KWANINI TUNAWAHESHIMU NA KUWAENZI WANASIASA PEKE YAO?

Antar Sangali, Bagamoyo

Wanamichezo pia ni Mashujaa tusiwafagilie Wanasiasa peke yao katika jamii. Inashangaza sana kwa jinsi ambavyo utamaduni wa ki-tanzania unavyoweka mbele wanasiasa na kuwakumbutia wao peke yao na kuwaheshimu kuliko makundi mengine ya kijamii kama vile wanamichezo, wanamuziki kadhalika wasanii wetu wa nyanja mbalimbali nchini.

Ukitazama kwa haraka haraka utaona kana kwamba Wanasiasa ni watu wenye mchango mkubwa kutokana na hoja kwamba: uwanja wao wa kisiasa ndio uliozaa uhuru wa Taifa letu na hatimaye kuwapita wananchi fursa ya kuwa huru na kujitawala.

Lakini kwa upande wa pili wa sarafu wanasiasa aghala huwa hawafikii malengo na dhamira za uenezi wa siasa zao ndani ya umma bila wasanii, wanamichezo, pamoja na wanamuziki kushirikishwa.

Katika kueneza siasa zao, wanasiasa wanategemea sana ushawishi wa wanamuziki, utunzi na uimbaji wao, wanamichezo kupenyeza siasa katika vilabu vyao vya michezo na wasanii kuigiza tamthilia zilizobeba ujumbe wa sera na itikadi zao.

Tanzania tuna mifano hai ya kusifika kwa Taifa letu nje ya mipaka yetu kwa sababu tu za kimichezo katika uwanja wa utamaduni na sanaa kwa ujumla wake.

Mathalan Filbert Bayi, Suleiman Nyambui na Mwinga Mwanjala ni baadhi tu ya wanariadha waliolitangaza Taifa letu katika medani za ridha kimataifa.

Marehemu Mbaraka Mwinshehe Mwaruka wa Morogoro Jazz , Ahmed Kipande wa Kilwa , Marijani Rajab wa Dar International, Ahmed Maneti wa Vijana Jazz, Salum Abdallah Yazid (SAY) na Juma Kilaza wa Cuba Marimba Morogoro, Sitti binti Saad -, Sami Haji Dau,Mwapombe Khiyari -Unguja, Shakila Said, Sharmila, Mohamed Mrisho -Tanga, Bakari Abeid -Unguja, Abas Mzee -Dar es Salaam ni mutrib wa taarab waliotamba na kuheshimika katika jamii.

Wanasoka kama vile Yungi Mwanansali, Abdulrahman Lukongo,Kepten Abdallah Aziz,Hija Saleh, Saleh Zimbwe na Abdalah Luo walitamba katika michuano ya Gossage. Wengine akina Mustafa Choteka, Mbwana Abushiri, Miraji (Kipa),Sharif, Ather Mambeta,Yusuf Mwamba, na Khamis Kilomoni Gibson Sembuli, Sunday Manara. Omar Dilunga (Black Pancer)(Computer) , Abdallah Kibaden (King), Willy Mwaijibe, Mohamed Kajole (Machela), Hussein Ngulungu, Kassim Manga, Suleiman Jongo, Abdallah Mwinyimkuu (Pele), Omar Kapela (Mwamba Kifua). Wengine wengi mathalan Hassan Gobos, Patick Nyaga, Athuman Mambosasa, Shaaban Baraza, Hassan Mlapakolo, Abuu Ali, Mohamed Salim, Salim Omar, Mohamed Tall , Mohamed Chuma, Hamis Gaga, Hussein Tindwa, Omar Chogo (Mluya) na Leopard Tasso.

Lakini katika Taifa letu hawa wanaonekana kama si mali kitu mbele ya jamii na kwasababu walitoa mchango wao viwanjani na kwenye majukwaa ya muziki sasa si lolote na si chochote na walichokipata ndo' hicho hicho na kama hawana kitu ndo' hivyo hivyo.

Tazama mitaa yote ya Mwanza, Dar, Mbeya, Morogoro na Zanzibar imepewa majina aidha ya mikoa, wanyama, nchi au majina yake ni ya wanasiasa wa ndani au wa nje na si wanamichezo na wasanii wetu. Kwanini lakini?

Hulka hii na utamaduni huu nadiriki kuuita kinagaubaga ni ukiritimba mkongwe na haufai kuendelezwa katika jamii yetu kwani ni mfumo unaokandamiza wengine ambao si wanasiasa wasiheshimike zaidi na kuenziwa katika jamii.

Wanasiasa wanapodhamiria kutimiza na kueneza sera za vyama vyao aidha katika nyakati za kudai uhuru na baada ya uhuru ili kufikisha ujumbe kwa mwendo wa haraka wenye usahihi huwatumia wanamichezo na wasanii. Hebu tujiulize akina Moses Nnuaye, Mwinamila, Hukwe Zawose, Mayagila Joseph Che-Mundugwao, Ibrahim Raha (Jongo) hawakutoa mchango wao mbele ya jamii? Na kama jibu ni "ndiyo," kwanini leo hakuna hata mitaa yenye majina yao, ama kumbi za mikutano na kujengewa sanamu kama ambavyo wanasiasa wanavyofanyiwa na kuenziwa?

Tuyatazame mataifa ya wenzetu jinsi wanavyothamanini wasanii na wanamichezo wao kwa kuwafanyia matamasha makubwa ya kutangaza kazi zao na tazama hata hivi karibuni jinsi marehemu George Best aliyeichezea Manchester United alivyozikwa kwa heshima.

Lakini wanamichezo wa Tanzania wanatumika kama mihuri ya kuhalalishia utashi wa wanasiasa na pale wanasiasa wapofikia malengo yao, kwa haraka huwasahau na kuwatia kapuni. Huu si uungwana na ni kwenda kinyume na utu.

Wanamuziki waliimba na kutunga nyimbo za kuhamasisha ujenzi wa umoja wa kitaifa, siasa ya ujama na kujitegemea, umoja, na hata kuharakisha ukombozi kusini mwa Afrika na kupinga ubaguzi wa rangi popote duniani.

Sifa ilizojipatia serikali ya Tanzania katika mataifa mengine hazikuletwa na wanasiasa peke yao pia umo mchango mkubwa wa wanamichezo, wasanii na wanamuziki katika jamii ndani na nje ya mipaka ya Taifa hili.

Mitaa yote inaitwa Kawawa, Nyerere, Karume, Kandoro, Nkuruma, Lumumba, Seke Toure , Kenytatta, Idd Tulio, Mwinjuma Mwinyikambi, Dosa Aziz , Grey Mataka na kadhalika. Lakini huikuti ikiitwa Mohamed Tall, Yanga Fadhil Bwanga, Sam Kampambe, DaudI Salum, wala Mosaes Mkandawile kwa nini?

Ni vema tubadilike upesi tuamke katika usingize mzito ,tutanabahi na kuanza kuwajali na kuwathamini wanamichezo wetu, wanamuziki na wasanii wet-- kwani nao pia ni sehemu nyeti katika jamii.

Katika awamu nyingine ijayo ya utawala wa nchi itapendeza sana iwapo kutaonekana tunafungua ukurasa mpya wa kuwajali na kuwathamini.

Mungu ibariki Tanzania !

Tuma maoni yako [hapa]

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.