IGENI TOKA BOTSWANA

Na, Edward Chacha <04/07/10 >

Mara baada ya uhuru wa 1966, nchi ya Botwana ilikuwa ni moja ya nchi masikini kabisa barani Afrika na duniani kwa ujumla. Na kama zilivyo nchi nyingi za kiafrika, GDP per capita enzi hizo (1966) lilikuwa ya kiwango cha chini kabisa sawa na dola za kimarekani 80 tu. Kando ya hilo, nchi hiyo ilikuwa pia inakabiliwa na ukosefu mkubwa wa maji ambao ulioathiri mfumo mzima wa kilimo; ikichangiwa zaidi na hali ya nusu jangwa inayoizunguka nchi hiyo hivyo kusababisha tishio kubwa la upungufu wa chakula. Miundombinu yake pia ilikuwa mibovu kupindukia.

Lakini leo Botswana inatajwa na kusifika duniani kote kama kioo angavu cha maendeleo ya kiuchumi kusini mwa jangwa la shahara ambapo uchumi wake umekuwa ukikua kwa asilimia kati ya 7.5 - 13 mwaka 1966-1999. Na asilimia 5-7% mwaka 1999-2008. Mwaka 2004 GDP - Per Capita: ilikadiriwa kuwa dola za kimarekani 9,200 sawa na mara 13 ya GDP-Per Capita ya Tanzania ilyokuwa imekadiriwa kuwa sawa na dola za kimarekani 700 tu. Leo hii GDP per capita ya Botswana inakadiriwa kuwa dola za kimarekani 14,700, wakati ya Tanzania inakadiriwa kuwa chini ya dola za kimarekani 1000 (2009 est).

Ingawa Botswana bado inakabiliwa na tatizo kubwa la Ukimwi, bado nchi hiyo ni miongoni mwa nchi chache duniani zinazoogopeka kwa kuwa na uchumi mzuri (sawa tu na nchi za Korea ya Kusini na Thailand; na bora hata kushinda nchi nyingi za Ulaya Mashariki).

Swali ni kwamba: Je, Botswana imefikafikaje huko iliko? "ni kwa kupuuza ushauri wa kilaghai toka tasisi za Washington kama vile IMF, na kuamua kufuata mashauri nasaha ya kiuchumi toka kwa wachumi waliobobea wa mashirika binafsi kama vile Ford Foundation..," Mr. Stigliz, mpinzani mkubwa wa shirika la fedha dunia (IMF) anaeleza katika kitabu chake kiitwacho, "Globalization and its Discontents".

Ni kweli kwamba almasi imechangia kwa kiwango kikubwa sana katika ukuaji wa uchumi wa Botswana kama wengi tujuavyo; lakini mbona nchi kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nigeria, Tanzania na Sierra Leone zenye almasi nyingi bado uchumi wao haukuwi kwa kasi kama ilivyo kwa Botswana?

Jibu: katika nchi hizo (Nigeria, Tanzania, Sierra Leone, DRC), viongozi wake wamejawa na harufu kali ya rushwa pamoja na kung'ang'ania ushauri mbovu wa kilaghai toka tasisi za Washington kama vile IMF na Benki ya Dunia zenye kutoza riba kubwa kwa kisingizio cha kusaidia kwa njia ya kukopesha mikopo ambayo ina masharti magumu sana yasiyotekelezeka.

Moja ya sababu kubwa ya mafanikio ya kiuchumi ya Botswana ni hatua madhubuti walizochukua viongozi wa ngazi za juu wa serikali za kuchagua washauri wazuri wa kiuchumi wasiokuwa na uhusiano na tasisi za Washington. Mfano mzuri ni pale IMF ilipoipatia Botswana mtaalamu wao kuwa naibu gavana wa Benki ya Botswana, lakini management ya benki ya Botswana ikakataa kufanya hivyo na badala yake ikaamua kupendekeza wataalamu toka Ford Foundation kuwa washauri wakuu wa suala zima la uchumi pamoja na utadawazi.

Mfano, muda mfupi baada ya uhuru wa 1966, Botswana iliingia mkataba na kampuni moja ya Afrika kusini kuhusu uchimbaji wa almasi ambapo kampuni hiyo iliipatia Botswana $20 million kwa kipindi miaka mitatu huku kampuni hiyo ikiingiza faida ya $60 million ndani ya mwaka mmoja. Lakini kutokana na washauri wazuri wa mambo ya uchumi, serikali iliamua kutumia wana shaeria wake kujadili mkataba mpya wenye maslahi mazuri kwa taifa lao mara baada ya kugundua kuwa walikuwa wanapunjwa.

Wapi leo hii katika Tanzania utakapokuta serikali inafanya hivyo? Viongozi wetu wa ngazi za juu serikalini wanachojali zaidi ni asilimia 10 wala sio maslahi ya taifa kama ilivyokuwa na ilivyo hata leo hii huko Botswana.

Angalia huko Nyamongo wilayani Tarime, kwa mfano. Huko tunaambiwa kuwa wananchi waliokuwa wakijishughulisha na uchimbaji mdogomdogo wa dhahabu na wakulima waliokuwa na mifugo pamoja mashamba karibu na machimbo ya Nyabigena, Nyabirama na Gokona walitimuliwa kama si watanzania vile, pale kampuni moja ya kigeni ijulikanayo kama Place Dome (sasa, Barrick Gold Corporation) iliponunua machimbo hayo na kuanza kuyamiliki. Wengi wa wananchi hao hawakupatiwa fidia yoyote ile na kampuni hiyo, na Wale waliojitokeza kupinga uonevu huo waliishia kuswekwa jela.

Sio hilo tu, serikali pia inatizama uchafuzi wa mazingira unaofanywa na kampuni hiyo ya kigeni bila hata ya kuchukua hatua zozote madhubuti za kuwakinga wananchi wake. Vifo vya watu wapatao 21 na ng'ombe zaidi ya 200 katika kata ya Kibasuka, wilayani Tarime vilivyotokana na kunywa maji ya yenye sumu ya cyanide na mercury toka mto Tigithe, ni mfano mzuri wa kutizamwa.

Ni kweli kwamba: "Utandawazi upo na haukwepeki, ni sawa na hewa tunayoivuta ya oksijeni...," kama waziri wa zamani wa nchi katika ofisi ya Rais (mipango na ubinafsishaji) enzi hizo Dk. Kigoda alivyowahi kukaririwa akisema. Lakini pia hatupaswi kuingia katika ulingo huo wa utandawazi kichwakichwa huku tukiwaacha wawekezaji wanufaike zaidi na utajiri mkubwa wa nchi yetu hali wananchi walalahoi wa kawaida wakitengwa na kusahaulika kabisa.

Tunapaswa kuiga mfano wa Botswana kwa kurekebisha mifumo yote inayo watenga watu wengi katika manufaa ya kiuchumi yatokanayo na utandawazi ili wananchi wengi wanufaike na sio tu kuimba wimbo wa Dk. Kigoda wa "utandawazi upo na haukwepeki."

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.