ISIWE KAULI MBIU TU, TUNATAKA VITENDO PIA...

By , G

Baada ya siku chache za makabidhiano na kuonyeshwa ofisi na pengine orientation ndogo, wakati umefika sasa wa mawaziri na manaibu wao katika baraza hili jipya la mawaziri kuanza kazi. Ingawa wajibu wa wengine uko wazi na hakuna tofauti kubwa sana wanayoweza kufanya isipokuwa kuendeleza na kuboresha huduma za wizara zao, ni wakati sasa kwa wizara zingine kuanza kufikiria nje ya kawaida ili kufanya mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika wizara hizo.

Katika siku hizi chache tumeshaona wizara na waziri mpya wa usalama wa raia wakipatiwa changamoto kubwa kwa kutokea matukio makubwa kadhaa ya ujambazi jijini Dar Es Salaam yanayohusisha mauaji na uporaji. Hivyo labda waziri Mwapachu angefikiri kuacha kuzungumza sana kwenye vyombo vya habari na kuanza kuonyesha utendaji. Na kama hana mawazo mapya, tungemshauri angalau kuanza na mawazo yaliyomsaidia saana waziri wa zamani wa mambo ya ndani Bwana Augustine Lyatonga Mrema maana kwa kweli kwa upande wa usalama wa raia--Tanzania hasa miji mikubwa haikuwahi kuwa na amani na usalama kama ilivyokuwa chini ya uongozi wa bwana Mrema. Lakini kwa hivi sasa jeshi la polisi chini ya IGP Mahita linaonekana kuzidiwa mbinu na majambazi na mbinu mpya zinahitajika.

Kenya bado inaongoza kwa utalii na juma lililopita tu imechaguliwa kuwa miongoni mwa sehemu bora kumi duniani iliyopendekezwa kwa utalii kwa mwaka huu wa 2006. Ingawa tunafurahia mafanikio yao, ila inasikitisha kwamba bado wanatumia malisili za Tanzania kutangazia biashara yao ya utalii. Bado inasikitisha unapofika kwenye viwanja vya ndege vya ulaya na nchi zingine za magharibi na kukuta matangazo ya biashara ya utalii ya Kenya yakitumia mfano mlima Kilimanjaro. Mheshimiwa Diallo, kazi kwako na tunaamini kama mfanyabiashara unaelewa jinsi isivyo vyema kibiashara kama mtu akitumia jina lako au bidhaa zako. Hivyo katika orodha yako ya majukumu, tafadhali weka katika kipaumbele cha juu suala la kuboresha mazingira ya utalii Tanzania, suala la kutangaza maeneo yetu ya utalii huko nje, na kuwachukulia hatua wale wote wanaotumia maliasili zetu kwa manufaa yao ya kiuchumi. Tunataka fedha yote ya utalii ije hapa kwa maendeleo ya wananchi wetu.

Kwa wale ambao mmeshughulika na kubadilisha hati za kusafiria hasa pale Dar Es Salaam, mtakubaliana nami kwamba ingawa juhudi nyingi za raisi mstaafu Bwana Mkapa za kukomesha rushwa zimefanya maendeleo, lakini bado tuna safari ndefu saaaaana ya kusafiri. Na si katika uhamiaji tu, bali katika kila nyanja ya maisha. Rafiki mmoja akielekea Tanzania alipewa ushauri wa kufanikiwa shughuli zake Tanzania akaambiwa kwa Tanzania "It's not Know How, it's know Who". Na ili kujua the whos, lazima wallet ijeruhiwe. Kwa hiyo Mheshimiwa Marmo, utawala bora ni msingi mkubwa sana wa maendeleo na katika majukumu yako, rushwa ukiikomesha, kazi yako itakuwa rahisi zaidi.

Bibie meghji, kwanza tunakupongeza saaaaaaaana kwa nafasi hiyo kubwa na kukutakia heri na fanaka katika jukumu hilo zito. na unapoanza majukumu yako, katika kutekeleza malengo yako, tunajua kuwa baada ya Tanzania kusamehewa deni la nje, fedha zilizokuwa zinalipa hayo madeni kama ukizitumia vyema kwa maendeleo na ustawi wa jamii, nchi itapiga hatua.  Pia ukishirikiana na  Mheshimiwa Karamagi na mheshimiwa Maghembe, mnaweza kufikiria namna ya kupunguza kodi ya wawekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi, ambao watawekeza na kutengeneza nafasi za kazi na kusaidia kukua kwa uchumi wa nchi na ongezeko la ajira nchini Tanzania. Hili linakwenda sambamba na kuhimiza sekta isiyo rasmi na kuhimiza biashara ndogo ndogo na kuongeza utoaji wa mikopo kwa watanzania wengi wanaoanzisha biashara ndogo ndogo ili kujiajiri wenyewe na wachache wengine wanaoweza kuwaajiri hili pia litaongeza ajira nchini. Swala la muhimu ni kwamba kadri sera ya nchi inavyoongeza ajira ndivyo pato la nchi litakavyokuwa, uhalifu kupungua na adui umaskini kutokomezwa.

Waziri wa elimu naye tunamtakia kila la heri maana wananchi wana matumaini makubwa sana kwake. Najua kwamba anayo mipango mingi saaaaaaaana ya kuendeleza mfumo wa elimu rasmi lakini sambamba na hilo, ushauri wetu kwako Mama Sitta ni kufikiria namna ambayo unaweza pia kuendeleza elimu isiyo rasmi. Kwa wale ambao wameshindwa kwenda katika shule za msingi, sekondari na vyuo wanaweza pia kupatiwa elimu ya kujitegemea kwa njia ya masomo ya ufundi wa aina mbali mbali kama ujenzi, useremala, ushonaji n.k. Ingawa elimu hii hutolewa katika vyuo kadhaa vya ufundi, wizara ya elimu ineweza kufikiria namna ya kuunga mkono mafunzo ya kujitegemea ambayo vijana wanapata katika mfumo usio rasmi na labda kuona kama inaweza kuunga mkono kwa namna moja au nyingine karakana zinazojihusisha na utoaji wa elimu hiyo. Pia imefikia hatua sasa kwa Tanzania kubadili vigezo vinavyotumika kuwachagua wanafunzi kueledela na elimu ya juu. Kutegemea matokeo ya mwisho ya mtihani wa taifa sio kigezo madhubuti kabisa kwani wanfunzi wengi walio na akili na upeo mkubwa wa kuelewa mambo hujikuta wapoteza nafasi ya kuendeleaa kimasomo wanapotokea kufanya vibaya katika mtihani wa mwisho. Ni vema basi ukawepo utaratibu wa kuratibu maendeleo ya mwanafunzi darasani na kisha kujumulishwa na asilimia fulani (itakayoweka) ya mtihani wa mwisho ili kupata uwiano mzuri wa kufaulu.

Kwako Mama Sitta tena, kama hukuwahi kulifahamu hili basi sasa utafahamu kwamba watanzania kwa ujumla, hatuna utamaduni wa kujisomea. Nikisema kujisomea ninamaanisha kujisomea situ kwa kuongeza maarifa bali pia kwa burudani na taarifa. Hili ni swala zima la kusoma, vitabu, majarida, magazeti vijizuu na fasihi andishi nyinginezo. Hiki ni kigezo muhimu saaaaaana kwa raia yeyote yule kwa ajili ya kuongeza upeo wake wa mawazo na kufikiri na katika uzoefu huo anaongeza pia maarifa katika nyanja ambazo labda asingalifahamu mengi kulihusu isingekuwa kwa kujisomea. Kwa hiyo tunatoa wito kwa Wizara ya elimu kufundisha na kuhimiza na kuweka mipango ya kusaidia wananchi kujijengea utamaduni wa kujisomea maana wakati tunao mwingi. Jengeni Library nyingi za kisasa kufanikisha hilo

Ingawa hatutaweza kuangalia wizara zote, lakini hatuwezi kumaliza bila kuangalia waziri mwenye nafasi kubwa zaidi ya kuanza vizuri kimataifa. Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa Dkt Asha-Rose Mtengeti Migiro anaanza kazi rasmi huku Tanzania ikiwa zamu kuwa raisi wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa mwezi mzima huu wa Januari. Mpaka sasa Balozi Augustine Mhinga ambaye ndiye raisi wa baraza hilo kumuwakilisha waziri, ameshafanya kazi kubwa kutoa mwelekeo wa baraza hilo chini ya utawala wa Tanzania. Ajenda kubwa ya Tanzania kufuatana na balozi Mhinga ni kuelekeza umakini wa baraza hilo kuangalia Afrika hasa eneo la maziwa makuu. Amezungumzia mafanikio ya kisiasa huko Burundi na Rwanda na ameelekeza baraza kuangalia changamoto katika mgogoro wa Ethiopia na Eritrea, Swala la kusini mwa Sudan ambapo walipokea taarifa rasmi ya mwakilishi wa umoja wa mataifa huko Sudan. Kuna swala na Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Kongo na mambo mengine yanayohusu eneo hili la maziwa makuu.

Kwa maswala ya kimataifa balozi Mhinga ameliongoza baraza la usalama kuitaka rasmi Haiti kuharakisha uchaguzi wake ikiwezekana kabla ya februari saba. Pia balozi Mhinga anasaidia kampeni ya kutaka katibu mkuu anayefuata wa umoja wa mataifa atoke nchi za Asia, mara muda wa katibu wa sasa utakapoisha mwishoni mwa mwaka huu. Pia kuna mkutano wa dharura unaoitishwa nchini Uingereza kujadili suala la Iran.

Hayo yote ni utangulizi na msingi ambao Balozi anamuwekea waziri Migiro kwa ajili ya mkutano wa mawaziri wa nchi za nje walio wanachama wa baraza la usalama utakaofanyika tarehe 27 ambapo Waziri Migiro kama akiwepo, na tunaamini atakuwepo, atakuwa Raisi wa kikao hicho. Hadi sasa mawaziri wa nchi za nje wa nchi kubwa za magharibi wameshaonyesha nia yao ya kutokuhudhuria kikao hicho na badala yake kutuma wawakilishi. Mawaziri wachache tu ambao wanatoka eneo la maziwa makuu na marafiki wa eneo hili toka nchi za Ulaya ndiyo wameonyesha uwezekano wa kuhudhuria ingawa Marekani, Canada na nchi za Scandnavia pia walialikwa.

Kwa hiyo hii ni changamoto kwa Tanzania rais wa baraza la usalama na waziri Migiro ambaye ndiye atakayeongoza mkutano huo. Waziri Migiro na timu yake wanapaswa kuwa na mwanzo mzuri kwa namna watakavyotumia muda huu hasa mkutano wa Januari 27 ili kueleza dunia sera ya nje ya Tanzania ni nini. Na sera hiyo inapaswa iwe makini na nzuri ili kuendelea kurudisha heshima ya Tanzania kwenye umoja huo na kuirudishia Tanzania mvuto tuliowahi kuwa nao kimataifa siku za nyuma. Ila katika yote tunaamini Waziri Migiro atafanya vizuri na Tanzania itatumia muda wake wa uongozi wa baraza la usalama kuieleza rasmi dunia sera na mipango ya kimataifa ya serikali ya awamu ya nne.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.