DARWIN'S NIGHTMARE:JE, KUNA UKWELI NDANI YAKE?

Na,mwandishi wetu

Gazeti la kila siku la kiswahili, Alasiri [01, August, 2006] lilichapa habari iliyokuwa na kichwa "Rais kufa na mtu" na kuelezea jinsi Rais Kikwete alivyo kasirishwa na tuhuma nzito ndani ya mshito (documentary) ya Darwin's Nightmare iliyoteng'enezwa na mzungu Hubert Sauper mzaliwa wa Austria aishiye Ufaransa. Rais, alikaririwa akidai kuwa madai ya Bw. Sauper yalikuwa ya kizushi na yasiyo na ukweli wowote ndani yake. Lakini kwa uchunguzi uliofanywa na tovuti hii, madai ya Bw. Sauper huenda yana ukweli fulani ndani yake.

Darwin's Nightmare ni mshito (Documentary) ambao ulitengenezwa mwaka 2004. Filamu hii imejengeka katika swala zima la biashara ya minofu ya samaki katika ziwa Victoria nchini Tanzania.

Tunajua kwamba utumwa, ukoloni, njaa, magonjwa na mauaji ya halaiki, vimeathiri sana historia ya bara letu. Lakini filamu hii inajaribu kuifahamisha dunia kwamba utandawazi (Globalization) na swala zima la mfumo mpya wa dunia ndiyo chanzo hasa cha udhalilishaji wa kisasa wa bara letu la Africa.

Filamu hii ina-shita (Document) unyonyaji na dhuluma wanayofanyiwa watanzania na waafrika katika nchi zote zile ambazo zina rasilimali zinazohitajika nchi za magharibi, katika suala hili, minofu ya samaki ambapo inaaminiwa kwamba tani 500 za minofu ya samaki zinazalishwa kila siku na kusafirishwa hasa nchi za ulaya kulisha watu zaidi ya milioni 2 kila siku, wakati raia wanaozunguka ziwa Victoria, kwa sababu ya umaarufu wa minofu hiyo huko Ulaya, bei yake imekuwa juu sana kiasi kwamba wanakijiji hawawezi kumudu kununua na wao kuishia kula vichwa na mifupa ambayo imetupwa kutoka viwandani.

Mshito (documentary) huo unaeleza kwamba biashara ya minofu ya samaki huko Mwanza ndiyo kitovu kikubwa cha silaha zinazoendeleza vita za wenyewe kwa wenyewe katika nchi za kusini mwa Afrika na eneo la maziwa makuu (japo Rais Kikwete anakataa na kusema kuwa hakuna ushahidi wowote wa kuthibitisha madai hayo).

Filamu yenyewe inaonyesha madege makubwa ya mizigo ya kirusi ambayo yanaleta shehena ya silaha na kuondoka na shehena ya minofu ya samaki. Wakati mwingine madege hayo ya mizigo yanakuja na misaada kwa wakimbizi kama chakula kutoka nchi za magharibi lakini pia shehena hizo zinajumuisha silaha za kuwaua wakimbizi hao hao wanaojifanya kuwasaidia.

Kwa mujibu wa Shirika la haki za binadamu ulimwenguni ( Human Rights Worldwide) ushahidi unaonyesha kuwa mnamo October 2, 20001 kuna ndege moja ya shrika la UCA [Ukrainian Cargo Aiways] yenye namba za usajiri UR-UCK ilitua mjini Mwanza majira ya saa 8.40 asubuhi na kuzuiliwa na maafisa usalama wa Tanzania kwa madai kuwa ilikuwa na silaha (undeclared weapons) ndani yake. Lakini cha kushangaza ni kwamba ndege hiyo iliruhusiwa kuondoka baadaye kwa amri toka kwa maafisa wa juu wa usalama serikali.

Kuna ripoti nyingine nyingi tu huko nje zinazodai kuwa Tanzania imekuwa ikitumia ardhi yake kuruhusu silaha kusafirishwa kwenda katika nchi jirani za Rwanda, Burundi, Angola na Zaire ya zamani.

Pia katika filamu hiyo, utaona marubani wa kirusi wakieleza jinsi wanavyoleta silaha kuendeleza vita huko Congo na Angola na kuondoka na minofu. Mmoja wao anaeleza matumaini yake kwamba labda siku moja watoto wote duniani watakuwa na furaha. Anaeleza hilo kwa kusikitika akisema watoto huko Angola walipata silaha kwa ajili ya Krismas, wakati huko ulaya watoto wao walipewa zabibu. Anasema hii ni biashara lakini anatamani watoto wote wangepata zabibu. Utaona binti wakitanzania aliyeishia kufanya biashara ya ukahaba na kuwaimbia wateja wake wimbo maarufu wa “Tanzania, Tanzania, nakupenda kwa moyo wote.” Ingawa binti huyu bado ana ndoto za kujiendeleza kielimu. Utaona mlinzi ambaye analinda viwanda vya kusindika minofu kwa upinde na mishale yenye sumu. Anaelezwa kuwa ni askari hodari aliyewahi kupigana vita kadha wa kadha. Lakini, kana kwamba ni kitu kibaya, amani iliyopo Tanzania inamfanya sasa badala ya bunduki kubwa kama 'Riffle,' sasa ana upinde na mshale na badala ya kupigana vita, anaishia kupigana na mbu usiku katika kazi yake ya ulinzi. Huyu naye ana ndoto kwamba kijana wake atakuja kuwa rubani kama marubani anaowaona kila siku wakija kuchukua shehena za mizigo. Utaona pia mchungaji ambaye amezika wanakijiji wengi kwa ugonjwa wa ukimwi lakini bado hakubaliani na swala la matumizi ya condom maana ni dhambi. Wote hawa wanaonekana kuwa wahanga wa mfumo mzima wa ubepari na utandawazi.

Kimsingi filamu inaonyesha jinsi wakulima na wavuvi wenyeji, wanavyotegemea saaaaana biashara ya kuuza mazao yao nje na kuwaacha wenyeji bila chakula jambo linalopelekea baa la njaa, umaskini, ukahaba, ukimwi, uhalifu na matumizi ya madawa ya kulevya. Mtengenezaji wa mshito (documentary) huu anasema ingawa katika filamu hii anazungumzia samaki, lakini angeweza kutengeneza filamu nyingine kama hii kuhusu Sierra Leone, ingawa samaki huko ingekuwa almasi. Angeweza kutengeneza filamu kama hiyo kuhusu Honduras, ingawa huko samaki ingekuwa ndizi. Na angeweza kutengeneza filamu kama hiyo kuhusu Libya, Nigeria au Angola ingawa huko samaki wangekuwa mafuta. Na anasema inashangaza jinsi ambavyo mahali popote panapogunduliwa rasilimali kubwa, taratibu wenyeji wanaanza kufa kinyonge, vijana wao wanaishia kuwa askari wa vita na mabinti zao wanakuwa watumishi au makahaba.

Kimsingi filamu inaeleza mzunguko wa biashara hii tandawazi ya ndege kubwa za mizigo zinazodhaniwa kuleta misaada ya chakula na madawa Africa lakini badala yake zinaleta silaha nyingi zaidi ya misaada. Na kuondoka na minofu yenye lishe nyingi ya samaki wa ziwa Victoria ambao kama wangeliwa na wenyeji, wenyeji wangenufaika kiafya. Lakini kwa sababu ya mahitaji ya nchi ya fedha za kigeni, basi minofu inaenda kwa wenye fedha za kigeni. Na katika mzunguko huo, filamu hii ina-shita(Document) madhara, maafa na athari kubwa zinazobakia kwa wenyeji baada ya ndege hizo kuondoka. Njaa, magonjwa, umaskini, ukahaba, matumizi ya madawa ya kulevya na vita za wenyewe kwa wenyewe. Ubaya tu ni kwamba, huo siyo mwisho wa tatizo, ndege hizo zitarudi tena na tena na tena na kuleta silaha zaidi na kufanya madhara na maafa zaidi.

Ingawa mshito (documentary) huu ulitengenezwa mwaka 2004, lakini filamu iliteuliwa kushindania tuzo maarufu ya Oscar--march 5, 2006. Ingawa filamu hiyo haikushinda, lakini kwa namna moja ama nyingine imechangia kuongeza ufahamu wa watu wengi kuhusu tatizo hili la utandawazi (Globalization) katika nchi za dunia ya tatu.

>MAONI YA WASOMAJI WETU: [Kongoli hapa>]

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.