KWANINI SEKTA YA AFYA NCHINI HAIPEWI KIPAUMBELE?

Na, <bongotz.com> [First posted on: 08/11/06]

Upatikanaji wa huduma ya afya ni haki ya msingi ya kila mwananchi. Na ni wajibu wa kila serikali yoyote ile duniani kuhakikisha kuwa wananchi wake wote wanapata huduma hiyo ya msingi bila ubaguzi wala upendeleo wowote ule, aidha wawe wanaishi vijijini ama mijini. Afya ni uhai na uhai ni Afya.

Lakini kwa muda mrefu sasa serikali yaTanzania imekuwa ikilifumbia macho tatizo sugu la upatikanaji wa huduma bora za afya nchini na kujikausha kana kwamba tatizo halipo huku ikiwaacha wananchi wake waendelea kuteseka bila msaada wowote ule na kusababisha ongezeko kubwa la vifo kwa maradhi ambayo yangeweweza kutibika kirahisi.

Uhaba mkubwa wa wauguzi, madawa, na vitendea kazi katika sekta ya afya limekuwa tatizo la kudumu nchini, na marais huja wakapita bila hata mmoja wao kujihangaisha wala kujishugulisha kulitafutia tatizo hili ufumbuzi wa kudumu.

Si kweli kwamba serikali yetu ni masikini kiasi hicho hata kushindwa kusambaza madawa ya msingi kama Panadol na Asprini kwenye kliniki na hosiptali kuu; ila tu ni utendaji mbovu wa baadhi ya viongozi wa chama na serikali ambao [binafsi] wanajua kwamba hata wakiugua hawawezi kutibiwa katika hizo hospitali ucharwa isipokuwa ulaya.

Ukweli ni kwamba, nchi wafadhili na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi wamekuwa wakijitolea mno katika kuinua sekta ya afya nchini ila viongozi wetu tu ndio wasiopenda kuwajibika.

Na kwakuwa hawataki kuwajibika, sasa umefika wakati sisi wenyewe [wananchi] tuamke na kuwawajibisha viongozi wote wabovu wasio taka kutumika kwa maslahi ya taifa ila yao binafsi.

Tutawawajibisha vipi, lakini?

Rahisi.

Kama ilivyo kwa nchi za magharibi, tunapaswa sasa kuanzisha vikundi vidogovidogo (grassroots movement) vitakavyo hakikisha kuwa viongozi hawa wanawajibika. Sio kuwajibika tu bali pia kuhakikisha kuwa wanasikiliza hoja zetu na kuzifanyia kazi.

Kwa wale wote wanaotaka kukimbilia Dodoma pamoja na Ikulu ya magogoni lazima watueleze watakavyotatua matatizo yetu. Kwamba, Dr. Harrison Mwakiyembe ataporudi kuomba kula Kyela, movement imuulize, "mwaka huu unaahidi kuongeza vitanda vingapi katika hospitali ya wilaya?" Kadhalika wananchi wa Tarime nao wamuulize Mbunge wao "umejiandaa vipi kututatulia tatizo la ukosefu wa madawa katika hospitali yetu ya wilaya?" Na watu wa Mbulu nao wamuulize Philipo Sangka Marmo, "nini mikakati yako katika kutatua tatizo lililopo la upungufu wa wauguzi katika hospitali yetu ya wilaya/mkoa?"

Ni wajibu wetu sisi wenyewe (watanzania) kucharuka na kudai haki zetu za msingi katika maeneo ya msingi kama vile afya., elimu na ajira; vinginevyo, wanasiasa hawa watakuja, tutawachagua, nao watarudi kwenda kupewa mashangingi na kulala bungeni huku sisi tukibaki kumia na kuteseka.

Kwa upande wa serikali kuu: wito wetu wa kwanza ni kwa mheshimiwa waziri Mwakyusa. Ndugu waziri, ili kupunguza tatizo la wauguzi nchini, ni jukumu lako wewe binafsi kupitia watumishi mbalimbali wa wizara yako kuhakikisha kwamba: wanafunzi walioko mashuleni, wanashawishiwa na kuvutiwa kuchukua masomo ya sayansi ya utabibu ili kwamba waganga, waganga wasaidizi, manesi, wafamasia n.k. wapatikane wa kutosha.

Ndugu Waziri, uwepo mfumo wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wa masomo ya utabibu wanaelimishwa vizuri katika vyuo vyetu vinavyoelimisha watumishi wa sekta ya afya na hata wengine kupewa nafasi kwenda nje kupata elimu ya juu zaidi (scholarship).

Wanapohitimu na kupata kazi katika sekta hii muhimu ya afya, basi serikali ihakikishe kwamba wanalipwa vizuri kiasi cha kuwaridhisha ili kwamba waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi bila kuwa na wasiwasi wa kutokumudu maisha. Hili ni muhimu sana. Maana kama hawaridhiki watagoma. Na kama hawatagoma, basi wataondoka na kwenda nchi jirani kutafuta malipo mazuri.

Na ikitokea bahati mbaya wakagoma [sakata la Muhimbili tunalikumbuka] madhara yake ni makubwa zaidi. Wafanyakazi wa sekta zingine wakigoma, utendaji na uzalishaji unapungua au kusimama, wafanyakazi wa sekta ya afya wakigoma, watu wanakufa.

Mheshimiwa waziri, afya ya wananchi haiishi hospitalini tu. Serikali inatumia gharama nyingi sana kuhudumia na kutibu magonjwa na matatizo yanayoweza kuzuilika kwa njia rahisi. Hivyo tunakushauri kama ukiona vyema, angalia namna ambayo pamoja na mambo mengine, utaielekeza serikali kuwekeza katika kuelimisha wahudumu wa afya ili kwamba nao waweze kuelimisha jamii kuhusu usafi binafsi na kanuni za asili za kuzuia magonjwa. Waswahili husema, kuzuia ni bora kuliko kutibu.

Wananchi wafundishwe kunawa mikono kabla ya kula na baada ya kutoka msalani. Wafundishwe kuosha vyakula vinavyoliwa bila kupikwa. Pia wafundishwe kula chakula bora na kuhakikisha uwiano wa lishe katika kila mlo wanaokula. Waelimishwe kwa mfano, mlo wa kila siku ili kuwa na afya njema unatakiwa uwe natakribani protini kiasi gani, vitamini kiasi gani, wanga kiasi gani, hamirojo kiasi gani, n.k.

Wananchi waelimishwe kuhusu umuhimu wa kufanya mazoezi pia. Nchi za magharibi zinatumia fedha nyingi sana kujaribu kusaidia raia wao kupunguza uzito. Kwa hiyo kama Tanzania itaanza kulishughulikia hili mapema, basi itaokoa fedha nyingi mbeleni ambazo zingelazimika kutumika kusaidia watu wenye uzito mkubwa na matatizo yanayotokana na uzito huo kama magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, n.k.

Maji safi. Serikali iandae mpango maalumu wa kuchimba visima nafuu ili wananchi hususani katika maeneo ya vijijini wapate maji safi na salama, kwani wakati wa ukame wanachi wengi vijijini hulazimika kunywa maji machafu ambayo ni chanzo kikubwa cha magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.

Serikali pia iangalie namna ya kuwezesha wananchi kupumua hewa safi. Hili ni jukumu la serikali, maana uchafuzi mwingi wa hewa unaweza kudhibitiwa na serikali kama kudhibiti kiwango cha hewa taka (Exhaust gases) zinazosababishwa na viwanda, mashine na magari. Ni vema kama maeneo maalumu ya viwanda yakitengwa sehemu ya mbali kabisa na makazi ya wananchi.

Mtazamio wa maisha(Life expectancy) kwa nchi yetu ni miaka 42 kwa wanaume, na miaka 44 kwa wanawake. Hiki sio kiwango kizuri. Hali na huduma ya afya nchini inapaswa kuboreshwa ili mtazamio wa maisha (Life expectancy) uongezeke.

Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.