OLE WAKO TANZANIA, NI NANI ATAKAYEKUSAIDIA?

Na, G: <03/30/10 >

Katika toleo la Alhamisi August 29, 2002 la mtandao wa madini (MiningWeb), kulikuwa na makala yenye kichwa kisemacho:- Tanzania - Africa's most attractive mining destination. Baada ya kusoma kichwa hicho nikajiuliza, je Tanzania inawavutia wawekezaji hawa kwa sababu tuna madini bora na mengi kuliko nchi nyingine yoyote ya Kiafrika, au inawavutia kwabababu wawekezaji hao wanadhani wanaweza kupata faida zaidi hapa nchini (kuliko sehemu yotote ile duniani) kutokana na sera mbovu za madini zilizopo? Baada ya kufanya utafiti kidogo, nimegundua kuwa wawekezaji hao wanakimbilia Tanzania kwasababu ya sera karimu za madini zilizopo pamoja na upeo duni wa viongozi wetu wasiojua kiundani kuhusu suala zima la madini na thamani yake katika soko dunia.

Katika kampeni ya uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi Tanzania mwaka 1995, suala hili lilitajwa sana na Wapinzani, kwamba mwaka 1994 Kenya ilipata zawadi ya ndege kwa kuuza Tanzanite nyingi kwenye soko la dunia. Tatizo ni kwamba, Kenya hawazalishi Tanzanite. Madini hayo hupatikana sehemu moja tu duniani--Tanzania. Sasa iweje wenzetu wazawadiwe kama wauzaji bora wa Tanzanite duniani hali madini hayo yanapatikana Tanzania peke yake?

Wakati swali hilo likiwa halijajibiwa, serikali ikaanza kampeni kubwa ya ubinafsishaji wa sekta ya madini kwa makampuni ya kigeni. Hilo peke yake halikuwa jambo la kushangaza. Jambo la kushangaza ilikuwa ni kasi, asili na mwenendo wa ubinafsishaji huo. Hadi leo hii, serikali bado haijatoa maelezo ya kutosha kuridhisha wananchi kwamba ni nini hasa kinaendelea katika suala zima la ubinafsishaji wa migodi yetu. Serikali bado haijaeleza kwa kina faida iliyopatikana kutokana na ubinafshaji huo.

Ingawa tunampenda na kumheshimu Rais mstaafu Mkapa, ilikuwa ni udhalilishaji mkubwa wa fahamu zetu pale serikali yake iliposema kwamba asilimia 3 ya mafao kutokana na mapato ya madini inatosha huku wakikataa ukweli kwamba wamekuwa wakarimu kupita kiasi kwa wawekezaji wa sekta ya madini toka nje.

Madai kwamba walilazimika kufanya hivyo ili kuongeza ushindani hasa kutaka kuzifikia nchi ambazo zimekuwa katika masoko ya madini kwa muda mrefu na wana miundombinu mizuri ya madini, ni utetezi unaostahili kupuuzwa. Tunachodhani ni kwamba: hatufikiii ushindani kwa kupunjwa, bali kwa kuingia kwenye soko la dunia la madini tukiwa na nidhamu binafsi pamoja na bidhaa bora. Viwango vya kimataifa vinakubali asilimia 3 ya mafao kwa mapato ya madini kati ya dola za kimarekani 10,000 hadi milioni moja. Ikizidi milioni moja, kiwango cha mafao kinaongezeka kufikia asilimia 5, hadi mapato ya dola milioni 5. Baada ya hapo kiwango kinaongezeka kwa asilimia 1 kwa kila ongezeko la mapato la dola milioni 5, hadi kufikia asilimia 12. Kwa hiyo kuweka kiwango kimoja kwa mapato yoyote, hasa kiwango chenyewe kinapokuwa cha chini, haitoshi. Na haya ni malipo ya aina moja tu; kwani wawekezaji hawa hawa wakienda nchi zizlizoendelea kama Canada, watatozwa mafao ya jumla. Kwamba, serikali kuu itawatoza kodi, na serikali za mitaa (ilipo migodi) pia itawatoza kodi. Iweje sisi tutoze mafao mara moja, tena ya kiwango cha chini mno?

Nikilitolea hilo mfano, kwa kanuni ya kutoza kiwango kimoja kwa mauzo yoyote yale, muwekezaji akifanya mauzo ya madini yanayofikia dola za kimarekani milioni 40, serikali itapata mafao ya dola za kimarekani milioni 1.2. Lakini tukifuata utaratibu huu wa kimataifa. Kwa mauzo ya madini yale yale ya thamani ya dola za kimarekani 40, (hayo ni mauzo ya kutosha kutoza kiwango cha juu kabisa ambacho ni asilimia 12) Tanzania ingejipatia, kwa halali kabisa bila kupunjwa na wekezaji, pato la dola za kimarekani milioni 4.8. Hii ni tofauti ya dola za kimarekani 3.6. Tunajua kwamba sheria ya madini inawatoza ada kadhaa za kupata leseni zao takribani dola 800 na tunajua wanakodisha maeneo hayo kwa ada inayofikia hadi dola 1500 kwa kilometer za mraba kwa mwaka. Lakini hapa tunazungumzia baada ya kupata vibali hivyo na kukodisha maeneo, uzalishaji wao pia unatakiwa kutozwa kodi na ushuru halali kwa biashara wanayofanya.

Swala jingine hapa ni kuhusu ahadi amabazo Rais Kikwete aliwaahidi watanzania wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi mwaka 2000. Ahadi za kupitia mikata yote ya madini na kurekebisha kasoro zilizopo. Tunashukuru kuwa tume ya Bomani imefanya kazi vizuri na kuwakirisha mapendekezo yake kwa Rais. Ni wakati sasa kwa mapendekezo yake kufanyiwa kazi ili pato halali la taifa linalotokana na madini liweze kupatikana kwa wakati husika.

Ingawa hakuna uwazi katika mikataba ambayo serikali imekwisha fanya na hao wawekezaji, mfumo wa makubaliano ya serikali na hao wawekezaji si wa kukubalika kabisa. Kwa namna Fulani makampuni hayo yalifanikiwa kushawishi serikali kupewa muda wa kufanya utafiti, na muda wa kurudisha gharama za uwekezaji wao, kabla hawajaanza kutozwa kodi na ushuru unaotokana na uchimbaji wao. Kwa mfano, kampuni inawekeza kufanya uchimbaji mkubwa huko Mwaduina kupewa miaka mitano ya kufanya utafiti. Ingawa hatujui kwa nini wafanye utafiti wakati Mwadui ni mgodi ambao tayari ulishahakikiwa kutoa Almasi safi, lakini kampuni hili inapewa miaka mitano kufanya utafiti huo. Na katika miaka hiyo mitano, bila usimamizi wowote, wanaendelea kuchimba na kupeleka “SAMPLE” (Hapa yabidi nitumie neno rasmi, bila hata ya kulitafsiri na kuliweka kwa herufi kubwa maana walakini mkubwa wa hii mikataba uko kwenye hizi “SAMPLE”) huko Afrika Kusini. Ukweli ni kwamba ingawa mimi si mtaalamu wa madini na sijui ni "SAMPLE" nyingi kiasi gani makampuni haya yanahitaji kuhakikisha kwamba haya madini yanayotoka Mwadui ni Almasi, ila hata mimi nisiye mtaalam, sidhani kwamba wingi wa "SAMPLE" hizo unaoondoka Mwadui kila siku wote (if at all) ni "SAMPLE" tu.

Kama hulifahamu hili mheshimiwa waziri, kuna kiwanja kidogo cha ndege hapo Mwadui, na kila siku inayopita shehena kadhaa ya "SAMPLE", inarushwa toka Mwadui kwa ndege kadhaa ambazo hazisimami mahali pengine popote. Ni kuja Mwadui, kuchukua "SAMPLE" na kurudi Afrika Kusini. Ndege hizi hufanya safari kadhaa kwa siku na wakati wa kufunga na kusheheni "SAMPLE" hakuna mzalendo anayeruhusiwa kuwepo eneo hilo. Kampuni imeajiri wataalam wa madini kadhaa na wanalipwa fedha nyingi tu. Lakini pale utaalamu wao unapohitajika, yaani kwenye ukaguzi wa "SAMPLE" eti wanazuiwa kushiriki? Ni nini ambacho wawekezaji hawa hawataki wataalam wa kizalendo waone? Yawezekana "SAMPLE" hizi zimekuwa nyingi zaidi ya mahitaji ya yakwaida ya sample. Sasa fikiri kampuni imepewa miaka 5 au 10 ya kufanya utafiti na kila siku ndege kadhaa za mizigo zikiwa zimejaa shehena ya "SAMPLE" zinaondoka. Baada ya miaka 10 ni "SAMPLE" kiasi gani hiyo ambayo imepatikana bila kutozwa kodi wala ushuru wa namna yeyote, na bila hata kukaguliwa kuwa ni kiasi gani kimeondoka ??? Na hili si Mwadui tu, bali na sehemu zingine za migodi kama Geita, Bulyanhulu n.k.

Kana kwamba hiyo haitoshi, baada ya miaka ile ya awali ya "SAMPLE", mikataba inayapatia makampuni haya muda mwingine sawa na ule wa kwanza wa kuchimba migodi bure, ili kurudisha gharama zao za uwekezaji. Hatuna ugomvi na makampuni kurudisha gharama zao, lakini faida ya biashara yao ndiyo itarudisha gharama zao, ndiyo maana biashara zinahitaji mitaji. Na kama serikali inaona vyema kuwasaidia ingewapunguzia kiwango cha kodi na si kuwapa miaka mitano au 10 ya kuchimba bure kwa madai kwamba wanarudisha gharama zao wakati walisharudisha gharama na kupata faida wakati wakichukua "SAMPLE".

Tuchukulie Tanzanite, kwa mfano, ambayo tunajua haina chanzo kingine chochote duniani isipokuwa Merelani, Tanzania. Kila mwaka Marekani peke yake inanunua Tanzanite yenye thamani zaidi ya dola za kimarekani milioni 400. Lakini takwimu za serikali zinaonyesha kwamba mwaka jana Tanzania iliuza Tanzanite yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 16 tu. Sasa tikifanya kana kwamba Marekani pekee ndiyo inanunua Tanzanite, kitu ambacho si kweli na kwamba Tanzanite Tanzania iliyouza, iliiuzia Marekani, tunaona kiujumla Tanzania iliuza asilimia 4 tu ya Tanzanite iliyonunuliwa Marekani. Swali ni kwamba hiyo asilimia 96 ya Tanzanite Marekani iliyonunua, ilitoka wapi wakati hakuna chanzo kingine chochote cha Tanzanite duniani isipokuwa Tanzania?

Na hili ni kiwango cha chini sana kwani Marekani si mnunuzi pekee wa Tanzanite. Kuna nchi nyingine nyingi zinazonunua Tanzanite, na hayo mauzo ya Dola milioni 16 tuliyopigia mahesabu ni mauzo ya nje ya ujumla ya Tanzanite yaliyotolewa taarifa na serikali, si yale tu yaliyouzwa Marekani. Kwa hiyo ukipata takwimu zote na kuangalia ukweli halisi wa mambo utaonyesha matokeo mabaya zaidi. Je, yawezekana kwamba tunazalisha "SAMPLE" asilimia zaidi ya 96 na Tanzanite inayotozwa ushuru na kodi ni pungufu ya asilimia 4 tu? Je, hii ni halali kwa uchumi wa taifa letu kwamba madini mengi zaidi karibu asilimia 100 yanauzwa nje bila ridhaa na ufahamu wa serikali? Nauliza hili kwa sababu hili halitokei kwa Tanzanite peke yake, inatokea kwa madini mengine yote tunayozalisha, dhahabu, shaba, zinc, almasi n.k. Ila ni rahisi kulielezea kwa mfano wa Tanzanite maana haina chanzo kingine chochote isipokuwa Tanzania, hivyo Tanzanite yoyote itakayopatikana mahali popote huko duniani ni lazima kwa namna moja au nyingine (SAMPLE au siyo SAMPLE) ni lazima iwe imetoka Tanzania.

Mheshimiwa Rais, hatutaki kuonekana kana kwamba tunaipinga serikali, la. Ila tunajua kwamba serikali inaongozwa na binadamu kama sisi, na binadamu hukosea. Kwa hiyo tunalojaribu kufanya ni kukufahamisha wewe na jamii kwa ujumla nini kinachoendelea, na kwa sababu ya dhamana yako kubwa, na mamlaka yako kiutendaji, tunakusihi kwamba ulizingatie suala hili na kuona linabadilishwa na kuhakikisha kwamba biashara ya madini inafanywa kwa uwiano mzuri bila kuwaumiza wawekezaji, lakini zaidi sana bila wao kutunyonya.

Kulingana na makala ya hivi karibuni ya gazeti la Washington Post, sekta ya madini itachangia zaidi ya dola za kimarekani Billioni moja (inayoanza na B siyo M) kwa mwaka kwa pato la taifa kutokana na kodi, mafao, ushuru n.k . Hii ni baada ya miaka mitano ya kutuibia kupitia kisingizio cha "SAMPLE". Na yawezekana huu ni wakati ambao makampuni haya sasa yataanza kutozwa kodi baada ya miaka kadhaa yakuchimba bure kwa kisingizio cha kurudisha gharama zao.

Ukweli ni kwamba hatuna hakika kwamba baada ya kunyonya nchi yetu kwa miaka yote hiyo, bado wawekezaji hao watadhani kwamba kuna madini yaliyobaki ya kutosha kwao kutulipa dola Billioni moja kwa mwaka. Wanaweza kusema "SAMPLE" hazikuwa nzuri na kuondoka. Tutawafanya nini? Na watakuwa wamechimba madini mengi, mengi sana kutoka katika migodi yetu kwa miaka mingi BURE. Ndiyo, bure bila ya taifa kupata manufaa yoyote.

Kwa nini lakini, mheshimiwa Rais, tusikatae huu unyonyaji na kuanza, ingawa tumechelewa, kupata pato hili mwaka huu? Sekta ya madini ambayo kwa takwimu za mwaka 1998 imekua kwa asilimia 17, lakini kufikia mwaka 1999 imekua kwa asilimia 27 na wizara ya madini ilikadiria kwamba mikataba yote itakapopevuka na makampuni yote kuanza kutozwa, sekta ya madini itachangia asilimia 10 ya pato la taifa kufikia mwaka 2025. Kwa nini tusikomeshe unyonyaji huu na kuongeza pato la taifa leo kwa manufaa ya taifa na si kusubiri mwaka 2025 ambapo wengi wetu hatutaona matunda ya rasilimali hizi nzuri na muhimu kwa taifa?

Tunaamini Mheshimiwa Rais utafanya kila lililo ndani ya uwezo wako kulichunguza hili na kulifanyia kazi kuhakikisha kuwa hatuendelei kutawaliwa na kunyonywa na nchi zilizoendelea. Lau sivyo, hutakiwi kupewa idhini ya kurudi ikulu ya magogonikwa mika mitano mengine..

.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.