BARUA YA WAZI KWA RAIS KIKWETE

Na, Mlenge Fanuel

"Mtu akikushauri jambo la kijinga, huku anajua jambo hilo analokushauri ni la kijinga, na wewe ukakubali, basi atakuona, wewe zuzu!" -- Mwalimu Julius K. Nyerere, 1994/5.

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tafadhali isome barua hii ya wazi ya kukufikishia ujumbe kwamba Tanzania haiko tayari kujiunga na Shirikisho la Afrika Mashariki (East African Federation, EAF) wala “Soko la Pamoja” la Afrika Mashariki, na kwamba Watanzania hatutaki Tanzania ijiunge na Shirikisho hilo.. Yatakuwa ni maafa makubwa kwa Tanzania na Watanzania iwapo Tanzania itajiunga na EAF hasa kwa mpangilio ulioko wa “fast track”. Ndiyo maana nimeanza na nukuu ya Mwalimu Nyerere, ambaye tayari baadhi ya watu, hasa wa nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda, wameanza kumsingizia kwamba kwa kujiunga na EAF tutakuwa "tunamuenzi" Mwalimu Nyerere, huku wakijua fika ushauri wanaotupa wa kujiunga na Shirikisho na Soko la Pamoja la Afrika Mashariki hauna manufaa yoyote kwa Tanzania, wakidhania sisi Watanzania ni mazuzu tunaoendekeza wema wa mshumaa kuwaangazia wengine huku wenyewe unateketea, kwa minajil ya kupata misifa isiyo na tija.

Ni kweli Mheshimiwa Rais umeunda Tume ya Kupokea Maoni kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, lakini inatia mashaka iwapo huo siyo tu ni utaratibu uliouweka kuhalalisha maamuzi yaliyokwishafikiwa ya kuidumbukiza Tanzania kwenye EAF. Nasema hivyo kwasababu kuna kila ishara zinazoonyesha kuwa uamuzi Tanzania kujiunga na EAF umeishafikiwa tayari; na suala la kutaka watanzanaia kujadili kujiunga/kutokujiunga si kinginecho kile isipokuwa kiinimacho tu.

Mheshimiwa Rais, palikuwa na muswada uliopelekwa Bungeni wa Tanzania kujiunga na EAF, ambao Waheshimiwa Wabunge waliukataa, na serikali ikabidi iuondoe. Lakini mchakato wa Tanzania kujiunga na EAF ukaendelea tu, na kupuuza maoni ya Wabunge wetu tuliowachagua watuwakilishe. Ikiwa sikusikiliza vibaya, katika Bunge la Bajeti 2006/2007, Mheshimiwa Waziri wa Afrika Mashariki aliliambia Bunge kwamba patakuwa na KURA YA MAONI kuhusu Afrika Mashariki. Matokeo yake tumeletewa Tume badala ya kura ya maoni! Kana kwamba hiyo haitoshi, iliripotiwa kwenye vyombo vya habari kuwa wewe Mheshimiwa Rais wetu, ulimhakikishia Rais Yoweri Museveni wa Uganda kwamba utafanya kila unaloweza kuhakikisha kufanikiwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki, kwenye mkutano wenu uliofanyika Mwanza. Je, maoni tunayotoa Watanzania kukataa kujiunga na shirikisho si "kilio cha samaki kweli huko machozi yakitokomea majini...?" Wenyewe, [ninavyoona] "wenye nchi" mshaamua mloamua na maoni yetu hayana faida yoyote ile?

Pana maswali mengi mheshimiwa Rais ambayo ukitupatia majibu utakuwa umetuwezesha Watanzania tulio wengi kuelewa kuhusu mustakabala wa maisha yetu na Tanzania yetu:-

[1] Je, Ni sera ya CCM Tanzania kujiunga na EAF au Soko la Pamoja la Afrika Mashariki au nikukurupukia tu mambo yasiyokuwepo hata ndani ya sera za chama? [2] Je, Ilikuwa kwenye ilani ya Uchaguzi 2005 ya Chama Tawala CCM Tanzania kujiunga na EAF? [3] Je, Nani aliyependekeza Tanzania ijiunge na EAF? (Inabidi tumfahamu ili tuweze kumpamba maua iwapo Tanzania itafanya tunalodhani ni kosa la maisha la kujiunga EAF kumbe ikathibitika EAF ni manufaa tele kwa Tanzania; vinginevyo inabidi tumfahamu ili tuweze kumzomea na kumuimbia nyimbo za kumsimanga pindi machungu ya EAF yatakapoanza kudhihirika muda si muda iwapo Tanzania itafanya kosa la maisha kujitumbukiza kwenye EAF. Vinginevyo itakuwa kama mikataba ya madini -- hatuelezwi nani aliwaalika na kuingia mikataba na 'wawekezaji' kwenye migodi.) [4] Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameshajitangaza kuwa Rais wa Kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki -- ikiwa na maana yote mengine yanayojitokeza sasa ni kuhalalisha na kusafisha njia ya Museveni kuwa Rais wa Kwanza wa Shirikisho la Afrika Mashariki, hasa ukitilia maanani Rais wa Kenya na wewe Rais wetu mko kimya, ikielekea mmekubaliana na matamshi ya Museveni. Je, hivyo ndivyo ilivyo ama...[Tafadhalitueleze!]? [5] Kutokana na maneno yanayosemwa na Wakenya na Waganda, Wanyarwanda na Warundi, inaonekana kama vile serikali ya Tanzania HAINA UBAVU wa kusema HAPANA kwa EAF -- kila mara Tanzania inazomewa inapohoji maslahi yake kwenye EAF -- au inapotaka kutumia uhuru wake ISIJIUNGE na EAF. Mathalani, hivi karibuni Waziri wa Afrika Mashariki wa Tanzania alisemwa kwenye vyombo vya habari kwamba hahudhurii vikao vya Afrika Mashariki -- na kumfanya Mheshimiwa Waziri Mkuu ajitokeze kumtetea -- na baadaye Waziri yule akaondoshwa toka Wizara ya Afrika Mashariki kwenye mabadiliko ya Baraza la Mawaziri uliyoyafanya hivi karibuni. Mheshimiwa Rais, ina maana Tanzania ni kama mbwa anayeelekea kwenye mdomo wa chatu [EAF] -- huku amefyata mkia, na kutoa kilio cha mwisho, asiwe na la kufanya zaidi ya kufanywa asusa na kumezwa. Je, hivyo ndivyo ilivyo [Tafadhali tueleze!]? [6] Ni kwa nini Kiswahili SIYO lugha rasmi EAC, na badala yake ni kiingereza? * Kama shida ni ushirikiano, kwa nini Tanzania isijiunge na Msumbiji na Zambia , na kutengeneza shirikisho? * Kwa nini EAF inaharakishwa namna hii? [7] Ni nini Tanzania inahitaji kwenye EAF ambacho haiwezi kukipata bila kuwemo kwenye shirikisho hilo? (Mbali na ngonjera za kisiasa, pengine na watu fulani kupata posho za vikao vya EAC na baadhi kuandikwa kwenye vitabu vya historia, vitu ambavyo havimsaidii Mtanzania mpiga kura wako anayesubiri neema tele na maisha bora...) [8] Ni bidhaa zipi za Tanzania ambazo hazifiki kwenye soko Kenya au Uganda , ambazo EAF itazifanya zifike huko? [10] Nani atakuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Afrika Mashariki, na ni upi mchango wa EAF kwenye uvamizi dhidi ya DRC? [11] Mheshimiwa Rais, hivi "Usalama wa Taifa" wa Tanzania una majukumu gani makubwa zaidi ya kulinda (uhuru) "Sovereignty" ya nchi yetu? Kwa nini "Usalama wa Taifa" haukupi picha kamili ambayo itakufanya usijisumbue hata kuja kutuuliza iwapo tunataka uhuru wa nchi yetu uondoke kupitia "soko la pamoja" na "Shirikisho la Afrika Mashariki", badala yake tukaendelea kulijenga taifa "letu changa" na kuulizana maswala ya maendeleo kama vile tutanufaikaje na maliasili tulizojaaliwa nchini mwetu? [12] Kwa kuitumbukiza Tanzania kwenye "Soko la Pamoja" la Afrika Mashariki, huoni kwamba utakuwa umekiuka kiapo ulichokula cha kuulinda uhuru wa, na mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ? [14] Kulikuwa na sababu gani ya kupambana na Idd Amin aliyetaka kipande "kidogo tu" cha nchi yetu, ikiwa leo tunaigawa sandakarawe nchi nzima kwa kisingizio cha soko la pamoja? [15] Je, Tanzania itaondoka SADC? (Tayari nchi nyingine za Afrika Mashariki zimeanza kutuamuru tutoke SADC. SADC imeweka bayana kwamba wakati umefika wa kuchagua kati ya EAF au SADC.) Unadhani itakuwa ni busara kuondoka SADC? Kwa nini usitoe tamko kwamba Tanzania ya kesho ni ndani ya SADC? [16] Je, sisi wananchi wa Watanzania tutaulizwa kuhusu kujiunga na "Soko la Pamoja la Afrika Mashariki" au ni uamuzi uliofikiwa tayari kwamba tutajiunga na soko la pamoja la Afrika Mashariki? [17] Huo Mkataba wa EAC/EAF uko wapi ili tuweze kuuona na kuusoma? Ni Watanzania gani waliousoma na kuuridhia kwamba SASA tunaanza kuwa kwenye mchakato wa kuelekea kwenye Shirikisho? (Inaripotiwa kwamba Tume yako ni sehemu tu ya taratibu ‘chovu' za mchakato huo...) Watanzania tutafanyaje ili kuondoka kwenye EAF, iwapo Tanzania ijajikaanga yenyewe kwa kuingia kwenye EAF? Vipengele vya kujiondoa kwenye EAF viko wapi? Hautakuwa ni uhaini kuzungumzia kujitoa EAF, kama ambavyo si ruksa kuzungumza kujitoa kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ?

Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, maswali hayo na mengine mengi yanaleta changamoto kwako binafsi kwamba zawadi kubwa kuliko zote unazoweza kutupa sisi Watanzania, ni kutukabidhi Tanzania yetu yenye "sovereignty" ileile au zaidi ya uliyokabidhiwa pale utakapoacha madaraka mwaka 2010 au 2015, panapo majaaliwa.

Kwa taarifa yako Mheshimiwa Rais, Tanzania ndiye "Mbuzi wa Shughuli" kwenye Shirikisho la Afrika Mashariki. Na mbuzi huyu amepangwa "kuchinjiwa kwenye maji" ili hata ukelele wake wa mwisho usisike. Hawatarudia makosa ya Jumuia ile iliyokufa 1977, kwa kutuacha bado tunafurukututa. Kujiunga kwa Tanzania EAF kwafanana na Punda wa kwenye hadithi moja iliyochapishwa Tanzania ambamo Simba baada ya kujeruhiwa, alishindwa kuwinda; na Sungura, Fisi na Punda wakaenda kumpa pole. Kumbe Fisi na Sungura walikuwa na lao jambo. "Simba kwa kuwa huwezi kuwinda naomba unile mimi", alianza kusema Sungura. " ...Asante sana kwa kunijali, siwezi kukula wewe rafiki yangu. Sasa nimefahamu wewe ni rafiki yangu wa kweli katika kipindi hiki kigumu cha dhiki!," alijibu Simba. Fisi naye akajitoa aliwe na Simba, ambaye pia alikataa kumla, akitoa sababu zilezile. Sasa Punda akawa njia panda: "Nikikaa kimya nitaonekana mbaya kwa Simba. Kwanza Simba mwenyewe kakataa kuwala wenzangu, na mimi atakataa... acha nijisemee tu kwamba najitolea anile..." aliwaza. Akaropoka, "Simba kwa kuwa huwezi kuwinda naomba unile mi..." Kabla hajamaliza maneno yake alirukiwa na kuraruliwa palepale.

Kenya, Uganda , Rwanda na Burundi zina ajenda kadhaa kwenye EAF: mbali na zile "rasmi" zinazotangazwa hadharani. Ili ajenda zao zitimie, lazima "Punda" Tanzania awemo kwenye EAF ili aweze "kuliwa". Mheshimiwa Rais, ni wajibu na heshima kwako kuhakikisha Tanzania haijiungi na EAF kwa kuwa Tanzania haina ajenda mbali na ngonjera za kisiasa, pengine na posho za vikao kwa baadhi ya watu. Hata hivyo, Tanzania siyo lazima ijiunge au ikubaliane na kila kitu kwenye ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wachache wanaounga mkono kujiunga na shirikisho la afrika mashariki, wanadai upo umuhimu wa kujiunga kwa vile "dunia nzima mwelekeo ni kujiunga pamoja, kama vile Jumuia ya Ulaya, EU". Kama sababu ni hiyo, kwa nini tusibakie SADC tuliko? Hivi tulipigania uhuru wa kusini mwa Afrika ili iweje? Watanzania tulitoa damu zetu, mali na uhai wetu, kukomboa Ndugu zetu walio Kusini mwa Afrika, sasa ukombozi umepatikana, pana wakati gani muafaka zaidi ya huu kuendeleza undugu wetu? Majirani zetu wa Afrika Mashariki tutaendelea kushiriana nao, kama tunavyoendelea kushirikiana na majirani zetu wengine. Kutojiunga kwenye shirikisho siyo maana yake tutakuwa maadui!

Tanzania lazima ikae mbali na EAF, hata ikibidi kwa miongo kadhaa ijayo, ikiwa si moja kwa moja. Kwanza, Muungano wetu wenyewe una "mipasuko" ambayo haijasilibwa bado. Kabla ya kuulizwa kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, tuulizwe basi kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Tanganyika na Zanzibar , mara baada ya kupata Uhuru, hazikutimiza miaka mitano, "zikaishia" na kuwa Taifa moja Tanzania . Sasa jamani, Tanzania hata miaka hamsini haijafikia, nayo "iishie", tena kusikoeleweka? Tanzania ina manufaa tele SADC, kuliko kwenye shirikisho la Afrika Mashariki. Hivi, wakati tulipokuwa "Mstari wa Mbele wa Ukombozi Kusini mwa Afrika", majirani zetu wa Kenya na Uganda walikuwa wapi? Leo hii tukiwakubalia kuondoka SADC, watatuona timamu kweli?

Mheshimiwa Rais Kikwete, kiasi inaeleweka ikiwa unaona pana ugumu wa wewe kuonekana unakwenda tofauti na Watawala wetu waliotutangulia, ambao huenda wanapendelea kuona EAF ikizinduliwa, Tanzania ikiwemo. Lakini mheshimiwa Rais, ndiyo maana kukawa na kikomo cha utawala cha vipindi viwiliviwili! Kwa kuwa umechaguliwa kwa ushindi "wa kishindo", imani yetu Watanzania imekuwa kwako kwamba utaweza kuipeleka Tanzania kule tunakotaka. Na tunakotaka sisi Watanzania siyo kwenye "soko la pamoja la afrika mashariki" wala EAF. Huo Muungano tu wa Forodha wa Afrika Mashariki unatekelezwaje? Matatizo na mizengwe iliyoko panaashiria nini pindi tukiwagaia nchi hii yote kwenye Shirikisho au "soko la pamoja"? Siyo maafa, Mheshimiwa Rais?

Mheshimiwa Rais Kikwete, kwenye Jumuia ya Ulaya --EU, Uingereza na Jamhuri ya Ireland SIYO mataifa yaliyoko kwenye "Mkataba wa Schengen" wa Jumuia ya Ulaya, mkataba unaoondoa mipaka na vizuizi baina ya nchi za Jumuia ya Ulaya kwenye masuala ya Uhamiaji, japo Uingereza na Jamhuri ya Ireland ni wanachama kamili wa Jumuia ya Ulaya. Hii haikuzuia Ufaransa, Uholanzi, Ubelgiji, Ujerumani na nchi nyinginezo za EU pia zilizokubali kusaini kuendelea na "Makubaliano ya Schengen". Kadhalika, Iceland , Norway na Uswisi zimesaini "Mkataba wa Schengen" japo nchi hizo SIO wanachama wa Jumuia ya Ulaya. Kila taifa linaangalia maslahi yake kama taifa.

Ni vema tukumbuke pia kwamba, ulipoanzishwa umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki takriban karne moja iliyopita, Tanganyika haikujiunga mpaka ilipoona vema kwamba itakuwa ni kwa maslahi yake kujiunga. Hii haikuzizuia Kenya na Uganda kuanzisha Umoja wao wa Forodha. Tanganyika ilijiunga baadaye! Hata ile Jumuia ya Afrika Mashariki iliyovunjika, ilianzishwa baada ya kupita MIAKA HAMSINI tangu kuanzishwa ule Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, japo nchi hizi zote tatu zilikuwa zinatawaliwa na Mkoloni mmoja takriban muda wote huo. Haraka ya sasa hivi ya nini? Wanajua wakituachia muda, tukienda hatua kwa hatua, hawataweza tena kuigeuza Tanzania koloni lao. Tanzania iendelee kuwa mwanachama wa SADC, na kuendelea kuwa imesaini kwa muda makubaliano ya Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki mpaka pale SADC itakapoanzisha Umoja wa Forodha wa SADC, ambapo Tanzania itajitoa kwenye Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki. Au busara zaidi, ni vyema Tanzania ikajitoa SASA HIVI toka Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, na kuelekeza nguvu zake kwenye SADC. Kenya , Uganda , Rwanda na Burundi zinaweza kuendelea na Umoja wao wa Forodha, Soko la Pamoja na Shirikisho (waliite vyovyote wapendavyo), bila Tanzania kuwemo.

Mheshimiwa Rais, ukubwa wa eneo la ardhi ya Tanzania ni zaidi ya Jumla ya eneo lote la ardhi ya Kenya , Uganda , Rwanda na Burundi ukizichanganya pamoja -- bila kuzungumzia rasilmali zilizoko. Halafu wanasema tuchanganye ardhi yetu na zao, halafu tugawane sawasawa kwa jina la "Soko la Pamoja la Afrika Mashariki". Hivi tukikubali ujuha huo, ni kwa nini wasituone sisi mazuzu?

Swali kuu tunaloulizwa Watanzania na Tume yako mheshimiwa Rais ni iwapo Watanzania tunaona bado kama kuna sababu za msingi kwa Tanzania kuendelea kuwa nchi huru ambayo ni "dola", wakati ambapo kuna shinikizo la kuitaka nchi yetu igawe uhuru wake kwa kisingizio cha "soko la pamoja" na "shirikisho la Afrika Mashariki". Tuchukulie kwa mfano, tume itawahoji na kupokea maoni toka kwa watu laki mbili. Kati yao 80% wakasema Tanzania ijiunge kwenye "Soko la Pamoja" na "Shirikisho la Afrika Mashariki", 20% wakasema tusijiunge. Je, Mheshimiwa Rais, hiyo itakuwa na maana uamuzi utakuwa umesilibwa wa Tanzania kufikia mwisho wake, kwa kujiunga na Soko la Pamoja na Shirikisho la Afrika Mashariki? Je, hutatumia busara kama ilivyotumika kwenye Tume ya Nyalali ya Vyama Vingi pale Tanzania ilipoangalia maslahi ya taifa, na kuruhusu mfumo wa vyama vingi, bila kuangalia asilimia zilizotokana na tume? Ikiwa kweli kabisa umedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye mwisho wake machinjioni Afrika Mashariki, kwa nini usiweke KURA YA MAONI kwa kila Mtanzania kupiga kura yake, badala ya kutumia Tume, angalau basi kuchelewesha kwa muda wa mauti ya Taifa Tanzania?

"Soko la Pamoja" na pacha wake "Shirikisho la Afrika Mashariki" maana yake ni mwisho wa uhai wa Taifa la Tanzania . Ikiwa Tanzania itajinyonga (Mungu apishie mbali!) kwa kusaini mkataba wa "Soko la Pamoja la Afrika Mashariki" au ule wa "Shirikisho la Afrika Mashariki", basi Watanzania tutasahau "maisha bora kwa kila Mtanzania," na kwamba wewe Rais wetu, Jakaya Kikwete, utakuwa umefeli vibaya kabisa juu ya jukumu lako la msingi tulilokupatia -- kulinda uhuru na umoja wa Taifa la Tanzania na kubakisha Taifa la Tanzania kuwa dola huru kwa manufaa ya Watanzania mpaka pale utakapomkabidhi madaraka ya Urais wa dola la Tanzania huru Mtanzania mwingine. Kwa kuandika barua hii, imani yetu Watanzania kwako Rais wetu kwamba utaweza kuhimili mashinikizo yote ya nje, na kutusikiliza sisi raia zako, tunaotaka tubakie na taifa letu huru la dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Mwenyezi Mungu akujalie. Amin.

Ndimi, Mlenge Fanuel

Raia na Mwananchi wa Tanzania,

Simu: +255 75 4372902,

Email: mlenge@yahoo.com

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.