TANZANIA BADO INA SAFARI NDEFU!

Na, Antar Sangali (Bagamoyo): [Posted first on: 07/05/07]

Dhamira ni msingi unaohitajika kwa kila serikali inayotawala kwa maana ya wale walioshika hatamu za utawala dhidi ya wanaotawaliwa katika kufikia malengo  ya wazi na endelevu kwa maslahi ya watu na maendeleo yao.

Leo msomaji wangu nataka kuizungumzia awamu ya kwanza chini ya Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ambayo bado sijaipatia mfano wake baada ya miaka 46 ya Uhuru wa Tanganyika kupita.

Mwalimu alilaumiwa kwa mambo kadhaa katika utawala wake mambo ambayo leo ukiyapitia kwa umakini unaweza kuyapatia majibu chanya licha ya kwamba  dhana ya shukran na upongezaji wa mambo si ustaarabu wetu waafrika tulio wengi.

Dk. Nyerere na serikali yake ya TANU alilaumiwa mno kwa kukataa mfumo wa vyama vingi vya siasa, aliipiga teke nadharia ya ubepari na kuamini siasa ya ujamaa na kujitegemea, alichukia vikali ukabila, udini na ujimbo.

Aidha Mwalimu hakutaka kabisa na alilaumiwa kwamba hakupenda kukosolewa na waliomzunguka, lakini pia inatajwa hakupenda kusikiliza mawazo na fikra za wengine, kadhalika alikataza rasilimali za nchi zisitumike kwa faida ya wakoloni kwa maendeleo ya nchi zao.

Aliwachukia wezi, wabadhirifu wa mali ya umma na wasomi wababishaji ambao lengo lao ilikuwa ni kuleta blabla simulizi na andishi kwa nia ya kufikia matlaba yao. Mwalimu vilevile alihakikisha anayehoji kipumbavu muungano wa Tanganyika na Zanzibar afananishwe na mhaini.

Mwaka 1982 Kundi liloongozwa na marehemu Pius Mtakubwa Lugangira lilipanga njama za kuipindua serikali ya Mwalimu njama ambazo ziligonga mwamba na wahusika wakatiwa mbaroni na wengine kuikimbia nchi.

Lakini baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa tathmini, kwa mtazamo wangu hafifu nimefanikiwa kubaini ni kwa nini Mwalimu kwa wakati ule aliupinga mfumo wa vyama vingi vya siasa usiwepo.

Mwaka 1992 uliporudi mfumo wa vyama vingi: likaibuka kundi kubwa la watu waliofukuzwa katika serikali, waliofilisi mashirika ya umma, waliofukuzwa ndani ya mduara wa kisiasa wa CCM na ukijipenyeza upya katika vyama hivyo vipya.

Kimsingi walikuwa watu walewale walikuwa na makovu na vidonda vya dhambi katika jamii, waliokuwa bado wana mgando wa akili na maarifa kama urithi walioondoka nao/vuna katika chama walichofukuzwa.

Katika vyama hivyo vipya, wakahamia watu wale wale waliokuwa na hulka zilezile na mizigo ileile iliyojaa umimi, ubinafsi, ulaji na kutaka kuhodhi madaraka huku wakipinga wasikosolewe wala kusahihishwa pale walipoonekana kutembea nje ya mstari.

Hapa ghafla nilitanabahi na kukumbuka kwamba 1965 kupigwa marufuku mfumo wa vyama vingi ilikuwa sahihi kwasababu nilizoziona mimi kwamba: kwa watanganyika walio wengi, kilikuwa ni kitu kigeni kwao na Taifa kwa ujumla.

Nilipoona rasilimali za nchi zinatafunwa na mchwa wa ajabu wasio na huruma, nikakumbuka kumbe Nyerere alikuwa sahihi kukalia na kulinda migodi yetu na mbuga zisimalizwe na maharamia.

Kadri nilivyoona kundi jipya la mabepari weusi likiibuka nikaumbukuka ujamaa alioutaka Mwalimu Nyerere;( na penginepo bila ya kuwepo nadharia ya ujamaa kwa wakati ule) walalahoi na mababakabwela wa Tanganyika wangelikuwa wageni na watumwa katika ardhi yao wenyewe mbele ya mamwinyi na mabepari uchwara.

Kupitia vyama vingi vya siasa na wanasiasa wake waliojiingiza ndani ya vyama nikitazama jinsi wanavyoikosoa serikali iliyopo madarakani kwa lengo la kujipatia mtaji wa ushindi wa kidemokrasia na vile wanavyoboronga hoja nzuri, namkumbuka Mwalimu na jinsi alivyopuuza baadhi ya mawazo ya wanasiasa wetu hatimaye wakamdhihaki na kumwita bila hatia kwa jina la "Baba Haambiliki"

Niwatazamapo wale wanaojiita wasomi wasio na taadhima wala kujua thamani ya kuelimika kwao nazikumbuka kambi za JKT zilivyowatia adabu na ukakamavu na kisha kuwadharau kwa jinsi walivyoyatafuna mashirika ya umma ambayo Mwalimu kwa akili zake aliyaanzisha kwa makusudi ili kutanua wigo wa ajira.

Nikiitazama Somalia na wasomali jinsi wanavyopigana na kuteketezana kwa kutamani miliki ya koo na kabila zao, ndivyo akili yangu inavyomkumbuka Nyerere wa Uzanaki. Lakini hofu yangu kubwa ni kwa wale wanaohoji hoja ya Muungano wa Tanzania. Mara nyingi najiuliza, je wanatambua ni nini hasa kilichokuwa mbele ya Mwalimu Nyerere na Mzee Abeid Karume? -- wakoloni na maadui wa ndani?

Mwalimu na serikali yake waliunda mashirika ya umma, ajira zikapatikana, bodi za mazao zikaanzishwa nchini na tija ya uzalishaji ikapatikana huku mazao kadhaa yakiuzwa ughaibuni na kuleta fulusi za kigeni nchini.

Baadhi ya mazao kama pamba, pareto, korosho, ufuta na tumbaku ziliingiza pesa za kigeni na viwanda vya nguo vikazalisha nguo zilizokuwa na ubora kuliko hizi za Tahiland,China na Dubai.

Vilikuwepo viwanda vya viatu, mipira ya baiskeli, betri za tochi, bandari zilizozalisha, majani ya chai, sigara, Bia, viwanda vya vyuma na mashamba ya mkonge.

Lakini eo hii, tuna wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri wanaoshindana kwa kuvaa suti kali, kujiona wao wamesoma, kuteng'eneza nywele na kushiriki warsha na semina ili wajipatia posho ya vikao, huku nchi ikizidi kuzama chini siku hadi siku.

Ni RC, DC au DED wa yupi wa nchi hii leo anayetilia mkazo suala la kilimo? Bali kila kukicha njaa inakithiri, bei za vyakula zinapanda na maisha ya wananchi wa kawaida (hususani vijijini) yanazidi kuwa magumu.

Ukweli ni kwamba: uzalishaji wa ndani ukitiliwa mkazo, utasaidia sana kuweka ushindani/kukabiliana na soko huria na hatimaye kupunguza ughali wa bei za juu zinazopangwa na matajiri wanaoagiza bidhaa za nje katika zama hii ya utandawazi.

Watanzania wenzangu, Hivi ni kipi hasa kinafanya viwanda kama vile vya Urafiki, Mutex, Bora na Sungura Textile visizalishe nguo na viatu huku kile cha KTM cha Mbagala kinachomilikiwa na mtu bianfsi kikiendelea kuzalisha na kuajiri watu?

Tanzania itaendelea hadi lini kuwa jalala linalotupiwa bidhaa duni na ghafi toka katika viwanda vidogovidogo vya ughaibuni wakati nchi yetu ina rasilimali nyingi ambazo zingeweza kutumika kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu...!?

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.