NYOTA ILIYOCHOMOZA NA KUZIMIKA GHAFLA

Na, Antar Sangali (Bagamoyo)

Tarehe 26 Juni mwaka huu habari zilizagaa nchini na nje ya mipaka ya Tanzania kwamba Mbunge wa viti maalum kupitia CCM kundi la Vijana, Mhe Amina Khamis Gabriel Chifupa amerfariki dunia.

Tangazo ambalo baadaye lilithibitishwa na Baba yake mzazi Mzee Khamis Chifupa na kukiri kuwa ni kweli kifo hicho kilikuwa kimetokea katika hospitali ya Jeshi la Wananchi Lugalo jijini Dar es Salaam.

Mwanadada marehemu Amina Chifupa kijana mdogo aliyeitamani siasa, kimsingi alipata mafanikio makubwa mara alipothubutu kuingia katika uwanja huo na kuliandika jina lake katika mwendo wa haraka kuliko umri wake.

Historia ya Tanzania kisiasa inaonyesha jinsi wanawake mathalan  Marehemu Titi Mohamed, Lucy Lamek, Kate Kamba, Sophia Kawawa, Beatrice Kunambi, Julie Maning, Tabitha Siwale, Rufeya Juma Mbarouk walivyojingiza katika mbio za siasa na majina yao kukuwa haraka kulingana na jinsi walivyolitumikia Taifa letu.

Majina haya kwa ghafla yalimezwa na msichana Amina Chifupa ingawa kila jina kati ya hayo liliweza kutumika katika wakati na kwa kadri ya mtaji wa kila mwanasaisa alivyoonekana kutuna na kujiwekeza katika taswira husika.

Dhamira ya marehemu Amina kuitamani siasa ina mnasaba wa karibu na maisha ya Baba yake aliyekuwa mtumishi na kada wa muda mrefu wa TANU na hatimaye CCM.

Rais Aman Karume, Makongoro Nyerere, Vita Kawawa, Mahmoud Thabit Kombo, Mansour Yusuf Himid, Violet Mzindakaya, Ridhiwan Kikwete,Nape Nnauye na marehemu Ipiyana Malecela pengine hawakusukumwa na wazazi wao kujiunga na kambi ya siasa bali damu ya wazazi wao na mizimu ya siasa iliwamulika na kuwaangazia taa na hatimaye kuwasajili katika midundo ya ngoma za siasa.

Mwalimu Julius Nyerere alikijenga chama cha TANU, alikiwekea misingi kamili katika kushika utawala wa Tanganyika, kiongozi madhubuti ni kuwa na msingi wenye dhamira na utashi kamili hata kama atakabiliwa na kiwango kidogo cha elimu.

Kiongozi wa watu si ule uhodari wa kuiba na kutafuna fedha za serikali kama mchwa au kulimbikiza mali wakati watanganyika wengine kula yao ya siku ni bahati nasibu. Uongozi si majidai na mjigambo au kuwakoga watu kwa mbwembwe!

Bibi Titi alipanda katika majukwaa ya siasa za TANU kwa mara ya kwanza mwaka 1956 wakati wanawake wengi wakati huo hasa mjini Dar es Salaam kutokea mbele ya hadhira ya watu ilikuwa ni aibu au ni matusi yasiyo na kifani.

Titi hakusita, alitaka kuitetea nchi yake na kuhakikisha kuwa Mwingereza na utawala wake anaondoka na Tanganyika inajitawala kwa mapana na marefu katika demokrasia ya kweli, utawala bora wa sheria na kuheshimu haki ya kila binadamu ikiwa ni pamoja na kutetea haki za wengine popote duniani.

Marehemu Edward Moringe Sokoine alikuwa na dhamira na utashi wake hakuweza kuuficha wala kumpaka mtu mafuta nyuma ya mgongo wa chupa au kukubali utumwa wa kula masaza ya mtu kwa azma ya kujipendekeza na kutesa wengine.

Mrehemu Sokoine alikufa pale Kongwa akiwa shujaa kamili asiye na mfano unaofanana na wenzake wote aliyowaacha katika serikali ya Tanzania katika awamu ya kwanza, pili, tatu na ya nne ukimuacha Baba wa Taifa.

Bw Augustine Mrema na Bw Seif Sharif Hamad wakati wakiwa viongozi wa serikali kwa kadri ya uwezo wao nao walionyesha ni vipi wana wajibu katika kutimiza majukumu waliokubali kula kiapo cha utii.

Katika miaka takriban 25 iliyopita Tanzani ukimuacha Baba wa Taifa imekosa kumpata kiongozi aliyepita katika nyayo za Edward Sokoine, Augustine Mrema na Seif Sharif Hamad. Huu ndio ukweli wa mambo anayekataa akatae na atakayekuwa muungwana akubali.

Kiongozi anaposumbukia watu na kuwatumikia kwa uadilifu, uaminifu, na kutafuta njia za utatuzi na kuleta tija au kubuni mikakati sahihi na kuisimamia kwa maslahi ya jamii nzima ni vigumu kusahaulika au kumbeza kirahisi. Ni vigumu basi hata hivyo kulibeza na kulisahau jina la marehemu Amina Chifupa.

Amina alijua mikiki na mizengwe ya siasa akiwa katika umri mdogo lakini alijikita licha ya baadhi waswahili kumpaka matope kana kwamba wao walikuwa ni manabii watakatifu na watiifu mbele ya Mungu muweza. Alishinda mtihani na kuingia Bungeni.

Alijitahidi kuonyesha nini kiongozi anatakiwa afanye katika jamii. Na kadri Amina alivyojitahidi kufanya, kutoa, kushauri na kukemea kwa sauti ya juu ikwa upande wake ilikuwa ni kama ufunguo na kibali kilichomruhusu kupita katika safari yake kwenye barabara ya siasa.

Akiwa Mbunge Amina alidiriki kusimama hadharani na kutamka neno zito ambalo kila mbunge na mwananchi walizubaa.

"Nchi inakabiliwa na tatizo kubwa la madawa ya kulevya, serikali isipochukua tahadhari yan haraka na kulivalia njuga suala hili, mbele kuna hasara kubwa inatusubiri na kutugharimu." Aliwahi kukaririwa akisema.

Kimsingi Madawa ya kulevya ni tatizo na kadhia ya kutisha katika kizazi cha Tanzania, wanaofanya biashara hiyo majina yao hayatajiki, mengine yanatokana na mapande ya magogo kwa maana ya vigogo wenye maulufi ya ngawira na kushika nyadhifa katika serikali zote za SMT na SMZ.

Aliposimama na kutamka kinagaubaga kwamba kizazi cha nchi kinakwenda wapi kutokana na balaa hilo, hakuna aliyepinga na kusema Amina anaropoka na kupayuka bali wengi waliona kana kwamba Amina atasakamwa na kufanyiwa madhila na wauza unga wa ndani na nje.

Wenye kumiliki mali, waliokuwa na nyadhifa zao na ugogo wa ukubwa katika serikali hawakutokea hadharani na kufanya aliyoyafanya Amina, yeye alichopata alikula na kugawana na yatima, masikini wenziwe na watoto wa mitaani. Kutoa ni moyo baba usambe utajiri.

Wauza unga kimsingi wengi wao wamelikimbia jiji la Dar, baadhi ya vizabizabina nao wakajifanya kulivalia njuga suala la madawa ya kulevya nyuma ya sauti ya Amina, hali ilivyo leo Tanzania si kama kabla ya Amina hajasema na yeye kifo kumkuta, je? kabla ya Amina ni nani aliyesimama kwa ujasiri na kusema kinywa wazi kama kizazi na hasa vijana wanaangamia?

Nilimualika siku moja Amina katika kipindi changu cha saa moja kiitwacho Ajenda ya Leo studio nikimuuliza maswali mbalimbali yakiwemo: je, Amina umetumwa useme haya, huogopi, huna hofu au kuna unachotegemea nyuma ya Ajenda hii?

Msichana mdogo, alijibu kwa kujiamini huku akisema kama kufa yeye yu tayari kifo kimkute lakini vijana wanateketea, wanafisidika na kusawijika afya zao kwa faida za kundi dogo lenye uroho wa kupata utajiri wa haraka.

Amina alijibu bila hofu na kusema hata baadhi ya wabunge wenziwe walishaanza kumrushia vikaratasi na kumshutumu wakidai kauli yake hiyo ilikuwa ni nzito na ya hatari kwake

Amina Chifupa kama binadamu wengine hakuwa nabii, alikuwa na mapungufu na udhaifu wake, lakini mabaya yake yanamezwa na mema mengi aliyoyafanya (kivitendo) mbele ya jamii.

Ni nyota ya matumaini iliyochomoza na kuzimika ghafla mithili ya mshumaa katika upepo mkali jangwani.

Mungu mpokee Amina, muhurumie na kumsamehe dhambi zake,mpe makazi yalio mema na ummwagie manukato yenye uturi  faraja na huruma tele.

Amezikwa katika kijiji walichozaliwa wazazi wake Lupembe huko Iringa, udongo mwekundu huku Amina akiwa amevikwa  kitambaa cheupe cha sanda kama ambacho mimi nitavikwa siku roho yangu itakapokatika amelazwa chini ya ardhi.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

 

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.