HEKO TAIFA STARS

Na, G

Ikiwa zimebakia siku chache tu kabla ya kipindi  cha siku kuu  nyingi za dini zote yaani Christmas kwa wale wakristo, Eid ul-Adha kwa wale waislamu na nyinginezo kama Hanukkah kwa wenzetu wayahudi, basi labda pamoja na mambo mengi ambayo ni matatatizo yanayoikabili nchi yetu, labda ni wakati wa kuangalia yale mafanikio kadhaa ambayo tumeyafikia.

Na kabla hatujaingia kwenye mada yenyewe, tunawatakia nyote sikukuu njema. Merry Christmas, Eid ul-Aidha kwa wale wanaohusika. Happy Hanukkah kwa wanaohusika pia. Na kwa wengine wote waliosalia, tunawatakia Heri ya Mwaka mpya. Kwa pamoja, BongoTz tunaamini kwamba tunapojiandaa kuuaga mwaka huu na kuukaribisha mwaka mpya [2007]; kama raia wema wa dunia, tutajitahidi ndani ya uwezo wetu kuufanya mwaka ujao kuwa bora zaidi ya huu tunaoumaliza.

Sasa tukirudi katika mada yetu, moja ya mambo ambayo binafsi naona ni mafanikio kwa kiwango fulani cha uongozi wa awamu ya nne ni timu yetu ya taifa ya mpira wa miguu [Taifa Stars]. Kama tukikumbuka hapo mwanzoni mheshimiwa Rais alitoa ahadi kwamba maendeleo ya soka ya Tanzania hasa maendeleo ya timu yetu ya taifa, ni mambo ambayo yeye binafsi atayafanyia kazi. Na tukikumbuka vyema alitoa changamoto kwamba yeye atagharamia kocha yeyote shirikisho la mpira wa miguu litakayempendekeza na kwa kweli wakaleta kocha ambaye ana sifa nzuri duniani. Shukrani Mh. Rais, sasa tunaye Mbrazil Marcio Maximo.

Tangu kuwasili kwa Maximo ambaye amewahi kuzifundisha timu kubwa duniani kama vile club ya Livingston (2003/2004) na timu ya taifa ya vijana ya Brazil under-17 & under 20 (1992/1993); timu ya taifa imeanza kufanya maendeleo mazuri na si tu kimchezo bali pia hata idadi ya mechi za kimataifa za kujipa nguvu nazo zimeongezeka hivyo kufanya nafasi ya timu yetu ya taifa katika hadhi ya timu za soka duniani kupanda kwa kiasi fulani katika daraja la timu za soka duniani inayotolewa kila mwezi na shirikisho la soka duniani (FIFA).

Katika miezi ya hivi karibuni timu yetu ya taifa imejitahidi sana kuwa na michezo kadhaa ya kimataifa na hata viongozi wengi wa kitaifa wameonyesha kuiunga mkono timu ya taifa kwa kuhudhuria michezo mingi inayofanyika Tanzania akiwemo Rais mwenyewe. Hivi karibuni, katika sherehe za kusherehekea miaka 45 ya uhuru timu yetu ya taifa ilifanya vizuri na kuifunga timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mbele ya umati mkubwa wa wananchi na viongozi wa taifa. Hii ni baada ya timu ya bara Kilimanjaro Stars kufanya vizuri pia katika kombe la chalenji na hata kuzifunga timu kadhaa zenye hadhi ya juu zaidi yetu kwenye mashindano ya yaliyofanyika Addiss Ababa, Ethiopia. Ingawa hatukutwaa kombe lakini tulifika robo fainali.

Katika miezi minne iliyopita hadhi ya timu yetu ya taifa - Taifa Stars, imekuwa ikipanda katika daraja la orodha ya timu za taifa za soka duniani. Ingawa nafasi iliyopo sasa bado hairidhishi lakini kwa sababu kumekuwa na maendeleo nadhani ni vyema kutoa pongezi kwa wadau mbalimbali wa soka ndani na nje ya nchi waliochangia kwa mafanikio yaliyopatikana.

Kwa takwimu za hivi karibuni, mnamo mwezi wa tisa, timu ya taifa ilikuwa inashikilia nafasi ya 164 katika orodha ya timu 198 zinazotathminiwa kila mwezi na shirikisho la soka duniani na kutolewa katika FIFA Coca Cola World Ranking. Cha kufurahisha zaidi mwezi uliofuata (Octoba) Taifa Stars ikapanda kutoka nafasi hiyo ya 164 hadi kufikia nafasi ya 120 ambapo ilikaa kwa miezi miwili yaani mwezi wa kumi na wa kumi na moja. Mwezi wa Disemba, Taifa stars imepanda tena kutoka nafasi hiyo ya 120 kati ya timu 198 hadi kufikia nafasi ya 110. Kulingana na taarifa ambayo inaweza kupatikana katika tovuti yao [http://www.fifa.com]

Kama tulivyosema hapo awali, ingawa nafasi hiyo bado hairidhishi lakini ni maendeleo mazuri ya kutia moyo. Toka nafasi ya 164 kufikia nafasi ya 110 ina maana kwa miezi hii mitatu Taifa Stars imefanya vizuri zaidi ya timu za mataifa 54 duniani na hilo si jambo dogo. Na kwasababu hiyo basi, tulipongeza shirikisho la mpira wa miguu nchini (TFF), wizara na waziri wa michezo na pia mheshimiwa Rais kwasababu ni dhahiri kuwa kwa kasi hii huenda njozi zake za kuiona Taifa Stars ikipeperusha bendera ya Tanzania huko Ghana na Afrika Kusini zitatimia. Lakini zaidi sana, pongezi za dhati kwa kikosi kizima kinachounda Taifa Stars.

Ingawa inaonekana kama ndoto za alinacha kuwaona watanzania wakiwa wamevalia mavazi ya rangi ya njano, nyeusi, kijani na blue wakiishangilia Taifa Stars kwenye mashindano ya kombe la dunia mwaka 2010 huko Afrika ya Kusini, kwa miezi hii michache timu yetu imeonyesha kwamba ikiwa na maandalizi mazuri inaweza kufanya vizuri. Kwani kama kwa miezi mitatu/minne Stars imeweza kupiga hatua na kuzidi mataifa 54 katika rank ya Fifa, kuna miaka zaidi ya miwili kujiandaa kwa kombe la dunia, na kwa sababu timu zinazoenda kombe la dunia ni 32, kwa nafasi iliyopo sasa ya 110, inahitaji kuzidi timu angalau 78 kujihakikishia nafasi ya kwenda Afrika ya kusini. Na ikiendelea kwa kasi hii ya kuwa bora zaidi ya timu 54 kwa kila miezi minne, ni imani yetu kuwa kufikia katikati ya mwaka ujao, Stars itakuwa katika nafasi nzuri ya kujihakikishia nafasi ya kombe la dunia mwaka 2010.

Basi tuendelee kuishangilia na kuiombea timu yetu ya taifa, Taifa Stars maana kama ikifanya vizuri inaweza ikawa moja ya vitu ambavyo vitaitangaza nchi yetu vyema kimataifa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

NB: Ingawa kwenye orodha ya FIFA timu zinazoonekana kwenye rank ziko 198; jumla ya timu ziko 206. Timu 8 za mwisho hazina pointi yoyote kwa hiyo zote zinakuwa ranked namba 198.

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.