BARUA YA WAZI KWA VIONGOZI WALA RUSHWA

Na, G <Posted first on: 11/26/06> [Re-edited 02/26/10]

Kwa masikitiko makubwa tumepata taarifa kuwa hali ya uzalishaji umeme imezidi kuwa mbaya hadi kulazimisha shirika la umeme nchini kulazimika kuongeza mgawo wa umeme kwa wananchi wake. Kwa upande wa visiwani, hali ni mbaya zaidi kiasi kilchopelekea serikali ya Uingereza na Sweden kujitolea kupeleka majenereta yatakayozalisha umeme wa dharura/Megawati 25. Hili linasikitisha zaidi hasa pale ambapo serikali ilishaingia mikataba na makampuni kadhaa ya nje ili kuokoa hali hii lakini kwa bahati mbaya inaelekea baada ya mikataba kuandikwa na fedha kulipwa na waliodhamini mikataba kupewa bakshishi zao, kunakuwa hakuna ufuatiliaji wowote ule tena. Mfano mzuri ni mikataba mibovu ya Richmond na IPTL ambapo shirika la umeme nchini TANESCO lilishinikizwa na wizara ya nishati kukubali mikataba hii ambayo badala ya kutatua tatizo la mgao wa umeme, mgawo wa umeme umebakia palepale miaka nenda, miaka rudi.

Hii ni mojawapo tu ya maeneo mengi ambayo taifa letu limejikuta likizorota sana katika maendeleo yake kwa sababu ya watu wachache ambao wanapenda kujinufaisha binafsi kwa gharama ya ustawi wa taifa na wananchi wengine kwa ujumla. Viongozi hawa wachache ambao walielewa fika wakati wakikabidhiwa uongozi kuwa uongozi ni dhamana wanayopewa kwa niaba ya wananchi, lakini wao wanageuza nyadhifa zao hizo za uongozi kuwa miradi binafsi ya kuzalishia fedha.

Nchi yetu imekuwa ikiathirika saaaana kutokana na utamaduni wa viongozi wa ngazi mbali mbali za serikali kutanguliza tamaa zao binafsi kiasi kwamba miradi pekee wanayoiidhinisha ni ile ambayo itawapatia bakshishi fulani. Na mingi ya miradi hii inaishia tu kuwa miradi ya bakshishi ambapo viongozi wanapata angalau asilimia kumi ya gharama nzima ya zabuni na hili huwafumba macho wasione kwamba kiukweli miradi hii haileti maendeleo yoyote. na hata pale wanapoona kuwa miradi hii haileti maendeleo yoyote basi bakshishi hizo pia huwaziba midomo wasiweze kulisema hilo wazi kwa woga kwamba wakifanya hivyo wataadhiriwa kuwa wao ndio waliodhinisha mikataba hiyo kwa kukubali asilimia kumi (Rushwa) huku wakijua wazi miradi haitafanikiwa. Na miradi ile ambayo ndiyo kweli hasa ingeleta maendeleo lakini haina bakshishi, haipati idhini ya watendaji hawa wa serikali.

Tunalisema hili kwa kutumia tatizo la umeme nchini linaloendelea sasa hivi maana huo ni mfano hai wa namna ulaji rushwa wa viongozi wetu unavyodumaza maendeleo ya nchi yetu maana mara baada ya vyombo vya habari, wananchi binafsi na hata maafisa kadhaa wa TANESCO kupigia kelele mizengwe iliyokuwepo katika mikataba ya umeme hasa ule wa Richmond, maafisa wa wizara (ambao yawezekana ndiyo walipata mgao wa bakshishi) walilipinga hilo kwa nguvu zote na matokeo yake tumeyashududia wenyewe.

Sasa kwasababu inaonekana rushwa imeshakuwa sehemu ya utamaduni wetu kwamba hakuna kitu chema kwa ustawi wa jamii ya wa-Tanzania ambacho kitaidhinishwa bila rushwa kutolewa; na kwasababu inaanza kuonekana dhahiri kwamba hata kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya ya awamu ya nne kutokomeza rushwa nayo imegonga mwamba, nataka kutoa mapendekezo mawili, kwanza kwa wananchi wote na pili kwa viongozi ambao tayari wameshajenga utamaduni wa kula rushwa ambao kwao inaonekana ni ngumu kuacha tabia hii.

Kwa wananchi: ushauri ni kwamba inabidi sasa tukubaliane tu na hali halisi kwamba tulizembea kwa muda mrefu kuacha viongozi wetu wafanye wanachotaka na kudumisha fikra za viongozi hao na sasa rushwa imeshaota mizizi mikubwa katika mfumo wa uongozi wetu na hatuwezi kuing'oa. Inabidi tukubaliane tu kwamba viongozi wetu wameshakuwa wala rushwa kwa asili na wako wengi tu wenye umoja na nguvu kiasi kwamba hata serikali kama ya awamu ya nne inayokuja na nia njema ya kung'oa mizizi ya rushwa imeshindwa. Kwa hiyo labda badala ya kutumia nguvu nyingi kupigia kelele rushwa, labda tungetumia nguvu hizo kwa shughuli zetu zingine binafsi ambazo yawezekana kama tukizifanya kwa nguvu tunayotumia kupigia kelele rushwa, hali zetu za maisha zitaboreka zaidi. Huu siyo ukweli mtamu lakini ni ukweli kwamba kama serikali ya awamu ya nne iliyoahidi nguvu mpya, ari mpya na kasi mpya, na ni serikali yenye vyombo vya dola imeshindwa hata kupunguza rushwa, wananchi wasio na dola tutakuwa tunatwanga tu maji, maana viongozi hawa wala rushwa inaelekea hawasikii na hawana nia ya kusikia vilio vyetu na pili hawana mpango wa kutosheka kula rushwa hivi karibuni.

Na kwa viongozi wala rushwa: Kwasababu inaonekana kiini kikubwa cha kutaka kula rushwa ni tamaa ya fedha na nia ya kujilimbikizia mali nyingi kadri inavyowezekana. Ikiwa ndivyo, basi inawezekana kama mkitulia na kufikiri, mnaweza mkagundua kuwa mngeteng'eneza fedha nyingi zaidi kama nchi ingekuwa imeendelea zaidi ya ilivyo sasa. Kwa nchi maskini kama Tanzania ambayo uchumi wake bado ni mdogo, fedha ambayo inaingia na kutoka katika uchumi wetu ni kidogo, na asilimia kumi ya hiyo kidogo nayo ni kidogo. Kama uchumi ungekua umekua na kuongeza kiwango cha fedha kinachoingia na kutoka katika uchumi wetu, bakshishi zenu zingeongezeka na mngeweza kujilimbikizia  zaidi sana kuliko mnavyofanya sasa hivi.

Hivyo basi, pendekezo kwenu (ambalo pia ni ombi) ni kuchukua likizo ya kula ruswa. Au kwa lugha nyingine, tunawaomba kama mkiona vyema mchukue likizo kidogo ya kula rushwa. Siyo kwa sababu mnaacha habari ya rushwa, hapana, bali sababu ya kuboresha hali ya uchumi ili mafao ya rushwa yaongezeke. Ni ukweli usiopingika kwamba endapo mtasimama kula rushwa kwa muda kidogo na mhimize kuidhinisha miradi ile ambayo italeta na kuinua maendeleo ya nchi (kama vile Stiegler's Gorge huko Rufiji), uchumi utaongezeka ghafla na mapato ya nchi na wananchi yataongezeka na mkondo wa fedha zinazoingia na kutoka serikalini utaongezeka na hiyo kupelekea hata bakshishi zitakazopatikana baada ya uchumi kukua kuongezeka na ninyi pia kujinufaisha zaidi na viwango hivyo vikubwa vya rushwa. Kuna mifano mingi ya hili lakini tukitazama nchi kama India ambapo rushwa ipo, lakini wadau wa nchi waliacha uchumi wa nchi ukue kwanza na sasa India ni nchi ya dunia ya pili na uchumi wao unashindana na nchi tajiri duniani hata sasa ni moja ya nchi zenye nguvu za Nyuklia duniani.

Tukirudi kwenye mfano wa umeme, miradi yote ambayo imeshaidhinishwa ya umeme ya megawati 20, au 40, au 80 au 100 inawezekana iliwanufaisha kwa kiwango ilichowanufaisha, lakini ukweli utabaki kuwa miradi hii yote haitafanya tofauti yoyote katika maendeleo ya jamii ya watanzania. Endapo aidha msingeidhinisha miradi hii au mkaidhinisha miradi hii sambamba na mradi wa bonde la mto Rufiji wa Stiegler's Gorge ambao unaweza kuzalisha umeme hadi megawati 2000, takribani mara kumi ya miradi hii mingine yote kwa pamoja, Tanzania ingeweza kupata umeme wa kutosha kabisa na kulingana na taarifa ya utafiti wa mradi huo hata kuzidi na kuuzwa nje. Hili lingeweza kuwa na manufaa mengi sana kwa taifa. Kwanza umeme ungetosheleza wananchi na wananchi wangeridhika sana kiasi kwamba kusingekuwa na kelele hata kwenye vyombo vya habari kuhusu tatizo la umeme. Pili kuwepo kwa umeme wa uhakika nchini kungevutia hata wawekezaji wengine wengi ambao wanatamani kuja kufanya biashara nchini lakini wanasitasita kwa sababu ya kutokuwa na chanzo cha uhakika cha nishati. kama wafanyabiashara hawa wakija na kuleta biashara zao, uchumi wa taifa utaongezeka. Tatu wafanya biashara hawa wakileta biashara zao, pamoja na mambo mengine wataongeza ajira nchini, hivyo kuongeza nguvu kazi na hata mapato ya serikali kwa kodi inazotoza yataongezeka hivyo kuongeza kiwango cha bakshishi zenu. Na kama tulivyosema hapo awali uchumi mkubwa huongeza wigo wa biashara na kuongeza kwa kiwango kikubwa kiasi cha fedha zinazoingia na kutoka katika uchumi huo na kama tukikua kiasi hicho na kuongeza kiasi hicho cha fedha hata rushwa itaongezeka. Kama uchumi wa Tanzania ni uchumi wa (kwa mfano) shilingi milioni moja, na kama bakshishi yeni ni asilimia kumi ya miradi ya uchumi huo, kiwango cha juu kabisa mnachoweza kupata ni shilingi laki moja. Lakini mkishirikiana kuhimiza maendeleo ya nchi na kukuza uchumi kwa muda kuruhusu uchumi ukue na kwa mfano ukue kufikia kuwa uchumi wa shilingi Billioni moja. Bakshishi ile ile ya asilimia kumi itaongezeka ghafla kuwa shilingi milioni mia moja, hapa hata kama mko mia moja kila mmoja atapata shilingi milioni moja ambayo ingekuwa sawa ukubwa wa uchumi wa taifa hapo awali.

Kana kwamba hilo halitoshi, taarifa za utafiti wa Stiegler's Gorge zinasema umeme utakaozalishwa utakuwa mwingi wa kutosha matumizi ya nchi na kuzidi hata kuwa na uwezo wa kuuza nje. Wananchi wetu wa Tanzania ni watu wanaoridhika sana maana hata sasa hawapati umeme lakini hawaoni pia nia ya kufanya uasi wa aina yoyote. Sasa endapo mradi kama huu unafanikiwa wananchi wanaridhika na nishati wanayopata na miradi na kazi zao zinaendelea, bado nyie viongozi wa serikali mna nafasi nyingine ya kujilimbikizia mapato kwa kuuza ule umeme wa ziada nchi za nje na yoyote yaliyo mapato yatakayopatikana mkapata bakshishi humo.

Sasa basi tumesema tatizo la umeme ni moja tu ya matatizo mengi ya maendeleo ya jamii nchini ambayo yanakwamishwa kwa sababu ya rushwa. Na kama tulivyoona kwa umeme, ipo pia miradi mingi ya maendeleo ya kweli kwa taifa na kwa wananchi ambayo haina bakshishi lakini hapa ikiiidhinishwa na kufadhiliwa na serikali, itatatua matatizo na kero za wananchi, kuongeza maendeleo ya nchi, kukuza uchumi na pato la taifa na kuboresha hali ya taifa na kwenu (wala rushwa), kuongeza bakshishi.

Hivyo basi, pendekezo letu na ombi letu ni kwamba kwa sababu tumeshindwa kuwapigia kelele za kutosha kuacha kula rushwa, kwa sababu serikali imekosa nguvu za kutosha kuwakataza kula rushwa, tunawaomba mchukue likizo kidogo tu ya kula rushwa na kwa pamoja tuweke nguvu zetu zote kuhimiza maendeleo na kukuza uchumi wa taifa au kama hata hilo linakuwa gumu kwenu, basi muidhinishe miradi yenye bakshishi sambamba na ile itakayoleta maendeleo halisi na ya kweli kwa nchi na wananchi ili hatimaye maendeleo yatakapopatikana, uchumi utakapokua, na pato la nchi na wananchi litakapoongezeka, ndipo mrudi kazini kuendelea kula rushwa maana hata nyie mtanufaika (Katika kula rushwa) na maendeleo tutakayokuwa tumeyafikia.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.