ILI KUIBADILI BONGO, "WA-TANK MEN" WANAHITAJIKA

Na, Edward Chacha <Posted first on: 08/17/07>

Baada ya wandamanaji wengine wote kuwa wamenyamazishwa tuli na zaidi ya watu mia saba wakiwa wameripotiwa kuuawa, picha ya shujaa mwenye shati jeupe na suruali nyeusi akiwa amesimama peke yake mbele ya sanjari ya vifaru vya kijeshi vilivyokuwa vikiviringika kuelekea kwenye viwanja vya Tiananmen kuwatawanya wanafunzi-wandamanaji itabaki kuwa na sehemu ya pekee kila mara siku ya kihistroria ya jumatatu June 4, 1989 itakapokumbukwa. Wang Weilin ni jina bandia alilopewa Rais mstaafu Jiang-Zemin (kipindi hicho katibu mkuu wa CCP) alipotaka kujua zaidi kuhusu mwandamanaji huyo. Lakini ukweli ni kwamba, hadi leo hii hakuna anayefahamu jina lake halisi kiasi cha kupelekea abatizwe jina bandia--"The Tank Man".

Ingawa baadhi ya wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanadai kuwa umri wake ulikuwa umepita kwa mwandamanaji huyo kuwa mwanafunzi, kilichomsukuma kusimama peke yake mbele ya sanjari ya vifaru vilivyokuwa vikielekea Tiananmen square huenda ndicho pia kilichomsukuma Gandhi kuandamana kwa mfungo wa siku 21 bila kula. Huenda pia ndicho kichomsukuma mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Zuberi Kabwe kusema alichokisema bungeni hata kupelekea kusimamishwa kuendelea kushiriki vikao vya Bunge kwa kipindi cha miezi sita hadi januari 29, 2008.

Yumkini kitu hichohicho ambacho mwanafalsafa Lao Tzu alikiita "The Tao" (virtue), ndicho pia kilichowasukuma wanaharakati wa miaka ya sitini (1960s) kama vile Martin Luther King Jr, Ho Chi Minh, Patrice Lumumba, na wengine wengi kusimama kidete na kupinga vitendo vya udhalimu na uonevu vilivyokuwa vikiendeshwa na kundi la watu wachache waliodhani kuwa wanayohaki ya kufanya kila walichojisikia kufanya pasipo kuulizwa ama kuzuiliwa na mtu yoyote yule.

"The Tank man" anatukumbusha kuwa mchakato wa mabadiliko yoyote yale yawe ya kisiasa, kijamii ama kiuchumi hayataletwa na viongozi wenye majina makubwa yaliyozoeleka masikioni mwetu (Malecela, Kingunge, Malima, Mwinyi, Chambiri, Msuya, Sitta); bali mabadiliko halisi yataletwa na raia wa kawaida watakaohiyari kujitoa mhanga ili kutetea maslahi ya taifa bila kujali yatakayowakumba hapo baadaye. Kama Rais Kennedy alivyowahi kusema, nami namnkuu: "utu wa kweli umekamilika ndani ya yule anayediriki kufanya kila awezacho kutetea haki na uhuru wake pasipokujali madhara yanayoweza kumkumba hapo baadaye."

Baada ya kupitia kwa kina hoja binafsi iliyowakilishwa bungeni na Bw. Zitto ya kuunda kamati teule ya Bunge kuchunguza mkataba mpya wa madini ambao Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamangi amesaini nje ya nchi London, Uingereza bila kuzingatia maagizo ya Rais, nashawishika kuandika kuwa Mbuge huyo hakustahili kupewa adhabu aliyopewa.

Kimsingi Bunge lilipaswa kwanza kuunda tume kuchunguza kama kweli mbuge huyo amepotosha Bunge na baadaye aadhibiwe endapo kama ingebainika kuwa amefanya hivyo. Lakini kitendo cha kumsimamisha mbuge huyo asiendelee kushiriki kwenye vikao vya Bunge vinavyoendelea huko Dodoma kabla hata ya hoja yake kuchunguzwa, ni ukiukwaji mkubwa wa kidemokrasia ambao haupaswi kufumbiwa macho.

Kitu cha kujifunza toka kwa Bw. Zitto aiyekubali kujitoa mhanga kwa maslahi ya Taifa (ingawa mahesabu ya kisiasa hayawezi kuupuzwa) ni kwamba: mustakabali wa taifa letu utategemea ujasiri wa "Wa-Tank Men" wengine wengi kama Mbunge huyo na si vinginevyo--kama kweli tunataka kuiona nchi yetu ikichukua nafasi yake katika karne hii ya 21.

Wanafunzi wa vyuo vikuu, shule za sekondari, wakulima vijijini, pamoja na tasisi mbalimbali nchini wanapaswa kuiga ujasiri wa "The Tank Man" na kuanza rasmi kutetea maslahi ya taifa letu pasipokujalli yanayoweza kuwakumba hapo baadaye.

Kama ilivyo kwa nchi za Magharibi, tunapaswa sasa kuanzisha vikundi vidogovidogo ( grassroots movement ) vitakavyo hakikisha kuwa viongozi tuliowachangua wanawajibika na kutumika kwa ajili ya wananchi na si vinginevyo.

Grassroots movement hizo zipange na ku-organize mambo mbalimbali yanayowabana viongozi waliowachaguliwa ili kuhakikisha kuwa maslahi ya taifa zima, na sio ya watu wachache, daima yanawekwa mbele.

Movement hizo zipange na kuandaa mambo kama vile:

Kwamba, Dr. Harrison Mwakiyembe ataporudi kuomba kula Kyela, movement imuulize, "...mwaka huu unaahidi kuongeza vitanda vingapi katika hospitali ya wilaya?" Kadhalika wananchi wa Mbulu nao wamuulize Philipo Sangka Marmo, "...nini mikakati yako katika kutatua tatizo lililopo la upungufu wa wauguzi katika hospitali yetu ya wilaya?" Endapo kama wataahidi kutatua matatizo hayo na kutoa maelezo ya kueleweka, basi wapewe nafasi ya kurudi Dodoma; lau wasipotoa maelezo ya kueleweka, movement itafute mbadala (alternative).

Kando na hayo, movement pia itoe kipaumbele kwenye suala la marekebisho ya katiba. Katiba ya sasa inampa Rais madaraka makubwa sana ya kiutendaji. Imefikia muda sasa kumpunguzia Rais madaraka hayo na badala yake Bunge na Mahakama ziwe na mamlaka makubwa zaidi ya kuidhibiti serikali.

Sambamba na hilo, wakati umefika pia kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wa Serikali kuchaguliwa kutoka nje ya Bunge kama ilivyo kwa nchi nyingi za Magharibi, mfano, Marekani. Haina maana ya kuwa na Bunge ambalo nusu ya wabunge ni viongozi wa serikali pia.

Umefika wakati wa kudai Katiba mpya itakayoweka bayana kwamba mawaziri wote watoke nje ya Bunge ili iwe rahisi kwao kuwajibika na kuwatumikia wananchi waliowachagua kuliko ilivyo hivi sasa.

Hivi karibuni sote tumeshuhudia ambavyo serikali kupitia Bunge ilikataa katakata kuundwa Tume ya Uchunguzi dhidi ya kashfa inayoikabili Benki Kuu nchini (BoT). Tumeshuhudia wizi wa fedha za EPA. Tumeshuhudia pia mikataba mibovu ya madini, na kashifa za Richmond na Kiwira. Hali kama hizi zitaendelea kujitokeza mpaka hapo " Wa-Tank Men" watakapoamua kujitoa mhanga na kusimama kidete kutetea maslahi ya taifa letu.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

 

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.