SERIKALI YA AWAMU YA NNE NA UWIANO WA KIJAMII

Na, G

Kama yalivyo maneno ya Remmy Ongala katika wimbo wake maarufu wa siku ya kufa, ndivyo lilivyo na baraza jipya la mawaziri la serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania. Katika wimbo huo Remmy anasema: ~~barabara murefu hakosi kona,~~ na ~~mwanamuke muzuri hakosi kasoro~~. Kwa hiyo kitu cha kwanza ni kumpongeza Mheshimiwa sana Rais Kikwete kwa sababu baraza lake kama lingekuwa barabara, ingekuwa ndefu na kama lingekuwa mwanamke angekuwa mzuri. Ingawa Remmy anasisitiza kuwa hata kama ikiwa ndefu haitakosa kona na mwanamke mzuri hakosi kasoro, lakini kwa upande mwingine anatuambia kwamba mwanamke huyo kwanza anakuwa mzuri ndiyo watu wamtafute kasoro maana labda asingekuwa mzuri watu wasingehangaika kumtoa kasoro.

Kwa hiyo hata katika baraza la mawaziri la Rais Kikwete labda ingekuwa vyema kuangalia uzuri wake kwanza kabla hatujaanza kulitoa kasoro maana hizo zitakuwepo kwani naamini baraza lake ni zuri.

Rais Kikwete ametangaza baraza lenye mawaziri 29. Hii ni waziri mmoja zaidi ya baraza lililopita lililokuwa na mawaziri 28. lakini tofauti na baraza lililopita lililokuwa na mawaziri wanawake wane, baraza hili lina mawaziri wanawake sita. Hii ni asilimia 20.69 ya mawaziri wote. Na hawa si mawaziri tu, bali mawaziri wa wizara kubwa na muhimu. Inaaminiwa kwamba tangu kupata uhuru Tanzania haijawahi kuwa na waziri mwanamke kuongoza wizara ya fedha wala ile ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa. Ila sasa tumepata si wizara hizo tu bali ile ya sheria na katiba, elimu na mafunzo ya ufundi pamoja na ile ya maendeleo jinsia na watoto ambayo ndiyo ilizoea kupewa wanawake ingawa katika jina tofauti kidogo. Ukichanganya na manaibu waziri, kati ya mawaziri na manaibu mawaziri 60, kuna wanawake 13 na hii ni asilimia 21.67 ya mawaziri wote na manaibu wao.

Kwa hiyo hii ni sura nzuri saaaaaaaana ya uwiano wa kijinsia hasa ukizingatia mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imesaini inayohimiza usawa huu wa kijinsia. Kwa mfano SADC inataka wanachama wake wote wawe na angalau asilimia 30 ya wabunge kuwa wanawake. Takwimu za Bunge zinaonyesha kati ya wabunge 319 wa bunge hili, 97 ni wanawake. Hii ni asilimia 30.4, zaidi kidogo ya kiwango cha SADC. Lakini Raisi bado anazo nafasi 4 zaidi za kuteua wabunge ili kufikisha idadi kamili ya jumla ya wabunge 323. Hata kama raisi hatateua mwanamke katika nafasi hizo tano, Ingawa tunaamini atateua, bado Tanzania itakuwa imefikisha lengo hili la SADC kwa kuwa na wabunge asilimia 30.03. Ila hata akiteua nafasi zote wanawake, hilo halitatusaidia kufikia lengo la Umoja wa Afrika unaohitaji wanachama wake wawe na idadi sawa ya wabunge wa kike na kiume.

Ukija kwa upande wa elimu, baraza hili la mawaziri limepiga hatua kubwa sana maana kuna asilimia kubwa zaidi ya wasomi. Kati ya mawaziri 29, 11 kati yao ni wasomi wanaostahili kuwa na herufi chache nyuma ya majina yao, yaani Dokta au Professa. Hii haina maana kuwa hao tu ndiyo wasomi maana tunaamini wako wengine wenye digrii moja au mbili ila kwa sababu hatuna hakika sana na hayo, tutaangalia tu wale ambao walifika kiwango cha juu kustahili kuwa na herufi hizo chache nyuma ya majina yao. Wasomi 11 kati ya mawaziri 29 ni asilimia 37.93, karibu asilimia 40 ya baraza letu la mawaziri tunawaita wasomi. Huu ni uwiano wa juu sana. Ukichanganya na manaibu wao, kati ya mawaziri na manaibu 60, kuna wasomi 21, hii ikiwa ni asilimia 35.

Miongoni mwa mawaziri hao 12 ni wazoefu waliokuwamo pia katika baraza lililopita. Hii ni asilimia 41.37 ya mawaziri wote. Hii inaonyesha umakini alioufanya Rais Kikwete kuweka uwiano mkubwa katika baraza lake. Uiwano wa wanawake na wanaume kama tulivyoona awali. Uwiano wa mawaziri wazee na vijana. Uwiano wa mawaziri wapya na wale wa zamani maana ukileta wapya wote, wanakuwa hawana ujuzi, hivyo wale 12 wa zamani wanaleta ujuzi na uzoefu wao wa kazi katika baraza la mawaziri na kusaidia hawa wapya ambao ni wengi zaidi kuelewa na kufanya kazi zao na maamuzi kwa busara zaidi. Katika uwiano huo pia tumeona ongezeko la mawaziri wenye elimu ya juu.

Najua kuwa makala hii haitakamilika kama tukiangalia tu urefu wa hii barabara na uzuri wa huyu mwanamke bila kuangalia kona zake na kasoro zake.

Watu wengi saaaaaana wameonyesha kutokuridhishwa kwao na uteuzi wa Profesa Juma Athumani Kapuya (mb) kushikilia wizara ya ulinzi. Ingawa waziri huyu ni mkongwe ila inasemekana hakuwahi kufanya vizuri katika wizara yeyote ile aliyowahi kuiongoza hapo awali. Kwa hiyo wengi tunadhani kuendelea kumpa nafasi ni kuwanyima askari wetu uongozi bora maana alishapewa nafasi ya pili na zaidi kuona kama angeweza kurekebisha ila hilo halikutokea.

Katika ukurasa huo huo yupo pia Mheshimiwa Joseph James Mungai (mb) ambaye inasemekana katika awamu iliyopita hakufanya vyema kwani alikuwa akifanya maamuzi binafsi bila kushirikisha wataalamu, wahusika na watu ambao wataathiriwa na maamuzi aliyokuwa anafanya. Waziri huyu inasemekana kwa kipindi kilichopita hakuchukua muda kupata mashauri au kusikiliza hoja za wale anaowaongoza hivyo kupelekea kufanya maamuzi ambayo yalikuwa yakiharibu, kuathiri au kuumiza wale yaliowahusu.

Ingawa tunataja wachache tu, ila hatuwezi kumaliza wachache bila kuangalia pia uteuzi wa mheshimiwa Kingunge Ngombale Mwiru (mb) kuongoza Wizara ya nchi-siasa na uhusiano wa jamii. Ingawa wengine hawakufurahishwa na uteuzi huu kwa sababu zozote zile, lakini nadhani kama Rais alitaka wizara hii ifanye kazi, hakuwa na jinsi ila kumteua tena mheshimiwa Kingunge kuiongoza. Inasemekana kwamba katika propaganda ya kuhimiza na kukuza siasa ya chama ni mtu mmoja tu anayeweza kuwa sawa au kumzidi mheshimiwa Kingunge, naye ni Paul Sozigwa. Wanaowakaribia hao ni kama katibu wa chama bwana Phillip Mangula. Kwa hiyo ukiacha mzee Sozigwa na kwa sababu Bwana Mangula tayari ana kazi muhimu ya chama, kama Rais alitaka uenezi katika itikadi ya chama, hakuwa na ujanja ila kutumia jeuri ya chama na kumpa mkongwe huyo wizara hiyo muhimu kwa maendeleo ya chama.

Kuhitimisha, pamoja na kona na kasoro za baraza hili la mawaziri, lakini kwa sehemu kubwa ni baraza zuri sana lenye uwiano mkubwa kuliko mabaraza yote tuliyowahi kuwa nayo hapo awali. Kwa hiyo tukiwapa nafasi na ushirikiano wa kutosha, wanayo nafasi ya kufanya vizuri kuliko tulivyotazamia na kufanya nchi iendelee zaidi ya nafasi ya 5 kutoka mwisho kwa umaskini duniani.

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.