PROF. MWAKYUSA, SEKTA YA AFYA NCHINI IPEWE KIPAUMBELE

Na, G <bongotz.com>

Kwa muda mrefu sasa Tanzania imekuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa wauguzi, wauguzi wasaidizi, manesi, wafamasia na watendaji wengine katika sekta ya afya. Kwa hiyo wito wetu wa kwanza mheshimiwa waziri ni kwa wewe binafsi kuanza kulishighulikia tatizo hili kuhakikisha kwamba: wanafunzi walioko mashuleni, wanashawishiwa na kuvutiwa kuchukua masomo ya sayansi ya utabibu na kuchagua yeyote kati ya nafasi nyingi zilizopo katika sekta ya afya ili kuwa waganga, waganga wasaidizi, manesi, wafamasia n.k.

Wanapochagua hili, mfumo unatakiwa uwekwe ili kuhakikisha kuwa wanaelimishwa vizuri na kwa haki katika vyuo vyetu vinavyoelimisha watumishi wa sekta ya afya na hata wengine kupewa nafasi kwenda nje kupata elimu ya juu zaidi ya maswala ya afya.

Wanapohitimu na kupata kazi katika sekta hii muhimu ya afya, basi serikali ihakikishe kwamba wanalipwa vizuri kiasi cha kuridhisha ili kwamba waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi bila kuwa na wasiwasi wa kutokumudu maisha. Hili ni muhimu sana maana kama hawaridhiki na wanaamua kugoma madhara yake ni makubwa zaidi. Wafanyakazi wa sekta zingine wakigoma, utendaji na uzalishaji unapungua au kusimama, wafanyakazi wa sekta ya afya wakigoma, watu wanakufa.

Mheshimiwa waziri, serikali inatumia gharama nyingi saaaaana kuhudumia na kutibu wagonjwa kwa magonjwa na matatizo yasiyo ya lazima. Hivyo tunakushauri kama ukiona vyema uangalie namna ambayo pamoja na mambo mengine, utaielekeza serikali kuwekeza katika kuelimisha maafisa wengi iwezekanavyo wa afya ya umma ili kwamba waweze kuelimisha jamii kuhusu usafi binafsi na kanuni za asili za kuzuia magonjwa. Waswahili husema kuzuia ni bora kuliko kutibu. Kwa hiyo serikali ikielimisha maafisa afya ya umma wengi, wataelimisha jamii namna ya kuzuia magonjwa na matatizo mengi yasiyo ya lazima na mwishowe, serikali itakuwa inaokoa fedha nyingi sana zinazotumika kutibu magonjwa kama kipindupindu.

Maofisa hawa wa afya ya umma wawe ni kitovu cha kuelimisha jamii na wasambazwe nchini kote katika hospitali na zahanati za serikali na hata zile za binafsi na za mashirika ya dini, ili watumie kila nafasi wanayopata kufikia jamii, kuielimisha jamii namna ya kuepuka magonjwa yanayosababishwa na kutokuwa waangalifu wa kanuni za msingi za afya.

Wananchi wafundishwe kunawa mikono kabla ya kula na baada ya kutoka msalani. Wafundishwe kuosha vyakula vinavyoliwa bila kupikwa.

Wananchi wafundishwe kula chakula bora na kuhakikisha uwiano wa lishe katika kila mlo wanaokula. Najua kama tabibu, wewe unafahamu hili na zaidi, lakini wananchi si wengi wanaofahamu hili. Katika nchi za magharibi ingawa wananchi wao wameelimika kuliko sisi, lakini bado wanawasaidia wananchi wao kujua namna ya kupanga lishe yao. Kwa hiyo wanaandaa kitu wanaita “Pembetatu ya Chakula (Food Triangle)” inayoshauli wananchi wao kwamba katika mlo wa kila siku ili kuwa na afya njema unatakiwa ule takribani protini kiasi gani, vitamini kiasi gani, wanga kiasi gani, hamirojo kiasi gani, n.k. na kwa sababu wengine ukiwaambia tu wanga wanaweza wasijui ni vyakula gani vina wanga. Katika pembetatu zao za vyakula wanatoa mifano ya makundi ya vyakula wanavyoshauri. Na kulingana na mabadiliko ya ugunduzi na maendeleo ya afya, pembetatu hizi za vyakula, zinakua zinapitia kila baada ya miaka kadhaa kama mitano au kumi kufanya marekebisho yanayohitajika. Hivyo tunakuomba mheshimiwa waziri uiagize wizara yako kushirikiana na shirika la chakula na lishe, kuandaa mwongozo au mpango wa chakula cha kila siku ambao mwananchi wa kawaida anaweza kuutumia kupanga mlo wake.

Watanzania kwa msisitizo mkubwa toka kwa maafisa afya ya umma, wafundishwe kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi. Wewe unajua umuhimu wa mazoezi jinsi yanavyosaidia kuimarisha kinga ya mwili, kusaidia moyo, usambazaji wa damu na hata kusaidia ubongo kufanya kazi vizuri zaidi. Kama ukianza hili mapema utaweza kusaidia taifa kuepuka janga kubwa na kitumbo (obesity). Nchi za magharibi zinatumia fedha nyingi sana kujaribu kusaidia raia wao kupunguza uzito. Kwa hiyo kama Tanzania itaanza kulishughulikia hili mapema na kufunza maafisa afya ya umma na wao kuelimisha wananchi na kusaidia wananchi kutokuzidi uzito, itaokoa fedha nyingi mbeleni ambazo zingelazimika kutumika kusaidia watu wenye uzito mkubwa na matatizo yanayotokana na uzito huo kama magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, n.k.

Unywaji wa maji ni eneo lingine ambao maafisa afya ya umma wa serikali wanaweza kusisitiza kwa wananchi. Wananchi wachemshe maji ili kuepusha kunywa maji yenye vijidudu vya magonjwa. Na pia wafundishwe kunywa maji mengi ya kutosha maana sehemu kubwa ya miili yetu kama ujuavyo ni maji.

Mungu ametujalia pia kuwa na neema ya jua. Inawezekana kwa wengi wa wananchi hili sio tatizo, ila kutokana na maendeleo ya kiuchumi nchini, kumekuwa na jamii ya watanzania ambao wanafanya kazi zinazowagharimu muda wao mwingi kiasi kwamba wanaingia ofisini kabla jua halijachomoza na kutoka jua limeshakuchwa. Waelimishwe na wao kutumia muda kidogo hata mwisho wa juma kuota jua.

Wizara au shirika la chakula na lishe au wote kwa kushirikiana wakishateng'eneza pembetatu ya lishe, maafisa afya ya jamii wafundishe wananchi pia kwamba hata vile vyakula vizuri kwa mpango huo mzuri ulioshauriwa, bado inabidi wawe na kiasi maana kila kitu kikizidishwa, kina madhara. Kwa hiyo chakula bora kikiliwa bila kiasi kinaweza kikawa na madhara pia.

Serikali pia iangalie namna ya kuwezesha wananchi kupumua hewa safi. Hili ni jukumu la serikali maana uchafuzi mwingi wa hewa unaweza kudhibitiwa na serikali kama kudhibiti kiwango cha hewa taka (Exhaust gases) zinazosababishwa na viwanda, mashine na magari. Labda kugawa maeneo ya viwanda mbali na maeneo ya makazi.

Wananchi wafundishwe pia kupumzika maana katika shughuli zetu za kila siku kuna chembehai nyingi zinazokufa, na ingawa miili yetu inaweza kuzalisha chembehai nyingine badala ya zile zilizokufa, kazi hiyo hufanywa kwa ufanisi zaidi tukiwa tumelala.

Utafiti mwingi uliofanyika nchi za magharibi umegundua tofauti kubwa na kiwango cha uponaji kwa wagonjwa wenye matumaini hasa wale walio na imani Fulani. Utafiti huo unaonyesha hasa wagonjwa wale walioombewa walikuwa na kiwango kikubwa zaidi cha uponaji zaidi ya wengine. Kwa hiyo maafisa afya ya umma waweza kuelimisha na kuhimiza wananchi kuamini nguvu Fulani ya juu inayoweza kuwasaidia wakati wa mahitaji.

"Laughter is the best medicine," yaani kicheko ndiyo tiba bora zaidi, ndicho kichwa cha taarifa ya utafiti mwingine uliofanywa juu ya hali za watu. Utafiti huo ulionyesha kwamba watu wenye furaha na wenye watu wa kuzungumza na kufurahi nao, wanakuwa na afya njema zaidi ya watu wenye huzuni wakati wote. Hivyo wananchi wetu wafundishwe kujizoeza kushiriki, kufanya na kujihusisha na mambo yale yatakayowafurahisha ili kuboresha afya zao.

Ingawa hili laweza kuathiri pato la taifa lakini kwa sababu kazi yako mheshimiwa waziri ni kuboresha afya na ustawi wa jamii ya watanzania, unaweza kujitolea kusimamia elimu ya umma kuhusu madhara ya tumbaku, vileo na madawa ya kulevya. Ingawa sigara hupatia taifa pato kubwa lakini ni vyema wananchi waelimishwe madhara yatokanayo na sigareti kwa wao binafsi na wengine wanaozunguka wanaoathiriwa na uvutaji wao bila hiyari. Vivyo hivyo kwa pombe, na pia sheria zitungwe na zilizopo kutekelezwa kuhakikisha hakuna madawa ya kulevya yanayoingizwa na kutumiwa nchini.

Lengo kubwa mheshimiwa waziri liwe kuboresha kwa kiwango cha juu kabisa hali na huduma ya afya nchini. Wakati huo huo kupunguza gharama ya kutoa huduma hiyo kwa kuondoa gharama zisizo za lazima za kutibu magonjwa yanayozuilika. Na hili linapotendeka na wananchi watakapoelimika, basi uwiano wa watumishi wa afya na idadi ya wananchi itaboreka na kuongeza matazamio ya maisha (Life expectancy) ya watoto wanaozaliwa Tanzania.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.