KAMA NINGEKUWA RAIS WA TANZANIA

Na,Magabe Kibiti < Posted on: 04/16/07>

Miezi michache kabla ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa 1995, zaidi ya watanzania 15 walikuwa wamejitokeza kugombea hii nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa serikali ya nchi kwa tiketi ya CCM peke yake. Wingi huu wa wagombea ulianzisha maswali mengi kichwani mwangu kuhusu mwelekeo na hatima ya Tanzania hasa ukichukulia kwamba umri wangu ulikuwa bado hauniruhusu kupiga kura. Swali la msingi lililoisumbua sana akili yangu ni namna ya kupima kiwango cha uelevu wa wapiga kura ili kuhakikisha kwamba wanamchagua Rais wa nchi ambaye wana uhakika kuwa ataiongoza nchi vyema na kuwa wakili mwema wa mali na maliasili za nchi.

Kabla sijapata jibu la swali langu la msingi, nilijikuta nikijiuliza swali la nyongeza ambalo nalo lilionekana gumu vilevile. Hadi leo imekuwa vigumu kwangu kujibu kwa hakika swali hili la kuhusu uwezo wa Rais na baraza lake la mawaziri wa kuwaletea wananchi maendeleo. Labda hii ndio sababu iliyonifanya nisishangae sana kuona zaidi ya watanzania 15 wakijitokeza kugombea uraisi wa Tanzania kwa tiketi ya CCM pekee mwaka 2005. Sio nia ya makala hii kuichambua serikali ya awamu ya tatu na ya nne na kutoa hitimisho kuhusu uwezo wa serikali hizi wa kuongoza, nia ya makala hii ni kuuliza swali la msingi na kulielekeza kwa watanzania wenzangu wanaofikiria au wanaopanga kugombea urais wa Tanzania.

Katika makala zangu zilizopita, nimesisitiza haja ya wananchi kuwa na fikara huru (free minds) ili kujiletea maendeleo yao. Nimesisitiza pia haja ya wananchi kuacha tabia ya kuomba misaada au kubweteka huku wakisubiria serikali za nje ziwaletee maendeleo. Nimesisitiza pia haja ya vijana kuacha kukaa vijiweni huku wakisubiri viongozi wao wa serikali wawaletee maendeleo. Naomba msomaji uendelee kutambua kuwa bado sijabadili msimamo huu na sio nia ya makala hii kumtaka Rais wa nchi atuletee maendeleo. Swali la msingi hapa ni kuwa; je ni kwa kiwango gani Rais wa nchi anakubaliana na ukweli kuwa serikali ya nchi inaajiriwa na wapiga kura wa nchi hiyo? Ni kwa kiwango gani viongozi wengine wa serikali wanautambua ukweli kuwa wameajiriwa na wapiga kura na walipa kodi?

Nikiwa bado natafuta maswali ya majibu haya, nimeamua kuanzisha mjadala mwingine kichwani mwangu. Ninaisumbua akili yangu ijibu swali kuwa; kama mimi ningekuwa Rais wa Tanzania, je ningeifanyia nini nchi yangu na wapiga kura walioniajiri kuwaongoza? Ingawa najua kuwa katiba ya nchi hainiruhusu kugombea au kuwa Rais wa Tanzania kutokana na umri wangu wa sasa, hata hivyo bado nitaendelea kuuliza hili swali na kujaribu kulipatia majibu hadharani kwa matumaini kuwa mtanzania mwenzangu atakayefanikiwa kuwa Rais wa Tanzania kwa miaka ijayo atayatumia au atatafuta majibu yake mwenyewe.

Kama ningekuwa Rais wa Tanzania:

1. Ningehakikisha kuwa barabara ya Dar-Mwanza imejengwa kwa lami kurahisisha usafiri na kuunganisha zaidi ya raia millioni kumi wa nchi yangu kabla sijatumia mabilioni ya pesa kununua mashangingi kwa ajili ya wabunge na viongozi wa serikali.

2. Ningehakikisha kuwa miundombinu ya kisiwa cha Pemba ni ya kiwango cha kuridhisha kabla sijatumia mabilioni kujenga majengo mawili mapya ya bunge.

3. Ningehakikisha kuwa bandari tatu kubwa za Tanzania za; Unguja, Tanga, na Dar es salaam zimejengwa kwa kiwango cha kuridhisha kabla sijatumia mabilioni kununua ndege mbili za Raisi na rada mbovu.

4. Kabla sijawaambia watanzania wenzangu kufunga mikanda kubana matumizi, ningepunguza mishahara ya wabunge kwa ku-veto miswada yao ya kujiongezea malipo kila mwaka.

5. Kabla sija-sign bajeti ya serikali kuwa sheria, ningehakikisha kuwa mawaziri wanatoa maelezo ya uhakika kuhusu matumizi ya mabilioni ya fedha walizopewa kwa kipindi kinachoisha.

Ukweli ni kwamba, peke yangu sitafanya kila kitu. Nina uhakika kuwa kama nitatakiwa kufanya hayo mambo matano tu, wananchi wangu watakuwa na uwezo wa kupima kazi yangu kila mwaka ili kuhakikisha kuwa ninafanya kazi yangu barabara. Badala ya kuwa na ahadi kibao za maendeleo, Ningewaomba wananchi wanipime katika mambo machache tu kisha waamue kama niendelee kuwa Rais wao au la. Nimejifunza kitu kimoja kutoka kwa makocha wa timu za michezo marekani. Kwa wamarekani, kila wakati timu ikilegalega, kibarua cha kocha kinaota mbawa haraka sana. Ninategemea kuwa wale wenye mipango ya kugombea uraisi wa nchi yetu wanatambua hili.

OH, NIMEKUMBUKA KUWA NINAIOGOPA SIASA HIVYO UWEZEKANO NI MKUBWA SANA KUWA SITAWAHI KUWA RAISI WA NCHI, Nia ya makala hii ni kuwakumbusha viongozi wetu kuwa sisi watanzania ndio tumewaajiri na tunategemea matokeo mema ya kazi zao.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

 

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.