ZIARA YA KIKWETE MINESOTA-MAREKANI YAFANA, UKWELI WA MAMBO TANZANIA WATIA DOSARI

Na, Magabe Kibiti <posted first on: 10/01/06>

Mambo yamekuwa yakienda mrama kwa watanzania kwa muda mrefu sasa kiasi kwamba chochote kile tunachofanya watu wengi huwa hawana uhakika kama kitafanikiwa au la. Ziara ya Rais Kikwete katika jimbo la Minesota hapa Marekani siku chache zilizopita, inaweza kubadili mtizamo huu kwa kiwango fulani. Natanguliza ombi langu la msamaha kwa vile hata mimi sikutegemea kama ziara hii ingefanikiwa. Ninaweza kusema pia kuwa uamuzi wa ujumbe wa Rais wa kukataa kukutana nasi raia wa Tanzania hapa Minesota uliongeza idadi ya maswali kichwani mwangu kuhusu sababu hasa ya Rais kuja hapa huku akikataa kukukutana nasi. Hata hivyo baada ya kushuhudia baadhi ya mambo ambayo ujumbe wa Rais Kikwete ulifanikiwa kufanya, naweza kusema kwa hakika kuwa ziara hii ya Rais Kikwete ilikuwa ya mafanikio.

Ujumbe wa Rais Kikwete ulikuja hapa ili kuwashawishi wana-Minesota kuwekeza Tanzania. Kifupi, kwa wale msiolijua jimbo hili, Minesota ni makao makuu ya makampuni makubwa kama; Best Buy, Target, 3M, IBM, People Soft, United Health, n.k. Kwa kujua kuwa nisingeweza kupata nafasi ya kuhudhuria vikao hivi au kuonana binafsi na Rais au ujumbe wake, niliwashawishi wazungu marafiki zangu kutafuta namna ya kujua yote yaliyojadiliwa katika vikao hivyo. Mpango wangu ulifanikiwa kunipatia kwa undani mengi ya yaliyojadiliwa katika vikao hivyo. Cha kutia moyo zaidi, ni hitimisho kutoka kwa mashushushu wangu (ambao ni wanafunzi wenzangu wa uchumi) kuwa ujumbe wa Rais uliwasilisha ushawishi mkubwa kwa wafanyabiashara hawa.

Usihitimishe moja kwa moja kuwa ninaandika makala hii kujikomba au kujipendekeza kwa Rais Kikwete au serikali ya CCM. Kutokana na ukweli kuwa kwa sasa sijui ni lini hasa nitarudi Tanzania, sijaona bado kama nina sababu yoyote ya kuwa mnafiki katika hili. Ifahamike pia kuwa, Rais Kikwete alikuja hapa kutunikiwa shahada ya juu ya sheria na chuo kikuu cha St Thomas (tukio ambalo watanzania wa kawaida tuliruhusiwa kuhudhuria). Pamoja na kuwa na mashushushu wangu katika vikao binafsi vya Rais, mimi nilihudhuria sherehe fupi ya makabidhiano ya maelfu ya vitabu kwa watanzania ambavyo vilipokelewa na Naibu waziri wa mambo ya nje kwa niaba ya Rais. Nilifurahi kukutana na mmoja wa ma-profesa wa chuo kikuu cha mliman–Profesa Mkandala katika sherehe hii. Nilifurahi pia kujua kuwa Prof. Mkandala ni miongoni mwa washauri wa Rais.

Nilifanikiwa pia kusikiliza hotuba ya bodi ya biashara ya nje ya TZ kwa wafanyabiashara wa hapa, waandishi wa habari, wanafunzi na walimu wa biashara katika chuo cha St Thomas, na watanzania waishio hapa. Ninasikitika kuwa simfahamu kwa jina aliyetoa hotuba hiyo kwa niaba ya Rais, ila naweza kusema kuwa; wengi wetu tulikubali kuwa hotuba ile ilifanikiwa kuonyesha kwa hakika uwepo wa maliasili, wafanyakazi, utulivu, na nia ya watanzania kujikomboa kiuchumi. Sina hakika kama juhudi zote hizi zilikuwa ni longolongo kama ilivyo kawaida yetu. Kwa mtazamo wa nje, wajumbe hawa walijieleza vizuri sana. Nilifurahi pia kuwaona wafanyabiashara wa kitanzania wakianzisha mahusiano ya kibiashara na kibinafsi na baadhi ya wajumbe. Baada ya kupokea shahada yake, Rais Kikwete alitoa hotuba ambayo aliomba uvumilivu na imani kutoka kwa wafadhili kwa serikali yake changa.

Dosari kubwa katika ziara hii ya Rais, ni hali ya mambo ya Tanzania. Mmoja wa wazungu waliohudhuria vikao hivi amerudi kutoka Tanzania kama wiki mbili zilizopita baada ya kukaa bongo kwa zaidi ya mwaka akifanya utafiti. Wakati yote haya yakiendelea; alinikumbusha mgao wa umeme unaoendelea nchini, ukosefu wa maji, ukosefu wa wanazima-moto wa uhakika, wizi wa mabenki, rushwa na longolongo za bandari ya Dar, mawasiliano duni, barabara mbovu (akacheka kusema kuwa mwaka jana uharibifu wa daraja la wami ulikwamisha utafiti wake kwa zaidi ya wiki nzima), n.k. Alinishangaza zaidi pale alipotumia kishwahili kusema kuwa; “mapanga shaa shaa (baadhi ya lugha iliyotumika kwenye kampeni za mwaka jana) ni mbaya kwa Tanzania”.

Hayo yote aliyosema huyu mzungu ni kweli. Haitajalisha kama ujumbe wa Tanzania utatumia maneno mazuri kiasi gani kushawishi wageni na wawekezaji kama ukweli wa mambo Tanzania utakuwa ni huu wa sasa. Rais Kikwete aliahidi katika hotuba yake hapa kuwa serikali yake itafanya kila iwezalo kurekebisha hali ya mambo. Kwa sasa mpira uko kwa Kikwete. Kazi kwake kutimiza yale aliyoahidi. Yale yawezekanayo kama kuadhibu wale wanaotumia lugha za mapanga shaa shaa, au wale wanaoleta longolongo bandarini yanaweza kufanyika hata leo. Ziara ya Rais Kikwete imetia moyo kuwa hata watanzania wanaweza kufanya kitu cha maana. Tuna imani kuwa yote yaliyosemwa hapa yatatimizwa kwa vitendo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Tuma maoni [Hapa>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.