HUREE MAMA MWAFRIKA!

Na, Magabe Kibiti [Posted first: 11/19/06]

Siku moja nisiyoikumbuka kwa hakika kati ya mwaka 1991 na 1999, Watanzania walishtushwa na habari kwamba mwanamke mmoja katika mkoa wa Mara alikuwa amejeruhiwa vibaya sana sehemu zake za siri na mume wake kutokana na sababu ambazo hadi leo sijazielewa. Taarifa ya polisi ilieleza kwa undani kuwa, mwanaume huyo asiye na utu hata kidogo, alichukuwa vipande vya miti na kuviingiza katika uke wa mkewe ili kumkomoa mwanamke huyo aliyekuwa na mpango wa kumtaliki. Kulikuwa pia na habari kuwa mwanamke huyo alikuwa akipigwa na kudhalilishwa kila mara na mumewe mpaka akafikia hatua ya kutaka kuvunja ndoa yake.

Nasikitika kuwa; pamoja na mimi kuwa mzaliwa wa mkoa wa Mara na pamoja na sababu kuwa nimezaliwa na kukulia katika familia ya kidini, nilikaa kimya bila kufanya chochote kama mwanajumuia ili kumsaidia huyo mwanamke. Usishangae kuwa nimekiri hapo juu kuwa sikumbuki hiyo siku kwa hakika kwa sababu ni kweli kwamba sikutilia maanani ya kutosha hilo tukio kwa wakati huo. Labda kutokana na sababu kuwa miaka hiyo ya tisini nilikuwa bize sana na shule na kudhani kuwa mambo ya jamii hayakunihusu. Au labda pia kwa sababu kuwa mimi kwa macho yangu nilikuwa sijashuhudia vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake hadi wakati huo kwa kutokuwa makini au kwa kutojali. Nasikitika kuwa kuna wakati nilipoteza muda wangu mwingi kubishana na watu waliokuwa wakiwasema wanaume wa Mara kwa vitendo vyao dhidi ya wanawake.

Sio nia ya makala hii kuwasulubisha wanaume wa Mara kana kwamba ni watu waovu sana au kwamba ndio wanaume pekee huko Afrika na Tanzania wanaonyanyasa na kudhalilisha wanawake. Miaka mingi sasa imepita na labda watu wengi wamesahau tukio hili ovu lilitokea Mara. Nimeamua kutumia tukio hili kwa sababu nina hakika lilitokea na moyo waniuma sana kuwa sikufanya chochote kusaidia. Kinachoumiza zaidi ni ripoti ninazopata kila siku kuwa waafrika fulani huko Afrika bado wanawanyanyasa na kuwadhalilisha wanawake muda mwingine hata wake zao wenyewe. Kuna wengine wanatumia vigezo vya dini eti kuadhibu na kudhalilisha wanawake wanaovaa nguo fupi huku wakikaa kimya kuhusu wanaume kibao wapiga debe na makuli wanaotembea na kufanya kazi vifua wazi katikati ya miji.

Labda utashangaa ndugu msomaji ukisikia matokeo ya utafiti wa mwanauchumi Dr. Kamato Huseni Kamato. Utafiti huu uliofanywa kwa zaidi ya miaka 15 katika nchi zaidi ya 20 za Afrika unaonyesha kuwa wanawake (sio wanaume) wa Afrika wanachangia zaidi ya asilimia 70 ya mapato ya bara hilo. Inashangaza kwa sababu wanawake wengi sana hawapewi nafasi sawa na wanaume ya kumiliki uchumi na maliasili Afrika. Wanawake wengi hawaruhusiwi kuendelea na masomo ya juu Afrika. Pamoja na hayo bado ninashawishika kuamini matokeo ya utafiti huu kwa sababu nikiangalia maisha ya mama wa kiafrika ambaye anaamka saa kumi za asubuhi na kwenda shambani na mumewe. Ikifika saa tano asubuhi, mumewe anakwenda nyumbani au kutembea wakati mama wa kiafrika anakwenda msituni kusenya kuni, baadae kama saa saba mchana atakuja nyumbani na kupika chakula ili baadae atembee kilomita 10 kutafuta maji. Kama saa kumi jioni atatoka kwenda kutafuta mboga mwituni au kwenye bustani yake na baade kurudi nyumbani na kufanya shughuli zote za ndani kila siku.

Kama bado huamini nenda kasome ripoti ya uchumi ya serikali na uone kuwa serikali yenyewe inakiri kuwa kilimo bado ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu na kisha uwaulize hao wakulima juu ya mgawanyo wa kazi kati ya wanaume na wanawake. Kwa mtaji huu nasema kwa sauti ya juu kuwa; HUREE MAMA MWAFRIKA. HONGERA KWA KUCHANGIA KATIKA UCHUMI WA NCHI NA POLE SANA KWA DHARAU UNAZOPATA KILA SIKU. Sijali wazungu, waarabu, au wahindi wanasema nini kila siku kuhusu waafrika. Hainitishi hata kidogo kwamba kuna wanaume wenzangu wameapa kutowapa wanawake wa kiafrika heshima wanayostahili. Ninaandika makala hii mahsusi kwa mama mwafrika ambaye anafanya kila kitu kwa ajili ya jamii ambayo bado haijaamua kumtambua na kumuheshimu mama huyu.

Tuamke watanzania na waafrika wenzangu. Tuachane na mila au dini za ajabu na tuanze kuwaheshimu na kuwajali wanawake. Kama mmoja wa wanafunzi wa kiuchumi nimejifunza sera moja kubwa ya kiuchumi toka kwa wanawake wa kiafrika. Wamama waafrika ninaowafahamu wanajua sana kubajeti matumizi na mapato ya familia zao. Kama umekulia mikoani kama mimi utakubaliana nami kuwa kwa asili mama zetu hawana tabia ya kukopakopa au kuombaomba misaada kutoka kwa matajiri kila wakati wanapokabiliwa na upungufu. Mama jasiri wa kiafrika atatembea pori zima kutafuta mchicha mwitu ili kulisha familia yake kuliko kujidhalilisha kwa majirani. KAMA VIONGOZI WA SERIKALI ZETU WAKIFUATA ASILI HII YA MAMA MWAFRIKA YA KUISHI KWA KUJITEGEMEA, BASI NINA HAKIKA KUWA WATAFUATA PIA SERA YA UCHUMI YA MAMA MWAFRIKA NA KUPANGA SERA ZA MAENDELEO YA NCHI ZETU BILA KUTEGEMEA MIKOPO NA MISAADA KWA KILA KITU WANACHOPANGA KUFANYA.

Huree Mama Mwafrika. MUNGU akubariki na kukulinda siku zote.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.