KWANINI UPINZANI HAUKUFANYA VIZURI KATIKA CHAGUZI ZA 1995, 2000, na 2005?

Na, BongoTz < 08/22/06>

Vyama vingi viliporuhusiwa tena mwaka 1992, ilikuwa ishara nzuri iliyoibua hamasa kuashiria ukuaji wa demokrasia nchini Tanzania. Hamasa hiyo ilipelekea kuanzishwa kwa utitili wa vyama mbalimbali vya siasa, ambapo hadi leo hii tayari kuna vyama vya siasa vipatavyo kumi na saba (17) vinavyotambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. JAHAZI-ASILI, NCCR-MAGEUZI, PPT-MAENDELEO, CHAUSTA, CHADEMA, DEMOKRASIA-MAKINI, FORD, NRA, PONA, SAU, NLD, UPDP, UMD, UDP, CUF, CCM na PPP.

Ingawa tunajua kwamba nchi yetu bado ni changa kwa siasa za vyama vingi kutokana na ufinyu wa elimu ya uraia waliyonayo watanzania walio wengi hususani sehemu za vijijini, lakini hata hivyo, uroho wa madaraka wa baadhi ya viongozi wa vyama vya Mageuzi umechangia kwa kiwango kikubwa kwa chama tawala kuendelea kuviburuza vyama hivyo katika kila chaguzi zilizowahi kufanyika tangu mwaka 1995, 2000 na 2005.

Mtu yeyote mwenye akili timamu atakaa na kufikiri kuwa baada ya mageuzi kufanya vibaya katika chaguzi zote tatu zilizopita, upinzani ungekaa pamoja na kufikia uamuzi wa pamoja wa kuandaa mikakati kabambe ya kukabili uchaguzi ujao wa 2010. Lakini badala yake, bado kila chama kinadhani kuwa kina ubavu wa kutosha kupambana na CCM ambayo imekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 45 (ukiunganisha na miaka ya TANU).

Watanzania walio wengi wangependa kuona vyama vya upinzani vikiungana au hata kushirikiana ili kukiondoa chama kinachotawala madarakani. Lakini kutokana na uroho wa madaraka wa baadhi ya viongozi wachache wa upinzani hilo linaweza lisitokee tena kwenye uchaguzi mkuu ujao kwani kila dalili zinaashiria kuwa huenda tena vyama vya Mageuzi nchini vitarudia makosa yaleyale (kwa Kila chama kuamua kuingia kivyakevyake) kwenye uchaguzi mkuu wa 2010 kwa matumaini bandia kuwa huenda muujiza utatokea na hivyo kuwashindisha viti vingi vya ubunge na hata penginepo kuwaweka ikulu.

Umefikia wakati sasa kwa vyama vya Mageuzi nchini kuachana na ndoto za mchana na kutambua kuwa mfumo wowote ule wa vyama vingi unahuishwa na uimara na uthabiti wa vyama hivyo ambavyo vinakuwa tayari kuchukua fursa za kuongoza nchi kama chama tawala kikidorora. Wakishatambua hilo, basi waache kabisa kulalamika eti chama tawala kinatumia dola kuwamaliza nguvu, na badala yake waanze mikakati ya kuimarisha vyama vyao mapema kabisa ili kujiandaa na uchaguzi ujao. Wasisubiri mpaka 2009 kuanza mikakati hiyo, kufanya hivyo watakuwa wanakosea.

Vyama vyote vya Mageuzi nchini vikae pamoja na kuandaa mbinu za kukabiliana na nadharia ambayo chama tawala kimefanikiwa kupandikiza vichwani mwa watanzania kwa muda mrefu. Nadharia kuwa, "Mageuzi ni upinzani." Semina ziendeshwe nchini kote kuelimisha wananchi kuwa Mageuzi sio upinzani, bali Mageuzi ni mbadala wa chama fulani kuiongoza nchi pale chama kilichopo madarakani kinapokuwa kimedorora. Mabango yenye sera-mbadala yabandikwe sehemu zenye mikusanyiko ya watu wengi kuainisha mapungufu ya chama tawala na kutoa mbadala toka Mageuzi. Pia matangazo kwa njia ya Radio na Runinga yatumike kueneza kampeni ya kuzima nadharia kuwa "Mageuzi ni upinzani." Vyama vya mageuzi vina wasomi wengi, tunaamini kabisa hawawezi kushindwa kulielezea jambo hili kwa ufasaha zaidi.

Sambamba na hilo, vyama vya Mageuzi vitafute njia nzuri ya kuelimisha wafuasi wao kuhusu umuhimu wa kura hata kama ni kura moja. Ukweli ni kwamba: ufinyu wa elimu ya uraia kwa wanachama wengi wa vyama vya upinzani [Mageuzi] umechangia kwa kiwango fulani kuvikosesha vyama hivyo kura halali tena nyingi tu katika chaguzi nyingi zilizopita. Mfano, wadadisi wa mambo ya kisiasa wanadai kuwa wananchama wengi wa chama cha CUF waliongozwa na jazba zaidi kuliko hekima katika uchaguzi mkuu wa 2005 na badala ya kupiga kura ya "HAPANA" kwa mgombea wasiyemtaka, wengi wao waliishia kuandika matusi na maneno ya kejeli mbele ya picha za mgombea wa chama tawala. Matokeo yake: kura hizo zilihesabiwa kama zimeheharibika.

Kadhalika, kama ripoti ya Profesa Mukandala ilivyowahi kubaini, vyama vingi bado havijajikita mizizi vijijini na wala havijulikani sana ukiachilia mbali sifa za waanzilishi wake ambao nao pia wanasumbuliwa na uchu tu wa kuingia ikulu hata kama sifa walizonazo haziwavutii wananchi kuwapigia kura.

Mathalani, katika chaguzi mbili zilizopita, wagombea waliosimama kugombea kiti cha urais ni walewale wa sikuzote--Mrema na Lipumba. Wananchi wamewachoka! Itakuwa busara basi endapo kama vyama vya Mageuzi vitarekebisha mapungufu haya mapema na kusimamisha wagombea wapya wenye sifa ambazo zinatosha kuvutia wananchi kuwapigia kura, na sio kusimamisha wagombea kwa misingi ya kufahamika. 

Badala ya kupoteza muda mwingi kutoa malalamishi mengi yasiyo na msingi dhidi ya chama tawala, vyama vya Mageuzi vinatakiwa kuweka sera za kueleweka mahala pake. Malalamiko tunayoyasikia kila siku toka upande wa Mageuzi kuwa: CCM ni wala rushwa..., CCM haijafanya lolote lile kwa kipindi chote cha miaka 45 madarakani..., hayawaingii wananchi maskioni kama malalamishi hayo hayaambatanishwi na sera-mbadala zinazo-onyesha kuwa ni nini tofauti ambacho Mageuzi wangefanya kama wao ndio wangekuwa madarakani. Kinachotakiwa sio kelele na lawama tu dhidi ya chama tawala, bali ni sera za kueleweka zenye makusudi ya kulichukua taifa letu kwenda hatua nyingine, hatua bora zaidi.

Athari za migogoro katika vyama vya siasa nazo zinatakiwa kuepukwa kabisa. Migogoro sikuzote inaashiria uwezo duni wa kutatua hitilafu kati ya pande husika (Mageuzi kwa ujumla) kwa njia ya mazungumzo/maelewano.

Uwepo wa migogoro hiyo ndani ya vyama na baina ya vyama unawatia wananchi hofu na kuwafanya waondokewe na imani kama kweli vyama hivyo vinastahili kupewa dhamana ya kuongoza nchi. Kando na hilo, migogoro hiyo imechangia pia kudorora kwa vyama hivyo na hivyo kuendelea kufanya vibaya katika kila chaguzi zilizojitokeza. Tumeshuhudia mgogoro mikubwa ndani ya vyama ya kugombea madaraka ndani siku za nyuma. Mfano mzuri ni ndani ya chama cha UDP ambapo kamati kuu ya chama hicho ilitimua Mwenyekiti Bwana John Momose Cheyo, na baadaye ikafuatia timua-timua. Athari zake ni kwamba: baadhi ya wabunge waliotuhumiwa kushirikiana na Bw. Amani Jidulamabambasi kumpindua Mwenyekiti wakawa wa kwanza kutimuliwa. Matokeo yake: aliyekuwa Mbunge wa UDP na Madiwani 9 walihamia CCM na wanachama 1,147 wa wilaya ya Bariadi walihamia CCM pia. Tumeshuhudia kitu hichohicho pia ndani ya vyama vingine vikubwa kama TLP na NCCR -MAGEUZI.

Migogoro baina ya vyama na ndani ya vyama haichochewi na kingine kile isipokuwa uroho wa madaraka wa baadhi ya viongozi ndani ya vyama hivyo. Hivyo basi, Mageuzi hapa wasipoteze muda kutafuta mchawi nje, wao wenyewe ndio wachawi.

Kimsingi, mpaka hapo vyama vya Mageuzi vitakapojipanga upya na kujua kuwa, njia mbili kubwa za wao kushinda uchaguzi ni: [moja] kuhakikisha kuwa wanasimamisha mgombea chini ya kivuli cha chama chenye nguvu na mvuto. Kwamba, hata kama mgombea atakuwa hovyo, bado atabebwa na kuchachaguliwa kwa sababu tu ya nguvu na mvuto wa chama anachowakilisha.  Na [pili] ni mgombea mwenyewe kuwa na sifa ambazo zinatosha kuvutia wananchi wampigie kura, na sio chini ya kivuli cha chama chake tu. Na kama Mageuzi watashindwa kufanya marekebisho haya mapema, basi chama tawala kitaendelea kushinda na kuisabaratisha ngome  ya Mageuzi tena na tena na tena...

P.S. Chama Cha Jamii (CCJ) ni chama kipya kilichosajiliwa hivi karibuni.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.