SWALI TUNALOHITAJI KUWAULIZA WAGOMBEA

Na, Ed <04/23/10 >

Tarehe 31 Octoba mwaka huu watanzania wengi mijini na vijijini wataingia katika vituo vyao vya kupigia kura kumchagua mtu atakayeongoza Taifa letu kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Tayari vyama mbalimbali vya siasa vimetangaza wagombea watakao viwakilisha vyama hivyo katika kinyang'anyiro cha Urais, Wabunge na Madiwani. Nia ya vyama vya upinzani/mageuzi kutaka kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni dalili nzuri kwamba demokrasia inazidi kukomaa na kuimarika nchini Tanzania.

Swali tunalohitaji kuwauliza waliojitokeza kugombea Urais, Ubunge na Udiwani mwaka huu ni hili: Je, wamejipima kwa vigezo gani hata wakaona kuwa wanafaa kuwa Marais, Wabunge na Madiwani wa nchi yetu? Maana tunaambiwa kuwa wamo hata wale walioshindwa katika kuwajibika/tumika vizuri katika nyadhifa mbalimbali za kiserikali hata ikabidi waondolewe madarakani au walazimishwe kujiuzulu.

Wamo pia wale ambao wana mipango ya makusudi kabisa ya kuligawa taifa letu la Tanzania kwa misingi ya udini na ukabila (Memo iliyosambazwa hivi karibuni na Mchungaji Mtikila ni mfano mzuri wa kutizamwa).

Wamo pia hata wale ambao imethibitika kuwa wamechangia katika kulipotezea taifa mapato ya kodi kwa kutunga na kupitisha sheria karimu na mbovu za madini zilizowaneemesha wageni na kuliacha taifa letu katika hali ya umasikini wa kutupwa (technically, wabunge wote wa CCM wamo kwenye kundi hii).

Wapiga kura nao wanahitaji kujihoji swali hili: kwanini watu hawa wanahitaji kuchaguliwa kuliongoza taifa hata baada ya mapungufu yote haya waliyoyaonyesha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita? Hivi wagombea hawa wanaojipaga kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu wanadhani watanzania hatuna upeo wa kina wa kufikiri, chambua na kufanya maamuzi mazuri ikiwezekana kuwaadhibu wale wagombea uchwara, mafisadi na wala rushwa kwa kupiga kura ya "HAPANA"?

Ni imani yangu kuwa watanzania wote wenye umri wa kupiga kura mwaka huu hawatapoteza kura zao bure bali watahitaji maelezo ya kina na ya msingi toka kwa wagombea wote ili wapate fursa ya kuchambua na kuwachangua watu safi na bora wanaostahili kuliongoza taifa letu. Na sio maelezo ya kina peke yake, bali pia sera nzuri zinazoeleweka na kuonyesha ni wapi wagombea hao wamekusudia kulipeleka taifa letu katika kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.