HULKA YA PEKEE ALIYONAYO KIKWETE: UPOLE NA HAIBA YENYE TABASAMU.

Na: Antar Sangali, Bagamoyo <03/07/10 >

Sehemu moja ya wimbo uliowahi kuimbwa na bendi ya Juwata Jazz inasema hivi: "......Mola mzidishie busara na nguvu mwenyekiti na walio chini yake uwape fikara na hekimaaaaa…. waiongoze nchi yetu kwa moyo wa kimapinduziii na kuendelea......."

Ujumbe huu wenye muwala wa bendi ya kongwe ya Juwata wana Msondo Ngoma, Magoma Kitakita kamwe hautakufa wala kuchakaa kutokana na kubebeshwa maudhui yalioshiba na kusimama katika dhana ya ukweli.

Kwamba, tabia ya upole iliyojawa na hekima na hatimaye kuzaa haiba yenye tabasamu ni jambo linalotakiwa kuenziwa na sio kubezwa.

Binadamu anaweza kubadili jambo lolote katika mtiririko wa maisha yake ya kawaida ikiwemo kuchunga kwa makini tabia zake, lakini hawezi kuibadili hulka yake ya asili. Hulka haina dawa na tabia njema sikuzote huelezwa kuwa silaha bora.

Hulka ya pekee aliyonayo Rais Kikwete ni ile ya kupambwa na upole na haiba yenye tabasamu la kuambukiza. Na hili kwa mtazamo wangu hafifu, haimuondolei wala kumpunguzia chochote katika kufikia dhamira anayoikusudia ima ikiwa ya uongozi katika medani za kisiasa, diplopmasia, au kijeshi.

Mwenyewe Rais Kikwete wakati akilihutubia Bunge mjini Dodoma aliwahi kunukuliwa akisema kwa Kiingereza kuwa "I may be wearing a smile but Iam firm on serious issues." (Tafsiri isiyo sahihi sana ni kwamba "naonekana kuvaa haiba ya tabasamu lakini nina umakini katika mambo nyeti ya msingi'.

Hili kwake halina ubishi na kila mtanzania aliyelelewa katika malezi ya kuamini dhana ya ukweli atabaini kwa mwendo mwepesi na hasa ikiwa mtu huyo si mbishi mbishi, mjuvi na aliyejawa na kiherere, kuwa Rais Kikwete ana moyo wa ujasiri wa kupigiwa mfano katika historia ya nchi yetu.

Tabia ya upole ni umbile ambalo Mungu anaweza kumjaalia au kutomjaalia (mja) binadamu wake kama ambavyo wanavyojaaliwa baadhi ya watu wengine kujawa na hisia za ukatili, ukabila, udini, tabia za kufanya uharamia, ujambazi, ukahaba, au kufuata amri za Mungu mkuu na maandiko matakatifu ya vitabu vyake.

Wazazi wengi huomba kwa mungu usiku na mchana waajaliwe kupata watoto wenye haiba ya tabasamu, upole, akili, hekima na busara kwa matarajio kuwa vitu hivyo aghalab humnasibisha sana mtu na maisha yake katika kumjengea muktadha wenye satua katika mahusianmo na jamii ili mtu huyo aweze kupata matlaba na matarajio yake.

Nataka kubainisha ili kutoa ufafanuzi mpana wa mambo mengi magumu aliyobebeshwa na kurithishwa Rais Kikwete katika utawala wake ambayo kwa namna kubwa hayatokani kabisa na zama yake ya kutawala bali baadhi yake ameyakuta yakiwa tayari yametendwa na kusimamiwa na awamu zilizomtangulia.

Hebu natulitazame sakata la Akaunti ya Malipo ya madeni ya Nje (EPA), ubadhirifu wenye israf kubwa katika Benki Kuu(BoT) ukimhusisha marehemu Daudi Balali na maafisa wengine wa juu katika chombo hicho. Mikataba mibovu ya madini isiyo na maslahi huku ikigubikwa na usiri, ununuzi wa ndege mbovu, pamoja na ile rada ya inayomtatiza ndugu Andrew Chenge.

Hamkani nyingine inayokanganya utawala wa Rais Kikwete kwa maana ya kurithi katika dhana ya uwajibikaji wa pamoja (collective responsibility) ni Meremeta, Tangold, pamoja na Tenesco na kusibabisha hasara ya zaidi ya bilioni 20 ukiwemo pia wizi wa mamilioni ya Fedha kupitia Wizara ya Elimu chini ya Miradi ya MMEM na MMES.

Hiyo kama haitoshi kulikuwa na mlundikano wa malimbikizo ya madeni ya makubwa ya walimu, matumizi mabaya ya madaraka serikalini, madai ya wafanyakazi wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na ukandamizaji wa uhuru wa habari.

Chini ya utawala wa Rais Kikwete hadhi ya waandishi na thamani yao imepata haiba na heshima ambayo haijawahi kutokea katika historia ya nchi hii tokea uhuru wetu wa 1961. Leo waandishi hasa wale wenye kujiamini na kutoyumbishwa wana hadhi, staha na kushirikishwa kuliko ilivyokuwa hapo awali tulipowahi kuitwa sisi ni "uchwara"

Neno "serious" linaonekaka kutumika vibaya ili kupata tafsiri kamili na watu wengi hifikiri na kudhani ni ile mikunjo ya sura (kupiga ndita) au ukunjaji wa wajihi kwa taaswira ya kijivuni au kujawa ujeuri mithili ya fahali awapo zizini.

Haiba ya upole aliyonayo Rais Kikwete kwa mtazamo wangu mimi ni ya kuogopwa na kukaliwa mbali kwa mtu mwenye kujua aina ya haiba hiyo ilivyo na siri iliyojificha.

Kujaaliwa kuwa na haiba ya aina hiyo na hasa unapokuwa kiongozi mtawala mimi kwangu naitazama ni kama 'sumu peremende' au naweza kusema "sweet poison," kwa lugha ya kigeni. Mtu wa aina hiyo anaweza kuthubutu kukulisha biriani ya nyama ya ngamia kwa mkono wa kulia na kisha ukajikuta ukitapika ugali mweusi wa muhogo kwa kitoweo cha kamongo kwa mkono wa kushoto.

Mhariri wa Gazeti la Rai na Mtanzania Muhingo Rweyemamu wakati fulani aliwahi kuandika makala yake iliyosema watanzania tumejawa na uvivu wa kufikiri na kuhifadhi kumbukumbu sahihi katika safari ya maisha yetu ili kujua tulitoka wapi, tutafikaje tunakotarajia kwenda na kubaini mahali tulipo sasa.

Akatoa mifano mingi sana na leo yaonekana pia tumesahau kuwa nchi hii tuliwahi tukipanga foleni toka alfajiri na kukimbiza magari yenye taka tukidhani yana magunia ya unga, barabara mbovu zisizopitika, kula unga wa manjano, tukivaa nguo za mipira na viatu vya matairi, magazeti yalikuwa ya mzalendo, Daily News na Uhuru na kusikiliza Radio Tanzania.

Kimsingi sisi watanzania kama alivyosema Muhingo ni wasahaulifu mno wa kuweka kumbukumbu na zaidi tumejitwika tabia au kujijengea utamaduni wa kumsifu na kumpamba mtu, kiongozi, mwanamuziki au mchezaji wa mchezo wowote mpaka pale umauti unapomkuta.

Akiwa hai ni nadra sana kusikia akisifiwa hata kama atafanya vyema kwa kiasi gani mtu huyo , huifumba midomo yetu na kuzisimamisha kalamu zetu za kuandika kama kwamba mambo hatuyaoni. Huu ni upuuzi usiofaa kufuatwa na kuenziwa.

Katika awamu ya kwanza Rais Julius Nyerere alijitahidi sana kupanua wigo wa ajira nchini kwa kuanzisha utitiri wa mashirika ya Umma, kutilia mkazo kilimo na ufugaji kwenye vijiji vya ujamaa na pia vipaumbele katika ujenzi wa viwanda ili kukuza uzalishaji wa ndani na mashirika hayo wakakabidhiwa watanzania wazalendo kuyaendesha. Badhi ya mashirika na viwanda ni pamoja na Besco, Gapco, Nafco, Napoco, Narco, Aisco, Bandari, NDC, Nedco Nasaco, Bora Shoe, Tanzani Tea Blenders, Umita, UFI na Kizaku. Mengine ni pamoja na Gapesco, Tanzania Fishnet, Urafiki, Sungura Textile, Mwatex, na Mutex, mashirika na viwanda vyote hivi vilikufa vikiwa mikononi mwa watazania wazalendo. Hapa neno ufisadi halikuzaliwa wala kutoholewa na kushikiwa bango na wanaojiita wapambanaji.

Nia njema ya Rais Nyerere ghafla alizamishwa mtoni na kundi la wajanja ambao wengi kati yao leo ndiyo wanasomesha watoto wao ughaibuni ,wamejenga majumba ya kifahari, wamejipimia viwanja Dar Estate, Usino, Kichangachui, Mbezi Beach na Msasani na leo baadhi yao wanajiita wapiganaji wa mstari wa mbele dhidi ya ufisadi; laiti wakati ule ungelipita uamuzi wa kuwafikisha mahakamani wale waliofilisi mashirika ya umma na wahusika wakafungwa lilikuwa ni eneo zuri sana la kusimamia ufisadi na wizi serikalini.

Nyerere alikataa katakata kubeba wataalam toka nje akiamini kuwa huenda wataalam wachache walioko nchini licha ya kuwa na elimu na utaalamu mdogo wa kiufundi na kiteknolojia; alichoamini yeye bila shaka wenzake wangelikuwa ni viongozi waaminifu na waadilifu kwa kulinda na kutetea maslahi ya nchi yao. Tarajio hili la Nyerere kimsingi liligonga ukuta na halikuleta tija.

Azma kama hii ndiyo anayoonekana leo akiifanya Kikwete lakini baadhi ya watu kwa makusudi na sababu zao mfukoni wanambeza na kumuona huenda akaandika historia ya kuwatumikia wananchi wake kwa bidii lakini pia akionyesha kuwaamini na kuwahimiza aliowakabidhi madaraka katika ngazi mbalimbali kuwa wabunifu na wachapakazi katika kusimamia sheria na utumishi wa umma.

Wako watu wanaomba kucha kutwa wakitaka kuibadili haiba ya upole wake wenye hekima aliyonayo Rais Kikwete ili awe mtawala mbogo, mbabe mwenye kujawa na vitisho huku wakisahau kuwa wajibu wake kama Rais ni kuwajibika na kuutumikia umma wa wananchi wanaokabiliwa na hali mbaya ya umasikini uisoelezeka.

Kuna waandishi wa habari na wengine waandishi wa makala leo wanaandika makala wakithubutu kudhihaki na kuponda kwa udhaifu wa hoja mambo hata yale yenye msingi na tija wakifikiri pengine mamlaka za utawala wa Rais Kikwete ziweze kuwatia mbaroni na wao wapate umaarufu ili hatimaye serikali iliyopo ihesabiwe kama ni kandamizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa watu kujieleza.

Uovu na mabaya kadhaa aliyoyakuta Rais Kikwete serikali kwa umakini wake amekataa kuyafumbia macho na badala yake amechukua hatua nyingi madhubuti bila ya kumuonea aibu mtu, rafiki na mtu anayemjua au kubeza kuwa hilo wakati likifanyika mtawala hakuwa yeye madarakani na halitambui.

Hivi kulingana na historia ya tawala zetu ni nani hadi leo aliyefikishwa mahakamani kwa kuua SU lolote katika awamu ya kwanza, Pili na ya tatu?

Kikwete yeye kimsingi amefanya uthubutu mpya na kuonyesha kuwa ni makini katika kusimamia mambo yanayohusu nchi na maendeleo ya jamii yakiwemo pia yale ya kisiasa katika chama chake kama Mwenyekiti. Serikali yake imechukua juhudi na sasa ameviachia vyombo vya sheria vipitishe uamuzi bila ya kuingiliwa na kushinikizwa.

Vyombo mathalan vya kisheria katika serikali vyenye dhamana ya kulinda mipaka, kupambana na uhalifu, rushwa na ujambazi vimepewa nafasi ya kutosha kuweza kumdhibiti kisheria mtu yeyote anayeendesha mambo kienyeji kuliko wakati mwingine wowote.

Kuna watu wengi walioanza kumjua Rais Kikwete zamani toka akiwa Katibu Mtendaji wa CCM hadi Waziri mara baada ya kumaliza masomo yake Chuo Kikuu Dar es Salaam mpaka leo hii wameshindwa kabisa kutambua usiri na dhamira aliyonayo Kikwete na wengine wameanza kumkalia mbali kwa kuhofia umakini na upole alionao kama mtu asiyependa masikhara kabisa awapo kazini.

Nchi nyingi Afrika zilijikuta zikingia kwenye mizozo na mitafaruku mikubwa ya umwagaji wa damu kutokana na kukosekana kwa viongozi wenye ustahamilivu, busara, hekima na maarifa ya utatuzi wa mambo ambayo kwayo yanaweza kuleta majanga na kujenga taharuki ya kutoelewana.

Zama hii kimsingi si zama ya kuongoza kwa ubabe, vitisho na kukithithirisha ujuvi utokanao na kuleweshwa na madaraka. Katika zama hii mpya, ni lazima busara, hekima na maarifa vitangulie mbele na wewe uvifuate. Lakini ukijaribu kutangulia wewe na kutaka vitu hivyo vikufuate nyuma, utajikuta ukipita katika jangwa la majuto.

Mzee Nelson Mandela aliwahi kusema kuwa: "The era is no longer for despotic leaders; but the era for democratic reform and any government in power must bend before the popular will." kwa tafsiri isiyo sahihi: "Hizi sio zama za viongozi wenye umimi na wasioambilika, bali ni zama ya mageuzi ya demokrasia na kila mamlaka iliyo madarakani inahitaji kufanya utii na kufuata maamuzi ya walio wengi."

Tanzania leo yameibuka mambo mengi makubwa yaliojificha kwa muda mrefu juu ya ubadhirifu wa mali ya umma, wizi wa fedha na mali za serikali vikiwemo pia vyama vya siasa, ujambazi, ushirikina wenye kuambatana na ukatili lakini vyote vinasimamiwa na kudhibitiwa bila ya utani na serikali ya Kikwete.

Hapa ilibidi Rais atiwe moyo, asiangushwe na aungwe mkono na kupongezwa japo kwa kufanyika maandamano nchi nzima lakini kinyume chake baadhi ya watu hawaitaki haiba yake ya upole wenye hekima na kumtaka awe mzee maamri na wa kukamatakamata bila kuzingatia sheria zilizopo.

Mzee Benjamin Mkapa alipojaribu kuuweka uso wake katika hali fulani ya uhodari ili kujikinga na matapeli wa kisiasa, wala rushwa, na watumishi wa serikali wababaishaji wasiowajibika ipasavyo, watu wakakamdhihaki ati hacheki wala hakenui, kwamba ni Rais gani huyu asiye na haiba yenye tabasamu! Huku chama cha CUF wakithubutu kwenda mbali zaidi kwenye mikutano yao ya kampeni na kudhihaki kwa nyimbo za kejeli "...picha ya mkapa inawatisha watoto..."

Hebu tufike mahali watanzania tuepuke kwa nguvu zetu zote na kuacha tabia ya upekepeke. Upekepeke si mwema kwani hata wazee wa kiswalihili wa zamani waliwahi kuasa kwa kusema kuwa kila anayeanza pekepeke ili kugombanisha viumbe atabaki peke yake kama ng'ombe aso na pembe.

Tabasamu la Kikwete ni adimu mno kuwa nalo kila mtu hasa katika safu hizi za viongozi watawala katika Bara la Afrika. Wahenga walisema, '"Haiba ya cheko ni kama umbile lakini kuweka lengo ndiyo njia ya kuyafikia mafanikio.

Tumempata Rais mwenye dhamira njema inayosukumwa na kiwingu cha ustawi wa busara na hekima. Anasifiwa na wenzetu nje. Kwani tukimsifu sisi wenyewe tutaharibikiwa na nini? Tusimvuruge na kujaribu kumtoa kinywani kipande cha tende ili kumlisha shubiri. Tabasamu lake libaki kuwa salama ya nchi.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.