. Matukio yanatokea kwa namna yake yenyewe na idara ya habari kuyachukua na kueleza wananchi. Kama ukiweza kuongeza uhuru wa vyombo vya habari kwamba wanahabari wasibanwe na mamlaka kuhusu habari wanazotoa (kama sheria na kanuni za uandishi zinafuatwa), italeta tofauti kubwa.

Uhuru wa vyombo vya habari ni kitu muhimu sana si tu katika kuelimisha jamii kuhusu mambo yanayoendelea kitaifa na kimataifa yawe mazuri au yakiwa mabaya. Uhuru wa vyombo vya habari pia unaweza kuwa kioo ambacho kwacho serikali inaweza kujiangalia na kuona maeneo ambayo yanaweza kurekebishwa au kuboreshwa. Lakini pia ukosefu wa uhuru wa vyombo vya habari unaweza kuwa sumu kubwa ambayo inaweza kuleta uhasama mkubwa kati ya wananchi au sehemu ya wananchi na serikali yao. Mfano mzuri kabisa na wa karibu ni matukio yaliyotokea juma lililopita ambapo askari wa usalama walivamia na kuchoma moto ofisi za gazeti la standard na mshirika wake televisheni ya KTN. Wananchi weeengi walichukizwa sana na kitendo cha serikali kuruhusu au kama wengine wanavyodhani kuagiza unyanyaswaji huo wa vyombo vya habari kwa sababu tu wameandika mambo ambayo serikali haikuyafurahia. Badala ya kuyarekebisha, wakawafitini. Matokeo yake ni kwamba gazeti la standard limeongezeka saaaaaaaaana umaarufu na usomaji huko Kenya na TV ya KTN vivyo hivyo. Na serikali ya Kenya imepungua sana umarufu na kudharauliwa na watu wake kwa kutaka si tu kuficha ukweli, bali pia kuwanyima vyombo vya habari uhuru wao.       

Jambo la kusikitishwa zaidi, moja ya mawaziri wa serikali alipoulizwa, alijibu kwenye chombo cha habari cha kimataifa, kwamba ukimchokoza nyoka, tegemea kuumwa na nyoka huyo. Na akasema hilo ndilo lililotokea kwamba vyombo hivyo vya habari vilimchokoza nyoka, yaani serikali. Na matokeo yake ni nyoka huyo (Serikali) akawang'ata. Na hili halikuanzia hapa kwa serikali ya Kenya maana kumekuwa na mololongo wa matukio kuanzia wakati mke wa raisi wa Kenya Mama Kibaki alipopiga mwandishi wa habari aliyekuwa tu ajanaribu kufanya kazi yake.       

Kwa hiyo wizara yako inaweza kujifunza kutokana na makosa ya nchi nyingine ya kuwanyima waandishi uhuru na kupoteza umaarufu, kwa kuwapatia waandishi uhuru wa kutosha na kushughulikia kero zile ambazo waandishi wanazitolea taarifa. Hata pale waandishi wanapovuka mstari na kukiuka maadili ya kiuandishi, basi kuna sheria za kushughulika nao, si kuchukia na kutumia vibaya vyombo vya serikali kama jeshi kwenda kuhujumu vyombo vya habari.

Kitu kingine ni kuboresha upeo, mwenendo na na ubora wa waandishi wa habari. Hili linaweza kufanywa kwa kuboresha mafunzo wanayopata waandishi na kuwafundisha nidhamu binafsi. Hii itasaidia waelewe maeneo wanayofanyia kazi na kuonekana kufaa katika maeneo hayo. Pia kuongeza ubora wa mawazo na maswali wanayouliza wanapofanya mahojiano na watu.

Kwa upande wa michezo, hatujafanya vizuri sana katika duru za kimataifa. Hivyo ushauri wetu kwako ni kujiwekea lengo moja au mawili ya kuanza nayo ili kutuweka katika kiwango cha kimataifa. Mahali pazuri pa kuanzia ni ahadi ya raisi ya kulipia kocha yeyote kutoka mahali popote kuja kufundisha timu ya taifa. Kwa kushauriana na vyama vya soka nchini, atafutwe kocha bora kabisa ambaye atapewa mamlaka yote ya kufundisha timu ya taifa bila kuingiliwa na viongozi wa vyama vya soka na mamlaka zinginezo. Hili ikiwezekana ulisimamie kwa karibu zaidi maana hata tukipata kocha mzuri, kama ukiritimba wa vyama vya michezo hautaondolewa kumpatia kocha huyu uhuru wa kutosha kuchagua, kufundisha na kupanga timu siku za mechi, hakutakuwa na matokeo tofauti. Lengo liwe kupeleka timu ya Taifa ya Tanzania kwenye mashindano ya soka ya kombe la Afrika mwaka 2010 ambapo Namibia ina nafasi kubwa ya kuwa mwenyeji wake, na mashindano ya soka ya kombe la dunia mwaka 2010 huko Afrika Kusini. Hayo ni malengo makubwa lakini kuna muda wa kutosha, na kocha kama raisi alivyoahidi, kama mkiitumia ahadi hiyo, kuandaa timu nzuri ambayo itakuwa na ujuzi na nidhamu na nafasi ya kutufikisha Namibia (Kama wakipewa uenyeji) na hatimaye, lengo kuu Afrika kusini hiyo mwaka 2010.

Wakati huo huo kwa michezo mingine kadhaa ambayo watendaji wa wizara yako na viongozi wa michezo wanaweza kuona vyema, weka lengo la kupeleka timu nzuri Beijing kwa mashindayo ya Olimpiki ya majira ya kiangazi huko Beijing, China mwaka 2008. Si lazima timu iwe kubwa ila ni muhimu iwe shindani (competitive). Chagua michezi kadhaa ambayo tuna nafasi ya kufanya vizuri, fanya mashindano ya awali ya kuchagua watakaoiwakilisha nchi katika mashindano hayo. Na wakishapatikana basi kambi ianze mapema na lengo liwe kuleta medali nyingi iwezekanavyo katika matukio yote yale watakayoshiriki.

Tukija kwa upande wa utamaduni, hapa panaweza kuwa na changamoto pia. Maana kwa kweli ni ngumu kwa sisi watanzania kujitambua kwamba sisi ni nani kama watu binafsi. Sisi ni nani kama familia, kama jamii, kama makabila na sisi ni nani kama taifa. Nasema hivi nikiwa na maana kwamba kwa kiwango kikubwa tumepoteza (Kama tulikuwa nacho) kitambulisho chetu kama taifa, ule utamaduni wa pekee ambao watu wakituona, wangetutambua kama watanzania. Mila zetu, desturi zetu na utamaduni wetu kwa ujumla umefifia sana na kuchanganyika na tamaduni za nje na kutupotezea ule upekee ambao utamaduni ulitakiwa kututambulisha kwao. Mavazi yetu, makabila yetu,nyimbo zetu, vyakula vyetu, mfumo wetu wa maisha n.k, vimechanganyikana saaaaaana kiasi kwamba ni ngumu kututambua isipokuwa kwa makabila machache kama wamasai au jamii za kimakonde. Tumepoteza mitindo yetu ya asili ya maisha, tumesahau hata lugha zetu za asili, hatuna hata vazi la taifa na mengineyo mengi.

Hivyo tunatoa wito kwako mheshimiwa waziri ili kwamba kama ikiwezekana upate jopo la wataalam wa utamaduni ambao, hata kama hawataweza kuwafanya watanzania kurudia tamaduni zao, lakini wafanye utafiti na kuhifadhi tamaduni zetu hizo ili kwamba kwa wale baadhi ambao wataona haja, wawe na mahali pa kujifunzia. Tupate mavazi au vazi litakalotutambulisha maalum kabisa kama watanzania, tuwe na aina ya muziki ambayo itatambulika kama mziki wa kitanzania, watu wafundishwe kupenda Kiswahili na lugha zao za asili n.k

Wakati huo huo, kama taifa twaweza pia kuwa na alama zinazotutambulisha kitaifa na kimataifa situ kama watanzania, lakini pia hata kutambulisha maeneo ya mikoa kulingana na matukio yali/nayotokea katika mikoa hiyo. Kwa mfano ukienda katika jiji na New York, kuna kisiwa cha uhuru (Liberty Island) ambapo ndipo ilipo sanamu maarufu ya uhuru (statute of Liberty). Katika hii sanamu jiji la New York na Taifa la Marekani wanajitangaza si tu kama taifa huru na linalothamini uhuru, bali pia kama taifa kubwa ambalo ni alama ya uhuru duniani. Wanachukulia hili kama utamaduni wao na kufanya bidii kueneza dhana hii duniani kote.

Nakumbuka miaka kadhaa nyuma, mnara wa azimio ulikuwa kitambulisho kikubwa cha Arusha. Inawezekana baada ya kuonekana kushindwa kwa Azimio basi na mnara wa azimio ukaacha kuwa kitambulisho kikubwa cha Arusha. Kama lilishindwa au halikushindwa, bado azimio la Arusha ni sehemu ya historia yetu na ingepaswa kuendelea kuwa moja ya vitambulisho vyetu. Lakini la muhimu ni kwamba pamoja na lugha, vyakula, mavazi, muziki, hadithi kwa ujumla mila na desturi zetu, lakini pia utamaduni wetu unahitaji alama za kututambulisha kama taifa, kimikoa ndani ya taifa, na kitaifa katika duru za kimataifa.

Basi tunakutakia kila la heri mheshimiwa waziri katika kutekeleza wajibu wako. Ila katika yote, tafadhali zingatia kupeleka timu nzuri Beijing 2008 na zaidi sana weka lengo la kupeleka timu ya taifa Afrika kusini 2010. Afrika kusini ni karibu sana kulinganisha na nchi zingine zinazokuwa wenyeji wa fainali ya kombe la dunia. Na kama timu yetu ya taifa ikifanikiwa kwenda (Tunaamini utaifanikisha kwenda), Afrika kusini ni mahali pekee mpaka sasa ambapo wananchi wengi sana wanaweza kumudu kwenda kuishangilia timu yao katika mashindano hayo ya kombe la dunia. Na kama kura ya kukuamini mheshimiwa waziri kwamba utafanya hili litokee, mimi naanza kudunduliza fedha tangu sasa ili kwamba niwepo kuishangilia timu yetu ya taifa ya soka katika mashindano ya fainali za kombe la dunia huko Afrika ya Kusini.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.