BORA UTU KULIKO USOMI

Na, Magabe Kibiti <Posted: 06/07/07>

Mabilionea watatu walikuwa wakisafiri kwa ndege binafsi kutoka Miami nchini Marekani kwenda visiwa vya Caribean. Mmoja wa matajiri hawa ambaye pia ndiye alikuwa rubani, ni mmoja wa wanasayansi maarufu wa fizikia na kemia. Tajiri wa pili ni profesa mstaafu wa uchumi na pia mshauri mwandamizi wa benki ya dunia. Tajiri wa tatu ambaye elimu yake ya shule ni darasa la nne, ni mmiliki wa visima vingi vya mafuta (oil wells) huko Texas. Kutokana na kujiamini kupita kiasi, mabilionea hawa waliamua kusafiri peke yao bila wasaidizi au walinzi binafsi. Kwa bahati mbaya ndege yao ilipata matatizo ya kiufundi wakiwa angani na ikabidi walazimike kutua kwa nguvu (forced landing) baharini.

Msimuliaji wa stori hii hatoi maelezo mengi ya namna ilivyotokea zaidi ya kuwa, matajiri hawa walitumia boti ya dharura kutoka nje ya ndege hii iliyokuwa ikiwaka moto. Baada ya kusubiri kwa masaa zaidi ya kumi bila ya kupata msaada wowote, wahanga hawa walianza mjadala mrefu wa namna ya kuokoa maisha yao. Tatizo la kwanza ilikuwa ni namna ya kufungua chupa yenye chakula cha dharura (boti za dharura huwa na vyakula vya chupa zilizofungwa sana na kuwekwa kwenye mifuko ya plastiki ili visiharibike). Mwanasayansi kwa haraka alianza kutunga kanuni ya namna ya kutengeneza kifaa cha kufungulia chupa zenye vyakula (kazi ambayo ingemchukua kama wiki mbili kumaliza).

Mwanauchumi akashauri kuwa mfuko wa plastiki uliotumika kupachika chupa kwenye boti uchanwe katika vipande vitatu vinavyolingana ili vitumike kugawa chakula katika uwiano ulio sawa. Matajiri wenzake walipomuuliza kuwa watagawana vipi chakula bila kufungua chupa ya chakula, mwanauchumi akawasihi wenzake wadhanie (assume) kuwa tayari wana kifaa cha kufungulia chupa. Tajiri wa tatu kwa hasira na mshangao mkubwa akawafokea wenzake kwa kupoteza muda. Kwa kujiamini akarudisha chupa ndani ya mfuko wa plastiki na kuufunga na kisha akatumia chuma kikubwa cha mkanda wake wa suruali (cowboy belt) kuigonga chupa ile hadi ikapasuka.

Stori hii huwa inanikumbusha kazi niliyofanya kama mtafiti msaidizi wa taasisi ya utafiti Tanzania ya REDET takribani miaka sita iliyopita. Mara baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2000, nilikwenda Songea kwa niaba ya REDET kukusanya maoni ya wananchi kuhusu uchaguzi huo. Nikiwa Songea nilikutana na mzee mmoja aliyebadili mtizamo wangu wa maisha milele. Kwanza alinishangaa kwamba niko Songea kuwauliza wananchi kuhusu uchaguzi wakati nikijua kuwa majibu yao hayatabadili matokeo ya uchaguzi. Pili alinishangaa kwa kupoteza muda kama msomi kuwauliza watu wasio na elimu maswali badala ya kutumia muda huo kuelimisha watu namna ya kujikomboa kiuchumi.

Kwa upole nilimuuliza mzee huyu kwa nini amenichukia wakati hanijui binafsi. Bila kusita mzee huyu akanijibu kuwa anawachukia wasomi au wale wanaojiita wasomi kwa sababu ya maamuzi yao ya kisomi yasiyo na hisia wala utu hata kidogo. Kwa uchungu akaniuliza nimweleze bila kuficha sababu iliyopelekea serikali kufuta ruzuku ya pembejeo za wakulima wa mazao ya chakula huku wakifuta kodi kwa waagizaji wa vifaa vya mawasiliano na kompyuta. Kwa uchungu akauliza; utawezaje kutumia kompyuta bila kula? Kabla sijajibu akaendelea; unahisi wazo hili lilitolewa na nani? Kabla tena sijajibu akahitimisha kuwa; wazo hili la kufuta kodi za kompyuta lilitolewa na msomi yuleyule aliyetoa wazo la kufuta ruzuku kwa wakulima.

Mzee huyu alikataa kujibu maswali na alinishauri kuandika kuwa; utu ni bora kuliko usomi - kama hitimisho la utafiti wangu. Nasikitika kuwa sikuandika hitimisho hilo aliloshauri mzee kwa kuogopa kuwa waajiri wangu wasingelipenda. Makala hii itamuenzi mzee huyu wa Songea (ambaye nalitunza jina lake) kwa ushauri wake makini. Hii ni kutokana na ukweli kuwa; kama yule tajiri mwanasayansi aliyeanza kutunga kanuni ambayo ingekuwa tayari kutumika baada ya yeye kufa kwa njaa, baadhi ya wasomi wetu hutoa mawazo kama ya kununulia vifaa vya kisasa vya kijeshi kujilinda bila kujali kuwa wakulima wengi nchini bado wanatumia majembe ya mikono kulima - hali itakayopelekea raia nchini kufa kwa njaa na sio uvamizi wa kijeshi kutoka nje.

Kama yule tajiri mwanauchumi aliyewashauri wenzake wadhanie kuwa (assume) tayari wana kifaa cha kufungulia chupa na waanze kufikiria namna ya kugawana chakula, kuna wasomi leo hii wanashauri kuwa serikali ijenge chuo kikuu chenye uwezo wa kuchukua maelfu ya wanafunzi kila mwaka kwa dhana (assumption) kuwa tayari kuna maelfu ya shule nzuri za msingi na sekondari. Kama yule mzee, namie leo nauliza; utawezaje kujilinda ukiwa umekufa kwa njaa? Utapata vipi maelfu ya wanafunzi kujiunga na chuo kikuu wakati huna shule za awali na walimu bora wa kuwaandaa wanafunzi kwa chuo kikuu? Kama yule tajiri asiye na elimu katika stori yetu (ya kufikirika), ni bora zaidi kuamua vyema hata kama uamuzi unapingana na elimu ya shuleni.

Nia ya makala hii sio kushauri watu wasifuate mawazo ya wasomi bali ni kushauri wasomi wetu kutoa sera zenye utu na hisia kwa wenzao kila mara wanapofanya maamuzi muhimu kwa nchi zetu masikini.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

 

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.