VIONGOZI HAWA SIO WAZALENDO KABISA!

Na,Nino Mkuu

Japo siafikiani na Msoshalisti Ngombale Mwiru katika mambo mengi, hususani mambo ya kisiasa, hapa inabidi niweke kando itikadi zangu na nikili kuwa: anachokisema mzee huyu ni kweli kabisa!: "ni ukosefu wa uzalendo!" Kama alivyowahi kukaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema katika ukumbi wa Urafiki alipokuwa akiwahatubia baadhi ya wanafunzi wa chuo kikuu (UDSM) waliojiunga na Chama Cha Mapinduzi--ukosefu wa uzalendo kwa baadhi ya viongozi wachache nchini ndio uliopelekea kwao kushiriki kuhujumu mali ya umma kwa kusaini mikataba mibovu inayolalamikiwa kote nchini. "Watu wetu wanashirikiana na watu wa nje kuuza maslahi ya nchi. Mikataba siyo wageni pekee wanaiweka, bali na watu wetu nao wanashiriki, lakini hawana uzalendo. Mzalendo wa kweli hawezi kushiriki kuhujumu mali ya umma," Kingunge.

Kwa muda sasa, wananchi wengi ndani na nje ya nchi wamekuwa wakipiga kelele kuhusu mikataba hiyo mibovu lakini mpaka leo hii tulichosikia toka kwa viongozi wetu, akiwemo rais Kikwete, ni kauli tu siziso na nguvu wala msisitizo wowote ule wa kutushawishi wananchi tulio wengi ili tuendelee kuamini kuwa tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi; badala yake tumebaki kukuna vichwa na kohoji wala tusijue kama kweli serikali hii ina dira inayoeleweka, ama inakwenda tu kwa kupapasa-papasa kama kipofo apapasaye kwenye kiza kinene, kiza cha utandawazi.

Ndiyo, tunafahamu kuwa ipo Dira ya Taifa ya maendeleo 2025, kadhalika ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2000, yenye lengo la kumwezesha mwananchi wa kawaida kushiriki katika shughuli za uchumi, lakini ukweli ni kwamba: yote hayo ni maandishi tu katika makaratasi yaliyopambwa kwa lugha nzuri na sanifu inayoshawishi na kutia kiini-macho mbele ya wananchi hali ufuatiliaji wa kuhakikisha kuwa dira hiyo inafikiwa/timizwa ni hakuna.

Sheria ya kuhujumu uchumi iliyofanyiwa marekebisho mwaka1983, chini ya kifungu cha sheria namba 16 cha mwaka 1979, makosa ya kuhujumu uchumi yanabainishwa waziwazi na tume ya kuwafuatilia wahujumu hao ipo mahala pake. Lakini inshangaza kuwa mapema mwaka huu (Jan.) wakati rais anatangaza adhima yake ya kutaka mikataba yote inayotiliwa mashaka hasa ile ya madini ipitiwe upya, hakuweka wazi ni vipi watakaopatikana na hatia za kuhujumu uchumi wa nchi watakavyosaidia kutoa maelezo. Yaani, hatua gani kisheria wakazochukuliwa endapo kama watabainika (bila shaka watabainika tu kama uchunguzi utaendeshwa kwa haki bila kubebana) kuwa walihusika kusaini mikataba kwa maslahi yao binafsi na si kwa maslahi ya nchi.

Rais anatakiwa kuweka wazi suala hili mapema kabisa na kuacha kutupigia hadithi za ...subiri hadi hapo watuhumiwa watakapopatikana. Kwanini ni muhimu rais atuweke wazi mapema? Kwasababu: kulingana na hali ya siasa nchini ilivyo ya kubebana, kuoneana aibu na kulindana; hadithi za "subiri kwanza" hazituingii kabisa akilini. Je, tutaaminije kuwa kama Sumaye ndiye atakayepatikana na hatia hataonewa aibu ama kulindwa? Rais, kama kweli unataka kulikomboa taifa letu toka kwenye dimbwi la ubinafsi, inakupasa pia uwe mwazi katika suala hili., tena mapema.

Nikerejea makala iliyochapiswa na tovuti hii (March 14, 2006) iliyokuwa na kichwa kilichosomeka: "Ole wako Tanzania..., ni nani atakayekusaidia,?" maswali mengi yaliyoulizwa ndani ya makala hiyo bado hayajajibiwa. Kiufupi, serikali mpaka sasa haijatoa maelezo ya kuridhisha kwa wananchi kuhusu ni nini hasa kinachoendelea katika suala zima la ubinafsishaji, hasa kwa upande wa migodi yetu.

Ingawa Rais mstaafu, Mkapa, alikuwa na nia zuri tu ya kuwavutia wawekezaji toka nje, lakini ni kudhalilisha fahamu zetu pale serikali yake iliposema kwamba asilimia 3 ya mafao, kutokana na mapato ya madini inatosha. Inatosha kivipi? Hivi hao wawekezaji wanatoa kweli takwimu halisi kuhusu faida wanazozipata kiasi cha serikali kuridhika na kusema, hiyo asilimia 3 inatosha? Ukweli ni kwamba hawatoi takwimu halisi, na katika hili serikali imefumbwa macho. Na hata kama wangetoa takwimu halisi, bado kiwango cha asilimia 3 ni kidogo mno! Hakitoshi!

Ukiambia serikali kuwa wamekuwa wakarimu kupita uwezo, wanakataa. Hebu ndugu mwananchi jiulize: Kama huu sio ukarimu kupita kiasi (kwa wawekezaji wa sekta ya madini toka nje) ni nini?--Kiongozi wa juu wa serikali ya awamu tatu, aliwahi kukaririwa ikidai kwamba, serikali ililazimika kufanya hivyo kuongeza ushindani ili kuzifikia nchi ambazo zimekuwa katika masoko ya madini kwa muda mrefu na zenye miundombinu bora ya madini. Hata kama ni kufikia ushindani, je hatuwezi kufikia ushindani bila kupunjwa?

Huu ni upunjwaji wa dhahiri kabisa! Hebu angalia, viwango vya kimataifa vinakubali asilimia 3 ya mafao kwa mapato ya madini kati ya dola za kimarekani elfu kumi hadi millioni moja. Ikizidi milioni moja na kiwango cha mafao kinaongezeka kufikia asilimia 5, hadi mapato ya dola milioni tano. Baada ya hapo kiwango kinaongezeka kwa asilimia 1 kwa kila ongezeko la mapato la dola milioni 5, hadi kufikia asilimia 12. Kwa hiyo kuweka kiwango kimoja kwa mapato yoyote (3 %) , hasa kiwango chenyewe kinapokuwa cha chini, haitoshi. Na haya ni malipo ya aina moja tu kwani wawekezaji hawa hawa wakienda nchi zilizoendelea kama Canada, watatozwa mafao ya jumla, serikali kuu itawatoza kodi, na serikali za mitaa (ilipo migodi) pia itawatoza kodi ili kuwanufaisha wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya migodi. Sisi tunatoza mafao mara moja, tena ya kiwango cha chini mno , aslimia 3 tu! Nao viongozi wetu wanaridhika kabisa na hilo!

Huu sio wakati wa kuoneana aibu, inapaswa wale wote waliohusika kulikosesha taifa mapato mengi ya kiuchumi na kuwanyima wananchi wa kawaida fursa ya kumega keki ya taifa kwa namna moja ama nyingine (ambayo wanastahili), wachukuliwe hatua kubwa za kisheria na za kutosha.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.