ACHENI KUTUYEYUSHA, PASIPOTI ZETU ZIKO WAPI?

Na, Edward chacha

Kinachokera zaidi ni pale tunaposoma kwenye magazeti na kugudua kuwa tatizo la ucheleweshwaji wa pasipoti mpya sio upungufu wa vitendea kazi kama ambayo maafisa wa uhamiaji walivyowahi kueleza hapo awali, bali tatizo ni kuwa-raia walalahoi wa kawaida bado hawajawa tayari kupaka mafuta viganja vya maafisa dhalimu wa uhamiaji. Shukurani za dhati kwa uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti la Guardian(Jan 30,06) na kisha kuanika wazi uvundo huo unaondelea katika wizara hiyo.

Tunatambua na tunakubali kuwa zoezi zima la ubadilishaji wa pasi mpya ni gumu na linahitaji tahadhali ya hali ya juu, lakini habari zilizoandikwa hivi karibuni kwenye gazeti la kila siku la kiigereza(Guardian) zinakatisha tamaa na kutufanya tuondokewe na imani kabisa na serikali hii ya kasi..., ari....na nguvu mpya.

Iweje leo wa-rundi na wa-kongomen wapewe pasi za Tanzania kwa urahisi kiasi hicho na bila usumbufu wowote ule eti kwasababu tu wanapaka mafuta viganja vya maafisa dhalimu wa Uhamiaji huku raia halali wa Tanzania wakisota kwa miezi yapata sita sasa bila hata ya mafanikio wala matarajio ya kuwa iko siku watakuja-pata hizo pasi mpya!? Hili ni swali ambalo kila mtanzania ana haki ya kuuliza na kudai majibu yake toka kwa viongozi wa serikali hii ya awamu ya nne inayoonekana kubwabwaja maneno mengi huku ikionyesha vitendo sifuri/hewa.

Na ikiwa ni kweli kuwa pasi zetu zimecheleweshwa kutokana na uhaba wa vitendea kazi katika wizara husika; swali linabaki kwamba, je kwanini serikali iliamua kujiingiza kwenye zoezi hili gumu la ubadilishaji wa pasipoti za zamani pasipo kujiandaa vya kutosha? Isitoshe, serikali kila mwaka inatenga fungu maalumu (bajeti) kuiendesha wizara hiyo, je, fedha hizo zinatumika kwa shughuli gani? Sio hilo tu, je fedha walizotutoza kama gharama ya hizo pasi ($85 kwa kichwa) zimekwenda wapi? Au zimetumika-tumikaje? Tunaomba serikali itupatie maelezo ya kina.

Kwa upande mwingine hii dhana ya serikali kuibuka na falsafa za "Emergency travelling documents" inamkanganyo ambao unahitaji kupewa mtazamo mpya. Mfano, hivi karibuni vijana wawili raia wa Tanzania waishio Marekani (majina tunayahifadhi) walisafiri kuelekea nyumbani kuwasalimia ndugu na jamaa. Kwakuwa walisubiria pasi zao mpya kwa miezi nenda rudi bila kuzipata kama tulivyo wengi wetu, basi wakaamua kwenda ubalozini kuchukua hizo hati za dharura za kusafiria (emergency travelling documents). Huko ubalozini walihakikishiwa kuwa pasi za zamani zinafaa kuingilia nchini ila watahitaji hizo "emergency travelling documents" wakati wakirudi Marekani. Lakini cha kushangaza ni kwamba, kwa mujibu wa vijana hao, waliingia nchini bila tatizo lolote kabisa ila walipokuwa wanarudi ndipo hasa kitimutimu kilipoibuka. Kwanza, afisa mmoja wa uhamiaji nchini Tanzania hakutambua hizo travelling documents kazi yake ni nini kitu kilichomfanya amzuie kijana mmoja asi-board ndege. Ila baada ya kijana huyo kumuona bosi wa huyo afisa(gumbaru)-kijana aliruhusiwa ku-board ndege. Songombingo hazikuishia hapo, walipofika Marekani maafisa wa uhamiaji wa Marekani wakakataa katakata kuwa hawazitambui kabisa hizo travelling documents ila kwa kuwa hao vijana walikuwa na uraia wa kudumu wa marekani walikubaliwa kuingia. Je, ingekuwaje kama wasingekuwa na huo uraia wa kudumu?

Wallahi, hata mimi ningekuwa hao mafisa uhamiaji ningewakatalia hao vijana kuingia marekani. Maana kama maafisa wa uhamiaji wa Tanzania wanatatizwa na hizo "emergency travelling documents" ambazo wao ndio wamezipendekeza, unategemea itakuwaje kwa maafisa wa nchi za kigeni ?

Swali ni kwamba: hivi kuna serikali tatu ndani ya serikali ya Muungano ama bado ni zilezile mbili? Nauliza swali hilo kwasababu ubalozi wa Tanzania Marekani una "act" kama serikali ya tatu ndani ya Muungano inayojitegemea na yenye mamlaka ya kuendesha mambo kivyake-vyake. Kwani ubalozi huo umekuwa ukitoa maelezo ya kiserikali yasiyo ya kweli na yanayotatiza wengi kana kwamba wenyewe ni serikali nyingine inayojitegemea ndani ya muungano. Ni zamu sasa kwa Mh.Kikwete kuzitembela hizi afisi zetu za kibalozi ili awapige madongo kama alivyofanya huko nchini wakati alipozuru wizara mbalimbali za kiserikali

Kando ya hilo, Kinachosikitisha zaidi ni kwamba baadhi yetu hapa tulipo tunaishi kwenye nchi za watu kinyume na sheria zilizowekwa kwasababu tu ya uzembe wa viongozi wachache wa idara ya uhamiaji. Nasema hivyo kwasababu hapa tulipo ni vurugu mechi unapokuja kwenye suala la pasi. Wapo wenye pasi mpya na wengine pasi za zamani kitu ambacho kinafanya tushindwe kutambuliwa kiurahisi kuwa ni yupi hasa raia halali wa Tanzania na yupi ambaye siye. Hebu tujiulize swali dogo lakini la msingi. Itakuwaje endapo kama itatokea bahati mbaya raia watatu wote wa Tanzania wakamatwa na kuombwa kuonyesha vitambulisho vya uraia wao na huyu akatoa pasi ya zamani, yule pasi mpya na mwingine traveling documents...!! Unadhani itaonekanaje mbele ya huyo aliyewakamata? Si itaonekana kuwa wote wamegushi pasipoti hizo? Kwanini serikali inatutakia matatizo yasiyo ya lazima lakini? Na kwanini tutelekezwe huku ng'ambo na kuachwa bila kuthaminiwa kama sisi sio raia halali wa Tanzania baada ya serikali yetu kuwa imekomba dola zetu 85 na kuzitia kibindoni?

Ingekuwa vema endapo kama serikali ingetueleza waziwazi kuwa, kutakotana na sababu hizi na zile, wameshindwa kutekeleza ahadi walizo ahidi kuwa wagetupatia pasi zenu ndani ya wiki sita kuliko kakaa kimya na kutufanya tushindwe kujua kinachoendelea.

Hivi ni lini serikali yetu itakaa na kusema, "basi, raia kwanza, matumbo baadaye?

Mungu ibariki Tanzania!

TUMA MAONI YAKO [HAPA]

<<BACK TO MAIN PAGE >>

©Copyright:BongoTz.Com -MMV. All Rights Reserved.