WALIOHUSIKA NA TUHUMA ZA IPTL WATANGAZWE HADHARANI

Na, Magabe Kibiti

Kimbembe cha IPTL kilianza kama mchezo vile pale Waroho wachache serikalini walipo shirikiana na magaidi wa kiuchumi wa ki--Malaysia kuandika mkataba ambao umesababisha hasara kubwa sana kiuchumi kwa serikali na wananchi binafsi. Kinachokera zaidi ni kwamba viongozi waliokuwa madarakani wakati huo na kusaini huo mkataba hawasemi chochote na hivyo kusababisha kila mtu ajitafutie majibu yake mwenyewe.

Sio kazi yangu leo kutaja viongozi wa serikali waliohusika kusaini mikataba hiyo maana bado naendelea kupata majina zaidi ya wahusika siku hadi siku. Cha ajabu zaidi baadhi yao wamo kwenye serikali ya  kasi, ari na nguvu mpya. Ninachojaribu kuongelea leo ni upande mwingine wa mkataba wa IPTL-- wahusika na wamiliki wa IPTL.

Tunajua na tunakubali kuwa itakuwa kazi ngumu sana kubatilisha mkataba wa IPTL kwa sababu kufanya hivyo itakuwa ni kwenda kinyume na mikataba na sheria za kibiashara duniani. Habari njema ni kwamba, mikataba na sheria hizo za nchi yetu na mataifa mbalimbali duniani, zinaturuhusu kuwafahamu wamiliki wa Kampuni yoyote ile inayofanya biashara nchini. Hii ni pamoja na Kampuni gaidi kiuchumi la IPTL. Yaani kwamba, jamii ina kila haki Kikatiba kuwajua kwa majina yao hao wamiliki wa IPTL ikiwezekana pia wale wote waliohusika kusaini mkataba huo kwa niaba ya serikali.

Ukweli ni kwamba, wengi wa hao maafisa wa kiserikali waliohusika kutia saini mikataba hiyo mibovu kwasasa hivi wanaishi maisha ghali kama peponi vile na kunywa juice iliyochanganyikana na damu ya maisha ya watanzania. Pamoja na kujua hayo, bado nitaendelea kuwauliza watanzania wenzangu wote kuungana na mimi ili kuishinikiza serikali iwatangaze hadharani kwa majina wamiliki wote wa kampuni hiyo ya ki-Malaysia ya IPTL.

Kwa upande wao, IPTL wanaweza kuamua kubadilisha mioyo yao na kuamua kujenga imani kwa wananchi kwa kuachana na ugaidi wao wa Kiuchumi na kuanza Kuwauzia watanzania umeme nafuu unaoenda sawia na hali halisi ya pato la watanzania wa kawaida. Na Kama hawawezi kufanya hivyo--basi wavunje mkataba huu kwa sababu kama ni utajiri wa kupindukia wameshaupata kwa sasa. Wasipofanya hivyo, watakuwa wamejibu wenyewe swali ambalo watanzania wanajiuliza siku hadi siku. Ni nini ajenda ya IPTL kwa Tanzania ?

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

Serikali yetu nayo imezidi mno kwa usiri..! Nasikia sasa wamekodi menejimenti ya kigeni ya Afrika kusini [ NetGroup Solutions (Pty)] itakayoiendesha TANESCO kwa usiri mkubwa..!! Kwanini tufichwefichwe kama mikataba hiyo siyo ya kuwanufaisha wajanja wachache?--Ed

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.