IKIJA KWENYE SUALA LA UWAJIBIKAJI, CCM BADO INA "PRE-EXISTING CONDITIONS".

Na: BongoTz.com <03/14/10 >

Uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kumtimua kazi aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwanzoni mwa mwaka 2008-Marehemu Daudi Balali mara baada ya kupokea taarifa ya ukaguzi wa hesabu katika akaunti ya malipo ya madeni ya nje (External Payment Arrears (EPA) iliyokuwa chini ya Benki Kuu, si kwamba ulipokelewa na wananchi, nchi wahisani, na Taasisi za kimataifa kwa mikono miwili, ilikuwa pia ni ishara katika kufungua ukarasa mpya wa utendaji wa serikali ya JK. Lakini miaka miwili tangu kitisho hicho kitokea, Serikali ya JK imerudi kulekule kwenye zama za kutowajibika na kuendelea kuchechemea na "pre-existing conditions" tulizodhani kwamba wameepa.

Ni dhahiri kuwa marehemu Balali hakushiriki peke yake kwenye upotevu wa mabilioni ya shilingi ya BoT. Kuna kundi kubwa la "walaji" katika sakata zima la BoT na ufisadi wenye israf kubwa uliofanyika ukilenga kuumomonyoa na kuufifiisha uchumi wa nchi hii masikini na kudumaza maendeleo yake. Waliohusika wapo na bado wanatesa mitaani. Kimsingi, Rais Kikwete ameshindwa kuwawajibisha hawa walaji. Na hili kwakweli linasikitisha sana!

Waandishi wa Habari wa Tanzania walianza kunusa na kuzama katika habari za uchunguzi na wakiandika dhahir shahir kwamba kuna mchezo mchafu BoT lakini ikaonekana kuwa sisi wenye taaluma hii ni "viherehere".

Umoja wa vyama vya upinzani ulilivalia njuga suala hilo na kulieleza wazi wazi tatizo la BoT ndani ya Bunge la Tanzania pale viongozi wa upinzani Bungeni Bw. Hamad Rashid Mohamed na Naibu Kiongozi wa upinzani Dk Wilbroad Slaa waliposema "liwalo na liwe" na kuamua kulipasua jipu pwaa.

Kundi la "walaji" katika BoT nimesema ni kubwa, ni kubwa kwa maana baada ya mpango wao kufanikiwa na kujipatia fedha walijihesabu wameukata, kwamba hakuna atakayewagusa. Na mpaka hivi sasa wengi wao wanaishi kama wako peponi huku wanainchi walalahoi wakihangaika huku na kule wasijue hata mla wao wa pili utakapotoka.

Kumtoa mtu aliyeingia peponi si jambo rahisi na kwamba anayeweza kuingia huko na kutoka kwa khiyari yake ni mjinga asiye na mipaka katika dunia hii.

Baadhi ya "Vigogo" waliohusika na kutajwa katika sakata la ubadhirifu huo walipoanza kutajwa hadharani kauli zao za "mikwara" ilikuwa ni kwamba tutakwenda mahakamani, tumevunjiwa heshima zetu mbele ya jamii, na wengine wakadiriki kusema hadharani bila aibu kuwa wanaonewa wivu.

Kuna kundi ambalo kimsingi awali halikutaka kabisa na wala halikuonekana kuafiki au kumfagilia Rais Kikwete awe mgombea wa urais wakihofu Kikwete ni "mtoto wa Nyerere" huku wengine wakimpigia debe ili wapate himaya ya ulinzi kwa kutenda kwao uchafu.

Habari za kina kutokana na uchunguzi wangu wa kihabari bado hazionyeshi kwa uwazi wenye alama ya mshangao kuwa Rais Kikwete ni miongoni mwa "walafi" wenye tamaa ya kujitajirisha.Hili pia linathibitika tokea uhai wa Baba wa Taifa marehemu Julius Nyerere pale aliposema Kikwete ni "msafi " lakini kuna watu mikono yao inanuka dhulma na harufu mbaya ya wizi.

Afrika ni Afrika, Afrika ndiyo yenye matatizo lukuki kuliko eneo lolote la sayari ya dunia (Zuhura), dhihaka katika kuzingatia misingi demokrasia, uvunjaji wa haki za binadamu, upuuziaji wa dhana ya utawala bora na wizi wa fedha uliokithiri ukiongozwa na viongozi walio madarakani.

Mwenyekiti wa Taasisi ya uandishi wa Habri kusini mwa Afrika Tawi la Tanzania Bw. Ayoub Rioba katika mahojiano yetu alinieleza kuwa uchumi wa Afrika uko katika mikono ya wachache walioficha mabilioni ya fedha ughaibuni na kuitolea mfano DRC ilivyoongozwa na hayati Rais Mobutu Seseseko Kuku wa Zanga na nchi ya Nigeria yenye nishati ya mafuta lakini watu wake wako taabani.

Katika Afrika ni lazima mtawala mwadilifu asakamwe na ikiwezekana "auawe"ili kundi la mafisadi watimize azma yao kwa kuitafuna nchi kiulani.Mifano ya viongozi waadilifu waliopigania maslahi ya wananchi wao na kisha wakauawa wako wengi na wanafahamika.

Kwa Mtazamo wangu hafifu nazimithilisha Tume ya Jaji Mark Boamani, Dk Harisson Mwakyembe na Tume ya Musa Kipenka ni mfano wa "makafara " tosha ya kondoo weusi katika kuifikia dhamira inayokusudiwa ya kumtoa mtu mhanga.

Maelekezo ya awali ya Rais akimtaka Inspekta Jenerali Said Mwema, Mpelelezi wa Makosa ya Jinai Robert Manumba na Mkurugenzi wa Takukuru Bw. Edward Hosea kulishughulikia suala hilo kwa kina na kulichukulia uamuzi wa kisheria ulikuwa nimchakato wenye bashara ya matumaini, lakini matumaini hayo yanazidi kufifia siku hadi siku.

Lakini huu ukiwa kama mtazamo wangu Rais Kikwete akumbuke tu kuwa umma wa wananchi wa Tanzania kumpigia kura mwaka 2005 ni wazi umma ule ulikuwa na imani kubwa na yeye katika kuisafisha nchi.

Lazima tufike sehemu tukubali kuwa nchi yetu "imechafuka" licha ya kuwepo kwa amani, utulivu na umoja wa kitaifa, nchi yetu imechafuka na inahitaji kusafishwa.

Kuchafuka huku ni kutokana na kuibuka kwa matabaka ya "wachache" wenye nacho na wengi wanaoendelea kuzama kwenye umasikini wakutupwa.

Mwalimu Nyerere amekufa lakini watoto wake mathalani, John, Madaraka, na Andrew Nyerere ni watu wa kawaida na kama kuijua pesa na kutafuta miradi ya kujiendeleza kimaisha wameanzia ukubwani na si wakati Baba yao akiwa hai.

Leo watoto wa viongozi wa Tanzania ndiyo wanaoongoza kwa kuishi maisha ya kifahari na hawaonekani tena kusoma katika shule zilizojengwa kwa miradi ya MMEM na MMES.

Watoto hao wanasoma International Schools na wengine wakisoma vyuo vikuu nje ya Tanzania wakati watoto wa masikini wakibwia vumbi katika shule zisizo hata na maabara, achilia mbali posho hafifu ya wale walioko vyuo vikuu.

Taarifa ya uchunguzi ya Tasisi ya REDET chini ya Profesa Rwekiza Mukandala imeeleza bayana kuwa Rais Kikwete bado anaaminika na kukubalika na wananchi lakini sehemu kubwa ya Baraza lake la mawaziri halina "mashamsham" liko doro mithili ya togwa lililo lala. Maoni ya REDET yaliungwa mkono hata na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Siasa na Uhusiano wa Jamii Mwanasiasa Mhe Kingunge Ngombale Mwiru akisema "swadakta bin kudra" jambo ambalo limeashiria kugusa ukweli.

Mataifa kadhaa likiwemo Taifa la Amerika na baadhi ya nchi nyingi za ulaya zimeonyesha kumuunga mkono Rais Kikwete katika mikakati yake ya ujenzi wa nchi. Ji jambo zuri, ila Kikwete anapaswa kupimwa si kutokana na maelezo yake, matamshi yake, bali kwa vitendo na mafanikio atakayotekeleza.

Piga ua, ukiendaa vijijini (sehemu kama vile Charambe Pwani au Kamachumu Kagera) na kumuuliza mswahili wa kawaida, "unamuonaje Rais katika utendaji wake?"Jibu utakalopewa ni, JK bomba sanaaaa!

Bomba sanaaa? Kafanya nini hasa kinachokufanya useme, "JK ni bomba sanaaaa!"?

Wananchi visiwani bado wanakumbuka utendaji wa Rais wa kwanza wa Zanzibar Hayati Mzee Abeid Aman Karume kama kiongozi aliyekuwa na kiwango kidogo cha elimu lakini amefanya maajabu ambayo viongozi kadhaa hata baada ya kufa kwake miaka mingi iliyopita hawajaufikia utendaji na maono yake ya mbali.

Marehemu Edward Moringe Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu hakuwa na elimu ya mikogo lakini alikuwa mchapakazi hodari, mzalendo wa kweli na mtumishi aliyejituma na alikufa katika utata wa ajali akiwa masikini wakutupwa.

Mzee Ali Hassan Mwinyi aliwahi kumteua Bw. Augustine Lyatonga Mrema kuwa Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi. Utendaji wake ulionekana na kila mtu alitambua kuwa kuna Waziri anaitwa Mrema.

Bw. Mrema wakati ule alikuwa Afisa Usalama wa Taifa wa wilaya, lakini alipokabidhiwa dhamana kuwa waziri wa mambo ya ndani, alionyesha kuwa anamudu kazi hiyo, na ufanisi wake ulionekana waziwazi.

Majambazi na wahalifu sugu wao wenyewe walilazimika kurudisha silaha katika ofisi ya Bw. Mrema na uhalifu ulipungua kwa sehemu kubwa nchini. Lakini leo hii majambazi yanatamba na kuua watu wasio na hatia.

Mtazamo wangu Rais Kikwete anaweza kuwa na dhamira njema ya kweli katika kuibadili nchi hii, lakini swali la kujiuliza anaibadili nchi kwa kushirikiana na akina nani, wako wapi, wana usafi upi, na je hawahusiki katika masakata ya wizi na ubadhirifu ?

Tunashudia kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu kwamba halmashauri za wilaya nchini zinapekelewa mabilioni ya fedha za maendeleo hivi sasa kuliko katika wakati mwingine wowote uliopita katika historia ya Tanzania.

Hii yote ni kuonyesha kodi za mapato kwa umakini zinakusanywa na Rais kama kiranja mkuu wa nchi, huna budi kusafisha macho ili kuhakikisha kuwa mapato yanayokusanywa yanatumika vizuri kukuza na kuboresha huduma za jamii.

Mheshimiwa Rais Kikwete, lilikuwa jambo la umakini mkubwa kumtimua kazi Bw. Daudi Balali (marehemu) kutokana na taarifa ya Tume uliowasilishiwa ikulu kuhusiana na wizi wa mabilioni ya fedha kwenye akaunti ya malipo ya madeni ya nje (External Payment Arrears (EPA). Na unastahili pongezi kidogo kwa hilo [makofi, tafadhali]. Lakini si Balali peke yake aliyehusika na wizi huu/huo. Wapo viongozi wengi na wataalam wabovu, wezi na "walaji" wabaya kuliko mchwa. Hebu "wafyagie" wakae nje. Hebu tumia kofia yako ya urais kuhakikisha kuwa uzio na vyombo vinavyohusika vinatumika kuwafikisha mahakamani hawa mchwa ili wawajibishwe .

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.