HATUJASAHU: ULIAHIDI KUINUA KILIMO WAKATI WA KAMPENI

By , Antar Sangali

Serikali ya wamu ya nne imepatikana nchini Tanzania ikiongozwa na Rais mpya Mhe Jakaya Kikwete kwa misingi ya demokrasia kupitia uchaguzi uliyokuwa huru na wazi Didemba 14 mwaka 2005. Tanzania, nchi iliyopata uhuru wake Tarehe 9 Desemba 1961 kutoka katika udhamini wa utawala wa Kiingreza imepita katika vipindi kadhaa vya mpito vya kisiasa, kiuchumi na kiviwanda.

Awamu ya kwanza ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ni awamu iliyoharakisha uhuru na kujenga misingi ya kujitawala kidemokrasia,umoja wa kitaifa na kufuta dhana za kikabila na kidini. Ni wazi na dhahiri mafanikio ya awamu ya kwanza ndiyo yaliotandika zulia la utulivu na maelewano miongoni mwa watanzania leo baada ya miaka 44 kupita ya kujitawala wenyewe.

Awamu ya pili ya Mzee Ali Hassan Mwinyi ndiyo iliyofungua milango ya demokrasia na mapinduzi ya hali ya uchumi na hasa pale alipoazimia kama Mwenyekiti wa CCM kulizika mchanamchana Azimio la Arusha baada ya kulipitisha Azimio la Zanzibar ambalo lilijulikana kama mabadiko ya 11. Aidha awamu hii ndiyo iliyotanua wigo wa uhuru wa vyombo vya habari,uhuru wa kujieleza na vyama vingi vya siasa nchini mwaka 1992

Mzee Ben Mkapa ameirithi Tanzania na kuiacha katika mafanikio makubwa ya kimaendeleo na kupunguza kwa kiasi fulani umasiki wa watu vijijni ingawaje ni vigumu kuaminika hilo, lakini kwa mtu kama mimi niliyezaliwa na kuishi kijijini natambua maisha ya leo Tanzania vijijini si yale maisha ya kupanga foleni na kula unga wa mahindi ya njano na kugawana lishe kwa kaya. Tuka ama tusitake Mkapa ameiacha Tanzania katika Bongo Mchicha inayotakiwa kwani laiti aliye nje ya Taifa hili lau kwa miaka kumi iliyipiita akija sasa hataamini macho yake kama kweli hiyo ndiyo ile Bongo meng'emen'ge ambayo barabara hazipitiki, zahanati zisizo na madawa,madarasa mabovu ya kusomea au kadhia ya madaraja yanayokwamisha usafiri kufika kwa urahisi baina ya Mkoa kwa Mkoa au nchi kwa nchi.

Huenda zama za siasa ya ujamaa na kujitegemea nchini Tanzania zinakoma kutokana na mlipuko wasasa wa utandawazi, tutakumbuka pia kuwa huko nyuma Tanzania ilifanya majaribu mengi ya kimaendeleo katika nyanja za viwanda ili kukuza uchumi kwa kuanzishaji mashirika ya umma chini ya mfumo wa chama kushika hatamu mpaka serikali kulazimika kufanya biashara kama vile RTC, NMC, DAPCO, DAFCO,NARCO, GAPCO, BHESCO na AISCO.Pia tutakumbuka kuwa katika kipindi cha utawala wa Mwalimu kilimo kilitangazwa rasmi kuwa uti wa mgongo wa taifa.

Ingawa Tanzania ina mito mingi, maziwa, mbuga na mabonde yenye rutuba yasiyo hesabika, bado kilimo chake kinategemea mvua za misimu licha ya kwamba sasa uharibifu wa misitu yetu umekuwa mkubwa na kuathiri mazingira na hali ya hewa hivyo kupungua kwa kiasi kikubwa kiwango cha mvua inayopatikana kwa mwaka .Ikumbukwe kuwa asilimia 80 ya watanzania bado wanategemea kilimo na kwamba: wakulima wake wadogo-wadogo waishio vijijni wanalima kilimo duni na kupata mavuno haba yasiyo wakwamua katika dimbwi la umasikini.

Ni wazi kuwa hakukua na msukumo uliofaa katika kukuza na kuimarisha kilimo na kuinua maisha ya wakulima hasa wale walioko vijijini ambao ni mababa-kabwela na walalahoi hohehahahe mbali na kauli mbiu ya siku nyingi, "kilimo ni uti wa mgongo wa taifa." Leo hii wakulima walio wengi wanapata mazao haba kutokana na kukosa ushauri wa kitaalam, nyenzo za kisasa, pembejeo na mbolea zisizofika kwa wakati kwa mkulima wa kijijini tukiweka kandao kwanza tatizo sugu la ukosefu wa mvua ingawa kuna vyanzo vingi vya maji vinavyoweza kutumiwa kufanikisha kilimo cha umwagiliaji.

. Mhe Kikwete amekuwa serikali kwa muda mrefu na anaumia sana maisha duni ya wakulima na wafugaji na amesikika akihimiza ni vema kilimo kikaimarishwa na wafugaji wakatoka katika kuchunga na kuwa wafugaji wenye tija na kipato. Hebu valia njuga kama ambavyo Mzee Mkapa alivyolivalia kibwebwe suala la ukusanyaji wa mapato na Taifa likawa limepiga hatua kwa mwendo wa haraka na kujizolea sifa lukuki kwa nchi wahisani na jumuiya ya Kimataifa.

"Kilimo uti wa mgongo," ni wimbo uliokuwa ukiimbwa kwa muda mwingi katika nchi yetu lakini utelekezaji na uchezaji wa ala za muziki huu umebaki ukielea hewani bila ya msimamizi na muongozaji wa midundo yake.

Hotuba yake aliyoitoa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ni hotuba nzito na kwa upande wangu naweza iita ilikuwa ni hadidu za rejea na au mipango kazi ya serikali yake katika miaka mitano ya awali katika utawala. Kimsingi ilikuwa ni hotuba iliyomgusa kila mtanzania mwerevu na mwenye kuumia na utaifa wetu na laiti Mwalimu angelikuwa hai angelifuraia kuona kijana wake aliyemlea katika mikono yake ni jabali, mahiri na mwenye upeo kulingana na jukumu la urais alilowaomba watanzania wenziwe wampatie. Hobuba yake ilimkuna kila mtu na kuamsha wengi usingizihasa wale walafi na wamero ambao wanaoitazama nchi kwa kutaka kuimaliza na kuzifisidi rasilimali zake, uchumi wake na kudumaza maendeleo ya jumla ya Taifa hili.

Watanzania wanasaubiri kwa hamu kubwa utekelezaji wa ahadi na malengo kumi aliyoyatamka Mhe Rais katika Bunge kwa kuamini ni funguo imara ya kufungulia matatizo ya muda mrefu katika nchi yetu. Mhe Rais ameapa serikali yake kuipitia mikataba yote ili kujua kama kuna ghiliba na udanganyifu wa kuiteketeza na kuiibia nchi na umma watu wake masikini sana. Lakini amepania pia kupambana na vitendo vya rushwa katika mwendo wa hali ya juu na wa kisayansi ili kukomesha wizi na ubadhirifu wa mali za serikali sambamba na kushamirisha demokrasia ya vyama vingi, uhuru katika mahakama, utawala bora wa sheria na kuheshimu haki za binadamu. Yote haya ni maeneo swadakta, lakini tafadhali Mhe Rais chondechonde tuitumie ardhi yetu yenye rutuba kwa kilimo na sasa iwe ni zamu ya wakulima kuoneneka na kustawi kimaisha na kimaendeleo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.