MHESHIMIWA RAIS, ISIWE NGUVU YA SODA

Na, G <bongotz.com>

Kwa heshima na taadhima tunapenda kuchukua nafasi hii kukupongeza Mheshimiwa Rais kwa ushindi wako mkubwa katika uchaguzi uliokupatia fursa na mamlaka ya kuongoza jahazi la uongozi wa taifa letu kwa miaka mitano ijayo na kama Mola akipenda kumi. Ni jambo la nadra sana katika mazingira ya kisiasa ya siku hizi na hata ya zamani kupata raisi anayechaguliwa kwa asilimia kubwa mno ya kura kama ulivyochaguliwa wewe. Kwa hiyo Mheshimiwa rais huo ni mtaji mkubwa sana wa imani ambao wananchi wamekupatia na ukiutumia vyema basi kutakuwa na faida ya mendeleo kwa taifa zima.    

  Pili tukupongeze pia kwa timu nzuri ya uongozi ambayo umeshaiunda na tunaamini unaendelea bado kuunda. Tunaamini Waziri Mkuu Lowassa ni kiongozi mzuri ambaye atakusaidia sana katika kufanikisha malengo yako ya mendeleo ya taifa letu na yeye pia ni mtu ambaye katika kipindi chako unaweza kumfunza vyema naye akajifunza kutoka kwako kama ambavyo wewe umejifunza kutoka kwa waliokutangulia, ili kwamba unapomaliza muda wako yeye aweze kuendeleza kutoka pale utakapokuwa umeishia . Na si yeye tu bali timu nzima ya mawaziri, manaibu wao na viongozi wengine wa serikali kwa ujumla imekaa vizuri. na tunakuwa na imani zaidi kila tunapoona mabadiliko ambayo unaendelea kuyafanya kwani tunaamini hujamaliza.   

  Tatu tunatiwa moyo na mwenendo wako hadi sasa wa kutekeleza ahadi yako ya nguvu mpya kwani hadi sasa umeonyesha kasi nzuri ya utendaji ambayo inatia moyo hata wengine ambao walianza kuwa na mashaka. Kasi hii na ari hii ya kazi unayoionyesha na ambayo inaambukizwa kwa watendaji wengine wa serikali ni chombo muhimu sana katika swala zima la maendeleo ambayo sisi wananchi tunatamani yafikiwe. Kwa hiyo tunakupongeza kwa hilo pia.     Ingawa hatuwezi kusema jambo moja moja ambayo tangu sasa sisi kama wananchi tumeshafurahishwa nayo, nasaha zako, hotuba zako, ahadi zako, mategemeo yako n.k. Tunaamini utapokea pongezi zetu za jumla kwamba kufikia sasa, tunakila sababu ya kukupongeza na kukuamini kwamba mtaji ule uliopatiwa na watanzania unautumia vizuri na kwamba utazaa faida siku moja hivi karibuni.    

 Pamoja na pongezi hizo mheshimiwa Rais, tunapenda kukupatia changamoto kadhaa. Kubwa zaidi ya zote ni wewe kudumisha au hata kukuza nguvu hii, ari hii ya kazi, kasi hii ya utendaji. Wahakiki wengine wanadhani kwamba hii ni nguvu ya soda na kwamba gesi ikiisha tu basi kila kitu kitarudia hali yake ya kawaida. na wengine wanadhani kwamba wewe ni binadamu kama binadamu wengine itafika mahali utachoshwa hasa pale ambapo unaona unaweka nguvu nyingi lakini mabadiliko yanakuwa polepole zaidi ya ulivyotamani. Kwa hiyo changamoto yetu kubwa na ya kwanza ni ya wewe na timu yako kuwa wavumilivu na wastahimilivu na kudumisha mwenendo wa kazi hii kama mlivyoanza. Pasipo kusahau kuwa wewe ni "Rais," na sio Makamba. Hivyo ni vema kazi zinazoweza kutendwa na Mawaziri ama viongozi wengine wa kiserikali ukatoa muongozo tu na sio wewe kusimama na kuonekana kuwa kila kona ya nchi ili kutekeleza yanayoweza tekelezeka bila uwepo wako. Maana yake ni kwamba, ndio maana kuna mawaziri.Haileti maana hata kidogo kwako wewe (Rais) kuanza kufukuza kazi makandarasi wakati waziri wa Ujenzi yupo na hiyo ni kazi yake.   

Pili kuna swala la uchumi. Rais Mkapa amefanya kazi kubwa saaaaana ya kuweka msingi wa uchumi wa taifa letu katika mahali bora kuliko, kwa mtazamo wetu, muda wowote katika historia ya nchi yetu. Sasa ingawa tunajua kwamba na wewe unataka kuendeleza kutoka pale alipoachia, tunakupa changamoto kwamba sambamba na hilo, fanya juhudi za makusudi za kutafsiri hatua hizo kubwa za maendeleo katika maisha ya kila siku ya watanzania. Watanzania wengi wanaposikia kuwa tumepiga hatua kubwa za maendeleo lakini nchi ina njaa, na mijini umeme ni kwa mgawo n.k, inakuwa ngumu kutafsiri maendeleo hayo katika maisha yao. Kwa hiyo fanya juhudi kubwa na za makusudi kabisa kusaidia maendeleo haya yaathiri maisha ya kila siku ya watanzania wote wa mijini na wa vijijini.    

Changamoto ya tatu ambayo ni kubwa na inaweza kukushtua mheshimiwa Raisi ni kero za wananchi. Kulingana na utafiti wa hivi karibuni wa ubora wa maisha ya watu duniani Tanzania ni moja ya nchi nne za mwisho duniani kwa watu wenye furaha. Inasemekana pungufu ya asilimia 20 ya watu nchini Tanzania, Zimbabwe, Ukraine na Moldova ndiyo wanaofurahia maisha na mwenendo wa maisha katika nchi zao. <http://www.unian.net/eng/news/news-95163.html> <http://en.for-ua.com/news/2006/01/10/142014.html> Utafiti huo umeonyesha kwamba kinyume cha mawazo ya wengi si tu elimu, au akili au mwonekano au jinsia au umri na vitu vingine kama hivyo, vinavyowapatia watu furaha. Ingawa vitu hivyo vina umuhimu wake, lakini utafiti ulionyesha mambo sita makuu ambayo yalionekana kama hayo yakirekebishwa, basi labda asilimia ya wananchi wenye furaha nchini inaweza kuongezeka kwa wingi. mahusiano ya kifamilia kilikuwa ni kigezo cha kwanza. Inaonyesha kwamba kutokana na shinikizo la uchumi watu wengi wanapunguza sana na sana muda wanaotumia na familia zao kwa ajili ya kazi na namna zingine za kutafuta kipato hivyo kuwapunguzia furaha ya kuwa na familia zao.    

Hali ya kifedha ilikuwa ni kigezo kikubwa cha pili. Na hali ya kifedha hawakumaanisha fedha ya kufanyia anasa, la, ni fedha za kutosha kupata mahitaji muhimu ya mtu binafsi na kwa wenye familia mahitaji ya familia. kama mtu ama familia ikiwa haina fedha ya kupata mahitaji ya kila siku wanashurutika kuishi kwa wasi wasi mkubwa na hii kuondoa furaha binafsi na furaha ya familia nzima. Kigezo sambamba na hicho ni kazi ambapo watafiti hao waliona kwamba kama mtu ana kazi ya maana hata kama hana fedha lakini lile tumaini kwamba kila mwisho wa wiki au mwezi kuna kipato kinaingia, kulileta furaha kubwa na matumaini kwa watu. Na pale palipokosekana kazi basi tumaini hilo na furaha inayoambatana nalo vinaondoka.    

Jamii na marafiki nazo zilikuwa vigezo muhimu. Ingawa hivi havihitaji sera inayoamuliwa na Rais, lakini Rais anaweza kutengeneza mazingira na kuonyesha mfano wa namna ambavyo sisi kama watanzania tunajali na kuthamini jamii zetu na marafiki zetu. Kwa hiyo wewe unaweza kuonyesha mfano kama mtu wa familia na kujenga mazingira ya kazi na utendaji yatakayohimiza mahusiano ya jamii na kujenga urafikia baina ya wananchi.    

Uhuru binafsi pia ulitajwa kama kigezo muhimu kuwapatia watu furaha. Watu wanataka kuwa huru na uhuru wa kweli huletwa na vitu kadhaa ikiwepo upeo wa kufikiri na kujiamulia mambo, uhuru wa kiuchumi ambao unahusisha kuwepo kwa kipato au fedha na kuamua kuzifanyia nini, Uhuru wa imani kuamua utaabudu, nini, nani, lini na wapi bila kuingiliwa na serikali. Uhuru wa mawazo kuweza kusema kile mtu anachofikiri bila kuogopa kuangukiwa na nguvu za dola (Isipokuwa pale mawazo hayo yanapohatarisha amani). Uhuru wa kuishi, kufanya kazi, kushiriki matukio yeyote popote, na wakati wowote bila kuwa na woga na serikali au kwa upande mwingine wahalifu. hayo pamoja na mengine mengi ambayo yanawafanya watu wajisikie huru, yanaongeza furaha yao.   

   Mwisho ni utunu wa mtu binafsi. Ni mambo gani hasa ambayo watu wanayathamini kama mambo muhimu katika maisha yao. Hapa kunakuja mambo ya imani, mila, utamaduni, n.k yaani ile nafsi ya ndani kabisa ya mtu, mwelekeo wa maisha ya mtu, mtazamo wa mtu kwa maisha yake na falsafa ya maisha kwa ujumla. Kadri mtazamo na mwelekeo wa maisha ya mtu unavyokuwa mzuri ndivyo navyokuwa na furaha zaidi na kinyume chake.     

Nilipokuwa naangalia tovuti hizo hapo juu mheshimiwa Raisi niliona aibu maana sikuwahi kufikiri kwamba kwa maendeleo nchi yetu iliyofikia, kuna namna yeyote ile tunaweza kulinganishwa au kuwa sawa na kiwango cha maisha wanayoishi watu wa Zimbabwe ambako wengi wao sasa ni wakimbizi wa kiuchimi na kisiasa katika nchi za nje hasa za magharibi. Sasa kuambiwa kwamba na sisi watanzania hatufurahii maisha na nchi yetu kama wazimbabwe, ilinishtua, kunishangaza na kuniogopesha. Hivyo nikaona kukupa changamoto mheshimiwa rais kwamba unapoliangalia hili, basi fanya kila linalowezekana kuondoa kero za wananchi zinazowaudhi na kuwaondolea furaha yao na utakapofanya hili na kufafsiri maendeleo yetu ya kiuchumi yaweze kuathiri maisha ya wananchi ya kila siku, utafiti watakaofanya mwaka mwingine utatuonyesha mahali fulani karibu na Malta ambapo asilimia 74 ya wananchi wao wanafuraha na kufurahia maisha yao katika nchi yao.  

   Kumbuka tu hili halina uhusiano mkubwa na utajiri wa nchi kwani nchi tajiri kama Marekani ni ya 16, Uingereza ya 21 na Ujerumani ya 22. Lakini nchi zinazofanya vizuri pamoja na malta ni Denmark, Austria na Columbia. Na nchi kama Ghana iko sawa na Canada na Finland ambapo asilimia 69 ya raia wao wana furaha. Hii inahusisha tu jinsia mbavyo wananchi wanaridhishwa na serikali zao na wanaamini serikali zao zinafanya kila zinachoweza kuboresha maisha yao na kuwaondolea kero na kuwapatia mahitaji ya msingi kuwawezesha kuishi maisha ya kawaida na kuridhika.    

Changamoto ya nne tunayokupatia ni kurudisha maadili ya maisha na ya kazi nchini. Serikali zilizotangulia zimejitahidi sana kutatua tatizo hili kwa njia nyingi ambazo ingawa inawezekana zilifanya mafanikio fulani, lakini haikubadilisha tabia za watu. Hili lilipelekea hata tume zilizoundwa kushughulikia maswala hayo kupata sifa mbaya mfano tume ya MAADILI kupelekea kuitwa huko mitaani tume ya MAADILI. Kwa hiyo tunakupa changamoto mheshimiwa Rais kuwa mbunifu. Na ubunifu si kitu kingine zaidi ya kutafuta njia mpya kutatua matatizo ya zamani. matatizo yapo na yataendelea kuwepo na watendaji wa kawaida wanatumia njia za kawaida kujaribu kuyatatua, ila viongozi wabunifu kama ambavyo tunakutia changamoto uwe, wanatafuta njia mpya kutatua matatizo hayo. Wahimize wananchi kwa mifano na sheria ikibidi, wananchi wa ngazi zote wajue kwamba ukiukwaji wa maadili si tu dhambi, na hatia na jinai, lakini pia ni tabia mbaya inayorudisha maendeleo nyuma. Hivyo wote kwa ujumla tubadili tabia katika maisha binafsi na katika utendaji wetu kuboresha hali ya maisha kama watu binafsi na kama taifa kwa ujumla.    Kila la heri mheshimiwa Rais na ukisahau mengine yote tunakuhimiza tu USIWE NGUVU YA SODA. Wananchi tumekuamini sana na wewe umeonyesha mwanzo mzuri na sisi tutaendelea kukuamini na kuamini kwamba na wewe utadumisha na kuendeleza kasi yako na ari yako ya utendaji.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.