Majina ya Vyama na Nadharia ya Kidemokrasia


 Na, Antar Sangali, Bagamoyo <11/14/09>

Kifupi cha neno CHADEMA ni kirefu cha maneno-Chama Cha Demokrasia na Mendeleo; chama cha siasa kilichoanzishwa mwaka 1992 na kupata hati halali ya kisheria katika ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nyuma ya Chama cha Union for Multparty Democracy-UMD.

UMD nayo maana yake iliyo nyepesi ni umoja katika kuamini dhana ya domokrasia ya vyama vingi. Chama hiki kiongozi muasisi wake ni marehemu Chifu Abdullah Said Fundikira ambaye kabla ya kifo chake alirudi CCM na kuwa Mbunge wa kuteuliwa na Rais. Fundikira aliwahi pia kuwa Waziri wa sheria katika serikali yaa awamu ya kwanza ya Tanganyika huru.

Katika mwaka huo huo kikazaliwa chama kingine kilichoitwa National for Convetion of Construction Reform-Mageuzi yaani NCCR-Mageuzi ambacho pia kifupi chake ni chama cha kupigania kujengeka kwa dhana ya utaifa juu ya ujenzi wa mabadiliko na mageuzi ya kikatiba; kadhalika kuna chama kiitwacho National League for Democracy-NLD kinachosimia kujenga haiba na ustawi wa demokrasia nchini.

Mwishoni mwa 1993 kikaibuka chama kinachoitwa United Democratic Party yaani UDP chini ya unahodha wa Mwenyekiti John Momose Cheyo (mzee mapesa) chama hiki kilianza kukubalika sana katika mikoa ya kanda ya ziwa huko Mwanza, Shinyanga na Tabora.

Wakati fulani chama cha CUF yaani The Civic United Front - Chama cha Wananchi kilimeguka na kundi lililojitoa likaanzisha chama kilichojulikana kwa kifupi kama FORD yaani Forum for the Restoretion of Democracy, hiki kwa fasiri fupi isiyo fasaha ni mhimili au jukwaa la ustawishaji wa demokrasia.

Ni majina mazuri yanayopendeza kuyaona machoni, kuyasoma vitabuni na kwenye magazeti, matamu kuyatamka mdomoni lakini ni machungu,yamejaa ukakasi na ugegezi pia yamegubikwa na nadharia tele kinyume na uhalisia au dhana kamili yenye maana halisi inayotazamiwa na jamii husika katika kuamini demokrasia ya kweli.

Nimelazimika kuandika makala hii kutokana na neno Chadema chama ambacho mwaka 1992 mwanzoni kabisa kiliwahi kusifiwa na Hayati Mwalimu Julius Nyerere kutokana na kuonekana kuwa na mfumo mzuri wa muainisho wa sera zake lakini kwa bahati mbaya Nyerere hakukitaja hata mara moja kama kina viongozi hodari wenye kumudu kujenga mtandao wa kisiasa unaoweza kukipa tija ya kukubalika ili kupata ushindi wa kushika utawala wa dola.

Mwenyekiti wa kwanza wa Chadema alikuwa Mzee Edwin Mtei ambaye alikuwa Waziri wa Fedha hadi wakati huo alijiuzulu katika serikali ya kwanza chini ya Rais Nyerere kutokana na sababu zilizoelezwa baadaye ni kutoafikiana na mkubwa wake juu ya sera na masharti ya mashirika ya fedha ya IMF na Benki ya Dunia.

Mtei hakufahamika kama mwanasiasa mwenye sauti kwa muda wote wa maisha yake ya uwaziri licha ya kushika nafasi ya ubunge inayotokana na siasa na zaidi ya yote alionekana ni mtaalam mweledi hasa katika masuala ya fedha na uchumi.

Mwenyekiti huyo wa kwanza hakuweza kabisa kuisaidia Chadema kuenea nchini katika kipindi chake kutokana na yeye kukosa haiba ya umachachari na mvuto kwenye majukwa ya siasa jambo ambalo lilikifanya chama hicho kuonekana kama ni chama cha mastla kilichofubaa. Mara nyingi kama si zote Chadema alijigamba majukwani na katika medani za kimataifa kutokana uhalisia wa jina lake linalosimama dhana ya Demokrasia ili kuleta haiba ya Maendeleo ya kweli na kusema bila ya demokrasia imara kuyafikia maendeleo ni kazi bure au ni sawa na kutwanga maji katika kinu.

Kung'atuka kwa Mtei na kumwachia usukani Bob Makani kulianza kuonyesha dira ya kupatikana umbile la chama cha siasa ingawaje nguvu ya uenezi wa sera na itikadi ya chama hicho ulielekea katika mikoa iliyo Kaskazini mwa Tanzania na hivyo umma wa wananchi werevu ukakiona na kukiita ni chama cha kikabila zaidi.

Kuondoka kwa Makani kama Mweneykiti wa pili na mrithi wake kuwa Freeman Mbowe kimsingi amekipotezea kabisa chama hicho dira, kukithiri kwa israfu ya ruzuku kuporomoka kwa amana yake ndani ya umma ikiwa ni pamoja na hadhi iliyoanza kujengeka na kupoteza imani kwa jamii kutokanana kuendeshwa kwa misingi ya kifamilia na kushamiri kwa ukabila usiojificha.

Tishio hilo lilimlazimisha Makamu Mwenyekiti wa Chadema marehemu Chacha Zakayo Wangwe kutoa matamshi kwa sauti ya juu huku akidai kunajengeka ukabila ,matumizi mabaya ya fedha za chama hicho na kuendeshwa kwa nasaba za kifamilia huku kukiwa na upendeleo wa wazi unaoweza kukigawa chama hicho na kupoteza imani kwa wananchi.

Wangwe alipoteza maisha katika mazingira ya ajali ya kutatanisha akitokea Dodoma huku akikutwa na mipasuko ya majeraha yaliokatisha maisha ya mwanasiasa huyo shujaa ambaye alitegemewa sana kumbwaga vibaya Mweneykiti Mbowe katika uchaguzi mkuu wa chama hicho mwaka huu.

Wanaharakati wenye mrengo wa kati na kutaka kujenga utetezi wa mageuzi ndani ya Chadema wanamhesabu marehemu Wangwe kana kwamba kilichokufa ni umbile lake lakini fikara na misimamo yake itadumu, kulindwa na kuendelezwa katika mapambano ya kukijenga chama hicho na kuwa cha kisiasa zaidi kuliko kilivyo sasa.

Mweneykiti wa UDP Cheyo alitofautina na kutimuana na wenziwe akina Danny Makanga, Erasto Tumbo, Benson Kigilai na Aman Nzugile Jidulamambasi huku wakidai Cheyo anakiendesha chama hicho kama kampuni yake binafsi na hataki demokrasia ya kweli istawi na kupata nafasi ndani ya UDP. Kundi la vijana hao mashababi waliokuwa mstari wa mbele yaani akina Nzugile na wenzake awali waliafikiwa moja kwa moja na Msajili wa Vyama vya siasa John Tendwa kwamba walimuondoa Cheyo katika kiti cha uenyekiti kwa taratibu halali za kikatiba lakini baadaye uamuzi huo ukabatilika na kupewa tena Cheyo uboss wa UDP.

CUF kwa kujiita na kujigamba kama ni Chama cha Wananchi kilimjengea mazingira ya utata na majungu mazito hadi kilipomtimua Mwenyekiti wake muasisis James Mapalala huku yeye akidai ukristo wake ndiyo uliomponza hata akazidiwa nguvu na wenzake akina Seif Saharif Hamad ambao ni waislam.

Wanachama waliojiondoa CUF na kuanzisha RORD waliongozwa na Ramadhan Mzee wakidai demokrasia ndani ya CUF haina hata pumzi ndani ya chama hicho ila ni kusikiliza na kutii matakwa na kuafiki maamuzi ya Maalim Seif chini ya kundi lake la KAMAHURU lilianzishwa na marehemu Shaaban Khamis Mloo.

Ile dhana ya wao kutoka CUF kwenda kujenga demokrasia walioiamini wao kama ni bora na kutafuta jina zuri la FORD ghafla ikapotea hewani na leo chama hicho kimefutwa kabisa na msajili wa vyama vya siasa kwa kukosa sifa huku CUF nayo kila ukicha kinakimbiwa na wanachama wake kwa madai ya kuimarika kwa upemba, uarabu na misimamo mikali ya kiislam.

Katika uchaguzi mkuu wa CUF; dunia na wapenda demokrasia wameshudia pia mchezo mchafu wa kisaliti uliofanywa na Profesa Ibrahim Lipumba dhidi ya mgombea mwenzake wa uenyekiti wa Taifa Profesa Abdallah Safari ambaye kama si ujasiri aliozaliwa nao Profesa Safari ilifaa aanguke na kupata kiharusi kwenye mkutano huo kutokana na wingi wa kedi na vituko alivyofanyiwa mwanasiasa huyo na wapambe wanaomuunga mkono Profesa Lipumba.

UMD kilikuwa ni chama cha kwanza kupata dhoruba na kuanza kutimuana kati ya Mwenyekiti Fundikira na Katibu Mkuu wake marehemu Kasanga Tumbo huku wakijisahau kabisa kama walikuwa na dhamana ya kulinda maslahi ya uhai wa Chama chao na kuonyesha uhalisia wa jina lao zuri na tamu kutamkwa kinywani katika kuthamini demokrasia waitakayo.

NLD nayo tokea imeanzshwa haijawahi kupata Mwenyekiti mpya zaidi ya mwanasiasa wa zamani maarufu katika kilichokuwa cha cha siasa cha ANC Dk Emanuel Makaidi ambaye tayari kimekwishamtangaza mapema kama ni mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010.

Hii ndiyo Tanzania yenye vyama vingi vya vya siasa vinavyopigania na kutetea nadharia ya demokrasia huku vikikwepa kuwa na vitendo vinavyokwenda sanjari na dhana ya demokrasia itokanayo na majina ya vyama hivyo.

Hebu tazama majina yalivyo matamu ya vyama vya siasa vya Tanzania katika nadharia mbovu na ya ajabu kabisa isiyo na ukweli wenye kufuata vitendo halisi huku vyama hivyo vya siasa vikijaa na kuongozwa na viongozi waroho wanaopalilia kustawi kwa uimla unaokwamisha pia hata ustawi wa demokarsia ndani ya nchi katika kufikia mabadiliko ya kweli yanayotazamiwa na wengi. Ama kweli chambilecho na wahenga wa kale wa kiswahili heri ya Musa kuliko yale ya Firauni.

Mwaka 2009 Chadema kalenda yake ya vikao yaonyesha kufanyika kwa uchaguzi mkuu wake na kupata safu mpya ya viongozi katika ngazi za matawi, kata, wilaya, mkoa na Taifa . Uchaguzi huu umefutika na kuviza kabisa malengo na madhumuni ya jina la Chadema yenye kutaka kujenga na kuendeleza dhana ya demokarasia iliyokusudiwa na kutazamiwa na jamii, Chadema katika uchaguzi mkuu wake kimejitia kitanzi na kujifunga spidi gavana ili kuivuruga demokrasia.

Kitendo kibaya na kibuvu ambacho hakivumiliki ni kile kilichofanywa na muasisi wa chama hicho Mtei akiwa na kundi lake la Baraza la wazee na hatimaye kulitoa katika kinyang'anyiro jina la Naibu Katibu wa chama hicho Zitto Zubeir Kabwe asiwanie nafasi ya uenyekiti unaonekana kumshinda Mbowe ndani ya Chadema.

Mtei ameliandika jina lake kwa wino wa dhambi kwenye kurasa za historia dhaifu na kufanya usaliti mkubwa wa demokrasia dhidi ya chama hicho, kwa Zitto mwenyewe na wapenda demokarsia ya kweli popote duniani. Mtei asifikiri kama amekisaidia Chadema, amemnusuru mkwewe

Mbowe lakini kwa kiasi kikubwa amekivunjia heshima na hadhi chama hicho kisiungwe mkono tena na wananchi wenye maarifa mapana ya upembuzi wa mambo katika kujenga mizizi stahili ya chama cha kisiasa ambacho kina madhumini ya kudumu na kuishi leo, kesho na siku nyingi zijazo. Mtei amepoteza na kuitupa mtoni turufu ya karata ya siasa aliyoikamata Zitto ambayo pengine ingekirahisisha sana na kubadili mitazamo ya jamii katika kukitazama Chadema kama chama cha kikoo na kikabila huku akijali zaidi kutetea maslahi ya kikanda na kikabila.

Chadema hivi sasa na wakati mwingine wowote ujao katika maisha ya siasa hawatakuwa na haki ya kukosoa au kushutumu ukiukaji wowote wa demokrasia aidha ndani au nje ya Tanzania kwakuwa wao ni wasaliti wakubwa wa jambo hilo wakiongozwa chini ya unahodha wa merikebu ya Mtei iitwalo Mv Usaliti.

Hivi ndivyo vyama vya siasa vya upinzani vya Tanzania vinavyoikosoa kila siku CCM na kusema vinaomba kura za wananchi ili kujenga utawala wa bora wa haki, sheria, maendeleo na kuimarisha dhana ya kidemokrasia?

Mungu Ibariki Tanzania

Tuma maoni [Hapa>>]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.