JE, KIKWETE ANASTAHILI SIFA ZOTE HIZI?

Na, Edward chacha <Posted First on: 08/15/06 >

Taasisi mbalimbali pamoja na vyombo vya habari nchini vimeendelea kumwagia sifa kibao Rais Kikwete kana kwamba kauli mbiu yake ya "...ari, nguvu, na kasi mpya," peke yake ndio jawabu tosha la kuwaondolea watanzania matatizo mbalimbali ambayo yamekuwa yakiwakabili kwa muda wa miaka arobaini na sita (46) sasa tangu Tanganyika ilipojiweka huru. Adha ya maji, upungufu wa nishati, tatizo la ajira, huduma mbaya mahospitalini, na utumiaji mbovu wa vitega uchumi na mali asili zilizopo (i.e mikataba mibovu), ni miongoni mwa matatizo hayo.

Sifa nyingi sana zimeandikwa juu ya Rais Kikwete kwa kipindi kifupi alichokuwa madarakani, lakini kwa tathmini ya haraka inakuwa vigumu kuelewa kama sifa hizo ni za kweli ama ni unafiki tu uliojificha ndani ya uwezo duni wa waandishi/wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari nchini katika uchambuzi/upambanuzi wa mambo ya kimaendeleo katika mtizamo mkubwa (big perspective).

Tatizo la maji nchini ni mfano mzuri wa kutizamwa. Rais, katika hotuba yake aliyoitoa bungeni tarehe 30/12/05 alisema nami namnukuu: "...Tatizo la maji ndicho kilio kikubwa cha Watanzania mijini na vijijini. Serikali ya Awamu ya Nne inakusudia kulikabili tatizo hili kwa Ari mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya. Ni makusudio yangu kuwa tuwe na mpango kabambe wa maji kwa nchi nzima. Mpango ambao utajumuisha mkakati na mbinu za kutekeleza kwa kasi sera ya maji na kutatua tatizo la maji. Aidha, tutakamilisha miradi mikubwa ya ukarabati na upanuzi wa maji safi na maji taka Dar es Salaam na ule wa kupeleka maji katika miji ya Kahama, Shinyanga na Vijiji vitakavyopitiwa mabomba kutoka Ziwa Victoria” Mwisho wa kunukuu.

Lakini ukiangalia bajeti ya wizara ya maji 2006/2007. Sekta ya maji imetengewa asilimia 8.47% tu ya fedha. Hivi kweli serikali inaweza kufikia malengo yake chini ya mpango wa MKUKUTA (Millenium Development Goals--MDGs) wa kufikisha maji safi karibu na makazi ya asilimia 65% ya wananchi wote wa Tanzania ifikapo 2010 kwa kiwango hicho kidogo cha bajeti kilichotengwa? Kwa bajeti kama hii, ni dhahili kuwa lengo hili haliwezi kufikiwa. Sijui kama waandishi na wahariri wa vyombo vya habari nchini wanaliona hili?

Si hilo tu, hata mradi wa kupeleka maji ya ziwa Victoria kwa wakazi wa Kahama na Shinyanga yaelekea ni mradi tu usio na mipango yoyote ya kueleweka. Na penginepo hii ni janja tu ya serikali kupeleka maji karibu na migodi ya madini kupitia kivuli cha wananchi. Ukweli ni kwamba, kama kweli serikali ingekuwa na mipango madhubuti ya kueleweka kuhusiana na mradi huo, basi ingeandaa mipango madhubuti ya kutumia maji hayo kwa shughuli za kilimo (umwagiliaji).

Nitakubaliana na msemaji mkuu wa kambi ya upinzani wizara ya maji, mh. Chacha Wangwe (Mb) Tarime (marehemu) kuwa: endapo kama maji ya ziwa victoria yatatumiwa vema kwa shughuli za umwagiliaji, basi Tanzania inaweza kabisa kuondokana na adha ya kuomba omba chakula.

"Teknolojia ya umwagiliaji kwa ajili ya kilimo ni ya kale mno kihistoria," aliwahi kusikikika mbunge huyo akisema, "Kwanini sisi itushinde?" "Hata nchi jirani ya Misri ni mfano bora wa kujifunzia. Teknolojia ya mifereji ya umwagiliaji (Canals) ilianza yapata miaka 4,000 iliyopita. Historia inaonyesha kuwa umwagiliaji ndio ulikuwa kitovu cha ustawi wa dola staarabu za kale kama Misri ya Kale kandokando ya Mto Nile, Kaldayo kandokando ya mito Tigris na Euphrates. Mifano mingine ni tamaduni zenye uchumi mzito zilizojengwa kandokando ya Mto Ganges (India) Mto Yang-Ze-Kiang (China), na hivi karibuni Mto Mississippi (Marekani), Maendeleo ya Viwanda Ujerumani (Ruhr Industrial Base) kandokando ya Mto Rhine Ustawi wa Kilimo viwanda na miji kandokando ya Mto Thames (Uingereza)."

Katika suala la kuimarisha uchumi wa nchi yetu, serikali bado haijui inachokifanya. Kimsingi, Rais haonekani kama amejiandaa vema katika suala hili. Kando na kulumbana na watu binafsi kama vile makandarasi wa barabara za mikoani (kazi ambayo ingeweza kufanywa na Waziri wa Miundombinu) na hivi karibuni mteng'enezaji wa mshito wa Darwin's nightmare (kazi ambayo pia ingeweza kufanywa na waziri wa Habari), bado Rais haeleweki kakusudia kufanya nini katika kipindi chote cha muhula wa kwanza ili kuinua hali ya uchumi katika nchi hii masikini iitwayo Tanzania.

Rais ni kiongozi mkubwa sana! Kwa mantiki hiyo basi, hapashwi kabisa kujiingiza katika malumbano na watu binafsi. Madhali Mawaziri wapo, madhali wakuu wa Idara mbalimbali za serikali wapo, madhali mabalozi wapo, madhali wakuu wa mikoa na wilaya wapo; Rais kama mkuu wa nchi, anapashwa kutumia vizuri muda wake na kofia aliyonayo kuwabana na kuwatikisa wanauchumi wake kujadili na kupanga mikakati mbalimbali ya kuimarisha hali ya uchumi nchini na kusimamia shughuli kubwa za kiserikali (ndio maana kuna mgawanyiko wa madaraka).

Angalia kwa mfano sekta ya utalii nchini. Wataalamu mbalimbali wa mambo ya uchumi duniani wanakiri na kuafiki kuwa, endapo kama serikali ingewekeza vema na kujiimarisha katika sekta hii, basi Tanzania ingejiweka katika ramani ya duniani kama moja ya nchi nyenye vivutio vizuri kwa watalii na hivyo kujipatia mamillioni kama sio mabillioni ya fedha za kigeni kupitia sekta hii kila mwaka.

Tanzania ni moja ya nchi nne (4) duniani kwa kuwa na bioanuwai (biodiversity) nyingi na za aina mbalimbali. Toka Kilimanjaro mpaka Rukwa, Tanzania imejaa vivutio vingi na vizuri vya asili: Mapori ya Akiba 34 (Game Reserves), mlima mrefu barani Afrika (Kilimanjaro), Hifadhi kumi na mbili (12) za Taifa (National Parks), ikiwemo hifadhi maarufu na kubwa duniani ya Serengeti yenye kusaidikiwa kuwa na aina mbalimbali za wanyama baadhi wakiwa wanapatikana Tanzania peke yake. Achilia mbali vivutio vingine vya kitalii kama vile, kisiwa cha kitalii cha Zanzibari, kilomita 800 za fukwe safi zakuvutia (beaches), bonde la Ngorongoro na makumbusho/magofu ya kihistoria (Kilwa, Sadani na Bagamoyo).

Lakini kando na vivutio vyote hivyo, Marais nenda rudi chini ya chama tawala cha CCM, na sasa akiwemo Rais wa awamu ya Nne Bw. Jakaya Kikwete, badala ya kuja na sera mbadala za kuinua sekta ya utalii nchini, wanahangaika na kukimbizana na vitu vidogovidogo kama vile wamachinga na wateng'eneza filamu (Jinamizi la Darwin, Hubert Sauper).

Ama ni vipi kuhusu utajiri wa madini mbalimbali kama vile dhahabu, almasi, bati, chuma, chumvi, makaa ya mawe na tanzanite inayopatikana tanzania peke yake!? Nini hasa Rais alichokifanya kwa kipindi chote alichokuwa madarakani zaidi ya kauli kavu ya kupitia upya mikataba mibovu ya madini hali ujasiri wa kuibadili/tengua mikataba hiyo hana?

Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania ina utajiri wa kutosha na inaweza kabisa kufanya vizuri zaidi ya kukurukakara za hapa na pale za kupapasa mambo madogomadogo zinazofanywa na serikali ya awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete. Tatizo ni kwamba, kama wananchi wenyewe wamelemazwa na kauli mbiu ya "...nguvu, kasi na ari mpya," ni vigumu kwao kuamka na kugundua kuwa kauli hizo ni kelele tupu zisizolipeleka taifa letu mahala popote pale.

Utajiri wa Tanzania hauishii kwenye madini na utalii tu, kuna vitu vingine vingi kama vile hekari millioni 44 za misitu (Lakini shule hazina madawati!), ziwa kubwa barani Afrika (Victoria) lililojaa kila aina ya samaki kama vile Sangara ambao wengi wanaishia Ulaya chini ya mikataba mibovu. Tanzania ina gesi za asili (songosongo) , bandari kuu nne za Dar-es-salaam, Tanga, Zanzibari na Mtwara lakini bado bajeti ya Taifa tunategemea nchi wahisani!?

Well, serikali ya awamu ya Kwanza, ya Pili na ya Tatu wangeweza kusingizia mzigo wa kulipa deni la nje. Je, serikali ya Kikiwete ina nini cha kusingizia?

Ni kweli kwamba serikali ya awamu ya Nne kwa muda wa miezi minane (8) tu madarakani haiwezi kuondoa matatizo ambayo yamedumu kwa kipindi cha miaka araobaini na tano (45) tangu nchi yetu ianze kujitawala, ila kwa kipindi hiki kifupi, tumejionea na kujifunza kuwa serikali ya awamu ya Nne haina mipango mbadala ya kiuchumi itakayosaidia kulichukua taifa letu kwenda katika hatua nyingine, hatua bora zaidi ya hii tuliyonayo.

Kumekuwa na mipito mbalimbali yenye kusudi la kuleta mageuzi ya uchumi nchini tangu mwanzoni mwa miaka ya themanini (80). Mpango wa NESP (National Economic Survival Programme--1981-1982), mpango wa SAP (Structural Adjustment programme--1982-1985), mpango wa ERP ( Economic Recovery Programme--1985-1989), na mpango wa ESAP (Economic and Social Action Programme--1889-1992). Lakini kando na mipango yote hiyo hali ya uchumi nchini bado inazidi kuzorota.

Mwishoni mwa miaka ya tisini (90) serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali nje na ndani ya nchi iliandaa mikakati mbalimbali ya kuinua uchumi na kupunguza umasikini, Dira ya Taifa ya 2025 (vision 2025) ya kupambana na umasikini ilikuwa miongoni wa mikakati hiyo. Lakini kwa takribani miaka kumi sasa tangu kuanzishwa kwake, Dira hiyo haijaleta mageuzi yoyote yale ya kiuchumi.

Watanzania kwa pamoja tunatakiwa kuamka na kuibana serikali ili iweke kipaumbele kwenye sera zinazoleta mabadiliko ya kweli ya kiuchumi na sio vinginevyo. Mabadiliko yatakayo boresha huduma za kijamii, inua kipato cha mwananchi wa kawaida, imarisha miundombinu na kupunguza tatizo sugu la ajira nchini. Pia, waandishi wa habari na wahariri wa vyombo vya habari ni wakati sasa wa kutizama mambo katika mtazamo kubwa (big perspective). Suala la kumpatia Rais sifa za kinafiki, huu sio wakati wake. Watanzania tuna kila sababu ya kuishi maisha bora kwa sababu nchi yetu sio masikini kama inavyotajwa.

Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.