LOWASSA NDIYE WAZIRI MKUU: JE, ATACHUKUA MKONDO GANI?

Edward Ngoyayi Lowassa mbuge wa Mondoli ndiye waziri mkuu wa tisa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uteuzi wa Lowassa kushika wadhifa huo ulifanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, na kuthibitishwa na Bunge jana mjini Dodoma.
Bunge lilimthibitisha Waziri Mkuu mpya kwa kupiga kura za siri, ambapo kura 312 zilimkubali ashike wadhifa huo. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Waziri Mkuu akishateuliwa na Rais, ni lazima athibitishwe na Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Matokeo ya kura ya kumthibitisha, yalitangazwa na Naibu Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambaye naye alichaguliwa bila kupingwa jana, muda mfupi kabla ya kura za kumthibitisha Waziri Mkuu mpya kutangazwa.

Lowassa anakuwa Waziri Mkuu wa tisa tangu uhuru, Waziri Mkuu wa kwanza akikuwa Hayati Baba wa Taifa, Julius Nyerere. Baadaye walifuata Rashid Kawawa, Cleopa Msuya, Edward Sokoine, Dk. Salim Ahmed Salim, Jaji Joseph Warioba, John Malecela na Frederick Sumaye.

Uteuzi wa jina la Lowassa ulifanywa na Rais Kikwete kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufuata vigezo ambavyo miongoni mwake ni kuwa mbunge wa kuchaguliwa kutoka chama chenye wabunge wengi ambacho ni CCM, awe mchapakazi, anayejituma, mkali na madhubuti kutekeleza majukumu yake.

Lowassa alizaliwa Agosti 26, 1953 na alisoma Chuo Kikuu cha Bath cha Uingereza na ana Shahada ya Uzamili.

Mwaka 1989 hadi 1990 alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Arusha (AICC), mwaka 1990 hadi mwaka 1993 aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, mwaka 1993 hadi 1995 aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, na hadi anateuliwa kuwa Waziri Mkuu jana, alikuwa Waziri wa Maji na Maendeleo ya Mifugo katika serikali ya awamu ya tatu ya Rais Benjamin Mkapa.

Lakini kando na sifa zote hizo, swali ni kwamba: Je, Mh. Lowassa atachukua mkondo gani katika dhana zima ya uchapakazi? Je, atakuwa mtu hodari na mchapa kazi kama alivyokuwa Sokoine, ama atakuwa "...ndio mzee," kama alivyokuwa waziri mkuu wa serikali iliyopita?

Tukumbuke kuwa : nchini Tanzania bado kuna tatizo kubwa la rushwa. Swali linalobaki wazi ni kwamba je, Mh. Lowassa anaweza kweli kuwatizama watanzania usoni na kuwahakikishia kuwa ana uwezo wa kupambana na rushwa kwa nguvu zake zote? Na sio kupambana na rushwa tu; je, anakerwa kweli na tatizo hilo moyoni mwake au ndio yaleyale ya akina Sumaye...?

Kama Mwl Nyerere alivyowahi kunukuliwa wakati wa uhai wake akisema: " Watanzania wanataka mabadiliko ya kweli ya uongozi na utendaji wake, wasipoyaona CCM (chini ya Kikwete na Lowassa) watayatafuta nje ya chama hicho."

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.