TUSILEWESHWE NA SIFA TOKA BENKI YA DUNIA

Na,G

Katika hatua inayoashiria kufuata nyayo za Rais aliyemtangulia, Rais wa kumi wa Benki ya Dunia Bw. Paul Wolfowitz aliitembelea Tanzania katikati ya mwezi huu na kuonyesha kuvutiwa na hali ya maendeleo ya kiuchumi ya nchi yetu na Jumuiya ya Afrika mashariki.

Kwa kipindi kirefu viongozi wa Benki ya Dunia na shirika la Fedha Duniani wamekuwa wakiliangalia bara la Afrika kama bara lililojaa rushwa, uongozi mbaya unaopelekea umaskini katika nchi za Afrika. Si hivyo tu, bali viongozi hao wamekuwa na mtazamo tofauti kwa nchi za Asia pamoja na zile za Marekani ya Kusini.

Mtizamo huu wa taasisi za fedha kwa nchi maskini ulianza kubadilika mwaka 1995 pale bwana James Wolfensohn alipoteuliwa kuongoza Benki ya dunia kama rais wa tisa wa benki hiyo. Bw. Wolfensohn mara tu baada ya kuchanguiwa, alianza kwa kutembelea miradi ya Benki hiyo katika nchi maskini hasa zile za Afrika, Asia na Marekani ya Kusini na kusaidia sana kuongeza ufahamu wa watu na viongozi wa nchi za dunia ya kwanza kuhusu hali halisi ya maisha katika nchi maskini.

Mpaka kufikia mwisho wa vipindi vyake viwili vya kuiongoza Benki ya Dunia, Bw. Wolfensohn alikuwa ameshatembelea nchi 120. Huo ni wastani wa nchi 12 kwa mwaka. Katika ziara zote hizo, alikuwa akifuatwa na makundi makubwa ya waandishi wa habari wakitaka kuona malengo ya ziara zake maana ni kitu ambacho kilikuwa hakijawahi kufanywa na rais yoyote wa taasisi hiyo kubwa za fedha duniani. Alipigwa picha akila na wanavijiji wa Afrika magharibi, akicheza ngoma za asili huko Asia, na kushiriki shughuli nyingine nyingi za kijamii na kiuchumi katika nchi zote zile alizo-dhuru katika harakati yake ya kukagua miradi mbalimbali ya tasisi hiyo.

Mwaka 2005 alitangaza kujiuzulu na rais wa kumi kuchaguliwa ambaye ni Bw. Paul Wolfowitz. Kufuatia historia yake ya awali, mategemeo ya utendaji mzuri hasa kwa manufaa ya nchi masikini hayakuwa makubwa sana maana kwa kipindi cha miaka mitano iliyotangulia, Bwana Wolfowitz alikuwa naibu waziri wa Ulinzi wa Marekani na inasemekana ni yeye aliyerasimu sera nzima ya mambo ya nje ya Rais wa sasa wa Marekani, ambayo kwa kiwango kikubwa ni ya kibepari na kibabe zaidi isiyokuwa na chembe nyingi za kuboresha maendeleo ya nchi maskini.

Lakini katika hatua isiyotegemewa, Bw. Wolfowitz ameonyesha dalili za kufuata nyayo za Rais aliyemtangulia kwa kuanza kutembelea nchi maskini. Na yeye kwenda hatua mbele zaidi kwa kufanya mazungumzo na jumuiya ya Afrika mashariki hata kufikia hatua ya kueleza kufurahishwa kwake na biashara huria, maendeleo ya miundombiu katika kanda hii na kufikia kusaini hati ya maelewano kati ya benki yake na jumuiya ya Afrika mashariki.

Zaidi ya mkutano huo na viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki uliofanyika huko Arusha, Rais huyo wa Benki ya Dunia alitembelea maeneo kadhaa nchini kuona maendeleo ya nchi ikiwemo ziara yake maarufu huko Manzese ambapo alishangazwa kuona jinsi watu walivyo maskini lakini wenye furaha.

Kwa tathmini yake anadhani Tanzania iko katika njia sahihi kufikia kundi la nchi zenye kipato cha kati kufikia mwaka 2025. Tanzania ambayo kwa sasa imeorodheshwa katika nchi maskini duniani inao uwezekano wa kufikia nchi za kipato cha kati, kwa sababu ya mipango yake ya maendeleo na matumizi mazuri ya fedha za misaada ya kigeni. Alivutiwa pia na amani, uthabiti wa siasa na umoja tulionao.

Lakini kando na sifa zote hizo, bado serikali yetu ya awamu ya nne haijakaa chini na kutulia kisha ikapanga mikakati/mipango madhubuti ya maendeleo ya kiuchumi inayoeleweka. Mipango endelevu ya kiuchumi kama ambayo Malaysia ilipanga chini ya waziri mkuu wao Dr. Mahathir Mohamad katika miaka ya tisini. Ili iendelee kwa haraka, Tanzania inahitaji kubuni mipango mikubwa-mikubwa ya kiuchumi, kama Malaysia na nchi zingine za ki-asia maarufu kama "Chui wa Asia" walivyokaa chini na kubuni [ Hong Kong, Taiwan, Singapore na Korea ya kussin.]

Tanzania inatakiwa kuandaa mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na wale wa kigeni. Hapa nikiwa na maana ya miundombinu bora na ya kisasa. Barabara nzuri (Highways) kwa kusudi la kufikia masoko kirahisi. Kadhalika maeneo ya kuvutia ya kibiashara yakiwemo majengo marefu yanayofikia mawingu (skyscrapers) yajengwe kwa wingi ili wawekezaji wa kigeni wavutiwe na hatimaye waweze kukodisha majengo hayo na kuyatumia.

Pia serikali ihakikishe kuwa inawekeza katika uzalishaji wa vitu ambavyo vitasafirisha nje ( exports ) kwa makusudi ya kuliingiza taifa fedha za kigeni. Tupinge/tusipinge hakuna nchi inayoweza kujikwamua katika janga la umasiki kwa kutegemea masoko ya ndani tu! Na kwasababu hiyo basi wana-uchumi wa serikali inabidi waamke usingizini na kuanza kukuna vichwa na kuja na mawazo ya wapi serikali iwekeze. Kama ni katika kilimo, basi watilie mkazo zao moja ama mawili na kuhakikisha kuwa hayo mazao yanaendelezwa na kuiwezesha nchi kupata fedha nyingi za kigeni zinazotosha.

Sambamba na hilo , suala la usalama nalo lapaswa kuimarishwa. Magari ya Zimamoto ya kisasa yanunuliwe na vituo vya zimamoto vijengwe karibu na maeneo ya kibiashara ili wawekezaji wajenge imani na kushawishika kuwa serikali inawajali na kuwathamini.

Benki ya Dunia imeonyesha matumaini mazuri kwa kuiamini serikali kwa mambo mazuri inayofanya. Swala kubwa hapa ni kuendelea mbele ili kwamba baada ya kupata sifa hizi kem-kem tusije tukabweteka na kuridhika kana kwamba tumefika. Bado hatujafika. Kuivutia benki ya dunia ni mwanzo mzuri ila bado safari ni ndefu na ngumu inayohitaji viongozi wanaotazamia mambo makubwa ambayo raia wa kawaida akiambiwa: "hili ndilo tunalokusudia kufanya," aseme: "hilo haliwezekani." Kusifiwa kwetu na Benki ya dunia isiwe ndio chanzo cha kulitia maji tembo letu.

Mungu Ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.