SERIKALI HAIFANYI BIASHARA, SERIKALI INAKUSANYA KODI

Na, G <First posted: 04/21/06 >

Kama maendeleo ya nchi yangekuwa gari, basi wizara ya fedha ingekuwa injini, chombo ambacho ni muhimu sana katika kuendesha gari hilo. Kutegemea na gia inayoendesha gari hilo, waziri wa fedha na timu yake ikiwemo mamlaka ya kukusanya mapato (TRA) wana sehemu kubwa sana kuamua katika mipangilio na sera za kiuchumi za nchi kwamba gari hili la uchumi wa Tanzania linaenda mbele au linarudi nyuma.

Kwa muda mrefu nchi yetu imekuwa mstari wa nyuma katika maendeleo ya uchumi kwa sababu tulikumbatia mfumo usio sahihi wa kiuchumi. Kwa hili simaanishi mfumo wa ujamaa, ingawa nao ulitugharimu. Ila namaanisha mfumo wa uchumi wa biashara huria. Ukweli usiopingika ni kwamba uchumi wa nchi yetote ile duniani unategemea kwa kiwango kikubwa jinsi ambayo serikali ya nchi husika, inavyojishughulisha katika suala zima la uchumi, nikimaanisha ukusanyanji wa mapato kwa njia ya kodi na nidhamu ya kifedha katika kutumia mapato hayo. Kimsingi serikali haifanyi biashara. Serikali yeyote ili kuweza kuendelea haitakiwi kufanya biashara yoyote. Serikali inahusanya kodi. Hivyo mfumo bora wa uchumi ni ule ambao chanzo kikubwa kama siyo pekee cha mapato ya serikali ni kodi inayotoza raia wake, makampuni, wawekezaji, na biashara zingine zinazofanyika chini ya mamlaka ya serikali.

Serikali ya awamu ya tatu ilianza kuliona hili na kwa kiwango kidogo kuanza kuiondoa serikali katika biashara kwa kubinafsisha mashirika ya serikali na kujenga mfumo wa kodi madhubuti ambao ungehamasisha maendeleo ya uchumi wa nchi. Na tumeona hatua kubwa na nzuri ambayo serikali ya awamu ya tatu ilifikia. Ila hatua walizochukua, yawezekana kwa kutotaka kufanya mabadiliko ya ghafla, haikutosha, ilitakiwa serikali kujiengua kabisa katika kufanya biashara na kuelekeza nguvu zote katika huduma za jamii na ukusanyaji wa kodi. Kulingana na taarifa ya maendeleo kusini mwa Afrika , mfumo huu wa serikali na taasisi tanzu za serikali kukiritimba biashara umerudisha nyuma na kudhoofisha sana sekta binafsi ambayo kimsingi ndiyo iliyotakiwa kufanya biashara na kulipa kodi.

Kulingana na taarifa hiyo ya maendeleo ya kusini mwa Afrika, mfumo wa uchumi wa nchi nyingi za Afrika haujabadilika sana kutokana na mchango wa sekta mbali mbali kwa uchumi wa taifa. Ingawa kilimo bado kitaendelea kuwa uti wa mgongo wa taifa letu, lakini kumetokea sekta nyingine kama madini, viwanda na huduma ambazo zinafanya vizuri na kuchangiakwa kiwango kikubwa katika uchumi wa taifa letu ingawa sera ya uchumi ya taifa haijabadilika kuakisi mabadiliko haya. Mathalani, ukilinganisha sekta ya kilimo, viwanda na huduma kama asilimia ya uchumi wa taifa (GDP) au asilimia ya ukuaji kila mwaka, kati ya mwaka 1992, 2001, na 2002, ni sekta ya huduma peke yake ambayo imeonyesha ukuaji dawamu. Kwa hiyo serikali inapaswa kuanza kuweka sera za uchumi ambazo zitazipa hizi sekta zingine kama madini na huduma kipaumbele kama ambavyo inaipa sekta ya kilimo kipaumbele. Hii haina maana ya kupuuzia sekta nyingine ila hoja hapa ni kwamba sera za uchumi zinatakiwa ziakisi hali halisi ya mwenendo wa maendeleo ya kiuchumi. Ingawa serikali haitakiwi ifanye biashara lakini serikali ndiyo inayounda sera za uchumi zinazotawala biashara na huduma mbali mbali.

Kuna msemo wa zamani wa kiingereza unaosema "What good is the sheep, if not for shear." Msemo huu ni msemo wa wafugaji kwamba wanapokuwa wanafuga mifugo yao kawaida wanahudumia mifugo yao kwa kuipa chakula, kuipatia mahali pazuri na salama pa kuishi, kuipatia mifugo yao maji safi na tiba pale mifugo inapopata magonjwa na huduma nyingine nyingi kwa sababu wana lengo moja tu kwamba mwisho wa siku kama ni kondoo wataenda kukatwa manyoya na wao kupata fedha kwa kuuza sufu. Kama ni ng'ombe watatoa maziwa au kuchinjwa na wafugaji kupata fedha kutokana na mauzo ya maziwa au nyama. Swala la msingi hapa ni kwamba wafugaji hawa waliitunza mifugo yao na kuipatia mahitaji yote ya muhimu ili mifugo iweze kunenepa na kunawiri hatimaye kutoa kama ni sufu, nyingi na nzuri. Kama ni maziwa mengi na bora, kama ni mayai mengi na makubwa, kadhalika nyama na mazao mengine ya mifugo.

Dhana hii ndiyo wizara ya fedha inatakiwa kuzingatia. Serikali inapaswa kuhudumia na kuneemesha wananchi wake ili kwamba wakati wa kutoza kodi, wananchi wawe na kodi ya kulipa kama ni kodi ya mapato, kodi ya mauzo, kodi ya ongezeko la thamani, ushuru wa forodha na aina zingine zote za kodi serikali inayotoza. Na kufanya hivi kwa mtazamo wa wafugaji ni kwanza kujenga mazingira ambapo wananchi watakuwa na mapato kwanza kama ni kazi wapate kazi, kama ni biashara wafanye biashara au mapato mengine yoyote yale, ndipo mapato hayo yatozwe kodi. Dhana hii ya kuondoa serikali katika biashara haimaanishi kuinyima serikali kipato, La! Ila ni kuwaacha wananchi wafanye biashara na serikali kupata mapato yake kutokana na kodi itakayowatoza wananchi wake na biashara zao. Kimsingi ni kwamba serikali kwa kufuata sera za wizara yako ijenge mazingira ambayo wananchi wake watafanikiwa katika shughuli zao za maendeleo na kupata kipato ambacho kitawanufaisha na hatimaye kuneemesha serikali kwa kuwatoza kodi muafaka kulingana na shughuli zao za kiuchumi.

Jambo la kwanza la msingi ambalo unaweza kufanya ili kuneemesha watu wako kabla ya kuwatoza kodi ni kuweka sera za kuongeza ajira ili watu wengi iwezekanavyo wawe na kazi. Kwa sababu wote tunajua ajira za serikali na idara zake zimeshajaa, na kwa sababu tumeshaona ukuaji dawamu katika sekta ya huduma, wazo kubwa linalokuja mawazoni ni wizara husika kuona namna ya kupanua sekta hii kuongeza ajira nchini. Mathanalani, wizara ya fedha inaweza kuanzisha benki maalum za mikopo ya masharti na riba nafuu kuwawezesha wananchi kupata mitaji ya kuwekeza na kuajiri katika sekta ya huduma au sekta nyingine yeyote wanayoona vyema. Hii itawezesha watu kuanzisha biashara ndogo ndogo, za wastani, na kubwa, ambazo siyo tu zitawapatia wao mapato, bali pia zitawawezesha kuajiri wasaidizi na hii kuongeza idadi ya ajira nchini.

Unaposhughulikia watu binafsi kupata kipato, usisahau pia kushughulikia waajiri wao na wafanyabiashara wengine. Tanzania inawekwa katika kundi la nchi zinazotoza kiwango cha juu zaidi cha kodi duniani. Na hili linakwamisha wananchi wengi iwezekanavyo kuwekeza na linarudisha nyuma ari ya wawekezaji kutoka nje kuwekeza katika biashara mpya zitakazoongeza nafasi za ajira nchini [Kulingana na taarifa inayotazama mfumo wa kodi nchini] Na hili linasababishwa na matatizo makubwa mawili.

Kwanza mianya ya kodi. Kuna mianya mingi ya kodi ambapo watu wengi wanaweza kwa namna moja au nyingine kukwepa kodi na kwa sababu serikali inahitaji kiwango fulani cha mapato basi mzigo wote wa mahitaji ya mapato ya serikali unawaangukia na kuwalemea walipaji wachache waaminifu. Waaminifu hawa wachache wanatozwa kodi nyingi sana na kwa viwango vya juu ili kukidhi haja ya mapato ya serikali kuu na serikali za mitaa. Taarifa hiyo ilichunguza mamlaka za miji 50 na kugundua walikuwa na aina 10 za kodi, aina 18 za leseni wanazotoza wafanyabiashara wao, aina zingine 41 za ada na vyanzo vingine 16 vya mapato, hii ni baada ya kulipa kodi, ada, na kupata vibali vya serikali kuu. Hii inaumiza wafanyabiashara na wawekezaji hawa wachache.

Tatizo la pili ni misamaha ya kodi kwa wawekezaji wapya. Hili nalo linasababishwa uwiano usio sawa wa mzigo wa kodi ambapo, wawekezaji wakubwa ambao wangeleta kipato kizuri, wanapewa msamaha wa kodi na kurudisha mzigo huu wa kodi kwa wale wachache waaminifu wanaolipa na kufanya kodi zao kuwa juu. Hili ni baya zaidi kwani wawekezaji hawa wanaopewa misamaha ya kodi wengine wao (kama siyo wote) wanatumia mwanya huu kukwepa kodi kwa kubadili majina. Kwa mfano hoteli ya Sheraton inapewa msamaha wa kodi kwa miaka kadhaa kwa sababu ni wawekezaji wapya. Baada ya muda ule wa msamaha kuisha wanafanya kana kwamba wamefunga biashara na kubadili jina la hoteli kujiita Royal Palm na kuonekana kana kwamba ni wawekezaji wapya na kupewa tena msamaha wa kodi. Muda ukiisha wanajibadilisha jina tena na Kuitwa Movin Pick na mchezo unaendelea hivyo hivyo. Na huo ni mfano mmoja tu ila wawekezaji wa aina hii wako wengi na wataendelea siku zote kuonekana kana kwamba ni wawekezaji wapya mradi tu wanakumbuka kubadili majina kwa wakati. Taarifa iliyochunguza ukwepaji na misamaha ya Kodi Tanzania na Madagascar inaonyesha hasara serikali iliyopata mwaka 1994/5 kutokana na ukwepaji na misamaha ya kodi ni kubwa sana!

Kwa hiyo, ili kulinda wafanyabiashara wetu na wawekezaji waaminifu wanaotengeneza ajira nchini, inapaswa serikali kupitia wizara ya fedha na na mamlaka za kodi nchini kuziba mianya ya kodi, kutoza kodi wawekezaji wote hasa wale wajaja wanaocheza mchezo wa kihuni kwa kutaka waonekane kuwa wapya kila siku. Ushahidi unaonyesha kwamba kama bajeti ya serikali itabaki vile vile na misamaha ya kodi ikishughulikiwa na wakwepa kodi kutozwa, ikiwa na maana kila anayepaswa kulipa kodi akitozwa kodi, kiwango cha kodi watakachotozwa kitakuwa kidogo sana. Hili litawezesha serikali kupunguza idadi na viwango vya kodi, hili kupelekea wawekezaji na wafanyabiashara ambao wamebeba mzigo wa kodi kwa taifa zima kwa muda mrefu waweze kuongeza mhimili wao wa faida na kupanua utendaji wao na biashara zao, hili litaongeza ajira hatimaye kuiongezea serikali kipato kwa ongezeko la ukubwa wa biashara na ongezeko la idadi ya watu wanaolipa kodi kutokana na ajira hizi mpya. Viwango vya chini vya kodi pia vitahimiza hata wawekezaji wengine kutoka nje kuja kuwekeza na labda hata kuhimiza wale wakwepa kodi ambao labda wanakwepa kutokana na ukubwa wa kodi, kulipa kodi. Ukweli ni kwamba kama mzigo wa kodi utagawanywa sawa sawa kwa wananchi na wafanyabiashara wote, kiwango cha kodi kitapungua kwa kiasi kikubwa.

Nchi nyingi duniani na hata mamlaka za miji ya nchi zilizoendelea katika juhudi ya kuboresha afya ya raia wao na kuongeza kipato, wameanzisha kodi inayojulikana katika nchi za magharibi kama kodi ya dhambi. Hii ni kodi ya ziada inayotozwa katika tumbaku na mazao yake kama sigara, na pia inatozwa kwa pombe. Serikali na mamlaka zake zinajaribu kuhimiza wananchi waache matumizi ya sigara na pombe kwa afya zao na wale wanaoamua kuendelea basi wanalipia kodi hii ya dhambi kila wanaponunua sigara na pombe. Na kwasababu viwanda vya sigara na pombe ni moja ya viwanda vinavyofanya vizuri zaidi nchini, kama ukiona vyema, waweza kuanzisha kodi hii maana una hakika kuwa itaongeza pato la serikali kwa kiwango viwanda hivyo vinavyokua.

Tunaamini wizara ya fedha na mamlaka za kukusanya mapato zina timu nzuri ya watendaji na tunaamini watafanya yote yaliyo ndani ya uwezo wako kupanua mazingira ya ukuaji wa uchumi wa taifa letu na kuwianisha bajeti ya serikali ili kupunguza utegemezi wetu wa misaada ya nje. Hatimaye kuboresha maisha ya kila mtanzania.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.