UHUSIANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBARI ULIANZA KWA NDOA AU TALAKA ?

Na, Magabe Kibiti

Kwa miaka zaidi ya kumi sasa nimekuwa natatizwa na jambo hili kubwa na lenye uzito wa maana sana katika maisha ya kila siku ya Mtanzania. Mara nyingi hujikuta nikicheka nisikiapo wanasiasa na wasomi wakijaribu kulielezea.

Sio swali rahisi kujibu kwa sababu watu wengi waliojaribu kulijibu, wamefuata hisia zao tu na kuacha ukweli wa jambo lenyewe.

Naomba wasomi, wanasiasa, wana-dini na wanahistoria mjibu swali hili kwa ukweli na acheni ubabaishaji wenu usio na msingi: Uhusiano wa Tanganyika na Zanzibari ulianza kwa talaka ? au ndoa ?

Kurahisisha swali hili kwa mtakaojaribu kujibu, nimeamua kuweka wazi baadhi ya majibu niliyopata mpaka sasa.

Kuna watu wanasema kuwa Uhusiano huu ulianza kwa ndoa iliyofanyika mwaka 1964. Kwamba, jamhuri mbili zisizohusiana kabisa ziliamua kuungana na kuwa jamhuri moja inayoitwa Tanzania.

Wengine wanadai kuwa Uhusiano wa jamhuri mbili za Tanganyika na Zanzibari ulianza kwa talaka. Kwamba, kabla ya ukoloni, hakukuwa na jamhuri ya Tanganyika wala Zanzibari, pande zote mbili zilikuwa kitu kimoja. Wanadamu wa pande zote mbili za bara na visiwani walikuwa ndugu na wamoja. Wakoloni kwa masilahi yao walizigawa hizi pande mbili ili kuwa rahisi kuzitawala.Yaani kwamba, Uhusiano wa Tanganyika na Zanzibari ulianza kwa talaka iliyoshinikizwa na dola za kikoloni.

Ukisikia majibu haya mawili yenye mwelekeo unaopingana utashangaa.

Ukweli ni kwamba, wengi wa waliosema kuwa Uhusiano huu ulianza kwa ndoa ya mwaka 1964 ni wale ambao wanapinga kuwepo kwa huo Muungano. Na wale waliosema kuwa ulianza kwa talaka ni wale wanaopenda Muungano huu uendelee.

Zaidi ya hapo kuna kundi la tatu linalodai kuwa Tanganyika na Zanzibari hazijawahi kuwa na Uhusiano wowote wa kweli, hakuna ndoa wala talaka ila matumaini matupu ya kuunganisha nchi mbili zisizohusiana kabisa kwa manufaa ya kisiasa. Hili kundi la tatu halina watu wengi sana.

Vitabu vingi vya historia nilivyosoma vinasema kuwa, mwishoni mwa karne ya kumi na tisa, wazungu wa ulaya walikutana nchini Ujerumani na kuligawa bara la afrika ili kulitawala. Huu ndio wakati ambao wamasai, wakurya, wanyakyusa na makabila mengi ya mipakani walijikuta wakiwa katika nchi mbili zilizotengwa. Wasomi wengi wameliita tukio hili `talaka ya karne`.

Ninajaribu kuwaamini wale wanaosema kuwa Uhusiano wa Tanganyika na Zanzibari ulianza kwa talaka kwa sababu kuna uwezekano kuwa pande hizi mbili zilitengwa na hawa wazungu wa mwishoni mwa karne ya kumi na tisa. Ninachosema hasa ni kwamba, mimi na zaidi ya asilimia hamsini ya wanadamu waliozaliwa katika hii sehemu ndogo ya dunia iitwayo Tanzania tumezaliwa baada ya mwaka 1964. Hii ni kusema kwamba wengi tumezaliwa baada ya talaka ya karne ya kumi na tisa, na hasa, baada ya ndoa ya mwaka 1964.

Nchi tunayoijua ni Tanzania. Kama vile wanadamu wanaozaliwa leo nchini marekani wanajulikana kama wamarekani na wala sio wa-texas au wakalifonia, mimi na wenzangu hawa tunajulikana kama watanzania.

Nimeuliza hili swali makusudi kabisa ili kuwakumbusha wale wanaotaka kuuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibari kuwa watakuwa na kesi kubwa sana ya kujibu kama wakifanikiwa. Kwanza, ni nani hasa atafaidika kama Tanganyika na Zanzibari zikitengana? Ni wananchi? au viongozi wachache wanaotaka kuongoza?

Dunia nzima imeshuhudia jinsi nchi zilizojitenga kutoka Urusi zinavyosota na umasikini wa kutisha. Dunia pia imeshudia jinsi nchi tajiri zinavyoungana ili kuwa na nguvu kubwa Kiuchumi na kijamii, jifunze kutoka marekani inayoundwa na nchi hamsini, jifunze kutoka Ujerumani iliyoungana, China inaungana na Taiwani na imeshaungana na Hongkong na sasa ni miongoni mwa mataifa yenye nguvu.

Nchi za Ulaya zinataka kuungana. Fikiria kama nchi za Afrika pia zingekanusha ile talaka ya dola zilizoshinikizwa karne ya kumi na tisa na zikaungana leo. Kama Uhusiano wa Tanganyika na Zanzibari ulianza kwa talaka na ndoa, bado ni swali ambalo nalitafutia majibu. Jambo moja najua kwa hakika sasa ni kwamba, Nchi tajiri duniani leo zinaungana na sio kutengana. Pili, kuna Ushahidi kuwa nchi nyingi za Afrika zilitenganishwa ili zitawaliwe kirahisi na wazungu.

Wanaotaka hizi jamhuri mbili zilizoamua kuungana tena (kwa ndoa) mwaka 1964 baada ya talaka ya karne kumi na tisa zitengane wajue kuwa wanatimiza malengo ya wazungu wale waliozitenga.

Nina ndoto ya kuona nchi ya Tanzania ikiendelea kuungana na ikiwezekana nchi zote za Afrika ziungane tena na kuikanusha ile talaka ya karne ya kumi na tisa.

Ninasikitika kusikia wanaopinga kuungana wakidai kwamba "ohooo kwa nini tuungane na Afrika kusini wakati ni nchi tajiri na sisi ni masikini". Ninawaomba wajifunze kutoka kwa marekani. Jimbo la Texas lingekuwa nchi, ingekuwa ya nne kwa utajiri duniani, jimbo la kalifonia lingekuwa nchi ya tano kwa utajiri duniani. Haya majimbo mawili tajiri yameungana na majimbo masikini ya Dakota, Iowa, Mississippi, n.k na kuunda taifa kubwa duniani. Nchi ya Ujerumani na utajiri wake inataka kuungana na nchi ya Polandi. Mbona watanzania twafikiria kutengana? Cha muhimu sana, ninajiuliza kwa mara nyingine. Ni tukio gani huambatana na furaha duniani. Ndoa ? Au talaka ? !!!!!!!!!!!!!!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.