JENGO JIPYA LA BUNGE NA HAIBA YA DEMOKRASIA NCHNI

Na, Antar Sangali (Bagamoyo), < 06/13/06>

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania Juni 11, 2006 alizindua jengo jipya la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lenye thamani ya Bilioni 30.9 huko Dodoma katika mji ambao kwa miaka dahari umefanyiwa mahubiri ya nguvu kwamba makao makuu ya serikali yahamie huko ingawa imebakia kuwa hadithi ya adili na nduguze.

Ni jengo zuri na limesifiwa sana na walioliona kwa macho yao na hata wasanifu wa ujenzi wamesema  ni imara na madhubuti linaloenenda na wakati hususani katika ufundi stadi wa kujenga majengo bora duniani.

Wengi tumeliona kupitia Televisheni ya Taifa-TVT, ITV, na katika magazeti yaliyobeba picha za kuvutia na kushawishi kwa macho. Kifupi, linafaa.

Rais akifungua jengo hilo katika hotuba yake amewahimiza na kuwataka wabunge kubadilika kama ambavyo jengo jipya lilivyo huku  fikara na mitazamo yao nayo ikibadilika na kutimiza utashi na matakwa ya wananchi waliowachagua kuwawakilisha.

Akihutubia huku akimwagia sifa lukuki Rais aliyeachia madaraka katika awamu ya tatu Mzee Benjamin Mkapa, Kikwete alitamka kinagaubaga kwamba hayo ni matunda yaliopatikana katika awamu iliyopita na akamsifu kwa kuidhinisha shilingi hizo za kodi za wananchi kutumika kwa utekelezaji huo kwa maslahi ya Taifa.

Rais amekazia jengo hilo lifungue ukarasa mpya wa haiba ya demokrasia kwa mustakabali wa Taifa na kutimiza matumaini na matarajio ya watanzania walio wengi na kwamba, ndani ya jengo hilo sasa kuamke mijadala endelevu itakayosukuma na kuiwezesha nchi kufika ufukoni mwa bandari ya maendeleo yakinifu kwa Taifa na wananchi kwa ujumla.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete ni dhahiri inawaamsha wabunge na kuwataka kuchemsha bongo zao kwa azma moja tu: kutupatia ile Bongo Mchicha itakayotokomeza maadui ujinga, maradhi na umasikini ulioenea Tanzania kote husasani vijijini.

Haiba ya Demokrasia kwa mtazamo wangu itategemea sana  ugalacha wa wabunge katika kupambana kwa nguvu ya hoja na  serikali kwa lengo la kujenga nchi na si kuingia bungeni kwa uwoga unaowakinga wabunge hao kwa kiwingu kizito cha uanachama wao katika vyama vyao vya siasa wanavyoviwakilisha.

Pale Mbunge mwenye nguvu ya hoja Bungeni anapoonekana ni msaliti kwa chama chake kwasababu tu ameikosoa hadharani serikali ya chama anachotoka sidhani kama haiba anayoitazamia Rais inaweza patikana kwa urahisi katika nchi yetu.

Lakini hali kadhalika Mbunge mpayukaji mithili ya mbayuwayu alimuradi aonekane katika TV kuwa kasema kwa minajili ya kuwafurahisha wapiga kura wa jimboni kwake ni wazi atayazinga na kuyakinga mazingira hayo ya haiba yasigote kileleni.

Nchi yetu ina umasikini mkubwa sana! Na fedha zilizotumika katika ujenzi wa jengo jipya la Bunge ni nyingi lakini pia umuhimu wa jengo hilo jipya la Bunge lenye hadhi-murua ni muhimu kwa mustakabali wa demokrasia yetu na ushiriki wa wabunge katika mijadala muhimu itakayoibuliwa katika jengo bora lenye hadhi.

Tanzania sasa ifike mahali Mbunge wa UDP, CHADEMA, FORD au Jahazi Asilia  aipongeze serikali kwa utendaji, umakini, ufuatiliaji, vita dhidi ya rushwa, uimarishaji wa demokrasia, na utawala bora huku wanachama wa chama kilichounda serikali kipige makofi ya hongera na si ya dhihaka pale mbuge wa kambi ya upinzani anapotoa hoja nzuri ili jamii iache tabia ya kumuona mbunge wa aina hiyo kama pingamizi. Zaidi sana,jamii isimuone mbunge huyo kama pandikizi la chama tawala.

Kadhalika iwe ni mahali kwa wabunge wa chama tawala kuinyooshea kidole serikali yao na kuikosoa kutokana na uzembe, ubadhirifu, wizi na ufujaji wa fedha za umma au maonevu ya vyombo vya Dola dhidi ya raia wasio na hatia.

Lakini pale inapoonekana wabunge wa CUF, CCM, au CAHDEMA wanaingia Bungeni wakiwa na hoja zao mikononi mwao za kutaka kuwafurahisha wenyeviti wao au makundi ya wanchama wao pia kutapoteza haiba ya demokrasia na matumaini ya jamii, Spika Sitta tunakushauri uwaongoze vema na kuwakumbusha kuwa wako pale kuwakilisha watanzania na si vinginevyo.

Zaidi ya yote inachukiza na kutia doa katika uwanja wa demokrasia pale wabunge waliochaguliwa na wananchi kwa kura wanapokalishwa kitako na kuwa kama kamati ya chama cha siasa huku wakipewa misimamo ya "taka usitake-kubali"

Hulka hii ni wazi haiwezi kufikisha dhamira ya kauli ya Rais ya kutaraji haiba ya demokrasia ipatikane ndani ya jengo jipya lililogharimu fedha nyingi za Taasisi za kimataifa, wahisani na walipa kodi masikini hohehahe wa Tanzania.

Imani yetu kwa serikali ya Rais Kikwete, Waziri Mkuu wake na uchapakazi wa mawaziri wake kama utapata nguvu ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya katika utekelezaji wa majukumu na sera zilizokubalika halafu kukaibuka na ushindani wa nguvu ya hoja mbungeni, serikali hii bila shaka itachupa katika mwendo wa haraka na kufikia maendeleo tunayoyakusudia.

Rais Nyerere alisalitiwa kinadharia na baadhi ya watendaji wake katika kutimiza matakwa ya Siasa ya Ujamaa. Nia ya Ujamaa ilikuwa ni njema lakini vita baridi iliibuka ndani ya TANU na kumtupa mkono Mwalimu asitimize aliyoyataka kwa jamii yake.

Bila siasa ya ujamaa leo Tanzania baada ya mika 44 kupita isingejigamba abadani na sifa ya kuwa na umoja wa kitaifa madhubuti,  amani na utulivu imara wa kudumu.

Kubwa ni ile hali iliyokuwepo ya kisiasa ya chama kushika hatamu na viongozi  mbalimbali  kuwa waoga kuliko kunguru hat kukosa ujasiri wa kokosoa na kutekeleza kwa usahihi wa hoja ya msingi aliyonayo hata kama ni njema mbele ya Taifa.

Serikali ikubali changamoto za Bunge, Bunge liafiki maamuzi ya kisheria ya Mahakama; na Bunge liisaidie serikali kutekeleza, kusimamia na kufikisha vilio na matakwa ya wapiga kura bila ya kuwa na soni yoyote ile. Ikiwa haya yatajitokeza na kuendelea kuwepo katika nchi yetu, ni wazi kuwa tutataraji haiba ya demokrasia katika jengo jipya la Bunge sawa na Rais Kikwete alivyotoa nasaha zake huko mjini Dodoma katika hafla za uzinduzi wa jengo hilo.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.