MWAKA UMEISHA, SERIKALI IMEFANYA NINI?

Na,G

Ikiwa ndiyo tu mheshimiwa rais na serikali yake ya awamu ya nne wamemaliza mwaka mmoja madarakani, si jambo baya tukichukua muda kufanya tathmini kuhusu walichofanya kwa mwaka wao wa kwanza. Ni kawaida kwa viongozi hasa wa serikali kujiwekea malengo ya muda na mara vipindi vya malengo hayo waliyojiwekea vinapopita, wanachukua muda kutazama nyuma na kutathmini kwamba wamefanikiwa (Au wameshindwa kufanikiwa) kwa kiasi gani.Tumeona marais na viongozi wengine mbali mbali wakijiwekea malengo ya masaa 100 ya kwanza, siku 100 za kwanza, ila sisi tumeona tuanze na mwaka wa kwanza.

Ingawa baadhi ya watu wanadhani kwamba mwaka mmoja hautoshi kufanya mabadiliko yanayoonekana, wakitilia maanani msemo usemao "mwanzo mgumu," lakini ni wahenga hao hao waliotuambia kuwa siku njema huonekana asubuhi na pia dalili ya mvua ni mawingu. Swali linalobaki wazi ni je, watanzania tushayaona mawingu? Hata kama hatuioni mvua, lakini je, si vyema kuangalia katika mwaka huu kama kuna hata mwelekeo wa kuwa na maendeleo? Na wengine wanadhani kwamba labda ili kuwa na maendeleo ya kweli na ya kudumu, labda ni vyema kuchukua muda kujenga msingi imara ambao ukishatokeza juu ndipo unaweza kuonekana hadharani. Lakini hata kama hilo ni sahihi, basi ni vyema hata kujiuliza maswali kadhaa ya kimsingi kuona kama msingi huo kweli upo.

Kwa kweli kuchaguliwa kwa Rais Kikwete kulitupatia watanzania matumaini mapya. matumaini ambayo labda tulikuwa tumeshayapoteza muda mrefu au hatukuwahi kuwa nayo hapo awali.  Lakini yeye, serikali yake na chama chake hasa ilani yao ya uchaguzi, ilitoa ahadi nyingi ambazo kama zikitekelezwa zitafanya taifa lipige hatua kubwa. Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 iliahidi kuboresha maisha ya watanzania na kuwaletea maendeleo katika kila nyanja ya maisha yaani kiuchumi, kijamii na kisiasa. Rais na chama chake waliahidi kuboresha huduma za jamii kama shule, hospitali, barabara, huduma za maji n.k. Lakini kwa walala hoi wengi, labda ahadi kubwa tunayoikumbuka ambayo mheshimiwa Rais aliitoa wakati wa kampeni na katika hotuba yake wakati wa kuapishwa ni ile ya kuleta nafasi mpya za kazi zipatazo milioni moja katika awamu yake ya kwanza ya uongozi. Lakini zimo nyingine nyingi alizotoa wakati wa kampeni na katika siku za kwanza za uongozi wake likiwemo tatizo kubwa la umeme na pia kero za Muungano. Kuna swala la mikataba isiyonufaisha nchi na wananchi ambayo pia aliahidi itapitiwa na kubadilishwa kama ikibidi.

Tutakubaliana kwamba kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja ndani ya ikulu ya magogoni, mheshimiwa Rais amesifiwa sana na watu wengi wa kila namna na nadhani imezidi kiwango hadi kufikia yeye mwenyewe kuanza kuwambia watu waache kumsifia. Akihutubia watendaji wake wa chama aliwapa mfano wa mwananchi wa jimbo lake la uchaguzi aliyempa lifti alipokuwa mbunge na mwananchi huyo akamwambia kuwa anapendwa sana jimboni hapo. Mheshimiwa Kikwete akamuuliza "Je wananipenda ingawa wana tatizo la maji?" Na mwananchi akamuuliza, "Kumbe unajua tuna tatizo la maji!" Mheshimiwa Rais alitumia mfano huo kuwaelekeza wana-CCM wenzake waache kumsifia kwa sababu bado matatizo ni mengi.

Swali la kujiuliza ni kwamba, inawezekana ameshaona kazi imemzidi uwezo na sasa ameamua kuanza juhudi nyingine ya kushusha mategemeo ya wananchi, au amekuwa tu mstaarabu na mnyenyekevu kutokutaka tu kusifiwa ila kazi bado ataifanya? Lolote lililo jibu ni ukweli usiopingika kwamba Rais kikwete amepata sifa kemkem na si nchini tu, bali hata nchi za nje. Tunakumbuka hata Rais wa Marekani, George Bush alimwagia sifa kibao hata kufikia kujadili naye matatizo ya kisiasa nchini Kenya, kitu ambacho wakenya hawakufurahishwa nacho. lakini jambo la msingi ni kwamba hata viongozi hao wa magharibi wanamuona kama kiongozi wa sifa kubwa kuweza hata kushauri kama si kuelekeza viongozi wenzake wa eneo la maziwa makuu na bara zima kwa ujumla. Lakini pamoja na sifa hizo kubwa, bado kuna wengine kama alivyosema Dr. Slaa, wanadhani kwamba matumaini aliyoleta Rais Kikwete ni matumaini ya kinadharia tu na hivyo hayawezi kuleta mabadiliko yoyote halisi kwa maisha ya watanzania. na kwa upande mwingine unaweza kusema  ni kweli maana ukiangalia matatizo ya nchi yanazidi kuongezeka. Umeme hakuna, bei ya mafuta inaongezeka, fedha yetu inashuka thamani, deni linaongezeka, rushwa ndiyo inazidi, Akiba iliyoachwa na awamu ya tatu nayo imekuwa ikiisha kwa kasi, maisha ya watanzania wa kawaida hayajaboreka, mikataba mibovu bado ipo na kuna mashaka mingine bado inaandikwa. Kero za Muungano bado zipo hasa sasa wanaposema kuna mpasuko wa kisiasa huko zanzibar,n.k.

Kwakweli kwa ujumla ingawa kumetokea mabadiliko katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Rais Kikwete, lakini si mabadiliko mema  kwa watanzania. Sasa tunakaa masaa mengi zaidi gizani hata zile kazi milioni moja zilizoahidiwa, kinachoonekana baada ya kubomolewa vibanda vingi vya wamachinga ni kupotea kwa ajira zao siyo kuongezeka kwa ajira. Na watanzania wengi pia tunasikitishwa kuona ari mpya na kasi mpya ya kuendeleza utamaduni wa kulea viongozi wabovu hasa pale alipofanya mabadiliko ya baraza la mawaziri ambalo ilionekana dhahiri kulikuwa na upungufu wa utendaji lakini mheshimiwa Rais akachagua kuweka viraka badala ya kutatua tatizo na kuleta watu wapya ambao wangeleta hiyo nguvu mpya.

Ila haitakuwa haki kuzingatia tu madhaifu hayo maana tunajua dhahiri kwamba kwa mipango ya muda mrefu inahitaji muda zaidi. Tunajua pia kwamba Mheshimiwa Rais na viongozi wenzake nao ni binadamu wana madhaifu yao. Na tunajua pia kwamba kama alivyoeleza vizuri katika hotuba yake ya siku ya uhuru, kumekuwa na mafanikio ambayo wameyafikia ndani ya mwaka huu mmoja. kwanza ni lile tulilosema la kurejesha imani ya watanzania kwa viongozi na uongozi. Hili linahusu pia imani ya wafadhili ambapo serikali ya awamu ya nne imeshasaini mikataba kadhaa ya misaada ya kigeni kama ule wa dola za kimarekani milioni 700 kutoka Marekani. Awamu ya nne pia imejitahidi sana kuhimiza ushirikishwaji wa wanawake jambo ambalo linaakisiwa katika idadi na nafasi za mawaziri wanawake katika serikali hii. Na kama mheshimiwa rais alivyosema, kuna mategemeo hata ya kuwa na rubani mwanaanga wa kwanza wa kike jeshini. Ujambazi umedhibitiwa kwa kiwango fulani na wananchi wananaanza kurudisha imani na jeshi la polisi. Kama alivyosema kumekuwa na ongezeko la shule na vituo vya afya n.k. Hata kwa upande wa michezo tumeona maendeleo madogo ambayo timu yetu ya taifa ya kabumbu imeyafikia.

Sasa tathmini hii, inakuwa kama kioo tu cha kujiangalia na kuona tumefika wapi. lakini kwa mheshimiwa rais, kwasasa juhudi za kwanza weka kwenye swala la umeme, maana maendeleo mengine yote hayatafikiwa kama hatuna nishati ya kuyaendeleza. Na sasa tunapofikiria kujiunga na nchi zingine za mashariki mwa Afrika kiuchumi tutakuwa dampo kama hatuna hata umeme na tunaingia kwenye soko huria na majirani zetu. Ili kukupa picha mheshimiwa rais, katika tetesi kwamba katika mazungumzo yako na rais Bush, aliahidi kuja kuitembelea nchi yetu, mwandishi mmoja wa Kenya aliandika barua ya wazi kwa Rais Bush akimwambia kwamba alifanya kosa kukuamini wewe kujadili mambo yao na wakampa ushauri wa bure kwamba kama akitekeleza ahadi yake ya kuja kututembelea, akumbuke kubeba jenereta yake mwenyewe. Na si swala la umeme tu, bali huduma zote za jamii ikiwemo maji safi, barabara, na huduma za afya. Na kubwa kwa ukubwa wa tatizo la umeme ni tatizo la rushwa ambalo tunaona kama umekata tamaa kulitekeleza. Kama waingereza wasemavyo kwamba Rumi haikujengwa siku moja, tunaamini kwamba huu ni mwaka wa kwanza ambapo labda umekuwa ukipata uzoefu wa ofisi. Kwa hiyo tutategemea mambo makubwa zaidi, tena sana tarehe kama hizi mwaka ujao na ujao hadi utakapomaliza muhula wako wa kwanza.

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.