HOJA YA KADHI MKUU NCHINI TANZANIA

Na, Antar Sangali (Bagamoyo) <09/16/06 >

Hoja  kuhusu mahakama ya kadhi si jambo la kuwafanya waumini wa dini ya kikiristo kutaharuki na kuona ni muujiza katika Tanzania.

Kimsingi Uganda na Kenya kuna mahakama za kadhi na nchi hizo zina Kadhi Mkuu wake [kila moja], jambo ambalo haliathiri sheria za nchi hizo na kuingilia uhuru wa dini nyingine.

Kadhi na mahakama zake ni suala linalotajika katika kitabu cha waislam [Quraan] Yaliomo katika kitabu hicho yakiwa mema au mabaya hayawakamati na kuwahukumu wasio waislam na hivyo si haki kwa asiye muislam kutia shaka juu ya mahakama hizo.

Lakini pia mashitaka au masaala yatakayopelekwa kwenye mahakama hizo yatawahusu waislam na kwamba hakuna mkristo, rastafarian, mpagani au mhindu atakayeitwa katika mahakama hizo kwa kuwa yeye si muislam,hofu hapa inatoka wapi?

Zanzibar kuna Kadhi Mkuu na waislam aghalab huamua kesi zao huko za kidini kwa Kadhi mkuu ilhali nchi hiyo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba mfumo wa Kadhi huko Zanzibar hauingilii abadan katiba na sheria za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ).

Nimemsikia Muhashamu Kadinali Polcap Pengo wa kanisa Katoliki na baadhi ya viongozi wakristo wengine wenye sauti katika Tanzania wakitia shaka  pengine kutokea kuidhinishwa kwa sheria ya kadhi mkuu na mahakama za waislam kutaleta hisia za kidini.

Jamani iacheni Tanzania izidi kutanua wigo wake wa kihistoria katika misingi ya kidemokrasia ili iwe mfano katika sayari hii ya dunia na pengine kama kuna viumbe hai katika sayari nyingine waje kujifunza maisha yalio na usawa na uhuru.

Mathalan Hadhi ya Balozi wa Vatican nchi Tanzania imelalamikiwa sana na baadhi ya waislam wenye mtazamo hasi,lakini kimsingi Vatican na mfumo wake ni tosha kuiita au kujiita Dola-Dini, ni maisha ya heshima ya dini na mkusanyiko wa imani za wakiristo wa madhehebu ya kikatoliki katika mtandao wake,ukipinga ni ujinga unaoweza kupalilia gumzo lisilo na ukomo.

Vatican si Dola inayotambulika na Umoja wa Mataifa(UN),haina kiti na si mwanachama katika Umoja huo si hasha kusema hata Katibu Mkuu Bw Koffi Annan hana nambari ya uanachama wa Dola hiyo yenye Balozi na bendera yake ikipepea hapa Tanzania.

Chonde chonde watanzania ya Kaizari tumwachie Kaizari na ya Mussa apewa Mussa,kutafuta nyingi nasaba ni kupata mwingi msiba, kimsingi wimbo mbaya habembelezewi mtoto na kila mtoto mbelekoni hutazama kichogo cha mamaye,Tanzania ni vyema ikaiga na kufuata nyayo zake.Kwa kungwi aghalab kukiliwa na kwa mwari nako kuliwe, washwahili husema kila mla cha mwenziwe na yeye chake huliwa,cha watu ukichukua na chako ukubali kukitoa, ndiyo ustahamilivu!

Aliyekuwa Rais wa Somalia Sied Barre, Kanali Mengistu Haile Mariam wa Ethiopia, Jafer Nimeir wa Sudan walikataa kubadilika mapema lakini mabadiliko yaliwabadili ghafla bila kutaraji. Tanzanaia imefanikiwa sana Barani Afrika kutokana na siri ya kukubali kwake mabadiliko,lakini isingekubali kubadilika kisiasa na kiuchumi mabadiliko yangeibadili kama yalivyozibadili nchi mathalan za Kenya, Zambia na Malawi.

Hoja ya Waislam na kupatiwa fursa ya kuwa na mahakama kwa ajili ya masaala yao ya talaka, mirathi na ndoa ni hoja isiyozuilika kutokana na ukweli kwamba inatajika katika kitabu chao,wakinyimwa kwa njia rahisi wanaweza kupata ushabiki na jazba ya kudai kwa njia isiyo na usahihi ambayo pengine inaweza kuitia doa historia ya nchi yetu(kwa mtazamo wangu mfupi).

Waislam, Wakristo, Wahindu, Marastafarian na Wapagani hebu tumuunge mkono kikamilifu Rais wetu mpendwa wa awamu ya nne Bw Jakaya Kikwete na serikali yake na wala tusilete mizengwe ya kumkwamisha kutokana na imani zetu.

Tumepata Rais Mzalaendo, mchapakazi na mahiri katika kuwatumikia watu wake,busara na dipolomasia vitumike katika kumsaidia zaidi badala ya kutaka kumvuruga na kumchanganya ili asifikie malengo anayoyataraji.

Waislam wanataka Kadhi Mkuu na Mahakama zao baadhi ya Wakristo hawataki hoja hiyo,baadhi ya waislam watataka kuhoji kuwepo kwa Balozi wa Vatican na bendera yake au idadi ya kubwa ya wakristo kupata nafasi serikalini au kwanini waislam ni wengi katika Baraza la Mawaziri la Rais Kikwete,litatoka kundi jingine litasema kwanini Baraza la mawaziri na Rais wa kwanza,pili na wa tatu kulikuwa na haya na haya na hayakuwepo,kimsingi masaala haya hayatajenga nchi,yataivuruga na kuiharibu.

Rais Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba ukimuona mtu anaumwa san na udini ni mdini,hafai na ni muflisi akiwa ni mwanasiasa,lakini kwa upande wangu leo nashuhudia kuwepo kwa waojifanya kulaani nasaba mbaya za  udini huku wao wenyewe wakionekana dhahir shahir kuwa na harufu za kidini.

Leo ni miaka 14 tokea kuruhusiwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania,hivi kweli serikali ya CCM laiti iosingetanabahi ingezuia ujio wa mageuzi ya kisiasa! ingemudu kisawasawa na kuthubutu kuzuia fikra za mabadiliko hayo ?,kuzuia ukweli kunataka ujuha na uzuzu kamili!

Iacheni Tanzania yenye makabila zaidi ya 120, wakristo waliochanganya damu na waislam wakiishi bila kubaguana, marastafarian wanaomuona Mfalme Haile  Sellasie ni Nabii katika kizazi cha Mtume Solomon, mabohora wanaomheshimu Sayydna wao, Masingasinga na vilemba vyao, mabaniani wakichoma moto maiti zao kule nyuma ya kijiji cha makumbusho na walokole wanaolia makanisani kama sehemu ya kutubu na kuabudu kwao.

Katika wilaya ya Lushoto kuna Askofu msataafu Kimweri wa kanisala la Kilutheri ,awali alikuwa muumin wa kiislam na jina lake aliitwa Rajab,alisoma Tanga School, akiwa shuleni alikuwa Imam katika kusalisha wenziwe anasoma baadhi ya aya za Quraan kwa ufasaha hadi leo hii, lakini baadaye aliaamua kuingia katika ukristo huko Ujerumani na akawa Askofu,ukimkuta pia hufanya matambiko ya kimila la kabila la wasambaa,mimi nimemshudia kwa macho yangu mbele ya Katibu Mkuu wa CCM  Yusuf Makamba katika ziara yake huko Lushoto.

Askofu huyo ni alama ya kutosha katika Tanzaania iliyo na uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa katiba yake,laiti angelikuwa katika nchi zenye waumini wenye misimamo mikali sijui leo maisha yake yangelikuwa yako wapi Yarabi,ahera au sijui duniani!

Katibu Mkuu wa CCM Mzee Yusuf Makamba aliwaambia waumini wa kiislam pale Tanga mjini katika Masjid Maarifatul,"masheikh na mapadri katazeni watu wasitumia kondom ndiyo kazi yenu,lakini yeye akasema ni mwanasiasa aliapa atazidi kuhubiri kwamba kinga inyofaa kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi ni kuvaa kondom".

Lakini katika kutia kwake bashasha kama ilivyo kawaida yake alisema hatawashangaa kamwe masheikh na mapadri pale wanapofanya duwa na sala zao za kumuomba Mungu alete dawa ya kuponyesha ugonjwa wa ukimwi unaowateketeza watu duniani hususan Barani Afrika.

Madai yenye hoja yanaweza kuwa na nafasi ya kusikilizwa kwa upana katika dunia ya wenye busara,maarifa na hekima,ujinga na ujuha ni siku zote ni vitanzi vya majuto. Mungu Ibariki Afrika

Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.