PUPA YA KUTAKA KUSHIKA MADARAKA, ITAIANGUSHA CHADEMA TENA

Na, Antar Sangali (Bagamoyo): [Posted on: 10/04/10]

Chama imara cha kisiasa ni lazima kwanza kiwe na muundo thabiti, mtandao mzuri wa kisiasa unaoanzia ngazi moja hadi nyingine pamoja na kuwa na mfumo unaosadifu wa kisera na kiitikadi na kutambulika, achilia mbali kukubaliwa na wananchi.

CHADEMA chama ambacho kwa bahati mbaya sana kimebahatika kukubalika kikanda na kuungwa mkono na kundi la kabila la Kichaga, bado hakijajipanga na kuonekana wazi kama "a real Political Party" ili kuivuta na kuishawishi hadhira kubwa inayoishi vijijini na mijini kwamba wao ndio wanaostahili kuiongoza Tanzania na sio CCM.

Mizizi na nguvu za CCM ni kubwa mno katika nchi yetu, anayepuuza ukweli huu ni mpuuzi jasiri asiyejua kupambanua baina ya mbivu na mbichi, na bila shaka hataki kwa makusudi kujua ukweli wa mambo ulivyo.

Msingi imara wa chama cha TAA ulijengwa kutokana na harakati za machifu wa Tanganyika katika dhati ya kupambana wakiwemo baadhi yao kina Mangi Meli, Kinjikitile, Mirambo, Kimweri, Mkwawa, Makunganya, Bushiri na wengine--wakati kukubalika kwa chama cha TANU ni matokeo ya nguvu na juhudi za chama cha TAA.

Kwa msingi huo kuimarika na kukubalika kwa CCM ni kutokana na kujijenga kwa vyama vya TANU/ASP ambavyo ni vyama viasisi vya siasa katika Tanganyika na Zanzibar tokea miaka ya 1954 na 1957.

CCM inatofauti sana kimtazamo na vyama kama UPC cha Uganda, MCP cha Malawi, na UNIP cha Zambia au KANU kilichokuwa kikitawala Kenya.

Vyama hivi navyo vilikataa kujikita na kuweka mizizi ili kulishika kundi la watu hasa mababa-kwabwela wanaoishi vijijini na kulazimishwa kutambua kwamba mafanikio na ujio wa uhuru wao ulitokana na vyama hivyo.

Kiuhalisia na kinadharia vyama hivyo mara baada ya uhuru vilibadilika na kuwa vyama vya kibwenyenye na kimwinyi kwa kuusahau kabisa kuutazama umma wenye nguvu za maamuzi na utafutaji wa ridhaa ya kudumu (CCM nayo ilijaribu kubadilika lakini sio kwa kasi kubwa ya kutisha kama ilivyokuwa kwa majirani zetu wa Uganda, Kenya, Malawi na Zambia. Shukrani za peee kwa hayati Kambarage Nyerere, mwasisi wa CCM).

Wanaojaribu kuitazama CCM kwa jicho rahisi wafanye pia utafiti mgumu ili kutambua matokeo kamili kabla na baada ya ujio wa vyama vingi huku wakiidurusu kwa weledi hali ya mambo na wakati ulikuwaje kwa nyakati hizo.

TANU haikupata kazi ya suluba ya kujenga matawi mapya toka mwaka 1954 kilipoanzishwa kuanzia kanda ya Mashariki, Lake zone ,Kaskazini na Kusini mwa Tanzania na hatimaye kusambaa nchi nzima, kutokana na kurithi matawi yoye toka kwa chama kikongwe cha TAA.

Kuzaliwa kwa CCM tarehe 5,2,1977 na kuenea kwake ilikuwa ni kama kuua tembo kwa bua kutokana na chama hicho kuiga tabia ya nyoka anayejibua gamba, na yeye kubaki akiwa ni nyoka yuleyule mwenye sumu kali.

TANU iliutumia vizuri mfumo wa chama kimoja na kueneza siasa zake hadi kwenye Taasisi za serikali, mashirika ya Umma, vyuo vikuu, sekondari hadi hata kwenye vikosi vya ulinzi na usalama.

Haikuwa kazi nyepesi inayoweza kuleta hasara haraka au kwa ulaini kama iliyovyazamwa na inavyoendelea kutazamwa na baadhi ya wahariri a mambo ya kisiasa.

Base ya TANU ni TAA. Base ya CCM ni TANU na ASP. CUF inatokana na vuguvugu la KAMAHURU, NCCR -Mageuzi ni mkusanyiko wa wanaharakati waliolilia mageuzi ya Kikatiba tokea miaka ya 1990. Lakini CHADEMA chimbuko lake halisi hasa ni nini na wapi? Au ndiyo ili iliyoelezwa kuwa something like "Chagga Develpement Manifesto"?

Takriban miaka 27 ilipita chini ya chama cha TANU kikiwaimbisha na kuwachezesha kwata wananchi chini ya zama ya nguvu ya chama kushika hatamu tangu pale mfumo wa vyama vingi ulipopigwa marufuku mwaka 1965; fursa na nafasi hii haikutumiwa ipasavyo huko Zambia, Uganda, Malawi na Kenya, na huu ndio ukweli wa mambo, ila anayetaka kubeza hawezi kuzuiwa.

CCM haikulala usingizi wa pono pale ulipoingia mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, ilianzaa kujichimbia kisiasa, kuingiza wanachama wapya, kujinadi mbele ya umma na kuubeza upinzani kwa nguvu ya hoja.

Ni kweli serikali zake zimekuwa zikikabiliwa na matatizo mengi tokea awamu ya kwanza hadi hii ya sasa tuliyonayo--huku chama chenyewe kikijitutumua kwa bidii kulinda hadhi yake na kujivunia rasilimali watu.

Katika awamu ya kwanza mashirika yote ya umma yalifujwa, hakuna aliyefikishwa mahakamani, awamu ya pili walikamatwa watu wakisafirisha dhahabu uwanja wa ndege wa kimataifa wa Dar ess Salaam, kesi ikayeyuka huku katika awamu ya nne tumeshuhudia mikataba mibovu ya madini na wizi katika akaunti ya EPA na BoT ikifanyika katika awamu ya tatu bila hatua zozote za kisheria kuchukuliwa dhidi ya waharifu/husika.

CCM mara kadhaa kimekuwa kikijikosoa na kujipanga kutokana na kupata msaada wa mtandao wake uliojengeka Tanzania nzima kwa miaka mingi.

Vyama vya Tanzania vina pupa ya kutaka kushika madaraka ya juu vianze kwanza kujijenga ndani ya halmashauri za wilaya, Bunge na Baraza la Wawakilishi huku vyenyewe vikitambua mitandao yao ili kupata ushindi ni dhaifu.

Serikali ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete imejitahidi kupambana na ubadhirifu wa mali ya umma, kukemea rushwa na kwa bahati nzuri kesi ziko mahakamani zikiwakabili vigogo wazito. Ingawa wengi wa hao wahusika wanataachiwa huru bila kupata adhabu wanayostahii, lakini hilo pekee ni jambo linalowaongezea wananchi mapenzi na hamu ya kuendelea kuiamini CCM, nje ya hilo ukifuatilia utekekezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM toka awamu ya tatu hadi ya nne, Tanzania imepiga hatua (ingawa sio kubwa sana kimaendeleo).

Barabara, zahanati na huduma za maji safi zinatia moyo kinyume na miaka ile mara baada ya kupata Uhuru, vyama vya Bongo vijizatiti, viongozi wake wajitume na wasitegemee wao kuja kufaidi matunda ya nguvu zao, wafanye kama walivyofanya kina Mkwawa na Mangi Meli.

Kuimarika na kujengeka kwa CHADEMA kuna tofauti sana na kujengeka kwa CUF. Chadema mwanzo wake unatokana na safu ya waasisi wa chama hicho. Brown Ngululupwi, Edwin Mtei, Bob Makani, Costa Shinganya, na Kimesera. Hili lilikuwa ni kundi la masetla watupu na halikuwa la wanasiasa waliotambulika na kufanya kazi za kisiasa.

CUF ni chama kilichomega nguvu ya CCM Zanzibar baada ya wanachama wake vigogo wapatao saba walipofukuzwa mwaka 1988 akiwemo Seif Sharif Hamad mtu aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi wa SMZ.

Vigogo wengine ni Khatib Hassan Khatib aliyewahi kuwa mhazini wa CCM na MNEC--Hamad Rashid Mohamed ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mambo ya Ndani ya Nchi, Juma Ngwali na Masoud Omar wakiwa wakuu wa Mikoa.

Wanasiasa wengine waliopevuka kisiasa ni pamoja Musa Haji Kombo aliyewahi kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM, Juma Othman Juma aliyekuwa mjumbe wa NEC, Ali Haji Pandu Waziri wa Sheria katika SMZ, Soud Yusuf Mgeni Waziri wa Kilimo pamoja na Maulid Makame Abdallah aliyewahi kuwa Waziri mdogo wa Afya Zanzibar.

Kundi hili la CUF kwa kiasi kikubwa liliweza kuibana mbavu CCM kutokana na wao kuitambua misingi ya kuunda chama cha siasa na kukieneza kama taasisi.

Nieleweke wazi kwamba sikipigii chapuo chama cha CUF ila nimefanya utafiti na kuiona tofauti kubwa kati ya CCM, CHADEMA na CUF. CHADEMA wajenge kwanza mizizi na kundi lililopo sasa lisitegemee kula matunda ya juhudi hizo.

Chama cha CHADEMA na vingine katika Tanzania vinapaswa kujifunza na kupita katika barabara ya chama cha Liberal Party cha Uingereza amacho hakikuwa na papara ya kushika madaraka haraka bali kilitafuta kwanza amana na hatimaye kikaaminiwa.

CUF wanaelekea kuingia katika medani za serikali Zanzibar baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hatua hiyo pekee ukiwa mtu mkweli utaweza kujua usahihi wa tathmini yangu.

Bado siamini kutokana na utafiti mdogo nilioufanya kwamba CHADEMA kimejiandaa na kimejijenga kimfumo, kisera na kimtandao kiasi kwamba kiweze kushinda katika uchaguzi wa mwaka huu na kuongoza dola.

Jambo hili kwa CHADEMA sitaki kabisa niliamini moyoni mwangu, naomba lisistawi kabisa kwenye mishipa ya fahamu zangu na kwenye ubongo wangu pia.

CHADEMA hakitashinda kutokana na kwamba bado ni kichanga, kiliwahi kusifiwa na Mwalimu Julius Nyerere kwamba kina sera zenye mwelekeo lakini kina upungufu wa wanasiasa, ni sawa tu na timu ya soka yenye nyota haba wa kuleta ushindi.

Safu ya kina Wilbroad Slaa, Zitto Kabwe, John Mnyika, Halima Mdee, Philemon Ndesamburo, Maulida Komu na Mabere Marando ni kundi la wasomi wa fani za kitaaluma wakikosa mtaji na ujuzi wa mizungu ya ufanyaji wa siasa.

Slaa ni mwanasiasa mahiri, mwepesi wa utambuzi wa mambo, hata kutoka kwake CCM baada ya kukatwa jina lake na kupachikwa kwa Patrick Qorro katika kura za maoni kulilalamikiwa sana na Mwalimu Julius Nyerere.

Slaa ni yeye peke yake kinara ndani ya CHADEMA akizungukwa na timu hafifu isiyo na uwezo ama ukomavu wa kisiasa wa kukiletea ushindi chama hicho. Kwa upande mwingine, CCM bado kina ngome kubwa, viongozi wengi wenye amana mbele ya umma ambao hawakuona umuhimu wa kujitoa ndani ya chama hicho kwa wingi na kujiunga na kambi ya upinzani.

Chadema, NCCR na TLP ni vyama vinavyoweza kuja kujiimarisha katika siku nyingi zijazo usoni, CUF kwa upande wa Bara nao wamo katika msafa wa vyama hivi vitatu, hawajawa na timu imara na pia Kiongozi wake Profesa Ibrahim Lipumba hajaungwa mkono na wasomi wenzake wa Chuo Kikuu cha Dare es Salaam kuonyesha kama anakubalika.

Hata yeye Lipumba anaonekana yuko peke yake. Ni sawa kabisa na kusema mchezaji nyota wa Brazil "Kaka" aamue kusajiliwa na Balimi ya Bukoba kisha timu hiyo ghafla itarajiwe kutandaza kabumbu safi uwanjani, aifungie magoli mengi timu hiyo, hata aiwezeshe ichukue ubingwa wa ligi kuu. Wa-da-nga-yi-ka wenzangu hebu tusijidanganye. Hiyo ni ndoto ya mchana. Hilo haliwezekani kwa mwaka huu na hata baada ya miaka kumi na tano ijayo, CHADEMA isitegemee kushinda kwasababu bado hakijajipanga vizuri.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.