FRANCO THE GREAT AKANYAGA ARDHI YA KALE

Na, Antar Sangali (Bagamoyo)

Mchoraji bingwa duniani toka jimbo la New York (Harlem) nchini Amerika Bw. Franklin Gaskin maarufu kama Franco The Great hivi karibuni alikanyanga ardhi ambayo babu zake wakizaliwa.

Mji wa Bagamoyo kama mlango mkuu uliokutanisha miingiliano ya tamaduni nyingi, makabila mbalimbali, lugha, dini na kupokea misafara ya watumwa na pembe za ndovu toka Bara ya ndani ya Tanganyika ujiji -Kigoma kupitia Tabora hadi Pwani ya Bagamoyo, unatajika kama ni mji ulio na hazina kuu ya historia ya kutisha, kusikitisha na kustaajabisha.

Siku moja kabla ya kuwasili katika mji huu Franco The Great alionekana usiku katika vituo vya luninga jiji Dar es Salaam akitambulishwa na wenyeji wake mbele ya waandishi mbalimbali wa habari.

Siku iliyofuata Franco akifuatana na mtanzania anayeishi nchi Marekani, Bill Mushi na kuingia moja kwa moja katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Luteni Kanali Mstaafu Serenge Mrengo kumjulia hali na kutambuana.

DC wa Bagamoyo baada ya kumtambua Frankilin na wasifu wake katika uwanja wa sanaa ya uchoraji; alifurahia kukutana na mtu mashuhuri toka Amerika na hasa kuja kwake kuutembelea mji wa Bagamoyo wenye vivutio vingi vya kuvutia.

Bila kusita DC alivitaja kwa kukariri vivutio vilivyotanda katika wilaya nzima ya Bagamoyo kiasi cha kumfanya Franco kuzubaa kwa dakika kadhaa huku akimtazama akiwa amevaa miwani yake ghali aina ya Ray Ban.

Alielezwa historia ya Bagmoyo na jinsi misafara ya utumwa ilivyopitishwa na kupelekwa katika soko kuu la Zanzbar kabla ya kusafirishwa watumwa hao katika mabara ya Asia, Ulaya na Amerika kisha kutumika kama nguvu kazi viwandani na majumbani.

Alitajiwa kuwepo kwa mbuga ya kipekee ya Saadan inayokutana na Bahari iliyojaa wanyama wa kila aina, msitu wa asili wa Saraninge, miingiliano ya mto Ruvu na Bahari ya Hindi na kuzaliana kwa kasa wa rangi ya kijani ambao ni adimu duniani, lakini pia maeneo ya kihistoria na mikoko iliyoko pembeni mwa bahari na mto sanjari na fukwe ndefu zenye mchanga mweupe wa kupumzika.

Franco The Great alimshukuru DC na kusema Bagamoyo ina vitu vingi vya kuringia na kujinasibu ingawaje bado havijatangazika duniani.

Aliitoa kalamu yake na kadi moja inayoonyesha baadhi ya kazi zake anazozifanya kwa mikono yake miwili iliyoshiba afya na kisha kuandika maneno kadhaa kabla ya kumkabidhi DC kama ukumbusho.

Akifuatana na mtembeza watalii mashuhuri katika mji wa kale Bagamoyo Profesa Samahani Kejeli, Franco alifika katika kituo cha mwisho cha misafara ya watumwa kitwacho Cravan Serai na kuelezwa masuala kadhaa ya kihistoria.

Alipotoka katika kasri hilo ambalo ndani yake limesheheni masuala kadhaa ya kihitoria, alikwenda moja kwa moja hadi katika kituo cha wasanii wachoraji kiitwacho Asante Arts Gallery and Baobao Studio ambako alikaa humo kwa takriban saa moja akistaajabu sanaa za kitanzania.

Mkurugenzi wa kituo hicho Bw Kingstone alimtembeza Franco katika eneo linalochorwa picha mbalimbali za wasanii na kwenye studio yao ya muziki ambako Franco alipoingia tu alikumbana na kibao cha Raggae kilichopigwa na Gregory Issack na bila kuchelea alionekana akisakata muziki bila kuzubaa.

Kabla ya kutoka katika jengo hili la Asante Arts Gallery kwa kauli yake Franco aliwambia waandishi wa habari kwamba atamtumia Kingstone kalamu za kuchorea za rangi, huku Mushi akiwaahidi wasanii wote kuwafungulia mtandao ili watangaze kazi zao duniani.

Akitoka katika kituo hicho mgeni huyo mchoraji bingwa toka Amerika alitembelea vituo vingine viwili vya uchoraji, ufinyanzi na uchongaji vya AMAP na Sea View ambako pia alioana kazi za wasanii, kupiga nao picha na kubadilishana mawazo ya kitaaluma.

Frankilin alionyeshwa jengo la bandari ya kwanza katika Tanganyika, Posta ya kwanza, akaliona Boma la wajerumani na ngome ya wajerumani kabla ya kufika katika mabaki ya mji wa Kaole ambao katika karne ya 11 na 12 ulijulikana kwa jina la Pumbuji.

Aliyashuhudia mabaki ya majengo ya washirazi na makaburi huku akihadithiwa habari moja hadi nyingine na Profesa Kejeli ikiwa ni pamoja na kuona kaburi la wapendanao, kaburi la mtoto mdogo wa kike ambalo baadhi ya watu hulitumia hadi leo kufanyia maombi kwa masahibu yanayowadhili kimaisha na kiafya na kufanikiwa.

Franco The Great muda wote akiwa na mwenyeji wake Bill Mushi alionekana mwenye furaha na bashasha kabla ya kuingia ndani ya gari lake na kuelekea jijini Dr es Salaam.

Kabla hajafunga mlango nilimsaili Franklin kuhusu ziara yake katika mji huu na vipi ameweza kufaidika kwa kuona kwa macho yake na yeye akanijibu kwa makato "kuona ni kuamini"

Ndiyo, kuona ni kuamini. Franco The Great amekuja akaona historia ndefu na pana ya nchi yetu na kuondoka. Swali linalobaki wazi ni hili: Je, serikali itaanza lini kuyatangaza maeneo mbalimbali ya kihistoria kama vile Bagamoyo (kupitia sekta ya utalii) kwa lengo la kuliingizia Taifa fedha za kigeni?

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

 

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.